Sikia masikitiko ya mwanasoka Owen Hargreaves

Muktasari:
- Lakini, kwa watoto wengi masikitiko makubwa huibuka pale wanapoona wameshindwa kutimiza baadhi ya ndoto za wazazi wao ili kuwafurahisha.
LONDON, ENGLAND: KWA wazazi wengi duniani, kama kuna kitu kinachowapa furaha ni kuona watoto wao wanafikia ndoto za juu kabisa za mafanikio kwa kile kitu wanachojishughulisha nacho.
Lakini, kwa watoto wengi masikitiko makubwa huibuka pale wanapoona wameshindwa kutimiza baadhi ya ndoto za wazazi wao ili kuwafurahisha.
Hicho ndicho kilichotokea kwa mwanasoka mahiri kuwahi kutokea kwenye mchezo huo, kiungo Mwingereza Owen Hargreaves.
Kwenye soka, Hargreaves amepata mafanikio makubwa akishinda mataji ya ligi ya ndani mara tano, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na kucheza kwa kiwango bora kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Three Lions.
Hakika, Hargreaves aliishi ndoto zake, kubeba mataji hayo makubwa na kuitumikia timu yake ya taifa ya England, si kwenye mechi moja, bali 42.
Bila shaka hata wazazi wake walikuwa wakifurahia kila kitu kilichofanywa kwa mafanikio na mtoto wao, Owen, lakini baba yake kuna ndoto yake moja, haikuwa imetimizwa na mwanaye na hilo ndilo linalomfanya mtoto huyo kuhuzunika.
Owen alizaliwa Canada na mama raia wa Wales na baba yake Mwigereza na aliamua kuchagua taifa la baba yake kwenye kulitumikia kwenye soka la kimataifa na mechi yake ya England, aliicheza alipopewa nafasi hiyo na kocha Sven-Goran Eriksson mwaka 2001, licha ya kwamba hakuwa amewahi kuishi kwenye nchi hiyo.

Baba yake, Colin, utotoni alikuwa mchezaji Bolton Wanderers na baadaye aliichezea Calgary Kickers kabla ya kuhamia Canada na mkewe mrembo Margaret mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Licha ya kuvuka bahari ya Atlantic, Colin aliendelea kuwa shabiki mkubwa wa Bolton - hivyo alikuwa na huzuni kwa mtoto wake kushindwa kuichezea Bolton katika maisha yake ya soka.
“Ndio, Bolton ilikuwa timu yake wakati anakua na bado timu yake anayoshabikia hadi sasa,” alisema Hargreaves.
“Alikuwa akiniambia nilipokuwa mdogo nitakwenda kuichezea Wanderers siku moja. Lakini, nilipata mafanikio makubwa kwa haraka na hivyo nikajikuta nikicheza kwenye timu za viwango tofauti kabisa kwenye soka – sina maana naikosea heshima Bolton, hapana.
“Timu yangu ya kwanza ilikuwa Bayern Munich na nilikuwa nacheza kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Ulayanna nilicheza Kombe la Dunia nikiwa na England.
“Ningependa kuichezea Bolton, ningeweza kufanya hivyo kwenye miaka yangu ya mwisho kwenye soka, ikashindikana. Baba yangu anajivunia mafanikio yangu na kila kitu nilichokipata kwenye soka. Lakini, naishi kwa masikitikio makubwa kwa sasa kwa sababu sikuwa mchezaji wa Bolton.”

Kinachomsikitisha Hargreaves ni kushindwa kutimiza ndoto za baba yake na maneno aliyokuwa akiambiwa utoto na mzazi wake huyo, siku moja atakwenda kuwa mchezaji wa Bolton.
Kwenye ishu ya uchaguzi wa timu ya taifa, Hargreaves alikuwa kwenye wakati mgumu wakati Canada ilipokuwa ikimhitaji aitumikie timu ya soka ya nchi hiyo kabla ya kufanya uamuzi wa kuwa staa wa kikosi cha Three Lions.
“Nilijiona nina mlima mkubwa wa kupanda wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2006. Mashabiki wengi wa England pamoja na waandishi walikuwa hawajawahi kuona nikicheza, lakini nilijua nitashinda mioyo yao,” alisema Hargreaves.
Baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa Bayern, Owen alipata dili la kujiunga na miamba ya soka ya England, Manchester United na kupata fursa ya kucheza Ligi Kuu England.
Man United ilinasa saini yake baada ya fainali za Kombe la Dunia 2006, ilipolipa ada ya Pauni 17 milioni na kipindi hicho alikuwa anapambana kupona majeraha yake ya kuvunjika mguu.
“Sikuweza kuwa sawa tena baada ya sindano zote na upasuaji wote nikiwa Manchester United – nilikuwa kwenye maumivu ya kudumu. Sikuwa na ufahamu majeraha yangu yalikuwa hatari kiasi gani,” alisema Hargreaves wakati anafunguka namna majeruhi yalivyomtibulia maisha ya soka.

Majeraha yalimtibulia Hargreaves maisha yake kwenye kikosi cha Man United, huku kubwa lililofanya hivyo ni maumivu ya goti, ambayo yalishindwa kupona vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji. Nyakati zake za mwisho kwenye soka, Hargreaves aliichezea Manchester City katika msimu wa 2011/12 na kustaafu kwenye miaka ya mapema ya umri wa miaka 30.
“Haukuwa uamuzi mgumu kwenye kumaliza soka langu, kwa sababu nilitaabika sana na maumivu ya goti,” alisema.
Pengine maumivu ya goti yalitibua maisha ya soka ya Hargreaves kwa kiasi kikubwa, lakini masikitiko ya kiungo huyo wa zamani wa England ni kushindwa kuichezea timu ya ndoto za baba yake, Bolton Wanderers.