Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Habari za usajili zisifedheheshe waandishi, wachambuzi

MSIMU wa usajili ni kipindi ambacho kimejaa habari zinazosisimua na kustua watu wengi, kiasi kwamba baadhi ya vyombo vya habari huona shida kuachana na habari hizo na kuziendeleza wakati ambao si wa usajili wakizipachika jina la “tetesi”.

Ni habari ambazo zina vuta wengi kwa kuwa kila shabiki hutaja kujua timu yake imesajili wachezaji gani, au mchezaji nyota na mkubwa katika nchi au duniani anaelekea timu gani, au vita iliyopo katika kumnyakua.
Hizi hupita na baadaye hufuatiwa na wachezaji kuthibitisha thamani yao na kukidhi matarajio ya mashabiki wa klabu mpya au ambayo anaendelea kuichezea baada ya kusaini mkataba mpya.

Wapo wanaofanikiwa sana katika hatua hii ya pili, na kusababisha mashabiki waingiwe na wazimu baada ya kuona nyota wao mpya anafanya kile walichokuwa wakitarajia atakifanya baada ya kuhamia klabu yao.
Juergen Klinsmann alijijengea jina kama mmoja wa washambuliaji hatari duniani, akiwa na sifa kubwa ya kufunga mabao ya magoli ya kichwa kwa kuchupa na baadaye kwenda kuserereka kwa tumbo kushangilia goli.

Baada ya kuifungia AS Monaco ya Ufaransa mabao 29 katika mechi 65 na kung’ara kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1994, Tottenham Hotspur ya England ilimsajili katika kipindi cha mwishoni wa uchezaji wake.

Akiwa bado na moto aliouwasha Kombe la Dunia, Klinsmann alifanya kile mashabiki wa Uingereza walichotarajia. Katika mechi yake ya kwanza alifunga bao safi na kama kawaida akaenda kulishangilia kwa kuserereka! Kwanini mashabiki wa Tottenham wasiingiwe na kiwewe? Walistahili, alikidhi haja ya mioyo yao. Na kama haitoshi, Klinsmann akawafungia mabao 20 katika mechi 41 alizocheza kwa mwaka mmoja.
Haikuwa ajabu kwa Bayern Munich kumnunua mtoto wa nyumbani, licha ya kwamba na umri ulikuwa unasogea. Huko alifunga mabao 31 kabla ya kwenda Sampdoria Italia na baadaye kurudi Tottenham kwa mkopo. Kote alikokwenda kulikuwa na majibu mazuri.

Lakini hali haikuwa hivyo kwa Andriy Shevchenko ambahye alitikisa soka la Italia akifunga mabao 24 kila msimu mara tatu, kutikisa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa mabao yake na hadi kuchaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia au kushinda tuzo ya Ballon d’Or.

Alitakiwa na tajiri wa Chelsea, Roman Abromovic kwa bei yoyote huku AC Milan wakisainisha mkataba mpya ili kukatisha tama klabu zilizokuwa zikimtaka. Hatimaye, Chelsea ikamnasa kwa bei ambayo ilikuwa rekodi kwa mchezaji aliye Uingereza, yaaniPauni milioni 30.8 za Uingereza, lakini mambo hayakuwa kama alivyotarajia.

Licha ya kuanza maisha mapya kwa kutikisa nyavu, majeraha yalimuandama na hakuwa akipata nafasi mara kwa mara katika kikosi cha Jose Mourinho na baadaye Avram Grant. Katika kipindi chote alichocheza Chelsea, hakuwahi kufikisha mabao 20, ambayo yalikuwa kawaida kwake nchini Italia.

Aliondoka Chelsea akiwa mchezaji wa kawaida tofauti na matarajio ya wengi kwa nyota huyo aliyeweka rekodi ya mabao kwa nchi yake ya Ukraine.

Kwa hiyo, soka ni mchezo unaochezwa na binadamu ambaye kubadlikabadilika kwake ni kitu cha kawaida. Majeraha, bahati, staili ya uchezaji ya kocha, nafasi anayopangwa, ushindani wa nafasi kikosini, uhusiano na wenzake na mambo mengine mengi huweza kusababisha akashindwa kuendeleza ubora aliouonyesha huko anakotoka au kipicha cha nyuma kabla ya kusaini mkataba mpya mnono zaidi.
Mambo hayo yopte hutegemeana na pale yanapokwenda vizuri, basi ustaa wa mchezaji huendelea na thamani yake kukua. Lakini ni vigumu kuwa na uhakika kwamba mchezaji fulani atafanya makubwa kwa kuwa huko alikotoka alifanya mengi.

