Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya Gravesen ‘Mad Dog’ alivyopiga, kutembeza ubabe!

Muktasari:

  • Soka kweli ni ulimwengu wa ‘mbwa kula mbwa’. Muulize tu Mdenmark huyo mwenye roho ya kutisha na moyo wa ajabu anayejulikana kwa upendo kwa baadhi ya mashabiki wake.

LONDON, ENGLAND; UNAMKUMBUKA Thomas Gravesen? Mchezaji wa soka aliyefahamika pia kama ‘Mad Dog’? Kiungo huyo wa zamani wa Everton Mdenmark  alipata jina la utani la Mad Dog akiwa Everton na haikuwa kwa bahati mbaya, kwani historia ya maisha yake ndani na nje ya uwanja inaonyesha hivyo.

Soka kweli ni ulimwengu wa ‘mbwa kula mbwa’. Muulize tu Mdenmark huyo mwenye roho ya kutisha na moyo wa ajabu anayejulikana kwa upendo kwa baadhi ya mashabiki wake.

Ni simulizi ya kiungo aliyewatisha wapinzani wake uwanjani, aliyefyatua fataki katika viwanja vya mazoezi, aliyening’iniza sehemu zake za siri juu ya mwenzake, aliyefanya mapenzi na mwanamitindo mtu mzima na ambaye inadaiwa alimng’oa jino mmoja wa magwiji wa mchezo huu.

Hizo zilikuwa tabia za Gravesen, nyota wa zamani wa Denmark ambaye sasa anafurahia maisha ya uzeeni akiwa na mkewe mwanamitindo nchini kwao baada ya miaka mingi huko Las Vegas, Hamburg, Everton, Celtic na kwa kushangaza Real Madrid akiwa pamoja na Galacticos kama Ronaldo de Lima, Zinedine Zidane na David Beckham.

MTU WA MIKASA

Akiwa amezaliwa 1976, alianza soka katika klabu ya nyumbani kwao ya Vejle Boldklub katikati ya miaka ya 1990. Kufikia alipojiunga na Everton mwaka 2000, hereni na mtindo wake wa nywele vilikuwa vimeondoka, lakini uvumi kuhusu tabia yake “isiyo ya kawaida” ulikuwa unaongezeka.

Kocha wa zamani wa Denmark, Bo Johansson, alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuzungumzia “wazimu” huo. Akiwa Vejle, Gravesen alijitokeza dhidi ya wapinzani wa Superliga na kupata uhamisho kwenda Hamburg 1997. Burudani yake uwanjani huko Bundesliga ilikuwa ya kuvutia.

Hata hivyo, Johansson alikuwa na shaka, akihoji kama Gravesen alikuwa “vyema kiakili” vya kutosha kuichezea timu ya taifa. Hofu yake haikuwa na msingi kwani kati ya 1998 na 2006, Gravesen aliichezea Denmark mara 66 na kufunga mabao matano.

Lakini, kulikuwa na misukosuko kadhaa njiani. Mwaka 2002, Gravesen alijikuta matatani baada ya mzaha mazoezini kugeuka ugomvi. Yeye na mwanasoka mwenzake mwenye mkorofi Stig Tofting walimvamia Jesper Gronkjaer wakati wa maandalizi kabla ya Kombe la Dunia, wakammwagia maji na kumsukumia vipande vya barafu ndani ya kaptura yake.

Winga huyo wa Chelsea hakuliona jambo hilo kuwa la kuchekesha. Baada ya kuonana na daktari wa timu kwa sababu ya jicho lililoumia, alibadilishana maneno makali na Tofting, jambo lililosababisha ugomvi, kulingana na ripoti za BBC.

Kwa bahati mbaya kwa wote waliohusika, vyombo vya habari vilinasa tukio la awali. Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka la Denmark alisema: “Wachezaji hawa wanahitaji mwalimu wa chekechea ili kuwanyosha.”

Mwaka uliofuata, staa wa Denmark alikuwa amerudi tena, ambapo Gravesen alinaswa na kamera akiwa ameinua kaptura yake juu akijianika sentimita chache juu ya kichwa cha nyota mwenzake Claus Jensen. Tukio hilo la kushangaza lilipigwa picha na kuwa habari kubwa.

Baadaye Gravesen alijutia tukio hilo katika mkutano na waandishi wa habari, kama ilivyoripotiwa na gazeti la Denmark la Berlingske akikiri: “Ilikuwa iwe mzaha, lakini ikaishia kuwa ujinga. Pia sikujua kwamba kulikuwa na mtu aliyepiga picha.”

Kufikia wakati huo, alikuwa amejiimarisha Everton na mashabiki walimpa jina la Mad Dog kutokana na mtindo wake wa kucheza na namna yake ya kushangilia. Alipendwa, lakini pia alihofiwa na wachezaji wenzake na wafanyakazi wa klabu, ikidaiwa kelele zake zilikuwa kubwa mno kambini.

