Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Snare; Kutoka kulala stendi ya basi hadi kurejea upya

NAMB 01

Muktasari:

  • Msanii huyo aliyepata umaarufu kupitia kundi la East Coast Team, anasema licha ya kutoonekana sana kwa kipindi kirefu, hakuwa ameacha muziki, bali alikuwa akiendelea kutengeneza kazi zake nje ya mfumo wa mainstream.

MWANAMUZIKI mkongwe wa Bongo Fleva, Adam William Semkwiji maarufu kama Snare, ameamua kurejea kwenye muziki  kupitia kazi zake binafsi, akianza na wimbo mpya wa Boom Shagalaa alioufanya kwa kushirikiana na Junior King.

Msanii huyo aliyepata umaarufu kupitia kundi la East Coast Team, anasema licha ya kutoonekana sana kwa kipindi kirefu, hakuwa ameacha muziki, bali alikuwa akiendelea kutengeneza kazi zake nje ya mfumo wa mainstream.

Katika mahojiano  maalumu na Mwanaspoti ambalo lilifunga safari hadi Kibaha Picha ya Ndege na kufanya mahojiano na Snare, anafunguka kuhusu safari yake ya muziki, historia ya jina lake, uhusiano wake na East Coast Team, mchango wa Profesa Jay katika Hip Hop, mirabaha na matarajio yake baada ya kurejea rasmi kwenye muziki.


SNAR 01

JINA LA SNARE LILIVYOZALIWA

Anaanza kuelezea safari yake, Snare anasema jina lake lilianza kutumika wakati akiwa kwenye harakati za muziki na marafiki zake, akiwamo Mwana FA, AY na wengine.

Anasema jina hilo lilipata nafasi wakati wakitengeneza wimbo Safi, uliohusisha Ray C, ambapo Mwana FA alikuwa akiandaa mistari yake ya rap.

“Wakati tuko studio tunatengeneza lyrics za Binamu, wimbo ambao Mwana FA, alirap verse yake, akianza na mistari inayotaja Hamisi Mwijuma na Ambwene Yesaya, kulikuwa na nafasi kwenye mistari ile, nikashauri tumwambie producer agonge ‘Snare’, lakini Binamu akasema hapana, hapo sisi tutasema neno Snare,” anasema.

Anaongeza kuwa baada ya tukio hilo, Mwana FA alianza kumtafuta kwa jina hilo la Snare kila alipofika maskani, na hatimaye likawa sehemu ya utambulisho wake wa kisanii.

Kwa jina lake halisi, anasema ni Adam William Semkwiji, mtoto wa Elizabeth Semkwiji na William Semkwiji. Anaeleza kuwa kwa upande wa mama yake ni mtoto wa pili katika familia, akiwa na dada watatu na mdogo wake mmoja wa kiume.


EAST COAST TEAM, BADO IPO?

Snare anajitambulisha kama mmoja wa waanzilishi wa East Coast Team, kundi lililokuwa sehemu ya safari ya Bongo Fleva katika miaka ya nyuma.

Anasema uhusiano wake na wenzake ulianza kupitia urafiki, kabla ya kuingia studio na kuanza kurekodi nyimbo zilizochangia kuimarisha umoja wao kama kundi.

“Baada ya kumaliza shule, tulikuwa mimi, Baff, AY na GK. Baff alikuwa anaishi Upanga, mimi nilikuwa Kibaha, wakati AY alikuwa Morogoro. Tulipokuwa tunaenda mjini, tulikuwa tunaingia kwa kina Baff,” anasema.

Anaeleza kuwa kupitia Baff walipata nafasi ya kufahamiana na GK, na baadaye walipoanza kwenda studio kurekodi nyimbo, ndipo East Coast Team ilipoanza kujengeka.

Kuhusu kama kundi hilo bado lipo, Snare anasisitiza kuwa halijafutika, licha ya yeye kuamua kufanya kazi zake binafsi.

“East Coast ipo, Sema tu sasa hivi ni wakati wangu kufanya solo project, yaani kazi binafsi ambazo nimeamua kuzifanya na Momb’s Records, kwa sababu mimi ni mmoja wa Momb’s,” anasema.

SNAR 04

ALIKUWA WAPI KIPINDI CHOTE?

