Siri ya mashuti Brighton kutoka katikati ya uwanja
Muktasari:
- Wengine walikuwa wameanza kuvuka mipaka ya nchi zao, kufanya ushirikiano na mastaa wakubwa na kuingiza muziki wao katika masoko mapya lakini vifo vyao viliacha maswali kuhusu kazi ambazo wangeendelea kuzifanya na ukubwa ambao wangeweza kuufikia.
BRIGHTON, ENGLAND: BAADA ya Diego Gomez kufunga bao dhidi ya Crystal Palace, Brighton inakaribia kuvunja rekodi ya Ligi Kuu England ya mashuti yaliyopigwa kutoka umbali wa mita 50 au zaidi ndani ya msimu mmoja. Ni kwa nini hali hii inatokea? Haiwezekani kujua kama kuongezeka kwa matumizi ya takwimu za mabao tarajiwa ndiyo sababu pekee, ni sehemu tu ya sababu au hakuhusiani kabisa na mabadiliko hayo. Hata hivyo, inavutia kuona jinsi umaarufu wa takwimu hizo ulivyokwenda sambamba na mabadiliko ya wachezaji kupiga mashuti wakiwa karibu zaidi na lango.
Huenda hali hii ingetokea hata bila maendeleo ya uchambuzi wa takwimu za soka. Kadiri mbinu za ufundishaji zilivyoendelea kuboreshwa na kuwa za kina zaidi, timu huenda zimeanza kufanya mazoezi ya kupeleka mpira karibu zaidi na lango kwa sababu kile ambacho takwimu za mabao tarajiwa zinatuambia tayari kilikuwa wazi; kadiri unavyopiga shuti ukiwa karibu na lango, ndivyo uwezekano wa kufunga unavyokuwa mkubwa zaidi.
HIZO NAMBA SASA
Hata hivyo, bila kujali sababu, takwimu zinathibitisha kwamba katika miaka ya hivi karibuni soka la Ligi Kuu England limekuwa likitegemea kwa kiwango kidogo zaidi mashuti ya umbali mrefu.
Misimu sita ya kwanza ambayo takwimu zinapatikana, kuanzia 2003/04, ndiyo iliyokuwa na asilimia kubwa zaidi ya mashuti yaliyopigwa nje ya eneo la penalti. Hiyo ndiyo misimu pekee katika kumbukumbu ambayo zaidi ya asilimia 45 ya mashuti yalipigwa kutoka umbali wa mbali.
Kwa upande mwingine, misimu mitano ya hivi karibuni, kuanzia 2022/23 hadi 2026/27, ndiyo iliyo na idadi ndogo zaidi ya mashuti ya aina hiyo. Kila mmoja kati ya misimu hiyo ulishuhudia asilimia 35 au chini ya mashuti yakipigwa nje ya eneo la penalti. Hali hiyo inaendana na matarajio , ukizingatia msisitizo uliotajwa awali wa kupeleka mpira karibu zaidi na lango. Bila kujali kama zimekuwa chanzo kikuu cha mabadiliko hayo, klabu zinazotumia takwimu katika kufanya uamuzi zimekuwa na mchango mkubwa.
Kocha Thomas Frank aliwahi kuzungumzia umuhimu wa “kupanua nafasi ya kufunga†alipokuwa akiifundisha Brentford. Kwa misimu mitatu mfululizo, timu yake ilikuwa miongoni mwa mbili bora za Ligi Kuu England kwa wastani wa thamani ya mabao tarajiwa katika kila shuti ililopiga.
Kwa maana nyingine, Brentford, klabu inayofahamika kwa kutumia takwimu katika kufanya uamuzi na ambayo imepata mafanikio makubwa kupitia mfumo huo, ilikuwa ikisubiri kwa uvumilivu fursa sahihi za kutengeneza nafasi zenye ubora wa juu badala ya kupiga mashuti kutoka umbali mrefu. Kufanya hivyo ni ishara ya timu nzuri. Timu zinazoweza kuuchezesha mpira na kuufikisha karibu zaidi na lango ili “kupanua nafasi ya kufunga†zina uwezo mkubwa zaidi wa kupata mabao kwa uhakika. Kupiga mashuti kutoka umbali mrefu ni mbinu yenye hatari kubwa ambayo imekuwa ikipoteza umaarufu kadiri miaka inavyopita kwa sababu uwezekano wa kupata matokeo mazuri kupitia njia hiyo ni mdogo. Hata hivyo, Brighton, inayoshika nafasi ya pili katika msimamo ambayo pia ni miongoni mwa timu zinazotambulika zaidi katika ligi hiyo kutumia takwimu kwa kiwango kikubwa katika usajili wa wachezaji na mbinu za mchezo, inaonekana kwenda kinyume na mwenendo huo.
