Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichoiangusha Tanzania Prisons

PRISONS Pict

Muktasari:

  • Prisons imeshuka daraja kupitia play off baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Polisi Tanzania, ikiwa ni timu ya tatu ya Ligi Kuu kufungwa na timu ya Championship katika historia ya mechi za mtoano.

LICHA ya kuwa na maumivu ya kushuka daraja, lakini upande mwingine ni msaada kwa Tanzania Prisons kujipanga upya kwa ajili ya kurejea na nguvu mpya Ligi Kuu kufuatia msoto waliokutana nao kwa kipindi kirefu.

Prisons imeshuka daraja kupitia play off baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Polisi Tanzania, ikiwa ni timu ya tatu ya Ligi Kuu kufungwa na timu ya Championship katika historia ya mechi za mtoano.

Timu hiyo ya jijini Mbeya, imeungana na Mbao FC na Mbeya City kutoka Ligi Kuu kushushwa daraja na timu za Championship ambazo ni Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars), Mashujaa na Polisi Tanzania kwa misimu tofauti. Katika msimu wa Ligi Kuu uliomalizika Juni 30, 2026, timu za Mtibwa Sugar na KMC zilishuka moja kwa moja, huku Prisons iliyovuna pointi 32 na Mbeya City pointi 30, zikicheza mtoano ‘Play Off’ na Mbeya City kushinda kwa jumla ya mabao 2-0.

Matokeo hayo yaliifanya Mbeya City kubaki salama Ligi Kuu huku Prisons ikikikutana na Polisi Tanzania ya Championship iliyomaliza nafasi ya tatu kwa pointi 66 na kushinda mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Mbeya Kwanza kwa mabao 7-1.

Ndipo Polisi Tanzania ikakutana na Prisons.

Kushuka kwa timu hiyo pendwa jijini Mbeya, yapo baadhi ya mambo yaliyochochea zaidi anguko lake na sasa huenda ikawa funzo kuanzia utawala hadi mashabiki namna ya kurejea tena.

PRIS 01

MISIMU 15 YA MOTO LIGI KUU

Tangu waliposhuka daraja 2019-2010 na kurejea Ligi Kuu msimu wa 2011-2012, Prisons haikuwahi kushuka tena daraja licha ya msoto mkali iliopitia ikiponea chupuchupu mara kadhaa na kuweka presha kubwa nje na ndani ya uwanja.

Licha ya heshima iliyoweka kwa soka la ushindani ikizipa ugumu timu kongwe za Yanga na Simba, lakini timu hiyo ya Jeshi la Magereza haikuwa na matokeo mazuri haswa ikisubiri matokeo ya mechi za mwisho.

Itakumbukwa kwa misimu takribani sita mfululizo imekuwa ikiponea chupuchupu ikiwamo 2021-2022 ilipoangukia mchujo dhidi ya JKT Tanzania na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1.


PRIS 02

MABADILIKO YA UTAWALA

Prisons haikuwa na uongozi uliotulia kutokana na kuwapo kwa mabadiliko ya mara kwa mara katika eneo la Mtendaji Mkuu ‘CEO’, hali ambayo ilichagiza anguko kwa chama hilo.

Kwa miaka mitano nyuma, timu hiyo imeongozwa na takribani watendaji wane tofauti, ambapo awali alianza Ajabu Kifukwe, kisha Anthony Hau, baadaye John Matei, Geofrey Madegwa na kurejeshwa Kifukwe aliyepo kwa sasa.

Pamoja na kwamba dhamira ya viongozi wa juu kuwa ni kuiimarisha timu hiyo na kupata mafanikio, lakini hali hiyo haikuweka utulivu kikosini na pengine kuwaharibu kisaikolojia wachezaji.

Mabadiliko ya mara kwa mara kwa uongozi wa timu hiyo baadhi yao hawakumaliza msimu badala yake wengi wao waliishia nusu msimu na kudhohofisha utendaji wa moja kwa moja haswa ndani ya uwanja.


PRIS 03

MAKOCHA WAPISHANA

Ukiachana na msimu uliopita kuwatumia makocha wawili, kwa takribani misimu minne, Tanzania Prisons imekuwa ikibadilisha makocha ambapo kwa rekodi hakuna aliyemaliza msimu mzima.