Kwa mashabiki ambao wamekuwa wakijiuliza alikokuwa Snare kwa kipindi ambacho hakuwa akisikika sana kwenye vyombo vya habari, msanii huyo anasema hakuwa ameiacha kabisa sanaa.

Anasema katika kipindi hicho alijaribu pia kujikita kwenye tasnia ya filamu, akianzisha kampuni yake na kufanya baadhi ya kazi, huku akiendelea na mambo mengine ya maisha.

“Nilikuwa nafanya muziki, sema sikupeleka kwenye mainstream, redio, televisheni na kadhalika. Kuna kipindi nilifungua kampuni yangu ya kutengeneza filamu, nikafanya kazi mbili tatu, nikaenda kufanya utafiti kuhusu filamu, nikarudi na maisha mengine yakiendelea,” anasema.

Kwa mujibu wake, uamuzi wa kuanza kupeleka kazi zake kwa umma zaidi sasa umetokana na kazi alizokuwa akizitengeneza katika kipindi ambacho hakuwa akionekana sana.


‘BOOM SHAGALAA’ NA JUNIOR KING

Sasa Snare anakuja na Boom Shagalaa, wimbo ambao anasema ulianza kama wazo wakati wa maandalizi ya studio ya Momb’s Records

Anasema baada ya kuchagua biti iliyomvutia, alianza kuijengea wazo la wimbo huo, akaandika mistari na kuwashirikisha wasanii wenzake waliokuwa naye katika harakati za studio.

“Wazo la ‘Boom Shagalaa’ lilikuja wakati tunafungua studio yetu ya Momb’s Records, nilikuwa nahangaika na maproducer, nikachagua biti, nikaenda kuifanyia kazi. Nikaja na wazo la ‘Boom Shagalaa’ kama mlipuko uliotawanyika, nikatengeneza idea na kuweka mistari,” anasema.

Anasema Junior King alishirikishwa katika kazi hiyo baada ya kuangalia namna ambavyo wimbo ungeweza kukamilika kwa ushirikiano wao.

“Nilishirikisha wanangu wa Mombs Records tukakubaliana Junior King aingie. Hapo ndipo ilipotokea ‘Boom Shagalaa’. Tulikuwa tumemaliza kufunga vifaa vya studio, tukatengeneza wimbo huo,” anaeleza.

Kuhusu aina ya muziki atakaoufanya katika kazi zake zijazo, Snare anasema hataki kujifunga kwenye aina moja ya midundo, iwe Hip Hop, Amapiano au Singeli.

“Music is universe. Natengeneza muziki kutokana na jinsi ninavyoona soko linahitaji, lakini pia kile ninachokipenda na ninachokiweza zaidi. Itategemea na soko, lakini tunafanya muziki wa aina yoyote,” anasema.

Anaongeza kuwa kwake muhimu ni kuhakikisha ujumbe unaowasilishwa unamfikia msikilizaji na kueleweka, bila kujali aina ya midundo iliyotumika.


SNAR 07

MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA MUZIKI

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata katika safari yake, Snare anasema muziki umemsaidia kujenga mahusiano na watu mbalimbali, yakiwamo ya kibiashara.

Anasema uaminifu alioupata kupitia kazi zake za muziki umekuwa na mchango katika ushirikiano wake na watu anaofanya nao biashara.

“Ukiangalia tulikotoka mpaka hapa tulipofika, kuna sehemu tumekutana na watu ambao wameweza kutusaidia kutokana na kazi ya muziki. Hata kwenye biashara zangu kuna watu tunashirikiana nao, na uaminifu umekuja kutokana na kuniona kwenye kazi za muziki,” anasema.

Hata hivyo, anataja mfumo wa malipo ya mirabaha katika mazingira ya kidijitali kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji maboresho zaidi.

Anasema pamoja na muziki kuendelea kuhamia kwenye majukwaa ya kidijitali, bado kuna haja ya kuhakikisha kazi za wasanii zinatambuliwa na kuingizwa kwenye mifumo inayowawezesha kunufaika na mapato yake.


MIAKA 30 YA BONGO FLEVA

Kwa Snare, tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva ni fursa muhimu ya kuwakutanisha wasanii wakongwe na kuwakumbusha mashabiki historia ya muziki huo.

