Ruben Amorim alivyomzidi ujanja Arne Slot
Muktasari:
- Man United ambayo imekuwa na mwanzo mbaya kwenye Ligi Kuu England, ndiyo kwanza ilionekana kujitafuta kabla ya kwenda mapumziko ya mechi za kimataifa wiki mbili zilizopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: RUBEN Amorim ametumia akili kubwa kumzidi ujanja Arne Slot wakati Manchester United ilipoiduwaza Liverpool uwanjani kwao Anfield.
Man United ambayo imekuwa na mwanzo mbaya kwenye Ligi Kuu England, ndiyo kwanza ilionekana kujitafuta kabla ya kwenda mapumziko ya mechi za kimataifa wiki mbili zilizopita.
Kutokuwa na matumaini hafifu sana wakati Man United inakwenda Anfield, uwanja ambao ilikuwa haijaandikisha ushindi kwa karibu muongo mmoja, tangu Wayne Rooney alipofunga bao pekee kwenye ushindi wa ugenini, Januari 2016.
Lakini, mwisho wa mechi, wanaume wa kutoka Manchester ndiyo walioshinda, ikifunga mabao ya kibabe kabisa katika kila kipindi na kushinda mabao 2-1.
Makocha wa timu hizo watakuwa na kitu cha kujifunza kutoka kwenye mechi hiyo ya Jumapili.
AMORIM AMEPATIA MACHAGUO MATATU
Kulikuwa na mabadiliko mawili kutoka kwenye kikosi cha Amorim, huku wachezaji wake watatu aliowachagua walianzisha mjadala mzito. Harry Maguire mara ya mwisho kuanza ilikuwa dhidi ya Brentford, Casemiro alicheza dakika 90 akiwa Brazil kwenye mechi za Korea Kusini na Japan, wakati Matheus Cunha akianza mbele ya Benjamin Sesko.
Kumweka benchi Sesko, mfungaji, kisha unamwaanzisha fowadi mwingine ambaye hajafunga bao ni timu ambazo wengi walimshangaa Amorim. Kocha Amorim alifahamu wazi Liverpool itakuwa imejiandaa kumkabili Sesko, hasa kwenye ile mipira ya juu, ambapo angepata shida mbele ya Virgil van Dijk na Ibrahima Konate.
Lakini, alimwaanzisha Cunha, alifahamu mabeki hao watapata shida kumdhibiti Mbrazili huyo kwenye mipira ya chini, huku akimtumia Casemiro kwenye kuzima mashambulizi ya fowadi ya Liverpool huku Maguire akiongeza safu ya mabeki.
SAPRAIZI KWA SLOT
Kocha Slot aliingia kwenye mchezo huo akiwa amekariri kwamba Man United itakwenda kucheza soka la pasi ndefu kama ambayo walifanya msimu uliopita walipokwenda Anfield.
Lakini, kabla ya mechi kuanza Jumapili, alipigwa sapraizi baada ya kuona straika Sesko hajaanza na Amerim amekuwa na mfumo tofauti wa “5-3-2”. Slot alikariri kwamba Man United itakwenda kucheza 3-4-2-1, lakini ilikuwa tofauti na haraka sana ikaongoza 1-0 ndani ya dakika mbili tu.
Slot alikosea pia alipodhani Mason Mount ataanza kwa kucheza fowadi, lakini baada ya kikosi kutoka, ikaonekana ni Cunha ndiye atakayecheza hapo.
Tofauti na Slot alivyodhani na kwenda kuukabili mchezo huo, mpinzani wake Amorim alichosema kabla ya mecho, kwamba Man United itakwenda kuzungumza ndani ya uwanja.
Kumwondoa Sesko kwenye kikosi kilichoanza kulilipa kwa Man United na miamba hiyo ya Old Trafford ilifanikiwa kuweka mpira chini na kuisumbua Liverpool kwa kufanya mashambulizi makali.