MAMBO NI MOTO
Shuti la kuvutia la Diego Gomez katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Crystal Palace lilipigwa kutoka umbali wa mita 51.3, jambo lililoliweka katika nafasi ya nane kwenye orodha ya mabao ya ligi hiyo yaliyofungwa kutoka umbali mkubwa zaidi katika kipindi ambacho takwimu hizi zinapatikana, kuanzia msimu wa 2006/07. Mabao manane kati ya tisa yaliyokuwa kwenye orodha hiyo yalifungwa angalau misimu tisa iliyopita.
Na linapokuja suala la wachezaji waliopiga mashuti mengi zaidi kutoka umbali wa zaidi ya mita 50, Charlie Adam, mchezaji wa zamani wa Blackpool na Liverpool anaongoza kwa tofauti kubwa. Ukweli kwamba yupo mbele kwa mbali akiwa na majaribio 25, pamoja na aina ya majina ya wachezaji wanaofuatana naye kwenye orodha hiyo, unaonyesha jinsi upigaji wa mashuti kutoka umbali huo ulivyokuwa jambo la kawaida zaidi katika kipindi cha zamani. Si kitu ambacho timu zimekuwa zikifanya mara kwa mara katika miaka ya karibuni.
Katika kipindi cha Charlie, mashuti hayo mengi yalikuwa ya kujaribu bahati, ambayo pengine hayakuwa na ulazima mkubwa. Kwa mfano, timu yake ya Blackpool ilipiga rekodi ya mashuti tisa ya aina hiyo katika msimu wa 2010/11 bila hata moja kulenga lango.
Lakini je, kwa sasa inawezekana kwamba kuna jambo la kiufundi linalozingatiwa katika mashuti ya Gomez? Kwa hakika, inashangaza kuona akifanya hivyo akiwa katika timu inayozingatia sana matumizi ya takwimu kama Brighton. Baada ya yote, mambo mengi yanayofanywa na klabu hiyo hayafanyiki kwa bahati mbaya. Cha kuvutia ni kwamba mashuti mengi ya umbali mrefu msimu huu yamepigwa na wachezaji wa Brighton.
ZAIDI YA HAYO
Kati ya mashuti 14 yaliyopigwa kutoka umbali wa mita 50 au zaidi katika Ligi Kuu England msimu wa 2026/27, sita yamepigwa na wachezaji wa Brighton. Hiyo ni sawa na asilimia 42.9. Mashuti hayo yanachangia asilimia 6.5 ya mashuti yote yaliyopigwa kutoka sehemu yoyote ya uwanja.
Jumla ya mashuti sita ya Brighton kutoka umbali wa mita 50 au zaidi, ikiwa ni baada ya kucheza michezo 10 katika msimu wa 2026/27, tayari ndiyo idadi ya pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa na timu yoyote ndani ya msimu mmoja wa ligi hiyo. Inazidiwa na Blackpool iliyotajwa hapo juu.
Kwa hiyo, je, kuna jambo jingine linaloendelea hapa? Je, wachambuzi wa takwimu wa Brighton wamegundua fursa fulani ambayo wanajaribu kuitumia ili kupata faida dhidi ya wapinzani? Je, kuna mpango maalumu wa kutishia wapinzani kwa mashuti ya umbali mrefu?
Kocha wa timu hiyo, Fabian Hurzeler, aliulizwa kuhusu suala hilo baada ya bao la Gomez, na alitoa jibu la moja kwa moja bila kuonyesha kusita. “Hatuifanyii mazoezi timu kupiga mashuti kutoka umbali wa mita 50, alisema.
Aina hii ya mashuti lazima iwe na kiwango fulani cha kutumia fursa inayojitokeza uwanjani. Baadhi ya mashuti ya Brighton kutoka umbali mrefu ni majaribio ya kuthubutu, yakilenga kutumia nafasi ya kipa anayekuwa ametoka mbali na lango lake.
Mfano mmoja ni shuti la Chema Andres dhidi ya Arsenal, wakati David Raya alikuwa ametoka mbali na lango lake baada ya kwenda kuokoa hatari iliyokuwa imetokea. Hata hivyo, takwimu zinazozingatiwa zinaashiria kwamba huenda kuna maelekezo fulani yanayotolewa kwa wachezaji wa Brighton, au angalau wanapewa uhuru wa kujaribu kufunga kutoka umbali mrefu wakati wa mchezo wa kawaida (open play).
NI MBINU AU MAELEKEZO?
Huenda kuna mtu ndani ya klabu hiyo aligundua kwamba makipa huwa wanacheza wakiwa wamepanda mbele zaidi wanapokutana na Brighton.
Ukiangalia nafasi ambazo makipa walikuwa nazo wakati Brighton ilipopiga mashuti yake sita kutoka umbali wa mita 50 au zaidi msimu huu, kuna dalili kwamba huenda dhana hiyo ina ukweli fulani. Hata hivyo, bao pekee lililofungwa katika mashuti hayo, lile la Gomez, lilitokea wakati kipa alipokuwa karibu zaidi na lango lake.