Mick Rathbone, aliyekuwa mtaalamu wa tiba ya viungo Everton alimtaja Gravesen kuwa mchezaji “mwendawazimu zaidi” aliyewahi kukutana naye. Katika kitabu chake The Smell of Football, anasimulia visa kadhaa ikiwemo aliposimamisha gari ili kujaza mafuta alipokuwa amemchukua Gravesen kwenda kula mahali fulani.

“Alinifuata dukani na kusimama pembeni yangu nilipokuwa nalipa,” anakumbuka Rathbone.

“Kisha alinifuata tena hadi garini na kukaa kwenye siti ya abiria bila kusema neno lolote.”

SIKIA HII

Hata hivyo, katika kitabu hicho anamwelezea Gravesen kama mtu aliyegeuka “kichaa” mara tu alipovuka mstari mweupe wa uwanja.

Baada ya kuumia katika mechi mojawapo, Rathbone anakumbuka: “Katika tukio hilo nilimkimbilia na kumuuliza tatizo ni nini. ‘Tatizo ni nini? Tatizo ni nini? Wewe niambie, mjinga mkubwa! Wewe ndiye mtaalamu wa tiba!’ alipiga kelele kwa Kiingereza chake kizuri, lakini akiwa na lafudhi ya Kidenmark iliyomfanya aonekane kichaa zaidi.

‘Hakuna kitu, hakuna kiwango cha mafunzo kinachoweza kumwandaa mtu kwa aina hiyo ya mwitikio, na sikujua nifanye nini, hivyo nikamuuliza Tommy kama anataka kinywaji. Hilo lilimkasirisha zaidi. ‘Kinywaji? Kinywaji gani? Mchezo umeanza dakika tano tu zilizopita, mpumbavu wewe!”

Mtaalamu huyo wa tiba ya viungo alijaribu kutuliza hali hiyo: “Kwa bahati nzuri, alikuwa anaanza kupoa kutokana na pigo lile na akasimama. Nilimshika mkono ili nimpeleke pembeni ya uwanja, na akawa kama amechanganyikiwa kabisa. ‘Ondoa mkono wako kwangu! Ondoa mkono wako kwangu au nitakupiga!’ Akanisukuma mbali.”

Walipofika pembeni ya uwanja, Gravesen alionekana kutulia. Rathbone anaandika: “Hatimaye tulifika pembeni ya uwanja ambapo alinipongeza kwa msaada wangu na akarudi uwanjani kwa utulivu. Tukio hilo halikuwahi kutajwa tena, lakini lilinitisha kiasi kwamba nilikuwa nikikaa benchi nikisali Tommy asiumie tena.”

Staa wa zamani wa everton na Manchester United, Wayne Rooney, ambaye alikuwa mdogo alipocheza na Gravesen Everton, anasimulia wakati waliposababisha vurugu kwa kutumia fataki katika uwanja wa mazoezi wa Bellefield. “Mimi na Thomas Gravesen tulikuwa tunarusha roketi kubwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine, tukilengana, halafu (kocha David) Moyes akaingia!” anakumbuka Rooney.

“Ndiyo. Moyes aliingia na unaweza kuona uso wake ulivyokuwa ukisema, ‘nini kinaendelea hapa?’ Nilikuwa na miaka 16! Tulikuwa tunaziwasha na kuzishika huku tukizimbiza kila upande!”

ALIVYOTUA MADRID

Mwaka 2005 alitua Santiago Bernabeu kwa Pauni 2.6 milioni uhamisho uliomshangaza hata yeye: “Wakala wangu alinipigia simu akasema; ‘Madrid wanapiga simu’. Nilidhani Everton au Atletico Madrid… nilikuwa napendelea Everton. Kisha akasema ni Real Madrid! Nilishangaa kama kila mtu mwingine.”

Kama msemo unavyosema, huwezi kumfundisha mbwa mzee mbinu mpya. Na Mad Dog aliendelea na vituko vyake akiwa La Liga, jambo lililomkera kocha Fabio Capello ambaye aliwahi kusema: “Tabia yake? Siipendi. Anataka kila mtu afanye anachotaka yeye, na nimemwambia hivyo.”

Mfano ni ugomvi unaodaiwa kutokea kati ya Gravesen na Robinho kama anavyokumbuka Julio Baptista aliyeiambia redio ya Cadena SER: “Ulikuwa wa kuchekesha. Fikiria Gravesen ambaye alikuwa kichaa kidogo akikimbia kwa kasi kumfuata Robinho huku akilalamika kwa hasira.

Alimpiga teke, kisha lingine. Robinho akasimama, akamtazama na kumsukuma kifuani ndipo mambo yakaharibika. Gravesen alitaka kumuua. Walitenganishwa lakini Robinho akarudi vyumbani na Gravesen akaniangalia na kusema, ‘nitamuua.”

