Serengeti Boys wasipotee kisoka
Muktasari:
- Hili ni jambo kubwa sana ukizingatia hapo nyuma hakujawahi kuwa na timu ya taifa ya wanaume katika hii nchi ya Tanzania iliyowahi kushiriki fainali za soka za dunia kwa umri wowote ule.
MJADALA mkubwa hapa kijiweni ni habari ya Serengeti Boys kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana wenye umri wa miaka 17 ambazo zitafanyika Qatar, mwishoni mwa mwaka huu.
Hili ni jambo kubwa sana ukizingatia hapo nyuma hakujawahi kuwa na timu ya taifa ya wanaume katika hii nchi ya Tanzania iliyowahi kushiriki fainali za soka za dunia kwa umri wowote ule.
Kwa hiyo sisi kwenye kijiwe kwa vile ni watu wa mpira na tunajua faida za timu kushiriki Kombe la Dunia, hilo la Serengeti Boys ni jambo ambalo tumelipokea kwa mikono miwili na limetufurahisha sana.
Lakini kitu kimoja ambacho wengi tunatamani kukiona ni hao vijana wawe na mwendelezo mzuri katika miaka ya usoni ili waje kuwa na mchango mkubwa katika timu ya taifa ya wakubwa kwa maana ya Taifa Stars.
Kumekuwa na changamoto ya vijana wengi ambao wanaonyesha kuwa na vipaji vya soka na wanaofanya vizuri katika timu za vijana, kushindwa kufikia matarajio ya wengi na mwishowe inabakia historia tu waliwahi kuonyesha kitu hapo nyuma.
Changamoto kubwa inayoonekana kuwa sababu ya hili ni wachezaji hao kukosa maandalizi mazuri kiakili ambayo yatawafanya walinde vipaji vyao na kuendelea kupewa nafasi katika timu mbalimbali.
Wanaowasimamia wanapaswa kuwajulisha vipaji pekee havitoshi kuwavusha katika soka bali pia wanahitaji nidhamu kubwa ya kimaisha hasa nje ya uwanja ambayo ina nafasi kubwa ya kuwatoa sehemu moja hadi nyingine.
Tunaamini hili litafanyika kwa Serengeti Boys na ushiriki wake katika Kombe la Dunia utakuwa fursa nzuri ya kuwapeleka vijana hawa katika daraja la juu kisoka.