Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Seif kutoka Bongo hadi mtaa wa kujidai wa Lamine Yamal

SEIF Pict

Muktasari:

  • Mji huo, ambao kwa sasa unatajwa kama kitovu cha uzalishaji wa vipaji vya dunia, umegeuka kuwa mahala pa kutimiza ndoto mpya kwa watoto hao wa familia moja.

NI umbali wa mita chache tu kutoka alikozaliwa na kulelewa nyota mpya wa FC Barcelona, Lamine Yamal, ndipo yalipo maskani ya vijana watatu wa Kitanzania Jabir, Tariq na Barka Seif wanaoishi na kujifunza soka katika akademi za kiwango cha juu huko Hispania.

Mji huo, ambao kwa sasa unatajwa kama kitovu cha uzalishaji wa vipaji vya dunia, umegeuka kuwa mahala pa kutimiza ndoto mpya kwa watoto hao wa familia moja.

Kwa mtu wa kawaida, inaweza kuonekana kama hadithi ya ndoto zisizowezekana, lakini kwa Seif Mpanda, baba wa watoto hao, ndoto hii ni zao la maamuzi magumu, kujitolea na maono ya mbali.

Akiwa mmoja wa Watanzania wachache waliothubutu kuvuka mipaka kwa ajili ya mustakabali wa watoto wao, Seif aliamua kubadili maisha yake yote ili kufanikisha ndoto ya kuwaona watoto wake wakicheza soka la kulipwa Ulaya.

"Ni kweli, tuliamua kuachana na maisha ya anasa. Badala ya kununua magari ya kifahari au kujenga nyumba za kuishi kwenye starehe, kila senti tuliyokuwa nayo tumeielekeza kwa watoto. Ni gharama kubwa, lakini tunaamini ipo siku matunda yatapatikana siyo tu kwa familia yetu, bali kwa taifa pia," anasema Seif.

SEI 01

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Seif anasema mafanikio ya watoto wake hadi sasa ni ishara tosha uwekezaji wa kweli unaweza kuzaa matokeo makubwa.

Kwa sasa, Jabir, mtoto wao wa kwanza, yupo mbioni kusaini mkataba wa kwanza wa kulipwa, hatua inayotazamiwa kufungua milango zaidi kwa ndugu zake.

Seif alishiriki hivi karibuni kikao cha kimkakati kilichoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kilicholenga kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Katika kikao hicho, Seif alipongezwa rasmi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali na alimtaja ni mfano bora wa mzazi anayeelewa thamani ya kuwekeza katika vipaji vya watoto.

Katika familia ya Seif, kila mmoja ana nafasi yake. Mama wa watoto hao kwa sasa anaishi nao Hispania kwa ajili ya kuhakikisha wanapata malezi bora na uangalizi wa karibu.

"Tulikaa mimi na mke wangu na tukakubaliana, yeye akae na watoto huko Hispania, nami nibaki naendelea kufanya kazi ili kufanikisha ndoto yetu ya pamoja."

SEI 02

Kwa sasa, watoto hao wanacheza kwenye akademi mbalimbali Hispania. Jabir na Tariq wapo kwenye timu za Turo, huku Barka ambaye anaonekana kuwa na kipaji cha ajabu licha ya umri wake mdogo wa miaka 11 akichezea akademi ya Damm yenye historia kubwa nchi humo.

Kwa mujibu wa Seif, tayari maskauti kadhaa kutoka klabu kubwa Hispania wameanza kufuatilia maendeleo ya watoto hao.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, Jabir aliweka historia Mei mwaka jana (2024) alipokuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kilichoenda kucheza mechi mbili za kirafiki Saudi Arabia.

Akiwa na umri wa miaka 16 tu, aliweka rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kuvalia jezi ya taifa.

Safari hii ya familia ya Seif ni ushahidi ndoto ya kuwa na kizazi kipya cha wanasoka wa Kitanzania kinachoweza kushindana Ulaya si ya mchana.

SEI 03

Ni jambo linalowezekana kwa wale walio tayari kujitolea, kuacha starehe na kuwekeza kwa moyo wote.


ILIVYOKUWA KWA LAMINE YAMAL

Lamine Yamal alizaliwa Julai 13, 2007, katika Mji wa Esplugues de Llobregat, karibu na Barcelona, akiwa mtoto wa baba mwenye asili ya Morocco na mama kutoka Equatorial Guinea.

Alikulia katika mazingira ya kawaida kabisa ya kihispania, lakini tangu akiwa na umri mdogo, alionyesha kipaji cha kipekee katika kuchezea mpira wa miguu. Wazazi wake walimwona kuwa na shauku isiyo ya kawaida kwa soka na walihakikisha anaingia kwenye timu za watoto mapema kadri walivyoweza.

Akiwa na umri wa miaka saba, Lamine alijiunga na akademi maarufu ya FC Barcelona La Masia. Hapo ndipo hadithi yake ilipoanza kuchukua sura ya kipekee.

SEI 04

Akiwa mdogo kuliko wenzake wengi, aliwashangaza makocha kwa kasi yake, uelewa wa mchezo na uwezo mkubwa wa kudhibiti mpira. Ilifika mahali makocha wa akademi walimchukulia kama mrithi wa wachezaji wakubwa waliopita hapo kama Messi, Iniesta na Xavi.

Kutokana na kiwango chake cha ajabu, alipelekwa kwenye vikosi vya juu vya vijana akiwa bado na umri mdogo. Wakati wenzake walicheza ligi za umri wao, Lamine alikuwa tayari anacheza dhidi ya vijana waliomtangulia kwa miaka miwili hadi mitatu. Hali hiyo ilimkomaza kiuchezaji, huku akiendelea kufundishwa na makocha wa hali ya juu walioamini anaweza kuwa hazina kubwa kwa klabu hiyo.

Mnamo Aprili 2023, akiwa na miaka 15 tu, Lamine Yamal aliitwa kujiunga na kikosi cha kwanza cha FC Barcelona na akawa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuchezeshwa La Liga kwa timu hiyo. Aliingia kama mchezaji wa akiba katika mechi dhidi ya Real Betis na kuacha gumzo kubwa, si tu kwa umri wake, bali kwa namna alivyocheza kwa kujiamini dhidi ya wachezaji wakubwa.

Tangu wakati huo, Yamal ameendelea kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Barcelona, akicheza mechi muhimu za La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pia aliitwa kwenye timu ya taifa ya Hispania akiwa bado kijana mdogo sana, akawa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga bao kwa La Roja. Safari yake kutoka mtaa wa kawaida hadi uwanja wa Camp Nou ni ushahidi tosha kuwa vipaji vikipewa nafasi, vinaweza kuvunja ukuta wowote wa vikwazo.