Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya kinda Mtanzania aliyetua La Masia

BARKA Pict

Muktasari:

  • Kijana huyo alipata nafasi ya kushiriki kliniki za vijana za akademi ya Ajax Amsterdam nchini Uholanzi, moja ya vituo maarufu zaidi duniani katika ukuzaji wa vipaji vya soka.

MIAKA mitano iliyopita, 2021 ndiyo ulikuwa mwanzo wa jina la Barka Seif kuanza kusikika nje ya Tanzania.

Kijana huyo alipata nafasi ya kushiriki kliniki za vijana za akademi ya Ajax Amsterdam nchini Uholanzi, moja ya vituo maarufu zaidi duniani katika ukuzaji wa vipaji vya soka.

Kwa miongo mingi Ajax imekuwa ikitambulika kama kiwanda cha nyota wa dunia, ikitoa majina makubwa kama Johan Cruyff, Marco van Basten, Dennis Bergkamp, Clarence Seedorf, Wesley Sneijder, Matthijs de Ligt na Frenkie de Jong. Kwa mtoto kutoka Tanzania kupata nafasi katika mazingira hayo tayari ilikuwa hatua kubwa kuelekea ndoto zake wakati huo akiwa na miaka saba, Mwanaspoti ilikuwa ikiripoti kilichokuwa kiendelea huko Ajax. Katika kliniki hizo Barka hakuonekana kama mshiriki wa kawaida. Alionyesha uwezo mkubwa katika mazoezi na michezo ya ushindani kiasi cha kuwavutia makocha na wasaka vipaji waliokuwepo huku akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa kliniki (MVP), kutokana na mchango wake mkubwa uwanjani, akashinda tuzo ya maarifa ya soka (Football Knowledge Award) iliyotolewa kwa mshiriki aliyeonyesha uelewa mkubwa wa mchezo, kabla ya kuhitimisha safari yake kwa kutangazwa kinda bora wa mwaka 2021 wa Ajax Camp ambayo ilikuwa tuzo kubwa zaidi katika programu hiyo. Mafanikio hayo yaliweka msingi wa safari yake ya baadaye na kuanza kuwafanya wengi waamini kuwa alikuwa na kitu tofauti.

BARK 01

GENK NA DARASA LA SAMATTA

Baada ya mafanikio ya Uholanzi, mlango mwingine ukafunguka nchini Ubelgiji baada ya kualikwa na KRC Genk. Kwa Watanzania, Genk ni klabu yenye nafasi maalumu kutokana na historia ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye alifanya makubwa akiwa hapo kabla ya kuhamia Ligi Kuu England.

Kufika Genk kwa Barka kulikuwa ni zaidi ya safari ya kawaida ilikuwa ni fursa ya kujifunza mazingira yaliyomjenga mmoja wa mastaa wakubwa wa Tanzania. Katika kipindi hicho alipata nafasi ya kukutana na Samatta na kushuhudia kwa karibu namna safari ya mchezaji wa Kitanzania inaweza kufika katika kiwango cha juu kabisa barani Ulaya. Kwa kijana aliyekuwa bado anaota kucheza soka la kulipwa, kukutana na mtu aliyepitia njia hiyo kulikuwa kama somo la moja kwa moja la maisha. Ilikuwa ni hatua nyingine iliyoongeza hamasa na imani kwamba ndoto zake zilikuwa zinawezekana kutimia.

BARK 02

KUREJEA TANZANIA

Baada ya kurejea Tanzania, maendeleo ya Barka hayakusimama. Aliendelea kushiriki programu mbalimbali za maendeleo ya vijana huku akifuatiliwa na watu waliokuwa wameanza kuona uwezo wake.

Kadri umri ulivyoongezeka, ndivyo alivyokuwa akiongeza maarifa ya mchezo pamoja na kuboresha uwezo wake kiufundi ambao ulikuwa unatofautiana na wengi wa rika lake.

Kilichowavutia wengi hakikuwa kipaji chake pekee bali pia tabia yake nje ya uwanja. Wale waliowahi kufanya kazi naye walieleza mara kwa mara kuwa alikuwa mtoto mwenye nidhamu, anayesikiliza maelekezo na mwenye utayari mkubwa wa kujifunza.

Katika soka la kisasa, vipaji vinaweza kufungua mlango lakini nidhamu na bidii ndiyo huamua nani ataendelea mbele. Barka alianza kuonyesha sifa hizo mapema sana.

