Siyo ndoto tena! Mashindano ya dunia yanarudi nyumbani
Muktasari:
- Kenya iliibuka mshindi mbele ya London ya Uingereza na Roma ya Italia, wakati Munich ya Ujerumani ikapewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka 2031.
KENYA imeandika historia mpya katika riadha baada ya kushinda zabuni ya kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2029, huku Nairobi ikiwa jiji la kwanza barani Afrika kupewa heshima hiyo.
Kenya iliibuka mshindi mbele ya London ya Uingereza na Roma ya Italia, wakati Munich ya Ujerumani ikapewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka 2031.
Haya ni mashindano makubwa zaidi ya riadha duniani na yamekuwa yakipewa heshima kubwa sana kutokana na upekee wake.
Rais wa Kenya, William Ruto, akizungumza juzi alisema uamuzi huo ni ushindi kwa vizazi vya wanariadha waliolifanya taifa hilo kuwa maarufu duniani katika katika mchezo huo unaoshika nafasi ya tatu kwa kupendwa Afrika Mashariki na Kati baada ya soka na ngumi.
“Michuano ya Dunia inarudi nyumbani,” alisema Ruto, akisisitiza kuwa Kenya itahakikisha inatoa mashindano yatakayokidhi hadhi ya wanariadha wake, bara la Afrika na dunia.
UZOEFU WA KENYA KWENYE RIADHA
Uamuzi wa kuipa Nairobi mashindano hayo ulitangazwa Budapest, Hungary, na Rais wa World Athletics, Lord Sebastian Coe, ambaye alieleza kuwa zabuni ya Kenya ilikuwa na hoja zenye nguvu na iligusa hisia.
Kenya ni moja ya mataifa yaliyofanikiwa zaidi katika historia ya Mashindano ya Dunia ya Riadha ikiwa na jumla ya medali 72 za dhahabu, ikizidiwa na Marekani pekee.
Mafanikio hayo yamejengwa zaidi kupitia mbio za kati na ndefu, huku taifa hilo pia likiwa limekusanya medali 38 za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki.
Miongoni mwa majina makubwa yaliyotajwa katika kampeni ya Kenya ni bingwa wa Olimpiki mara mbili Eliud Kipchoge, ambaye alihusika katika kushawishi kupatikana kwa zabuni hiyo, bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 800, David Rudisha, pamoja na bingwa wa dunia na Olimpiki, Faith Kipyegon.
Coe alisema riadha “imejenga ndani ya maisha ya taifa” la Kenya na kwamba Wakenya wamekuwa sehemu muhimu ya historia ya mchezo huo.
MASHABIKI
Mbali na mafanikio ya wanariadha, Kenya ilikuwa na nguvu nyingine kubwa mapenzi ya wananchi kwa riadha.
Kwa mujibu wa utafiti wa World Athletics, asilimia 68 ya Wakenya waliohojiwa walisema wana kiwango kikubwa cha kuvutiwa na riadha, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 39 duniani kote ambao wamekuwa wapenzi wa mchezo huo.
Riadha pia ni mchezo wa pili kwa kufuatiliwa nchini humo, nyuma ya soka hali ambayo inawafanya mashabiki wapagawe na uwepo wa mashindano hayo ambayo yatawahusisha mastaa wote wa riadha duniani kote..
Katika tathmini ya mitandao ya kijamii iliyofanywa na World Athletics, Kenya ilikuwa taifa la nne kwa idadi ya wafuasi, jambo lililoonyesha ukubwa wa mashabiki wa mchezo huo nchini.
SOMO LA 2025, UWEPO WA AFCON
Kenya ilikuwa imeomba kuandaa Mashindano ya Dunia ya 2025, lakini ilishindwa na Tokyo, Japan.
Moja ya changamoto kubwa katika zabuni hiyo ilikuwa ubora wa miundombinu.
Safari hii, Kenya ilirudi ikiwa na mpango mkubwa wa kuboresha miundombinu, hasa Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.
Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 48,000 unafanyiwa maboresho makubwa na unatarajiwa kutumika pia katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambazo Kenya itaandaa kwa pamoja na Tanzania na Uganda.
Barnaba Korir, aliyekuwa sehemu ya timu ya zabuni ya Kenya, alisema taifa hilo lilijifunza kutokana na kushindwa kwa zabuni ya 2025.
Alisema maeneo ambayo Kenya haikufanya vizuri awali yaliboreshwa kabla ya kuwasilisha zabuni mpya.
UTALII UPO
Kenya pia iliangazia uwezo wake katika sekta ya utalii na ukarimu.
Nairobi ni mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa mara kwa mara, huku jiji hilo likiwa na vivutio vya utalii, ikiwemo hifadhi ya wanyama iliyo ndani ya jiji.