Anawapongeza waandaaji kwa kuandaa jukwaa linalowapa nafasi wasanii walioshiriki katika kujenga safari ya Bongo Fleva kuonekana tena mbele ya mashabiki.

“Kiukweli, ni tamasha ambalo kwanza tuwapongeze waandaaji. Kama binadamu, mapungufu lazima yawepo, lakini kwa kiwango kikubwa wamefanya kitu kizuri kuweza kuwakutanisha wakongwe, wasanii waliotengeneza njia ya muziki wa Bongo Fleva,” anasema.

Snare anasema ameshiriki kupanda kwenye jukwaa hilo na anaona linatoa fursa kwa mashabiki ambao huenda hawakupata nafasi ya kuwaona wasanii hao wakitumbuiza wakati wa umaarufu wao.

“Jukwaa ni bomba sana. Unapokuwa pale unajisikia kama uko sebuleni, kwa sababu wanaonyesha kazi zetu na wewe upo pale. Kuna watu ambao hawakuwahi kuniona kwenye jukwaa, lakini leo wananiona na pia  kupitia chaneli za TV,” anasema.

Mbali na kuenzi historia, anaona tamasha hilo linaweza kuwasaidia wasanii kupata kipato kupitia maonyesho na kuendesha shughuli zao nyingine.

Anasema pia linatoa nafasi ya kulinganisha safari ya muziki wa zamani na wa sasa, huku likiwakumbusha wasanii walikotoka na wanakoelekea.


SNAR 08

BONGO FLEVA YA ZAMANI NA YA SASA

Tofauti kati ya Bongo Fleva ya zamani na ya sasa ni suala ambalo Snare analitazama kwa mtazamo wa mabadiliko ya vizazi.

Anasema haoni tofauti kubwa katika msingi wa muziki huo, bali mabadiliko makubwa yanatokana na lugha inayotumiwa, midundo na mazingira ya kizazi husika.

“Bongo Fleva ni midundo ya muziki ya aina zote, lakini tumeweka Kiswahili pale. Maneno yetu ya Kiswahili ndiyo yanaleta kile kitu kinachoitwa Bongo Fleva,” anasema.

Anafafanua kuwa kila kizazi kina misamiati yake, hivyo wasanii wanapaswa kuelewa lugha inayotumika katika jamii badala ya kutegemea maneno ya zamani pekee.

Anasema midundo nayo hubadilika kulingana na nyakati, akitoa mfano wa tofauti kati ya muziki wa miaka ya 1980, 1990, 2000 na wa sasa.

“Kilichobadilika ni wakati, lakini huu muziki naona uko vilevile. Maneno na wakati ndiyo vinabadilika, hata midundo lazima itofautiane kwa sababu sasa tuko mwaka 2026,” anasema.

Kuhusu malipo ya wasanii, Snare anaamini soko la sasa lina nafasi nzuri zaidi ya kuzalisha mapato kutokana na kuboreka kwa miundombinu ya usambazaji wa muziki.

“Miundombinu imeboreshwa. Kulikuwa na mifumo ya analojia kipindi kile, sasa hivi tuko kwenye mifumo ya kidijitali. Kwa hiyo tukitumia vizuri, mapato yataonekana,” anasema.


SNAR 03

WAKONGWE HAWAKUWA WAMEACHA MUZIKI

Snare anapinga mtazamo kwamba wasanii wengi wakongwe wanaorejea kuonekana sasa walikuwa wameacha kufanya muziki.

Kwa maelezo yake, baadhi yao walikuwa wakiendelea na shughuli zao za sanaa, lakini hawakuwa wakipata nafasi kubwa ya kuonekana kwa mashabiki.

Anasema tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva limechangia kurejesha umakini kwa wasanii hao, huku matumizi ya mitandao ya kijamii yakiongeza mawasiliano kati yao na mashabiki.

“Hao wasanii walikuwa wanafanya kazi, sema attention ilikuwa imepotea. Baada ya kupata kitu cha Bongo Fleva 30 Years, attention imerudi. Sasa watu wanaonekana kwenye mitandao, wakienda kwenye show, wakifanya mazoezi na kuposti shughuli zao,” anasema.

Anaamini ongezeko la mwingiliano huo linawapa mashabiki nafasi ya kufuatilia kinachoendelea katika maisha ya wasanii waliowazoea tangu miaka ya nyuma.


