Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shalulile na kivuli cha ustaa Yanga

SHALULILE Pict

Muktasari:

  • Kinyume chake, tabia zake ndogo ndogo zimeanza kumfanya awe mchezaji wa tofauti, huku baadhi ya watu wakimfananisha kwa namna fulani na kiungo wa Al-Ittihad ya Saudi Arabia na Ufaransa, N’Golo Kante.

UKIMWONA Peter Shalulile uwanjani unaweza kudhani kazi yake ni moja tu, kukimbia, kupambana na mabeki, kufunga mabao na kuwapa Yanga furaha, lakini ukimfuatilia nje ya dakika 90, utagundua unaishi na mtu ambaye ana dunia yake ya nidhamu.

Mshambuliaji huyo wa Yanga si aina ya mastaa wanaoamini ukubwa wao unawaruhusu kufanya kila kitu wanachotaka.

Kinyume chake, tabia zake ndogo ndogo zimeanza kumfanya awe mchezaji wa tofauti, huku baadhi ya watu wakimfananisha kwa namna fulani na kiungo wa Al-Ittihad ya Saudi Arabia na Ufaransa, N’Golo Kante.

Shalulile ni mtu anayependa mambo yawe katika mpangilio. Ni miongoni mwa wachezaji wanaowahi kula kwa wakati, anazingatia usafi na mara nyingi huonekana akiwa nadhifu, huku mtindo wake wa jezi kuchomekea ukiwa kama sehemu ya utambulisho wake.

Kocha wake Manqoba Mnqithi amesema huyu ni mchezaji wa kuigwa kwa nidhamu, kufuata utaratibu lakini pia kuishi kama wanavyotakiwa kuishi wachezaji wakubwa duniani.


SHALU 03

TUANZIE MAZOEZINI

Hata kwenye mazingira ya mazoezi, si mtu anayesubiri kila kitu kifanywe na wengine amekuwa akionekana kufanya mambo ambayo ni ngumu kwa wachezaji wengine kuyafanya.

Anaweza kushiriki kupanga vifaa vinavyotumika wakati wa mazoezi, kama vile koni na bipsi akiwasaidia watumishi wengine wa Yanga kufanya majukumu yake jambo linaloonyesha aina ya mchezaji anayejiona kuwa sehemu ya timu kuliko kuwa nyota anayepaswa kuhudumiwa kila kitu.

Lakini si hivyo tu hata baada ya kumaliza mazoezi magumu ambayo kocha amewapa kwa siku husika, bado Shalulile atasaidiana na wafanyakazi wa Yanga kukusanya vifaa na kuviweka mahali husika, Mwanaspoti lilimshuhudia akiokota bipsi chini ana kuweka kwenye mfuko maalumu, pia alikusanya mipira pamoja na koni na kuweka sehemu inayotakiwa jambo ambalo lilionyesha kitu cha tofauti kabisa kwake kwani wachezaji wengine ni ngumu kufanya jambo hilo .


SHALU 02

MUNGU KWANZA

Kisha kuna upande mwingine ambao unamfanya awe tofauti zaidi ambao ni imani yake.

Shalulile amekuwa akizungumzia nafasi ya Mungu katika maisha yake na safari yake ya soka, jambo linaloonyesha kwamba pamoja na umaarufu, fedha na presha ya kuwa mshambuliaji wa timu kubwa, bado ana misingi yake anayoshikilia na hali hii imekuwa ikimfanya kusali kila wakati kabla na baada ya kumaliza mazoezi, hili siyo jipya sana kwa kuwa wachezaji wengi wanafanya hivyo.

“Namjua Shalulile kwa muda mrefu, hapa nyie mnaweza kushangaa lakini ukweli ni kwamba ndio maisha yake, ni mchezaji ambaye amekuzwa maisha ya imani kubwa na ameshiba imani na anapenda kuona wenzake wanafanikiwa,” alisema kocha wa Yanga, Manqoba.