BARK 03

HISPANIA, NCHI YA NDOTO YAKE

Hatua nyingine kubwa ilifika 2022, alipohamia Hispania na kujiunga na Marcet Football University jijini Barcelona. Marcet ni moja ya vituo vinavyotambulika kwa kuendeleza vipaji kutoka mataifa mbalimbali na kuwapa nafasi ya kuingia katika mfumo wa soka la Hispania. Kwa Barka, huu ulikuwa mwanzo wa sura mpya kabisa katika maisha yake ya mpira wa miguu.

Ndani ya Marcet alikutana na ushindani mkubwa kutoka kwa vijana wa mataifa mbalimbali waliokuwa na malengo yanayofanana. Hata hivyo, aliweza kuendana na mazingira hayo na kuendelea kuonyesha ubora wake. Alifunga mabao, alitengeneza nafasi za kufunga na kuendelea kuwashawishi makocha kuwa uwezo wake haukuwa wa bahati mbaya. Kila msimu uliofuata ulimkuta akiwa amepiga hatua mpya katika maendeleo yake.

BARK 04

MWAKA WA KUVUNJA REKODI

Kiwango chake kilipanda zaidi baada ya kujiunga na CF Damm, moja ya akademi zinazoheshimika sana katika eneo la Catalonia. Huko ndipo alipoanza kuandika takwimu zilizowafanya wengi waanze kumtazama kama moja ya vipaji vinavyokuja kwa kasi katika soka la vijana nchini Hispania. Katika mechi 28 za ligi ya vijana, alifanikiwa kufunga mabao 41, rekodi iliyomweka miongoni mwa wafungaji bora wa kundi lake la umri.

Katika msimu huo kulikuwa na michezo kadhaa iliyomweka kwenye vichwa vya habari. Alifunga mabao manne katika ushindi wa mabao 10-1 na katika mchezo mwingine akafunga hat-trick dhidi ya vijana wa Barcelona. Takwimu hizo zilimfanya kutajwa mara kwa mara katika ripoti za vipaji bora vya Catalonia na hatimaye kuchaguliwa katika kikosi bora cha vijana chini ya miaka 12 cha Shirikisho la Soka la Catalonia. Hatua hiyo ilimfanya kuwa mmoja wa Watanzania wachache sana kufikia kiwango hicho katika mfumo wa soka la Hispania.

BARK 05

LA MASIA, KIWANDA CHA NYOTA WA DUNIA

Hatua kubwa zaidi katika safari yake imekuwa kujiunga na mradi wa muda mrefu wa La Masia, akademi maarufu ya FC Barcelona. Kwa zaidi ya miongo minne, La Masia imekuwa ikitajwa kama moja ya vituo bora kabisa vya ukuzaji wa vipaji duniani, ikizalisha majina makubwa kama Lionel Messi, Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Sergio Busquets, Carles Puyol na Lamine Yamal.

Kupata nafasi ndani ya mfumo huo si jambo linalotokea kwa bahati. Ni matokeo ya uchunguzi wa muda mrefu unaofanywa na wataalamu wa maendeleo ya vijana wa Barcelona. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, kiwango alichokionyesha akiwa CF Damm kilitosha kuwashawishi wataalamu hao kumuona kama sehemu ya mradi wao wa baadaye.

Hivyo, safari iliyotoka kwenye viwanja vya Tanzania, ikapitia Ajax, Genk, Marcet na CF Damm, sasa imefika katika kiwanda cha vipaji vikubwa zaidi vya soka duniani.

  • BARK 06

HADITHI BADO HAIJAISHA

Jambo la kuvutia zaidi kuhusu simulizi ya Barka ni kwamba bado yuko mwanzoni mwa safari yake. Bado ni kijana anayejifunza, anayekua na anayejenga msingi wa maisha yake ya soka.

Mafanikio aliyoyapata hadi sasa hayamaanishi amefika mwisho wa safari, bali yanaonyesha kuwa amefungua mlango wa fursa ambazo vijana wengi duniani huziota kwa miaka mingi bila kuzifikia.

Akizungumzia safari ya kijana wake, Seif alisema; ""Kama wazazi na familia kwa ujumla, tuna furaha kubwa kumuona mtoto wetu akipata nafasi hii muhimu sana katika maisha yake ya soka. Ni hatua kubwa ambayo tumeipokea kwa uzito na heshima kubwa kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya ndoto zake. Tunaamini hii ni fursa adhimu kwake kujifunza, kukua na kuendelea kuonyesha uwezo wake katika moja ya mazingira bora zaidi ya ukuzaji wa vipaji duniani."