Mashabiki Azam wana haki kumlaumu Ibenge
Muktasari:
- Na sisi hapa kijiweni tunawaunga mkono mashabiki wa Azam FC kwamba wanachokilalamikia kwa Ibenge ni kitu sahihi na wala haimaanishi kwamba hawampi heshima kocha huyo.
KILE kilio na malalamiko ya jamaa yetu shabiki wa Azam FC, Mwenezi Azam kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Florent Ibenge bila shaka yanawakilisha hisia za mashabiki wengi wa timu hiyo.
Na sisi hapa kijiweni tunawaunga mkono mashabiki wa Azam FC kwamba wanachokilalamikia kwa Ibenge ni kitu sahihi na wala haimaanishi kwamba hawampi heshima kocha huyo.
Hatufanyi hivyo kwa sababu tu ya matokeo ya uwanjani kwani timu kuangusha pointi kwa kupoteza mchezo au kutoka sare ni jambo la kawaida bali kuna sababu nyingine za msingi.
Sababu hizo zinafanya tuamini kama Ibenge bado harudishi angalau robo tatu ya thamani ya fedha ambayo Azam FC inatumia kuhakikisha anafanya kazi na majukumu yake kwa ufasaha mkubwa.
Iko wazi ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi hapa nchini lakini pia kila ambacho anakihitaji, anakipata hasa katika masuala ya usajili.
Kwanza amekuwa anafanya mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi jambo ambalo linafanya wachezaji wakose muendelezo wa kuzoeana ndani ya kiwanja.
Kufanya mabadiliko sio dhambi lakini timu inayokupa matokeo mazuri haipaswi kubadilishwa kama anavyofanya Ibenge.
Lakini pili wachezaji walewale ambao yeye alipendekeza wasajiliwe, hawapata nafasi ya kucheza jambo linalotoa ishara kwamba kuna namna hakujiridhisha kuhusu viwango vyao wakati anapendekeza wasajiliwe.
Ibenge halaumiwi kwa bahati mbaya, mashabiki wa Azam wako sahihi.