NIDHAMU

Shalulile pia ni mtu mwenye nidhamu katika mambo yote kuanzia kuvaa, lakini hata kocha wa kikosi hicho Manqoba  aliwahi kumzungumzia na kusema mastaa wanatakiwa kuiga mfano wake.

Kwangu nafikiri mastaa wa Yanga wanatakiwa kuiga baadhi ya vitu kwake, ana nidhamu na heshima ya hali ya juu sana,’’ alisema.

Unaambiwa Shalulile anazingatia kila kitu anachotakiwa kufanya kuanzia muda wa chakula, kulala, mazoezini, vikao na jinsi anavyotakiwa kuvaa muda wote akiwa kambini au nje ya kambi, lakini pia sio muongeaji sana.

Mshambuliaji huyo wa Yanga anaweza kuwa mmoja wa watu muhimu kwenye kikosi, lakini tabia zake zinaonyesha kwamba anapenda kufanya mambo ya kawaida kwa nidhamu.


KUHUSU SENDOZI

Sio rahisi sana kumuona Shalule amevaa makombazi (sendozi) kwenye maeneo ya wazi mara nyingi anapenda kuvaa viatu kama ambavyo wachezaji wengi wamekuwa wakivaa na hata akivaa na ni nadra kumuona amevaa sendozi akiwa nje ya kambi ya timu hiyo.


SHALU 04

MITANDAO SIO VITU VYAKE

Ukiachilia mbali maisha yake ya utofauti na wachezaji wengi, lakini imekuwa kawaida kwa mastaa kuwa watu wa mitandao, unaweza kumkuta mchezaji akiposti picha mbali mbali kwenye mtandao kama Instagram.

Ukimuangalia mchezaji maarufu kama Ronaldo utamuona muda mwingi akiweka maisha yake nje na soka, utaona kwa siku ameposti picha moja au mbili akiwa kazini au na familia.

Lakini kwa Shalulile yeye hana mzuka huo kabisa, kwani alivyotua tu Yanga mpaka sasa ameposti picha tano na video moja akiwa mazoezini, huku akiweka picha zingine tatu za biblia.

Hivyo anajumla ya picha nane na video moja pekee, akiwa na followers Laki mbili na themanini na saba, akiwa amewafollow watu Elfu tatu na hamsini na sita, licha ya kutokuwa na mambo mengi, lakini watu bado wanaemfuatilia kwa ukubwa, picha yake aliyoposti Agosti 8, ndio inaongoza kwa kuwa na likes Elfu tisini na nane na mia tatu (98.3k).


KUHUSU FAMILIA

Mpaka sasa hakuna anayejua mke wa Shalulile wala mtoto wake, kwani hakuna sehemu yoyote ambayo ameweka wazi mambo kuhusu familia yake, wala hakuna rafiki yake wa karibu ambaye amemposti.

Hii ikionyesha kwamba, Shalulile ni mtu wa kila mtu ambaye hajataka kuweka ukaribu na dunia wala watu ili kuweza kufahamika zaidi, kama ilivyo kwa mastaa wengine wanavyoweka wazi maisha yao na watoto wao kama vile staa wa Yanga Stephane Aziz KI.


SHALU 05

ANAFANYA USAFI VYUMBANI

Timu inapomaliza mechi na wachezaji kutoka kwenye chumba, chanzo kinasema kuwa unaambiwa Shalulile anabaki na kufanya usafi kwa kuokota uchafu wote ambao imetengenezwa wakati chumba husika kikiwa na wachezaji wa timu.


KAMA KANTE

Kama kuna jina linaloweza kuingia kwenye mazungumzo haya, basi ni N’golo Kante. Mfaransa huyo amejenga sifa ya kuwa mmoja wa mastaa wakubwa wenye maisha yasiyo na makeke. Wakati wachezaji wengi wakubwa wanapenda kuonekana na kutengeneza maisha ya kifahari yanayoendana na umaarufu wao, Kante amekuwa akijulikana kwa unyenyekevu na kutopenda kujitenga na watu.