SNAR 05

PROFESA JAY AMEBADILISHA MITAZAMO

Akizungumzia mchango wa Profesa Jay katika muziki wa Hip Hop, Snare anasema msanii huyo amekuwa na nafasi kubwa katika kubadili namna watu walivyoutazama muziki wa rap nchini.

Anamtaja kama mmoja wa wasanii waliochangia kuvuta usikivu wa watu waliokuwa na mtazamo hasi kuhusu Bongo Fleva na Hip Hop.

“My big brother Profesa Jay, Mwenyezi Mungu amtunze na ampe nguvu. Profesa amefanya vitu vikubwa sana. Nikimchambua hapa tutatumia muda mrefu,” anasema.

Snare anaitaja Mchaka Mchaka kama miongoni mwa nyimbo zilizosaidia kuonyesha uwezo wa Hip Hop kuvutia hadhira pana.

Anasema kazi za Profesa Jay zilisaidia kubadili mitazamo ya baadhi ya watu waliokuwa wakiuchukulia muziki wa rap kama uhuni badala ya sanaa yenye ujumbe na ubunifu.

“Kwa heshima yake, alifanya mchango mkubwa sana kuvuta masikio ya watu wengine ambao walikuwa wanadharau muziki wa Bongo Fleva au muziki wa kurap. Brother Profesa Jay alibadilisha mitazamo ya watu,” anasema.


SNAR 02

USHINDANI WA ZAMANI ULIKUWA NA FAIDA?

Katika kipindi cha nyuma, ushindani kati ya makundi ya muziki ulikuwa sehemu ya mazingira ya Bongo Fleva. Snare anasema ushindani huo ulikuwa na faida pale ulipojikita katika ubora wa kazi badala ya uhasama binafsi.

Kwa mtazamo wake, ushindani uliwafanya wasanii wajitahidi kutengeneza kazi bora ili kuvutia mashabiki.

“Ushindani wa makundi ulichangia sana kukuza muziki kwa sababu watu wanaposhindana wanazalisha vitu bora na kazi nzuri. Ushindani wa kikazi hauna shida, unasaidia kuboresha na kuongeza utengenezaji wa kazi nzuri,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa wasanii wa sasa wanapaswa kuendelea kuwa wabunifu bila kusahau utambulisho wa muziki wa Tanzania.

Anasema matumizi ya midundo ya kimataifa si tatizo, mradi wasanii waendelee kutengeneza kazi zenye alama zinazoonyesha asili yao.

“Tuendelee kuwa wabunifu, lakini kuna alama ambazo tunatakiwa kuziweka zinazoonyesha asili yetu. Tupambane kutengeneza midundo inayotoka kwenye asili zetu au tulivyozizoea,” anasema.


SNAR 06

WASANII ANAOTAMANI KUFANYA NAO KAZI

Snare anasema anatamani kushirikiana na wasanii wa kizazi kipya, lakini anasisitiza kuwa uchaguzi wa msanii wa kushirikiana naye utategemea aina ya kazi anayopanga kufanya.

Anasema hataki kufanya ushirikiano kwa sababu tu msanii ana jina kubwa, bali anataka kuona mchango wake katika wimbo na uwezo wa kazi kufikia hadhira pana.

“Natamani kufanya kazi na wasanii wapya wa kizazi kipya. Nikimuona ambaye anaweza kufit kwenye idea yangu, ndipo ninaweza kufanya naye kazi. Unapochagua msanii, unaangalia atakupa mileage gani. Muziki ni biashara,” anasema.

Hata hivyo, hakutaja majina maalumu ya wasanii anaopanga kufanya nao kazi, akieleza kuwa hilo litategemea mwelekeo wa miradi yake.


MIRABAHA NA NAFASI YA COSOTA

Akizungumzia suala la mirabaha, Snare anaona bado kuna nafasi ya kuboresha namna wasanii wanavyofahamu na kutumia mifumo ya usimamizi wa haki zao.

Anaitaja COSOTA, yaani Copyright Society of Tanzania, akisema taasisi hiyo inapaswa kuongeza ubunifu katika kuwahamasisha wasanii kujiunga na kuweka kazi zao kwenye mfumo.

