Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Je, akili ya De La Fuente itamzima Messi na Argentina?

PAMBANO Pict

Muktasari:

  • Hispania imefika hatua hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu kwa kuiondoa Ufaransa katika nusu fainali. Kikosi cha kocha Luis de la Fuente kilitawala mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu na kutumia vyema nafasi walizozipata, huku kikifanikiwa kuuzima kabisa ushambuliaji hatari wa Wafaransa.

ATLANTA, MAREKANI: HATIMAYE pazia la Kombe la Dunia 2026 linashushwa kwa pambano la aina yake, ambapo mabingwa wa Ulaya, Hispania, watakutana na mabingwa watetezi wa dunia na Amerika Kusini, Argentina, katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki duniani kote.

Hispania imefika hatua hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu kwa kuiondoa Ufaransa katika nusu fainali. Kikosi cha kocha Luis de la Fuente kilitawala mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu na kutumia vyema nafasi walizozipata, huku kikifanikiwa kuuzima kabisa ushambuliaji hatari wa Wafaransa.

Ushindi huo ulikuwa kilele cha kiwango kizuri cha Hispania katika mashindano haya. Safari yao ilianza kwa kuongoza Kundi H, ingawa mwanzo haukuwa rahisi baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Cape Verde. Baadaye waliinyoosha Saudi Arabia kwa mabao 4-0 kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi kwa ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Uruguay.

PAMBA 01

Katika hatua ya 32 bora waliichapa Austria mabao 3-0, lakini walikumbana na upinzani mkali katika hatua zilizofuata. Kiungo Mikel Merino aliibuka shujaa kwa kufunga mabao ya dakika za mwisho yaliyoivusha Hispania dhidi ya Ureno (1-0) na baadaye Belgium (2-1), mchezo ambao ndio pekee waliyoruhusu bao katika mashindano haya.

Kadri mashindano yalivyoendelea, kiwango cha Hispania kilizidi kupanda na ushindi dhidi ya Ufaransa ulithibitisha kwa nini walitajwa miongoni mwa timu zilizopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa. Fainali ya Julai 19 itakuwa ya kwanza kwa Hispania tangu ilipotwaa taji lake la kwanza mwaka 2010, nchini Afrika Kusini.

PAMBA 02

Messi alivyoibeba Argentina

Kwa upande wa Argentina, safari yao kuelekea fainali imejaa drama na mapambano makubwa. Mabingwa hao watetezi walifungua kampeni kwa ushindi wa mechi zote tatu za makundi wakiongozwa na nahodha wao Lionel Messi, ambaye tayari amefunga mabao manane katika mashindano haya na kufikisha mabao 21 katika historia yake ya Kombe la Dunia.

Argentina iliifunga Algeria mabao 3-0 kupitia 'hat-trick' ya Messi, ikaishinda Austria 2-0 kwa mabao mawili ya nyota huyo, kabla ya kuifunga Jordan 3-1 katika mchezo mwingine ambao Messi pia alifunga.

Hata hivyo, hatua ya mtoano ilikuwa ngumu zaidi. Walihitaji muda wa nyongeza kuiondoa Cape Verde kwa ushindi wa mabao 3-2, kisha wakafanya moja ya marejeo makubwa ya mashindano walipoifunga Misri 3-2 baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 79.

Katika robo fainali waliinyoosha Uswisi kwa mabao 3-1 baada ya muda wa nyongeza, huku Julian Alvarez na Lautaro Martinez wakihakikisha ushindi huo.

Drama iliendelea nusu fainali dhidi ya England. Waingereza walitangulia kufunga kupitia Anthony Gordon, lakini Argentina ilijibu kwa bao la mbali la Enzo Fernandez kabla ya Lautaro Martinez kufunga bao la ushindi kwa kichwa na kuipeleka timu yake katika fainali ya pili mfululizo baada ya kutwaa ubingwa nchini Qatar mwaka 2022.

PAMBA 03

Historia inasemaje?

Hii itakuwa mara ya pili kwa Hispania na Argentina kukutana katika Kombe la Dunia. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1966 mjini Birmingham, ambapo Argentina ilishinda mabao 2-1 kupitia mabao mawili ya Luis Artime.

Tangu wakati huo zimekutana mara 13 katika mechi za kirafiki, huku Hispania ikishinda sita, Argentina tano na mechi mbili kumalizika kwa sare. Mechi yao ya mwisho ilikuwa mwaka 2018 jijini Madrid, ambapo Hispania iliichapa Argentina mabao 6-1.

Pambano hili linatarajiwa kuwa la kusisimua, likizikutanisha timu mbili zenye historia kubwa na wachezaji wenye uwezo wa kubadili matokeo wakati wowote. Je, Hispania itarejesha taji la dunia baada ya miaka 16, au Argentina itafanikiwa kulitetea na kuandika historia mpya? Jibu litapatikana kwenye dimba la fainali.


Vikosi vinavyotarajiwa

Hispania: Simon; Porro, Laporte, Cubarsi, Cucurella; Rodri, Fabian Ruiz; Lamine Yamal, Dani Olmo, Baena; Mikel Oyarzabal.


Argentina: Emiliano Martinez; Nahuel Molina, Cristian Romero, Lisandro Martinez, Tagliafico; Leandro Paredes, Alexis Mac Allister, Enzo Fernandez, Giuliano Simeone; Lionel Messi, Julian Alvarez.