Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Aziz Ki anavyoudhi, kufurahisha mashabiki

Muktasari:

  • Kocha huyo raia wa Italia alisema ni kosa kubwa kusimama na kumuhimiza mchezaji mwenye mpira afanye kile ambacho kocha aliye nje anadhani kuwa ndio sahihi, na badala yake akasema ni muhimu sana kumuacha mchezaji atumie akili yake na kama hatafanya sahihi, basi maelekezo yaje baadaye.

KUNA wakati kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alieleza kuwa matatizo makubwa ya makocha vijana ni pamoja na kujaribu kutoa maelekezo kwa mchezaji wakati akiwa na mpira.

Kocha huyo raia wa Italia alisema ni kosa kubwa kusimama na kumuhimiza mchezaji mwenye mpira afanye kile ambacho kocha aliye nje anadhani kuwa ndio sahihi, na badala yake akasema ni muhimu sana kumuacha mchezaji atumie akili yake na kama hatafanya sahihi, basi maelekezo yaje baadaye.

Ndivyo walivyo mashabiki wengi wa soka Tanzania, ambao kwanza hupiga kelele sana kumhimiza mchezaji afanye kile wanachodhani ni sahihi na asipofanya hivyo na ikatokea mpira ukatoka, humuona kama ndiye ambaye hafai kuliko wote.

Kitu cha pili ni matarajio yao kwa mwalimu katika kufanya mabadiliko ya wachezaji. Utasikia, saa hizi amtoe fulani, aingie fulani kazi itakuwa imeisha.

Sikiliza sasa kocha asipofanya mabadiliko wanayotarajia. Utasikia “tatizo la kocha ni sub zake” na wimbo huo utaimbwa hadi na wachambuzi, bila ya kujua kocha alifundisha nini na wachezaji gani walimuelewa zaidi na hao walioanzia benchi, ni kina nani ambao wanafaa kumalizia mchezo.

Bahati mbaya sana, mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki ndiye anayekumbwa na maneno hayo ya mashabiki, hasa wale wanaoangalia mechi kwenye runinga.

Wengi huingia kichwani mwa kiungo huyo mshambuliaji na kutaka afanye uamuzi kama akili zao zinavyoona. Kila akamatapo mpira, kelele huanza “achia, achia”, lakini kitu kizuri ni kwamba hazisikii kauli zao kwa kuwa nyingi hutokea zaidi ya kilomita 30 kutoka uwanjani, yaani hutokea kwa watu wanaoangalia runinga.

Na kibaya zaidi, mara kadhaa mchezaji huyo hupoteza mpira kutokana na mikakati ya timu pinzani kumdhibiti kwa kuwa ukimuachia huru kufikiria, huweza kutoa pasi za mauaji na kuipa timu yake mabao.

Anaponyang’anywa mpira ndio maneno huongezeka na mashabiki kuanza yale mabadiliko yao ya kufikirika. Kwamba “hapa toa Ki, ingiza Cloutus Chama, biashara imeisha”.

Kitu kizuri kwa mchezaji huyo ni ule uwezo wake wa kubadili fikra za mashabiki katika kipindi ambacho hawatarajii. Mechi ya Jumamosi ni moja ya mifano ambayo Aziz Ki aliudhi na kufurahisha mashabiki katika wakati ambao hakutarajiwa, kiasi kwamba hata alipotoka hakuna aliyejua kirahisi wala aliyefurahia kubadilishwa kwake kwa kuwa alishafanya yake zamani.

Baada ya kukosa bao, na pasi zake kadhaa kutobadilishwa kuwa mabao, Aziz Ki aliingia kipindi cha pili kwa nguvu zaidi na dakika chache baadaye akafunga bao lililofufua matumaini ya Yanga.

Baada ya Khalid Aucho kusogea mbele akipita upande wa kulia, Azi Ki ndiye aliyefungua mbele yake kuomba pasi akielekeza kwa kidole pale anapotaka apelekewe mpira huo, na Mganda huyo hakufanya ajizi bali kuondoa lawama miguuni mwake na kuzihamishia kwa Ki, ambaye kwa utulivu aliukwamisha mpira wavuni akiupitisha katikati ya miguu ya kipa wa TP Mazembe, Badara Fatty.

Na kama haitoshi, akahusika katika bao la tatu lililowasaulisha kabisa mashabiki kuwa Aziz Ki ndiye aliyekuwa akichelewa na mpira na wakati mwingine akiupoteza.

Mchezaji ambaye anacheza nyuma ya mshambuliaji ndiye ambaye anatakiwa atumie akili nyingi kumsaidia mwenzake. Na akili nyingi huhitaji pia muda na nafasi kabla ya kuamua kufanya kitu sahihi.

Lakini mshambuliaji wa kati hatakiwi kutumia muda mwingi kufikiria cha kufanya, bali akili ya haraka kwa kuwa mabeki hawawezi kumruhusu apate muda wa kufikiria vizuri kuwaua.

Na timu pinzani inapojua mtengenezaji nafasi ni mshambuliaji wa pili, mara nyingi huingia na mkakati wa kumdhibiti, hasa kumgongagonga, kumsukuma au kumwendea kwa wingi na hivyo huwa rahisi kwake kupoteza mipira. Afadhali yake huwa ni kurudisha mipira sehemu salama, yaani kupiga pasi za nyuma, kitu ambacho Aziz Ki hukifanya pale anapokuwa mbali na lango.

Usipomuangalia kwa jicho na fikra hizo, ni lazima utatumia muda mwingi kumlaumu na kutarajia kosa kila anapopata mpira mchezaji wa aina ya Aziz Ki. Matokeo yake burudani inageuka kuwa kero na furaha ya bao inapokuja, unajikuta ukifurahia kwa shingo upande.