Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba wa Teranga mguu sawa marekani

SENAGAL Pict

Muktasari:

  • Kwa zaidi ya miaka 20 Senegal wameendelea kuwa moja ya mataifa yenye nguvu kisoka Afrika. Kutoka kizazi cha El Hadji Diouf mpaka  Sadio Mane, taifa hilo limezalisha vipaji vinavyotikisa duniani huku likionyesha ushindani mkubwa katika mashindano ya kimataifa.

DAKAR, SENEGAL: BAADA ya Morocco kuweka historia ya kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, taifa jingine ambalo linaendelea kubeba matumaini Afrika kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Amerika Kaskazini ni Senegal.

Kwa zaidi ya miaka 20 Senegal wameendelea kuwa moja ya mataifa yenye nguvu kisoka Afrika. Kutoka kizazi cha El Hadji Diouf mpaka  Sadio Mane, taifa hilo limezalisha vipaji vinavyotikisa duniani huku likionyesha ushindani mkubwa katika mashindano ya kimataifa.

Wakiwa na kizazi kipya cha mastaa wenye uzoefu Ulaya, Simba wa Teranga wanakwenda Kombe la Dunia 2026 wakiwa na ndoto ya kufika mbali zaidi kuliko awali.

SENE 01

WALIVYOANZA SAFARI

Senegal ilipata uhuru kutoka Ufaransa, Aprili 4, 1960 na mwaka huohuo ndipo Shirikisho la Soka la Senegal (FSF), lilianzishwa. Kuanzia ilianza kujenga mfumo wa maendeleo ya soka huku ikishiriki mashindano ya Afrika Magharibi.

Mechi ya kwanza baada ya uhuru ilichezwa Desemba 31, 1961 dhidi ya Dahomey ambayo sasa inajulikana kama Benin ambapo Senegal ilipoteza kwa mabao 3-2. Hata hivyo, pamoja na mwanzo mgumu, taifa hilo lilionyesha dalili za kuwa moja ya nchi zenye uwezo mkubwa kisoka Afrika Magharibi.

Katika miaka ya 1960 Senegal ilianza kushiriki Afcon na 1965 ilifuzu kwa mara ya kwanza. Ilimaliza  nafasi ya nne baada ya kupoteza dhidi ya Ivory Coast kusaka mshindi wa tatu. Kwa muda mrefu Senegal iliendelea kuwa taifa lenye vipaji lakini ambalo lilikuwa nyuma ya majirani wenye nguvu kama Ghana, Nigeria na Ivory Coast. Mara nyingi walionekana kama timu yenye uwezo lakini iliyokosa ubora wa kushindania mataji.


KIZAZI KILICHOBADILISHA

Mabadiliko ya Senegal yalianza mwanzoni mwa miaka ya 2000 chini ya kocha Bruno Metsu. Hiki ndicho kizazi kilichokuja kubadilisha historia ya taifa hilo.

Wakiwa na nyota kama El Hadji Diouf, Henri Camara, Khalilou Fadiga, Salif Diao pamoja na Tony Sylva, Senegal walijenga kikosi kilichokuwa na nguvu, kasi na ujasiri mkubwa dhidi ya timu yoyote.

Afcon 2002 iliyopigwa Mali ilikuwa hatua kubwa ya kwanza ambapo walifika fainali katika historia kabla ya kupoteza kwa Cameroon kupitia mikwaju ya penalti 3-2 baada ya sare ya bila kufungana. Ingawa waliumia kupoteza taji, dunia ilikuwa haijaona kile ambacho Senegal walikuwa wanakiandaa.

SENE 02

WALIVYOISHTUA DUNIA 2002

Kombe la Dunia 2002 nchini Korea Kusini na Japan liligeuka kuwa moja ya hadithi kubwa zaidi kuwahi kutokea soka la Afrika.

Senegal waliingia mashindanoni kwa mara ya kwanza katika historia, lakini walijikuta wakicheza mechi ya ufunguzi dhidi ya mabingwa watetezi, Ufaransa. Hakuna aliyewapa nafasi kubwa dhidi ya timu iliyokuwa imejaa mastaa kama Zinedine Zidane, Thierry Henry, Patrick Vieira na David Trezeguet. Lakini, Senegal waliandika historia baada ya kushinda bao 1-0 kupitia Papa Bouba Diop. Ushindi huo uliishtua dunia nzima na kuifanya Senegal kuwa gumzo katika mashindano hayo.

Baadaye walitoa sare dhidi ya Denmark na Uruguay kabla ya kufuzu hatua ya 16 bora. Katika hatua hiyo waliiondoa Sweden kwa mabao 2-1 baada ya muda wa nyongeza kupitia bao la Henri Camara. Senegal walifika robo fainali na kuwa taifa la pili Afrika kufanya hivyo baada ya Cameroon 1990.

Safari yao ilisimama baada ya kupoteza dhidi ya Uturuki, lakini walikuwa tayari wameandika historia kubwa Afrika na duniani.


PANDA SHUKA

Baada ya mafanikio 2002, Senegal walikumbana na kipindi kigumu. Walishindwa kufuzu Kombe la Dunia 2006 na 2010 huku pia wakipitia misimu mibaya Afcon.

