Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simbu aandika historia Tokyo, atwaa dhahabu ya Mbio za Dunia

SIMBU Pict

Muktasari:

  • Simbu alimaliza mbio ndefu za marathoni za kilomita 42.195 katika joto na unyevunyevu mkali, na kutwaa ubingwa huo kwa wanaume ambapo iliamuliwa kwa tofauti ndogo zaidi katika historia ya mchezo huo dhidi ya aliyeshika nafasi ya pili.

MWANARIADHA nyota wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu ameweka rekodi na historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha 2025 yaliyofanyika asubuhi ya leo jijini Tokyo, Japan.

Simbu alimaliza mbio ndefu za marathoni za kilomita 42.195 katika joto na unyevunyevu mkali, na kutwaa ubingwa huo kwa wanaume ambapo iliamuliwa kwa tofauti ndogo zaidi katika historia ya mchezo huo dhidi ya aliyeshika nafasi ya pili.

Katika kumalizia kwa kishindo ndani ya Uwanja wa Taifa wa Japan, Simbu alivuka mstari wa mwisho mbele ya Mjerumani Amanal Petros akishinda dhahabu ya dunia kwa muda wa saa 2:09:48.

Ushindi huo wa kishindo umemfanya Simbu aingie katika vitabu vya kumbukumbu kama mwanariadha wa kwanza wa Tanzania kushinda dhahabu katika riadha za dunia.

SIMB 01

Pia ushindi huo uliamuliwa kwa pengo dogo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya marathoni za mashindano ya dunia, kwani alitenganishwa kwa sekunde 0.03 pekee.

“Leo nimeandika historia nikiwa Mtanzania wa kwanza kushinda dhahabu ya dunia,” amesema Simbu akiwa amebebwa juu kwa shangwe na kuongeza:

“Nakumbuka mwaka 2017 nilishinda shaba huko London (Uingereza). Baada ya hapo nilikimbia mara nyingi bila kupata medali yoyote, lakini hatimaye ndoto yangu imetimia. Nilipoingia hapa, niliiambia nafsi yangu sitakata tamaa. Nilikaa kwenye kundi na mwishowe mambo yakaenda vyema. Angalia tu mbio za mwisho na ule mwendo wa kasi!”

Petros, ambaye pia alimaliza kwa muda sawa na Simbu alilazimika kujifariji na medali ya fedha licha ya kulala chini akijifunga utepe wa ushindi.

SIMB 02

“Ilikuwa kama mbio za mita 100,” alisema akiwa amehuzunika kidogo.

"Nilipokaribia kumaliza nilihisi ninaweza kushinda. Ni kweli nimevunjika moyo, lakini kama mwanariadha unatakiwa kujifunza, kuendelea kujituma na kushukuru kwa medali ya fedha,” ameongeza Petros aliyemtangulia Muitaliano Iliass Aouani aliyemaliza wa tatu na kuondoka na shaba kwa muda wa 2:09:53.

Katika mbio hizo zilianza kwa kasi ya makundi na hadi kufikia kilomita ya 30, kundi kubwa la wakimbiaji akiwemo Abel Chelangat wa Uganda, Clayton Young wa Marekani na Emile Cairess wa Uingereza lilikuwa bado liko pamoja huku tofauti ya sekunde moja pekee ikiwatenganisha wakimbiaji 12 wa mbele.

SIMB 03

Kadri jua lilivyozidi kupanda, joto la nyuzi 27 likaanza kuwaathiri washiriki. Washindani dhaifu wakaanza kupungua, huku wakali zaidi wakibaki kuamua hatima ya mbio hizo. Nyumbani kwao, Kondo Ryota wa Japan alijitahidi kubaki kwenye kasi lakini akaishia kushika nafasi ya 11 baada ya kuachwa kwenye kilomita ya 39.

Mashabiki waliokuwa wamefurika walilipuka kwa shangwe pale washindani walipoingia uwanjani kwa hatua ya mwisho. Lakini ni Simbu aliyesimama imara, akichanja mbuga kwa kasi ya ajabu kwenye mita 10 za mwisho na kuandika historia ya pekee.

Kwa ushindi huu, Simbu sasa ana dhahabu ya dunia kuungana na medali ya shaba aliyoshinda London mwaka 2017 na pia huu umekuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwake, baada ya kushika pia nafasi ya pili katika Boston Marathon 2025 zilizofanyika Aprili.

SIMB 04

MTAKA AMPONGEZA

Mara baada ya ushindi huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliyewahi kuwa rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) amempongeza Simbu kupitia akaunti yake ya Instagram.

Mtaka ameandika: "Hongera sana mwanariadha wa Tanzania Alphonce Simbu kwa kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya riadha ya dunia yanayoendelea jijini Tokyo, Japan. Simbu anakuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali hii ya dhahabu kwenye mashindano haya makubwa ya dunia mbio ndefu marathon za Kilomita 42. Ushindi huu ni fahari kwa taifa letu. Ni fahari kwa wanamichezo wote nchini. Ameliheshimisha taifa."

Pongezi zake zimeendelea kusomeka, "ameiheshimisha nchi yetu na hatimaye bendera ya Tanzania imepeperushwa duniani kupitia riadha. Ni uwekezaji wa wastani wa miaka 13, ikiwa ni safari ya milima na mabonde. Nakupongeza wewe binafsi, kocha na wote walioshiriki mafanikio ya safari hii. Nikiwa hai hapa duniani, nimefurahi kuyaona mafanikio haya makubwa ambayo niliyatamani. Kaka na rafiki yetu marehemu Kocha Frances Mungu ampe pumziko la milele mbinguni maana mbegu tuliyoipanda miaka 13 iliyopita leo imekuwa lulu ya taifa letu.

"Ushauri wangu ni uleule wa wakati wote kwako na kwa wanamichezo mafanikio yako yote ya kimichezo yastawishe mafanikio yako kimaisha katika kazi kama ofisa wa jeshi na katika maisha yako binafsi kiuchumi."

Mtaka amemalizia kwa kuandika: "Naamini umefungua mwanga wa uthubutu kwa wanariadha wa Tanzania kwenye kizazi cha sasa na kijacho. Hongera uongozi mpya wa RT na familia nzima ya riadha Tanzania. Mungu akubariki sana, awabariki wanariadha na wanamichezo wote wa taifa letu."