Simba ndio huwatoi tena Uwanja wa Uhuru
Muktasari:
- Ilianza kuwadunga wale Wamalawi wa Mighty Wanderers kwa mabao 6-1 halafu ikawafunga watani wao wa jadi, Yanga kwa mabao 2-1 na juzi ikagawa dozi nzito ya mabao 6-1 kwa Mashujaa FC.
PALE uwanja wa Uhuru, Simba imeshapiga watu magoli 14 katika mechi tatu tu ambazo imecheza hapo msimu huu.
Ilianza kuwadunga wale Wamalawi wa Mighty Wanderers kwa mabao 6-1 halafu ikawafunga watani wao wa jadi, Yanga kwa mabao 2-1 na juzi ikagawa dozi nzito ya mabao 6-1 kwa Mashujaa FC.
Hizo mechi zote sio tu imepata ushindi lakini pia imepiga mpira mwingi sana tofauti na ile Simba ambayo imeanza msimu huu ambayo ndio ilikuwa inashinda lakini haikuwa inapiga bolu jingi.
Kwa elimu ya Cuba tunayotumia hapa kijiweni, tunaona kabisa Simba ndio washakita nanga moja kwa moja pale katika Uwanja wa Uhuru na haitokuwa rahisi kuwatoa.
Maana mwanzoni walisema watautumia kwa mechi za kimataifa tu lakini za ligi, Uwanja utakuwa ni Meja Jenerali Isamuhyo lakini kwa hizi raha wanazopata sijui kitu gani kitawahamisha pale labda waondolewe na wamiliki tu.
Hizi timu zetu bhana tunajuana na pamoja na mambo mengine, huwa zinaangalia upepo unavyokwenda na zikijiona zina bahati na mambo fulani kadha wa kadha basi ni ngumu kuyaacha na ndio zinasimika akili hapo. Upepo wa Simba hivi sasa uko katika Uwanja wa Uhuru hivyo ndugu zetu wale wa jirani na kule Isamuhyo wajiandae tu kutoiona timu kwa ukaribu kama ilivyokuwa zamani.
Gia waliyoanza nayo katika ule uwanja ni kubwa sana na wameshaanza kutengeneza bondi fulani hivi kati ya wachezaji na mashabiki wao ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa wafanye vizuri.
Kutoka kupata ushindi wa kushika roho hadi kugawa dozi kubwa huku wakicheza vizuri, sioni Simba wakihama Uhuru hata ukiniwekea mchanga jichoni.