Vilevile kulikuwa na tukio ambalo Ronaldo wa Brazil alikutana na Gravesen, ambapo inadaiwa kwamba Mdenmark huyo alimwangusha chini kwa nguvu kiasi kwamba jino lake liling’oka.

Ronaldo anakumbuka ukorofi wa Gravesen katika mazungumzo na gwiji mwenzake wa Brazil, Romario, ambapo anasema: “Gravesen alikuwa mtu mzuri sana. Lakini katika soka alikuwa mkali mno. Alifunga mabao, lakini alipiga watu sana.”

Muda mfupi baadaye, Real Madrid ilimchosha na kumuuza Celtic mwezi Agosti 2006, ambako Aiden McGeady, mchezaji mwenzake wa zamani Celtic alikuwa na kumbukumbu nzuri kuhusu Gravesen akisema: “Alikuwa anaweza kusimamisha mazoezi kabisa. Nakumbuka siku moja alikuwa karibu kupiga shuti, nami nikawa napaza sauti ‘Tommy! Tommy! Tommy!’ Kisha akiwa tayari kupiga, akaacha. Akasema, “usipige kelele napokaribia kupiga shuti. Nachukia hilo. Ndilo jambo baya zaidi katika soka.” Nami nikasema, “Tommy, nilikuwa naomba mpira tu.” Akasema, “Hapana! Usimwite mpigaji shuti kamwe!”

Nyota huyo wa zamani anaongeza: “Nilikuwa karibu naye. Alikuwa anakuja kukaa nami mara nyingi, lakini nakumbuka wakati mwingine tukiwa chumbani, Strachan (kocha wao) anatoa maelekezo ya timu. Alipomaliza, nikamtazama Tommy alikuwa amekaa kona akiwa na gazeti lililokatwa sehemu ya macho na akiangalia kupitia humo.”

Nyota mwingine wa zamani, Paul Caddis, pia ana kumbukumbu ya ajabu kuhusu Gravesen ikimhusisha mpenzi wake wa wakati huo, nyota wa filamu za watu wazima Kira Eggers. “Mpenzi wake alikuwa nyota wa filamu. Tulikuwa tunamwambia, ‘Tommy una picha za mpenzi wako?’ Yeye anasema ‘tafuteni mtandaoni tu, kuna nyingi huko.”

Caddis pia alifichua jinsi Gravesen alivyotumia muda wake wa mapumziko kati ya mwisho wa msimu na maandalizi ya msimu mpya.

“Alikuwa anarudi nyumbani wakati wa maandalizi ya msimu na kukaa kwa mama au baba yake kwenye chumba kidogo sana kwa wiki sita. Humo alikuwa anakaa akicheza PlayStation tu. Kwa kweli alikuwa kichaa, lakini mtu wa ajabu na mzuri.”

Maisha yake Celtic hayakuwa ya mafanikio makubwa, kwani alikaa mwaka mmoja kabla ya kurejea Everton kwa mkopo, lakini kipindi chake cha pili hakikufikia kiwango cha kwanza, na kwa bahati mbaya alistaafu 2009 akiwa na umri wa miaka 32.

Lakini, hilo halikumkera kwa sababu alifurahia maisha baada ya soka na inasemekana alifanya uwekezaji mzuri wa kifedha wakati wa uchezaji wake. James McFadden, mchezaji wa zamani Everton, aliwahi kusema: “Hakuwa na matumizi makubwa wala bili. Alikuwa akiishi katika nyumba ndogo. Hakupenda bili. Alikuwa na gari zuri, lakini wakati wa baridi alikuwa analiuza na kununua lisilo na gharama.”

Baada ya kuhifadhi sehemu kubwa ya mshahara wake wa Pauni 85,000 kwa wiki na kuwekeza kwa busara, alihamia Las Vegas, Marekani akiwa na mwanamitindo wa Czech, Kamila Persse. Hata hivyo, maisha yao ya kifahari hayakudumu kwani 2018 walifunga virago na kurejea Denmark.

Sasa Gravesen anaishi katika nyumba ya kifahari ya ghorofa yenye thamani ya Pauni 1.6 milioni aliyoinunua 2010 katika mji wa Vejle. Pia ameanza kufanya kazi kama mchambuzi wa soka.

Sababu yake kubwa ya kurudi? “Nimeikosa soka na kila kitu kinacholizunguka, hivyo ilikuwa nafasi ya kuwa sehemu yake tena.”

Kila Mad Dog huwa na siku zake. Na sasa akiwa na miaka 50, Gravesen huenda hagombani tena au kusababisha vurugu uwanjani, lakini shauku yake ya maisha na mapenzi yake katika mchezo huo vinaonyesha bado ana nguvu nyingi. Yeye ni zaidi ya rafiki bora wa mwanadamu. Ni mmoja wa wachezaji wa kipekee na wa kusisimua zaidi katika historia ya soka.