Prime
Hivi zile ‘command’ za ratiba Ligi Kuu zimefutika?
Muktasari:
- Katika video hivyo anazungumzia jinsi mfumo huo unaotumia kompyuta jinsi utakavyofuta malalamiko mengi ya upangaji ratiba za mechi na uahirishwaji holela wa mechi.
Wakati tukiwa kwenye kipindi cha kujadili changamoto za mpira wa miguu kwenye kituo kimoja cha televisheni, iliwekwa video ya rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumzia jinsi mfumo wa upangaji ratiba ya Ligi Kuu ulivyobadilishwa na baadhi ya kanuni kuboreshwa kwa ajili ya fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Katika video hivyo anazungumzia jinsi mfumo huo unaotumia kompyuta jinsi utakavyofuta malalamiko mengi ya upangaji ratiba za mechi na uahirishwaji holela wa mechi.
Mfumo huo ulimaanisha kuwa kompyuta itaingizwa taarifa muhimu kuhusu timu, mechi na siku na kwamba kwa mfumo huo maana yake hakutakuwa na malalamiko ya uchovu wa wachezaji kwa kuwa taarifa zilizowekwa humo zinazingatia muda wa kupumzika wa timu na kwamba kwa wiki timu itaweza kucheza mechi tatu.
Karia alikuwa akizungumza kwa uhakika kwa kile kilichoonekana amehakikishiwa na watendaji wake kuwa kero hizo za uahirishaji mechi za ligi zitapungua na pengine kumalizika kabisa.
Siku hiyo, ndani ya studio kulikuwa na watu wanaojipachika sifa ya ‘infuencers’, au watu maarufu wenye ushawishi, walishajiandaa kusifu hatua hiyo bila ya kuzungumza kwa kina na kuangalia athari na faida zake.
Lakini sikutaka kuwemo ndani ya kundi la wajinga lililo tayari kujidhalilisha kwa kusifia kitu ambacho hakijaandaliwa vizuri na kinaonekana kabisa kwamba hakiwezi kufanya kazi vizuri kama akili na fikra za watumiaji zitakuwa zilezile.
Ili kukwepa kuwa sehemu ya ujinga huo, hapohapo nilisema bayana kuwa hata utumie kompyuta kukurahisishia kazi, kama matumizi yako ya kifaa hicho hayalingani na utashi wa teknolojia yenyewe, hakutakuwa na mabadiliko yoyote.
Karia alisema mfumo huo umewekewa ‘command’ zitakazozuia uahirishaji wa mechi na kupunguza malalamiko, lakini nikasema anayeweka command ni binadamu ambaye wakati wowote anaweza kubadilisha hiyo command ikafanya kazi kwa mazoea.
Nilieleza kuwa ni utamaduni wetu kuzipa klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa muda wa kutosha kujiandaa kwa mechi na hilo limekuwa likisababisha mechi kuahirishwa kila mara na hivyo kuvuruga msimu mzima.
Pia timu ya taifa imekuwa ikikusanywa kwa muda mrefu kabla ya mechi, tofauti na kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), kuhusu muda unaotakiwa wa klabu kuruhusu wachezaji kwenda timu zao za taifa. Timu ya taifa inapowekwa kambi ya muda mrefu, huathiri ligi, na hasa ratiba.
Hata kabla ya Ligi Kuu ya NBC kufikia raundi ya sita, tayari Bodi ya Ligi imebadilisha tarehe ya mechi ya Yanga na Fountain Gate kutokana na mabingwa hao wa soka wa Bara kuwa na mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa wiki jijini Gabarone.
Mechi ambayo ilikuwa ichezwe Jumatano ya Jumatano ya Septemba 2, ilirudishwa nyuma hadi Jumatatu ya Agosti 31 kuipa Yanga muda wa kutosha kujiandaa kwa mchezo huo utakaofanyika Gabarone.
Kwa hiyo, yuleyule aliyeweka command ya ratiba, ndiye yuleyule aliyeingia kwenye mfumo kwenda kuuamrisha ubadili tarehe hiyo na kuwa ile inayolingana na utamaduni wetu wa kuzijali Simba na Yanga.
Na huo ni mwanzo tu. Hapo ni kwa sababu kwa fikra zetu wapinzani wa Yanga katika mechi ya raundi hiyo ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, Gabarone United si timu hatari kama zile za kutoka kaskazini mwa Afrika. Ingekuwa hivyo, hata wiki nzima ingetolewa kwa vigogo hao wa soka Tanzania kujiandaa.
Na ikitokea vigogo hao na wenzao wa Kariakoo, Simba SC wanafika hatua za juu za mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu, basi mikiki yake itakuwa mikubwa na Bodi ya Ligi (TPLB) na TFF hawatakuwa na ubavu wa kusimamia command walizozisifu awali.
Matumizi ya teknolojia katika kila jambo inabidi yaendane na mabadiliko ya kifikra na tabia. Bila fikra kuendana na mahitaji ya teknolojia, hakutakuwa na umuhimu wala ufanisi unaoweza kuletwa na teknolojia.
Hivi sasa tumeanza kutumia teknolojia ya Football Video Support, au msaada wa video katika mechi za soka. Hii ni teknolojia inayotumia kamera za kampuni iliyopewa haki za matangazo ya moja kwa moja ya mechi za ligi, kumsaidia mwamuzi kufanya maamuzi sahihi.
Hakukuwa na jitihada kubwa za kuelimisha wadau kuhusu ujio na utendaji wa teknolojia hii zaidi ya kumuachia Karia aizungumzie kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Matokeo yake baadhi wameanza kutofautiana na matumizi hayo, wengine wakisema wataandika barua ili kuboresha mfumo huo.
Kauli kama hiyo inamaanisha watu hawakuandaliwa kiakili na kifikra kuipokea teknolojia hiyo na wanahisi imetengenezwa kuzisaidia baadhi ya timu.
Na kwa sababu fikra zetu ni hizo, kunaweza kuanza mipango ya kutumia waamuzi kuizunguka teknolojia hiyo kwa lengo ovu la kusaidia timu au michezo ya Kamari.
Kama makocha wanapewa nafasi mbili kila mmoja ya kuomba refa aangalie marudio ya tukio, utawezaje kumzuia mwamuzi kutofanyia maamuzi matukio tata baada ya kocha wa timu moja kumaliza kadi zake mbili?
Kwa hiyo, ni muhimu sana kubadili fikra kwanza kabla ya kuanza kutumia teknolojia kusaidia uendeshaji wa masuala yetu. Kama tusipoanza sasa kupigia kelele matumizi mabovu ya teknolojia, hali huko mbele itakuwa mbaya.