Maofisa wa serikali walisema uwezo wa nchi hiyo kupokea wageni wengi pamoja na uwepo wa hoteli za kutosha ni miongoni mwa mambo yaliyoiimarisha zabuni ya Nairobi.
Serikali ya Rais Ruto pia ilitoa dhamana kuhusu masuala ya fedha na usalama ili kuhakikisha Kenya inapata haki ya kuandaa mashindano hayo ambayo yamekuwa yakifuatiliwa kwa karibu zaidi duniani kote.
NDOTO IMETIMIA
Kwa mwanariadha wa mbio fupi, Ferdinand Omanyala, uamuzi huo umetimiza ndoto ya muda mrefu ya kuona Kenya ikiwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya riadha duniani.
Omanyala, ambaye amewahi kushindana katika Uwanja wa Kasarani, alisema imekuwa ndoto kuona taifa lake likiandaa mashindano hayo.
Kwa upande wake, Lord Coe alisema World Athletics imekuwa ikilenga kueneza na kukuza riadha katika maeneo mbalimbali duniani.
Alisema wakati umefika kwa Mashindano ya Dunia kwenda Afrika baada ya kupatikana mwenyeji, zabuni na mazingira yanayofaa.
MTIHANI UNAANZA
Baada ya kushinda zabuni, Kenya sasa ina takribani miaka mitatu kujiandaa kwa mashindano hayo ya kihistoria.
AFCON 2027 itakuwa mtihani muhimu wa kwanza, hasa katika kuangalia namna mashabiki watakavyoingia na kutoka Uwanja wa Kasarani.
Uwanja huo upo takribani dakika 30 kutoka katikati ya jiji la Nairobi kwa gari, lakini hauna huduma ya reli inayoufikia moja kwa moja.
Changamoto ya msongamano pia imewahi kujitokeza. Wakati Kasarani ilipotumika kwa baadhi ya mechi za Kenya katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2024, kulikuwa na msongamano mkubwa uliosababisha uwezo wa uwanja kupunguzwa katika baadhi ya mechi.
MAMILIONI YA FEDHA
Serikali ya Kenya imekadiria kutumia takribani Dola za Marekani 78 milioni, sawa na takribani shilingi bilioni 195, kugharamia maandalizi ya Mashindano hayo ya Dunia.
Fedha hizo zitatoka serikalini, huku mikataba ya udhamini ikitarajiwa kuongeza nguvu katika bajeti ya mashindano.
Elijah Mwangi, Katibu Mkuu wa Idara ya Michezo, alisema serikali iko tayari kuhakikisha fedha zinazohitajika zinapatikana kwa wakati.
Hata uchaguzi wa rais wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwakani hauonekani kuwa kikwazo kwa maandalizi hayo, huku Korir akisema fedha zilizotengwa zitakuwa sehemu ya makubaliano ya kimataifa yenye nguvu kisheria.
TIKETI MTIHANI
Suala jingine litakalokuwa muhimu ni bei za tiketi na kuhakikisha viwanja vinajaa.
Kenya iliwahi kuandaa Mashindano ya Dunia ya Vijana chini ya miaka 18 mwaka 2017, ambapo tiketi ziliuzwa kwa bei ghali na upatikanaji wake ulikuwa mgumu, lakini idadi ya mashabiki ilikuwa ndogo hadi pale waandaaji walipoamua kuingia bure ndiyo wakaanza kuingia.
Kwa upande mwingine, Mashindano ya Dunia ya Tokyo 2025 yalivutia jumla ya tiketi 619,000 zilizouzwa katika siku tisa za mashindano, huku London 2017 ikiweka rekodi ya tiketi 705,000.
World Athletics imechagua kupeleka mashindano Afrika badala ya kurejea London, ambako tayari kuna historia kubwa ya mashabiki wa riadha.
Sasa macho yatakuwa kwa Nairobi kuhakikisha Kasarani inajaa kila siku, ikiwemo vipindi vya asubuhi.
DAWA ZA MISULI
Pamoja na maandalizi ya miundombinu, Kenya pia itakuwa chini ya uangalizi katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo.
Katika miaka ya karibuni, taifa hilo limekumbwa na visa kadhaa vya wanariadha kufungiwa kutokana na ukiukwaji wa kanuni za dawa za kusisimua misuli.
Mwaka huu pekee, watu 11 kutoka Kenya walikuwa wamefungiwa na Athletics Integrity Unit wakati wa taarifa hiyo.
Hivyo, jukumu la Kenya halitaishia kujenga viwanja na kuandaa mashabiki pekee. Itabidi pia ihakikishe inatoa mashindano yenye uadilifu, usalama na viwango vya kimataifa.
Kwa Nairobi, 2029 sasa si ndoto tena. Ni jukumu la kuhakikisha historia inayoanza kama ushindi wa zabuni inaishia kuwa Mashindano ya Dunia yatakayokumbukwa kwa mafanikio.