Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta ya usafiri mguu sawa AFCON 2027

AFCON Pict

Muktasari:

  • Sekta mbalimbali zimeanza kujipanga kuhakikisha zinachangamkia fursa zitakazokuja sambamba na ujio wa maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya Afrika.

WAKATI Tanzania, Kenya na Uganda zikihesabu miezi kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, maandalizi yake hayapo kwenye viwanja pekee, sasa hadi nje ya uwanja kumeanza kunoga.

Sekta mbalimbali zimeanza kujipanga kuhakikisha zinachangamkia fursa zitakazokuja sambamba na ujio wa maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya Afrika.

Moja ya sekta hizo ni usafiri, hasa huduma za taksi mtandao, ambayo imeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha wageni watakaowasili nchini wanapata huduma salama, rahisi na yenye kiwango kinachostahili.

Chama cha Madereva wa Taxi Mtandao (TODA), kupitia mkutano uliofanyika Septemba 15 katika Karimjee Hall, Dar es Salaam, kilijadili kwa kina fursa na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, huku AFCON 2027 ikiwa miongoni mwa ajenda muhimu.

Kwa upande wa Tanzania, mashindano hayo yatakuwa zaidi ya burudani ya soka. Ni tukio linalotarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali, ikiwamo usafiri.


AFC 06

FURSA KWA MADEREVA

Neema Mushi, Mwenyekiti mstaafu wa TODA, anasema AFCON 2027 ni fursa kubwa kwa madereva wa taksi mtandao kutokana na ongezeko la wageni litakalotokana na mashindano hayo.

“Kwa kweli ni fursa nzuri kwa sababu wengi ni wageni na lazima wataulizia taxi mtandao. Itatusaidia kupata kipato chetu. Tumeifurahia na tumejiandaa kuwahudumia wageni wetu kwa kuwa waaminifu,” anasema Mushi.

Hata hivyo, amesema lugha inaweza kuwa moja ya changamoto kwa baadhi ya madereva kutokana na wageni kutoka mataifa tofauti.

“Japokuwa lugha itatupa changamoto kidogo, lakini tutajaribu kupambana nayo hivyo hivyo,” anaongeza

Diana Lazaro anasema mikutano kama hiyo ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea mashindano hayo, kwani inawapa madereva nafasi ya kujadili changamoto na kutafuta suluhisho mapema.

“Mkutano huu ni muhimu kwa ajili ya maandalizi. Tukiendelea kujumuika kwenye mikutano mbalimbali, itaongeza umakini zaidi kwa madereva kuelekea AFCON,” amesema.


AFC 04

TEKNOLOJIA KUIOKOA LUGHA

Kwa upande mwingine, TODA imependekeza matumizi makubwa zaidi ya teknolojia katika kuboresha huduma kwa wageni.

Ford amesema kuna haja ya kuwepo kwa mafunzo yatakayowawezesha madereva kutumia mifumo mbalimbali ya kidijitali, ikiwamo teknolojia za kutafsiri lugha.

Anaongeza jambo hilo litakuwa muhimu kwa kuwa Tanzania inatarajiwa kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali ambao baadhi yao hawatazungumza Kiswahili wala Kiingereza kwa ufasaha.

“Uwezo wa dereva kuwasiliana na abiria kwa kutumia teknolojia za tafsiri unaweza kusaidia kuondoa changamoto za mawasiliano na kuongeza ubora wa huduma,” anasema Ford.


AFC 02

UWANJA WA NDEGE, SGR BADO KERO

Pamoja na fursa hiyo, madereva wameibua changamoto inayowakabili wanapofanya kazi katika maeneo muhimu ambayo wageni wengi wanatarajiwa kuyatumia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Michael Mtalii amesema eneo la uwanja wa ndege na vituo vya SGR limekuwa changamoto kwa madereva wa taksi mtandao, hasa wakati wa kupakia na kushusha abiria.

Anasema wakati mwingine madereva hukutana na zuio au kufukuzwa wanapojaribu kuwahudumia abiria katika maeneo hayo.

“Changamoto kubwa ya madereva ni eneo la airport na kituo cha SGR ambako madereva wamekuwa wakipitia changamoto ya kushindwa kupakia wateja na wakati mwingine wanafukuzwa. Sasa wakati tunapoelekea kwenye mashindano makubwa kama AFCON, Wizara ya Uchukuzi iangalie eneo hilo lirekebishwe,” anasema.

Katibu wa TODA, Ebon Ford, amesema changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza hata kwa baadhi ya madereva ambao tayari wamesajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kupewa vibali vya kufanya biashara hiyo.