Moja ya tukio kubwa linalokumbukwa ni pale alipoonekana katika mchezo wa Al-Ittihad dhidi ya Al-Ahli na mchezo ulisimama baada ya mashabiki kutupa bendera nyingi uwanjani. Wakati wachezaji wengine wakitoka kwenda kupata maji, Kante alibaki uwanjani na kuanza kusaidia kuondoa vitu hivyo ili mchezo uendelee.

Makocha wengi wamemsifu kwa unyenyekevu wake na namna anavyoweka timu mbele. Hata baada ya kushinda Ligi Kuu England mara mbili na Kombe la Dunia, hakubadilika na kuwa mtu wa kutafuta sifa.


SHALU 01

RONALDO

Halafu kuna Cristiano Ronaldo, ambaye ukimtoa kwenye mijadala ya ubora wa soka, utapata somo jingine kubwa la maisha ya nidhamu.

Ronaldo amejijengea sifa ya kuwa mchezaji anayezingatia sana mwili wake, mazoezi na utayari wa kucheza kwa kiwango cha juu. Kazi yake ya mazoezini na kujituma kuboresha mwili wake imekuwa sehemu kubwa ya mafanikio yake.


SHALU 06

SIKIA KUTOKA KAMBINI YANGA

Kocha Manqoba Mnqithi amesema Shalulile sio staa pekee kwenye kikosi cha Yanga lakini kwa upande wa nidhamu na kutimiza majukumu ya ratiba na mengine yanayohusu kazi yake basi yeye ni kipaumbele cha kwanza.

“Shalulile ni wa kwanza kuingia uwanjani karibia kila siku, sio hivyo ni wa kwanza kwenye kila kitu anachotakiwa kufanya kwa wakati huo iwe ni mazoezi au chochote, hii inasaidia sana kwa timu kuelewa inamaanisha nini kwa timu kuwa mchezaji wa kulipwa (mkubwa).

“Naweza kusema kila kitu alichokipata kwenye mpira alikifanikisha kwa sababu ya level yake ya kujitambua yeye ni nani na umakini hasa kwenye utendaji wake wa kazi na nina hisi hicho ndicho anachoendelea kukifanya hata hapa Yanga,”  anasema kocha Manqoba.


MASALANGA ATIA NENO

Mmoja kati ya makipa wa kikosi hicho Hussein Masalanga anasema Shalulile ni mmoja kati ya wachezaji wapole na wastaarabu sana ndani ya timu hiyo na kuhusu kuwa mtu wa Mungu, ni kweli.

“Bahati nzuri kila mchezaji hapa Yanga anaimani yake, lakini kuhusu kumfananisha Maxi Nzengeli na Peter hawafanani kwa sababu ni watu tofauti ila Shalulile ni mpole zaidi, lakini Maxi naye ana vitu vyake vya tofauti.”


SHALU 06 (1)

MSIKIE SURE BOY

Kiungo wa Yanga Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amekiri kwamba Shalulile ni mchezaji wa tofauti akisema raia huyo wa Namibia amekomaa akiongozwa na nidhamu kubwa.

“Nikweli Shalulile ni mchezaji wa mfano mkubwa, kama Kuna mchezaji unaweza kumuweka mbele kwa mfano mzuri wa nidhamu basi ni huyu mafanikio aliyonayo angeweza kuwa na tabia zozote lakini sio kwa Shalulile,” alisema Sure Boy.

“Kila sehemu huwa anakuwa wa kwanza, kuanzia muda wa kula, wakati wa mazoezi na hata kwenye mikutano au hata safari anakuwa Yuko wa kwanza.

“Amekuwa sana anatenga muda wa kuongea na wachezaji vijana anawapa ushauri na wakati mwingine hata wachezaji wengine sio mtu mchoyo wa mafanikio, nadhani tuna nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwake.

“Nimecheza soka kwa muda mrefu hapa Tanzania, wengi wetu tunauchukulia mchezo wa soka kama usela lakini wenzetu wanauchukulia kwa heshima kubwa ndio maana unaona tabia zao ziko kama hivi, jambo linawaongezea thamani zaidi.”