Msimu wa 2022-2023, timu hiyo ilianza na Patrick Odhiambo ambaye hakumaliza msimu, nafasi yake ikachukuliwa na Ahmad Ally, kisha Mbwana Makata akampisha Amani Josiah na msimu wa 2025-2026, Zedekiah Otineo kupishana na Shadrack Nsajigwa.

Mabadliko hayo kwenye benchi la ufundi licha ya kuwaacha salama kwa kipindi kirefu, lakini hayakuwa na ufanisi kutokana na presha za mara kwa mara na kuponea chupuchupu kila msimu kunusurika kushuka daraja.


PRIS 04

USAJILI

Katika jambo wanalopaswa kulifanyia kazi zaidi ni sehemu ya usajili kuhakikisha wanarejesha heshima na hadhi ya timu hiyo kwani awali Prisons ilisifika kwa soka la ushindani ‘pira gwaride’.

Wachezaji wengi pia kikosini ni kama wamechoka kutokana na kucheza kwa muda mrefu, hali ambayo inaondoa ushindani kwa timu pinzani hivyo eneo hilo lazima liangaliwe kwa jicho la pekee.

Pamoja na kwamba timu hiyo inajivunia askari wake wenye uwezo na vipaji, lakini inahitaji kufanya uamuzi kwa kuingiza nyota wapya wanaojitafuta wakipewa sapoti na baadhi ya wakongwe wachache.

Wakati ikijiandaa na Championship msimu ujao, Prisons itapaswa kuwashikilia baadhi ya nyota walioonesha uwezo wao kuipambania timu na kusaka mastaa wapya wenye kiu ya mafanikio kupitia soka.


PRIS 05

BAJETI

Kwa sasa mpira wa Tanzania umekua. Hili halina ubishi na Prisons wanapaswa kubadilika na kuamua kutenga bajeti ya kueleweka kushawishi kufanya usajili wa wachezaji wenye ushindani.

Lazima timu hiyo ijifunze kitu kwa timu nyingine Ligi Kuu kwa kile zinachokifanya kwa kusajili nyota wenye uwezo na ushindani ili kuweza kuiweka kwenye hadhi ya timu za ushindani.

Badala ya viongozi wa timu kusubiri bajeti kutoka makao makuu, ingeweza kutengenezwa akaunti maalumu ya timu ili kurahisisha shughuli za uendeshaji kwakuwa Prisons makao makuu yake ni Mbeya.

Pia kuwepo na kamati ya mashindano na usajili ambayo itaundwa kwa kuzingatia uzoefu na uwezo wa viongozi kwenye soka ambao watahusika kutengeneza timu mpya na inaweza kuwajibishwa pale wanapokwama.


PRIS 06

WADAU, MASHABIKI WALIA

Tedius Peter anasema ni kilio kuipoteza timu hiyo ligi kuu kutokana na ushindani iliyokuwa ikionesha kwa Yanga na Simba akieleza kuwa matokeo hayo ni fundisho kwa uongozi na mamlaka za soka mkoani Mbeya.

Anasema licha ya Prisons kusuasua kwa muda mrefu, lakini haikuonekana nguvu ya wadau na chama cha soka mkoani humo (MREFA) katika kupanga na kuweka mikakati ya pamoja kuinusuru.

“Tunaoumia ni sisi mashabiki lakini ndani kuna cha kujifunza kuanzia viongozi wa timu, wadau, mashabiki na chama cha soka mkoa, hatujaonesha sapoti yoyote hadi kushuka daraja.

“Kwa namna tulivyopona kushuka moja kwa moja hadi kuangukia play off, ilikuwa nafasi nzuri kwetu kuungana kwa pamoja tukashinda mechi dhidi ya Polisi Tazania, sasa tukajitathimini,”  anasema Peter.

Naye Jackson Dickson amesema kwa muda mrefu Prisons imepitia magumu na kwamba kilichotokea kilitarajiwa na kwamba itakuwa funzo kwa sasa wanapoanza safari mpya akishauri maandalizi bora.

“Kila msimu timu za Mbeya haswa Prisons wamekuwa wakinusurika dakika za mwisho, sasa hiki ndicho wamevuna, wajipange vizuri kuanzia uongozi, usajili na maslahi kwa wachezaji,” amesema Dickson.