Hata kama hakuna matarajio ya kufunga moja kwa moja kupitia mashuti hayo, kuendelea kuwa tishio kwa wapinzani kwa kupiga mashuti ya umbali mrefu kunaweza kuwa mbinu nzuri sana. Iwapo makipa wa timu pinzani watalazimika kuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kupigwa shuti kutoka umbali mrefu, wanaweza kuamua kusimama karibu kidogo zaidi na lango lao.
Hali hiyo inaweza kutengeneza nafasi kubwa zaidi kati yao na safu yao ya ulinzi, jambo litakaloiwezesha Brighton kupitisha mipira ya kupenya katikati ya safu hiyo ya ulinzi. Chaguo jingine kwa wapinzani ni safu yao ya ulinzi kurudi nyuma zaidi, jambo linaloiwezesha Brighton kusogeza mpira mbele zaidi uwanjani. Hali hiyo inaendana zaidi na mtindo wao wa kucheza.
Bila kujali chaguo watakalolichukua wapinzani, uwezekano wa Brighton kupiga shuti kutoka umbali wa mita 50 utasababisha hali ya kutokuwa na uhakika katika safu ya ulinzi ya mpinzani, jambo ambalo linapaswa kuwa faida kwa Brighton.
Brighton ndiyo inayoongoza katika mwenendo huu, lakini kuna uwezekano pia kwamba hali hiyo imeanza kuwa mwenendo wa jumla katika ligi nzima. Msimu huu, shuti moja kutoka umbali wa mita 50 au zaidi linapigwa kila baada ya michezo mitano. Katika misimu 20 iliyopita ya Ligi Kuu England, kiwango cha juu zaidi cha mashuti ya umbali huo kilikuwa shuti moja kila baada ya michezo 17.3, katika msimu wa 2011/12.
Misimu mingine mingi ilishuhudia shuti moja tu la umbali huo kila baada ya michezo 20, 30, 40 au hata 50.
KWINGINEKO...
Hata ukiondoa mashuti ya Brighton, bado unapata kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa, ambacho ni shuti moja kila baada ya michezo 8.75.
Huenda pia umeona kwamba Hull City imepiga mashuti manne kutoka umbali wa mita 50 au zaidi msimu huu, jambo linaloiweka katika nafasi ya pamoja ya sita kwenye orodha ya timu zilizopiga mashuti mengi zaidi ya aina hiyo ndani ya msimu mzima. Lakini, hata ukiondoa Hull City pamoja na Brighton, bado kumekuwa na mashuti manne ya umbali huo katika Ligi Kuu England msimu huu.
Hiyo ni sawa na shuti moja kila baada ya michezo 17.5, kiwango ambacho bado ni cha pili juu zaidi kuwahi kurekodiwa, kikizidiwa kidogo tu na msimu wa 2011/12. Mashuti ya aina hiyo yamekuwa yakipigwa mara nyingi kiasi kwamba bila shaka ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuongezeka kwa wastani wa umbali wa mashuti msimu huu. Kwa wastani, umbali huo umeongezeka kwa mita 0.6, ikiwa ni ongezeko kubwa zaidi kati ya misimu miwili mfululizo tangu 2006/07. Hii ilikuwa ikichukuliwa kama mbinu ya zama zilizopita, iliyokuwa ikihusishwa na wachezaji kama Charlie Adam, Xabi Alonso na Wayne Rooney. Hata hivyo, sasa inaonekana kurejea tena.
Huenda ni mwenendo wa muda mfupi tu mwanzoni mwa msimu, au pengine kuna sababu za msingi zinazoeleza kurejea kwake. Jambo muhimu zaidi ni kwamba uwezo wa kiufundi wa wachezaji umeongezeka kuliko wakati mwingine wowote. Wachezaji wengi waliopo uwanjani siku hizi wanapaswa kuwa na uwezo wa kulenga lango wakiwa katikati ya uwanja. Huenda hali hiyo inawapa ujasiri wa kujaribu mashuti hayo mara nyingi zaidi. Wakati huohuo, makipa wanafanya kazi kubwa zaidi ya kutumia miguu na kucheza katika nafasi za juu zaidi uwanjani.
Siku hizi, kipa wa kila timu anakuwa kama beki wa ziada anayesafisha hatari nyuma ya safu ya ulinzi, huku wengi wakishiriki kwa kiwango kikubwa katika kuanzisha mashambulizi. Makipa wa sasa wanachukua hatari zaidi katika namna wanavyojipanga uwanjani ukilinganisha na makipa wa zamani. Hali hiyo inafungua uwezekano wa mpinzani kufunga bao wakati lango halina ulinzi.
Huenda Brighton imegundua fursa ya kweli, na Hurzeler alikuwa akificha mipango yake aliposema kwamba hawafanyi mazoezi ya aina hiyo ya mashuti. Au pengine yote hayo ni matukio yaliyotokea kwa bahati tu. Kwa kuzingatia jinsi Brighton inavyopanga kwa umakini kila jambo inalolifanya, pamoja na idadi kubwa ya mashuti ya umbali mrefu inayopiga, kuna uwezekano mkubwa kwamba imepanga mkakati huu kwa umakini mkubwa. Makipa wa timu pinzani, wawe macho!