Kulikuwa na mabadiliko mengi ya makocha, kushuka kwa viwango vya baadhi ya mastaa pamoja na changamoto za kiuongozi ndani ya mfumo wa soka wa taifa hilo.

Katika Afcon 2012 waliondolewa hatua ya makundi bila kupata pointi hata moja jambo lililoumiza mashabiki wao. Hata hivyo, taifa hilo halikuacha kuwekeza katika maendeleo ya vijana. Akademi nyingi za kisasa ziliendelea kuanzishwa huku wachezaji wengi wa Senegal wakianza kung’ara katika ligi kubwa za Ulaya.

Hatua hizo ziliibua kizazi ubora kiufundi.

SENE 03

ENZI YA SADIO MANE

Kipindi cha mafanikio sasa kimefungamana na jina la Sadio Mane.

Nyota huyo aliyewahi kuichezea Liverpool, Bayern Munich na sasa Al-Nassr ya Saudi Arabia amekuwa sura ya taifa hilo kwa zaidi ya miaka 10.

Kupitia Mane pamoja na nyota wengine kama Kalidou Koulibaly, Idrissa Gueye, Ismaila Sarr na Edouard Mendy, Senegal walirudi tena kuwa moja ya mataifa yenye nguvu zaidi Afrika.

Mwaka 2018, Senegal walirejea Kombe la Dunia kwa mara ya pili tangu walipong’ara 2002. Katika mashindano hayo huko Russia, Senegal walionyesha kiwango bora na kuonekana kuwa na nafasi kubwa ya kutinga 16 bora.

Wakiwa kundi H na Poland, Japan pamoja na Colombia waliianza hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Poland kabla ya sare mabao  2-2 na Japan.

Katika mchezo wa mwisho wa kundi walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Colombia huku Japan wakifungwa 1-0 na Poland. Matokeo hayo yaliifanya Senegal na Japan kumaliza makundi zikiwa na idadi sawa ya pointi, tofauti sawa ya mabao pamoja na mabao ya kufunga na kufungwa.

Kutokana na kuwa kila kitu sawa, sheria ya Fifa ya ‘fair play’  ilitumika kuamua nani afuzu kwenda hatua inayofuata. Sheria hiyo huangalia idadi ya kadi za njano na nyekundu ambazo timu imepata katika mashindano.

Japan walikuwa na kadi chache kuliko Senegal, hivyo wakafuzu hatua ya 16 bora huku Senegal wakitolewa mashindanoni. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika historia kwa timu kutolewa kwa kutumia sheria hiyo, jambo lililoumiza mashabiki wa Senegal licha ya kiwango kizuri walichokuwa wamekionyesha uwanjani.

SENE 04

ILIVYOBADILISHWA

Hatua kubwa zaidi katika historia ya Senegal ilikuja 2022 walipotwaa Afcon mara ya kwanza.

Katika fainali dhidi ya Misri, Senegal walipambana kwa dakika 120 kabla ya kushinda kupitia mikwaju ya penalti huku Mane akifunga ya ushindi. Ulikuwa usiku wa kihistoria kwa taifa hilo kwani baada ya miaka mingi ya kusubiri hatimaye Simba wa Teranga walitwaa ubingwa wa Afrika.

Shangwe kubwa zililipuka Dakar huku mamia ya maelfu ya mashabiki wakijitokeza kusherehekea mafanikio hayo yaliyogeuka kuwa moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya michezo Senegal. Ubingwa huo uliwapa Senegal heshima mpya ndani ya Afrika pamoja na kujiamini zaidi katika mashindano ya dunia.


WALICHOFANYA QATAR 

Katika Kombe la Dunia 2022 Qatar, Senegal waliingia wakiwa mabingwa wa Afrika lakini walipata pigo baada ya Mane kuumia kabla ya mashindano kuanza.

Licha ya kumkosa nyota  mkubwa walipambana vilivyo, lakini wakapoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Uholanzi mabao 2-0, wakizifunga Qatar 3-1 na Ecuador 2-1  kabla ya kufuzu 16 bora kwa mara ya pili katika historia.

Hatimaye waliondolewa na England kwa mabao 3-0 lakini waliendelea kuonyesha kuwa wao ni moja ya timu bora zaidi Afrika.


KIZAZI CHA SASA

Senegal ya sasa inaonekana kuwa moja ya vikosi vilivyojaa uwiano mkubwa wa uzoefu na vipaji vya vijana.

Nahodha Kalidou Koulibaly anayekipiga Al-Hilal ya Saudia bado anaendelea kuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi kutokana na uzoefu na uwezo wa kuongoza

Kipa Edouard Mendy (Al-Ahli)ni mmoja wa makipa bora Afrika. Katikati  kuna Idrissa Gueye (Everton), Pape Sarr (Tottenham), Lamine Camara (Monaco) na Habib Diarra (Sunderland). Washambuliaji kuna Sadio Mane (Al-Nassr), Nicolas Jackson (Chelsea), Ismaila Sarr (Crystal Palace), Iliman Ndiaye (Everton) pamoja na Boulaye Dia (Lazio).


MALENGO 2026

Senegal wanakwenda Kombe la Dunia 2026 wakiwa na ndoto kubwa ya kuvunja rekodi ya robo fainali ya mwaka 2002. Kwa ubora wa kikosi walicho nacho na uzoefu wanaweza kufika nusu fainali.