Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simu ya kocha mpya yatibua dili la ‘mamilioni’ Dar

KIUNGO Pict


HIVI karibuni, Mwanaspoti liliripoti kwamba, Simba imetua pale Afrika Kusini kwa ajili ya kuinasa saini ya winga wa kushoto, Keletso Makgalwa ambaye amemaliza msimu wa 2025-2026 akiitumikia Shekhukhune ya Afrika Kusini.


Winga huyo aliwahi kufanya mazungumzo na Yanga kipindi cha usajili wa dirisha kubwa mwanzoni mwa msimu uliomalizika 2025-2026, lakini Sekhukhune ikaweka ngumu kumtoa, ikawapa Yanga Andy Boyeli kwa mkopo.


Makgalwa anayetumia zaidi mguu wa kulia lakini anapenda kushambulia akitokea kushoto akiwa na kasi kubwa na ujuzi wa kujua kuwapangua mabeki, ameibua vita mpya kwa Yanga na Simba na huenda lolote likatokea msimu ujao kucheza Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo mojawapo.


KOCHA MPYA ASIMAMIA SHOO

Siku chache baada ya Yanga kumtangaza Manqoba Mngqithi raia wa Afrika Kusini kuwa kocha mpya wa kikosi hicho, imeelezwa kwamba jamaa huyo ameanza na kutibua hesabu za Simba akizuia dili la Keletso Makgalwa ambapo Wekundu hao wa Msimbazi walishakaribia pia kukamilisha makubaliano na mabosi wa klabu hiyo.

Simba kupitia kocha wake Steve Barker, alishatangulia kumshawishi winga huyo ili aje kuongeza nguvu kwenye kikosi chake, akiwaachia mabosi wake kumaliza hatua za mwisho ili Makgalwa aje kuvaa jezi nyekundu na nyeupe.

Inaelezwa kwamba, juzi baada ya Yanga kumtangaza Mngqithi, jamaa akasikia taarifa hizo kisha kumpigia simu moja kwa moja winga huyo na kubadlisha kila kitu kuhusu hesabu zake za awali za kutua Simba na kumtaka ajipange kwenda kuvaa jezi za njano na kijani kwa msimu ujao.

Awali, Yanga ilikuwa inasaka winga mpya kwenye kikosi hicho baada ya kutoridhishwa na Bubah Jammeh, ikirudi tena kwa Kipre Junior na kukuta tayari ameshamalizana na klabu yake ya zamani ya Azam, kutokana na makubaliano ya awali wakati anasajiliwa MC Alger ya Algeria.

Taarifa kutoka Yanga zinasema kwamba, Makgalwa jana alikuwa kwenye mazungumzo ya mwisho na mabosi wa klabu hiyo akimalizia makubaliano ya kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Tanzania kuwa mchezaji wao mpya.

“Karibu kila kitu kinakwenda sawa wakati wowote kutoka kesho (jana), anaweza (Makgalwa) kusaini mkataba na Yanga, unajua Makgalwa na wachezaji wengi wanafurahia sana kufanya kazi na Mngqithi kwani ni kocha ambaye anajua sana kujenga saikoloji ya mchezaji,” amesemammoja wa mabosi wa Sekhukhune.

“Ukiniuliza ni kipi kimetokea mpaka Makgalwa kwanini amegeuza mawazo yake kutoka meza moja kwenda nyingine nitakwambia tatizo ni ushawishi wa Mangqithi ndiye aliyeweza kubadili akili ya kijana na kubadilisha mawazo yake.”

Taarifa zaidi zinasema Yanga imekubali kutumia Dola 185,000 (Sh 486 milioni) kukamilisha dili la winga huyo ambaye msimu uliomalizika alihusika kwenye mabao nane akifunga mawili na kutengeneza asisti sita katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Faida kubwa itakayowabeba Yanga ni kuwa na mawasiliano mazuri na Sekhukhune ambayo iliwahi kuwapa mshambulkiaji Andy Boyeli kwa mkopo ambaye hata hivyo alirudishwa kutokana na kiwango chake na sasa ameachwa na Wasauz hao.


SIMBA ILIVYOANZA

Kwenye ripoti ya msimu uliomalizika, Barker ameonyesha kama Simba ikimkosa winga wake mmoja kati ya Anicet Oura au Libase Gueye, inakabiliana na changamoto ya kujenga mashambulizi kutokea pembeni.

Barker alitoa mfano ilivyotokea kwenye mchezo dhidi ya Yanga pale Uwanja wa New Amaan Zanzibar kwenye fainali ya Kombe la Muungano ambapo baada ya kuumia Oura, Wekundu hao wa Msimbazi hawakuwa na mashine nyingine kama winga huyo raia wa Ivory Coast.

Kutoka na hilo, Simba ikafanya juhudi za kumnasa Makgalwa kwenye mazungumzo yaliyofanywa na bosi mmoja wa juu kwenye bodi ya klabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinadai kwamba, winga huyo aliletwa Dar es Salaam wiki iliyopita na kukubaliana kila kitu na kusubiriwa kupewa mkataba wa miaka miwili asaini.

“Ni kweli alikuja Dar, amefanya mazungumzo na mabosi wa Simba, wamekubaliana kila kitu, ndipo akaondoka,” kilisema chanzo kutoka Simba.

“Makubaliano hayo ni dau la usajili kiasi cha dola 350,000 (Sh920 milioni), hadi mchezaji anaondoka, alionekana yupo tayari, hivyo kinachosubiriwa ni kusaini mkataba tu ambao ni wa miaka miwili.”

Chanzo hicho kimesema uamuzi wa Simba kumsaka winga huyo, ni kutokana na Anicet Oura dili lake la kutimkia Ulaya linakaribia kutiki kwani Simba imepokea ofa ya dola 750,000 (Sh1.9 bilioni).

“Oura alinunuliwa kwa 300,000 (Sh788 milioni), imekuja ofa kubwa zaidi kutoka Ulaya, Simba imeona ifanye biashara, kisha hela zitakapoingia, atafute mbadala wake,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti linafahamu klabu zinazomfuatilia kwa karibu Oura ni Bursaspor ya Uturuki, Víkingur Reykjavík ya Iceland na DAC 1904 Dunajská Streda ya Slovakia.

Oura mwenye miaka 26, alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili Januari 2026 akitokea IF Gnistan ya Finland na kusaini mkataba wa miaka miwili na tangu kutua Msimbazi amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika mafanikio ya timu hiyo msimu huu.