Ukifuatilia mijadala kuhusu wachezaji wapya wanaosajiliwa na klabu za hapa nchini, unaweza kudhani hao wanaokuja walikuwa wakicheza peponi na wanakuja kuleta soka ambalo halijawahi kuonekana duniani.
Wako waandishi au wachambuzi ambao wameshaanza kutabiri timu bingwa msimu ujao hata kabla ya hao wachezaji wapya hawajaonhyesha makali hyao uwanjani.
Baadhi wanaripoti takwimu za wachezaji huko walikotoka bila ya kuangalia mazingira yaliyowafanhya wawe na takwimu nzuri na kama mazingira hayo yapo klwenye klabu mpya kumuwezesha kung’aa zaidi.

Tulisikia ya ‘wadaka mishale’ sasa tunasikia ya wazuia nzi. Tunasikia mengi ambayo yanasababisha tujiulize hivi hao wanaozungumzia sifa za hao wachezaji wapya, walishafanya utafiti wa kutosha kuhusu takwimu zao za wanakotoka? Au ndio wale tuliowaona katika mechi moja au mbili dhidi ya timu za

Tanzania, tukafanya majumuisho kuwa hawa ni wazuri.
Wenzetu wanapoandika habari za usajili, huangalia zaidi lengo la kumsajili mchezaji fulani. Mfano, kuna udhaifu katika nafasi anayocheza? Au anasajiliwa kuongeza ukubwa wa kikosi kutokana na uwingi wa mashindano ambayo timu yake mpya itacheza?

Kama ni mshambuliaji, kuna tatizo lolote la ufungaji kwenye timu inayomtaka? Kwa ujumla, washambuliaji wa timu hiyo walifunga mabao mangapi msimu ulioisha kiasi kwamba kuonekane kuna haja ya kuimarisha sehemu hiyo?
Pia suala la umri huangaliwa sana. Mfano una mshambuliaji mzuri sana ambaye bado ana mkataba na klabu lakini umri wake unaelekea ukingoni hivyo kunahitajika mshambuliaji kijana ambaye atakuwa klabuni hapo kwa muda mrefu zaidi.

Suala jingine ni maombi kutoka klabu mbalimbali ya kumtaka mchezaji msimu mmoja kabla ya mkataba wake kuisha. Hii maana yake ni kwamba klabu haikuwa tayari kumuachia aondoke bure baada ya kumaliza mkataba na hivyo inalazimika kuachana naye kwa faida. Hali ndivyo inavyoelekea kwa Lylian Mbappe pale PSG.

Masuala hayo hufanya mwandishi aonekane anaripoti kwa uangalifu badala ya kuweka madudu ya kushangilia kana kwamba timu inasajili malaika.
Sifa zisizostahili husababisha mashabiki kuzipachika majina timu zilizosifiwa sana wakati wa usajili kuwa ni “timu za magazetini” au “mchezaji wa magazetini” kwa kuwa hakidhi zile sifa alizopewa wakati akisajiliwa.

Na hii ni fedheha kwa waandishi na vyombo vya habari kwa kuwa mashabiki hufikia kutamka maneno hayo baada ya kulinganishwa kile kilichoripotiwa na wanachokiona kiuhalisia.
Wapo pia wanaoungana na vijembne vya klabu pinzani kwamba mchezaji anayesajiliwa baada ya mkataba kuisha ni Yule ambaye uwezo umepungua au klabu haina fedha za kushindana. Si kweli!
Bayern Munich ni moja ya klabu kubwa duniani, lakini ni nadra sana kuikuta imesajili mchezaji kwa dau kubwa kushindana na klabu kama Real Madrid, Chelsea au hata klabu zote mbili za jijini Manchester. Ni kwa sababu ya sera yao ya usajili.

Huangalia zaidi sehemu ambako mchezaji mzuri na anayeinukia anakaribia kumaliza mkataba na kuanza mipango ya kumnasa. Hata Sadio Mane hawakumsajili kwa bei mbaya. Bayern husubiri mchezaji awe amebakiza muda mfupi na hivyo kumnunua kwa bei ndogo, au awe amemaliza mkataba na hivyo kumchukua bure.

Na hii huwawezesha kumuwekea mchezaji maslahi manono kwa kuwa hawapotezi fedha nyingi katika kununua. Nilidhani viongozi waliofikia viwango hivi wanatakiwa kupongezwa kwamba wanajua kubana fedha ili waweze kukidhi mahitaji binafsi ya wachezaji badala ya kuwanunua kwa bei mbaya nab ado kukumbana na kazi nyingine kubwa ya kulipa ada ya kusajili (sign-on fee), mishahara na posho nyingine.

Waandishi walitakiwa washike usukani katika mambo hayo muhimu ili kuelekeza mijadala ya usajili katika njia sahihi badala ya hizi za sasa za kusifu wachezaji na viongozi kuwa wana fedha au wametumia umafia.
Haya hayawezi kutufikisha popote zaidi ya kudhalilisha waandishi na kulisha takataka mashabiki wetu.