“Madereva wa taksi mtandao mara kadhaa wamekuwa wakipata usumbufu wanapopakia au kushusha abiria, wengine wamekuwa wakikamatwa katika maeneo hayo,” amesema Ford.

Anasema Serikali inapaswa kuweka maeneo maalumu kwa magari ya taksi mtandao yenye vibali ili madereva waweze kuwahudumia abiria bila kuvunja taratibu.

“Hatusemi taratibu za usalama zikiukwe. Tunachotaka ni mfumo unaomwezesha dereva aliyesajiliwa na LATRA kumpokea au kumshusha abiria katika eneo lililotengwa bila kukamatwa,” amesema.


AFC 03

LATRA YATOA WITO

Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dk Habibu Suluo, amewataka madereva wa taksi mtandao kuwa waaminifu katika kazi zao, akisisitiza kuwa wanabeba dhamana ya usalama wa abiria, muda wao na wakati mwingine mali zao.

Suluo amesema madereva wanapaswa kuhakikisha magari wanayoyaendesha yana bima halali, leseni na nyaraka zote zinazotakiwa kisheria.


KUJIFUNZA NJE

Mkurugenzi wa Idara ya Fedha wa TODA, Augustino Gasper, anasema maandalizi yanapaswa kuanza mapema, huku akishauri baadhi ya wadau kupewa nafasi ya kujifunza uzoefu kutoka mataifa ambayo yamewahi kuandaa mashindano makubwa.

“Tunayo mashindano ya AFCON na ni bahati kubwa. Sio jambo jepesi TODA tumeona tuanze maandalizi mapema, kwa sababu madereva ndio watu wa kwanza kumpokea mtu,” amesema Gasper.

Aliongeza Serikali inaweza kuchagua baadhi ya sekta na kuwapeleka watu kujifunza katika nchi zilizoendelea namna zilivyoandaa huduma wakati wa mashindano makubwa.


AFC 01

TODA YAJIPA MATUMAINI

Mwenyekiti wa TODA, Fey Mashala, amesema chama hicho tayari kimeanza kuweka AFCON katika ajenda zake za maandalizi.

“Tulifanya ajenda mojawapo ilikuwa AFCON. Sio mgeni anafika kwako leo ndio unajiandaa. Inapaswa kujiandaa mapema ili wageni waondoke na sifa kibao,” amesema Mashala.


WIZARA

Akizungumza na Mwanaspoti, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Abdallah Mitawi anasema "Tunategemea kwamba zaidi ya watu milioni moja kuingia Tanzania kwa ajili ya AFCON na Miss World bila shaka wote hao watahitaji huduma za usafiri,"

"Bila shaka ni namna ya kutayarisha ni kuhakikisha sekta binafsi inachangamkia fursa ya matukio hayo yanayoletwa na Serikali wajitayarishe kuhakikisha wanakabiliana na fursa hizo ili wageni wanaokuja waondoke na sifa nzuri,"

Baada ya changamoto zilizoelezwa na madereva Mitawi aliiagiza LATRA kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, mamlaka za viwanja vya ndege, SGR na taasisi nyingine husika kutatua changamoto zinazowakabili madereva wa taksi mtandao wanapowahudumia abiria.

Agizo hilo alilitawa katika hotuba ya Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abdallah Mitawi.

“Ninaielekeza LATRA ikae na Wizara ya Uchukuzi, mamlaka ya viwanja vya ndege, SGR na taasisi husika ili kuhakikisha changamoto wanazopata madereva wanaohudumia abiria, ambao ni wanachama wa TODA zinapatiwa ufumbuzi,” amesema Mbarawa.


AFC 05

SURA YA NCHI

Kwa mtazamo wa wadau hao, maandalizi ya AFCON hayapaswi kuishia kwenye viwanja, hoteli na miundombinu ya michezo.

Sekta ya usafiri nayo ni sehemu ya taswira ya Tanzania, kwani mgeni anapowasili nchini, mmoja wa watu wa kwanza kukutana naye ni dereva.

Ndiyo maana wadau wanataka madereva kujiandaa kwa kuwa na magari safi, huduma nzuri, uaminifu, nidhamu na matumizi ya teknolojia yatakayorahisisha mawasiliano.

Kwa hiyo, wakati wachezaji wakijiandaa kupambana uwanjani, nje ya uwanja nao maandalizi yameanza. Kwa madereva wa taksi mtandao, AFCON 2027 si mechi pekee, bali ni fursa ya biashara na nafasi ya kuonyesha kwa wageni sura ya Tanzania.