“COSOTA wanatakiwa waje na vitu vingi vya kibunifu. Kwanza, mbinu gani wanatumia kuwahamasisha wasanii ili waweze kujiunga? Wasanii wanatakiwa waitambue, waweze kwenda kuwa wanachama na kukabidhi kazi zao ili ziingie kwenye mfumo wa malipo,” anasema.

Anaamini uelewa zaidi kuhusu usajili na utunzaji wa kazi za muziki unaweza kuwasaidia wasanii kunufaika na mifumo ya malipo.

Anasema teknolojia inavyoendelea kukua, ni muhimu mifumo hiyo kuendana na mabadiliko ili wasanii wengi zaidi waweze kupata manufaa ya kazi zao.


BASATA NA NIDHAMU KATIKA SANAA

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na BASATA dhidi ya wasanii wanaokiuka maadili na taratibu, Snare anasema suala hilo linahitaji elimu zaidi kwa wasanii kuhusu kanuni zinazowaongoza.

Anakiri kuwa wasanii wanaweza kuwa na mitazamo tofauti ya ubunifu, lakini anasema hilo haliondoi umuhimu wa kufahamu na kufuata taratibu zilizowekwa.

“Unaweza ukawa unajaji vitu kwa wakati huu kwa kutaka kulinganisha na wakati wa zamani. Mambo yanaweza kuwa magumu kidogo, lakini si vibaya kuwepo kwa kanuni. Msanii anafikiri nje ya boksi, anaweza kuona anachokifanya kiko sawa, kumbe kuna mtazamo wa jumla kwamba hayuko sawa,” anasema.

Kwa mtazamo wake, wasanii wanapaswa kuelimishwa kuhusu mipaka na taratibu zinazohusika ili waweze kuendeleza ubunifu wao huku wakizingatia sheria.


ARENA KWA AJILI YA SANAA

Katika suala la ujenzi wa Arena kwa ajili ya sanaa na matamasha, Snare anaona miundombinu hiyo ni muhimu kadiri idadi ya watu inavyoongezeka na mahitaji ya burudani yanavyobadilika.

Anasema ingawa miundombinu hiyo inaweza kuonekana kuwa mipya katika mazingira ya Tanzania, ipo katika nchi zilizoendelea na inaweza kusaidia kuboresha namna shughuli za sanaa zinavyofanyika.

“Hivi si vitu vipya katika nchi zilizoendelea. Kwetu, kwa sababu hatujavizoea, ndiyo maana tunaona labda ni jambo la ajabu. Lakini hivi vitu vinatakiwa viwepo kwa ukubwa wake katika sehemu tofauti tofauti,” anasema.

Anaongeza kuwa uwepo wa Arena utategemea uwekezaji na matumizi yake, lakini anaamini miundombinu hiyo inaweza kuongezeka kadiri mahitaji yanavyoongezeka.

Maisha nje ya muziki

Mbali na muziki, Snare anasema anapenda shughuli za ufugaji na kilimo, mambo ambayo anasema ameyazoea tangu akiwa mdogo.

Anataja ufugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe, kanga, bata na sungura, pamoja na kulima mboga kama nyanya na pilipili, kuwa sehemu ya maisha anayoyapenda.

“Tangu nikiwa mdogo tunafuga mbuzi, kuku na ng’ombe. Kwa hiyo napenda maisha ya kuwa na mifugo, bustani na kulima mboga mboga kama nyanya na pilipili. Hiyo ndiyo lifestyle ninayoipenda,” anasema.

Maelezo hayo yanaonyesha kuwa maisha yake nje ya jukwaa yanahusisha shughuli tofauti na muziki, huku ufugaji na kilimo vikiwa sehemu ya mambo anayofurahia.


UJUMBE KWA MASHABIKI

Akihitimisha, Snare anawataka mashabiki wa zamani na wapya kuendelea kumpa nafasi kupitia kazi zake mpya, akiamini muziki anaoufanya una ubunifu unaoweza kuendana na mahitaji ya wakati huu.Pia jina la Snare kwasasa aitwe Uncle Snare.

Anasema mashabiki wa sasa wanachotaka ni kazi nzuri, bila kujali msanii anatoka kundi gani au amekuwa kwenye muziki kwa muda gani.