AMAD, MBEUMBO WAMEPIGA KWENYE MSHONO
Amad na Bryan Mbeumo walikuwa na wakati mzuri kwenye upande wa kulia wa Man United, ambao ni kushoto kwa Liverpool. Amad na Mbeumo walikuwa wakigongeana tu na kuipa shida Liverpool kwenye upande huo.
Beki wa kushoto wa Liverpool, Milos Kerkez hakuwa na wakati mzuri. Msimu uliopita, Man United kupitia kwa staa wake Diogo Dalot ililenga upande wa pembeni wa Liverpool kule kwa Trent Alexander-Arnold, ikifahamu wazi kwenye maeneo ya pembeni ya Liverpool ndiko kwenye udhaifu mkubwa linapokuja suala la kukaba.
Na safari hii, Man United iliishambulia Liverpool kwenye upande wake wa kushoto. Kerkez alikuwa kwenye wakati mgumu, lakini Man United ilifahamu wazi, eneo la pembeni ndipo ulipo msono unaoisumbua Liverpool. Ni hayo kwenye maeneo ya pembeni ya Liverpool ndiyo yaliyoiponza timu hiyo ikipoteza mechi nne mfululizo katika michuano yote.
VAN DIJK KUNA KITU HAKIPO SAWA
Liverpool kwenye msimu wake wa hovyo ilipokuwa chini ya Jurgen Klopp ni wakati Virgil van Dijk alipofanya kosa lililomsaidia Jadon Sancho kufunga bao Agosti 2022.
Van Dijk ni mchezaji mahiri, lakini kwa siku za karibuni mambo yake yamekuwa yakienda kombo. Katika mechi dhidi ya Man United, alimtaka mtu, yeyote baina yao kumdhibiti Mbeumo.
Hakukuwa na mtu wa kumdhibiti Mbeumo na kumruhusu afunge bao la kuongoza. Bao hilo lilitokea baada ya Van Dijk kuruka juu kugombea mpira na kumwaangusha mchezaji mwake, Alexis Mac Allister.
Badala ya kutafuta namna ya kwenda kukabiliana na hatari ya mpira huo, Van Dijk alimwaangalia mwamuzi Michael Oliver akimtaka asimamishe mpira. Refa aliona hakukuwa na faulo.
Katika kipindi cha pili, Van Dijk alifanya kosa jingine baada ya kukosea kuokoa mpira, ambao ulikwenda kumgonga usoni Kerkez na nusura uingie kwenye nyavu za Liverpool.
Van Dijk baadaye alionekana akimlalamikia Kerkez kwamba hakufanya mawasiliano. Man United imefunga mabao matatu katika mechi zao 10 zilizopita walipokwenda kucheza Anfield na Van Dijk alikuwa sababu kubwa ya jambo hilo. Lakini, makosa yake hakuna mchezaji yeyote wa Liverpool anaweza kuyalalamikia, wanamlinda.
FOWADI MPYA YA LIVERPOOL IJITAZAME
Mohamed Salah ni kinara wa mabao wa Liverpool kwenye mechi dhidi ya Man United akiwa amefunga mabao 16, lakini kwenye mechi hiyo ya Jumapili alionekana kama hajawahi kufunga dhidi ya wapinzani hao.
Imefika wakati hata mchezaji mahiri wa klabu anakuwa haaminiki, wakati Slot alipoamua kumtoa Salah, wakati Liverpool ikisaka bao la kusawazisha. Kinachoonekana kwa sasa Salah amepoteza njaa ya kufanikiwa zaidi baada ya mkataba mnono.
Liverpool imefanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo la ushambuliaji, ikimsajili Alexander Isak kwa pesa nyingi, lakini wote hao walishindwa kabisa kutamba mbele ya kipa Senne Lammens.
Kipindi cha pili Slot ilimwingiza mshambuliaji mwingine mpya, Hugo Ekitike, ambaye alijaribu kusumbua, akijaribu kuonyesha kile anachoweza kufanya, ambacho hakikuwa na tishio kubwa japo ya kwamba Liverpool ilifanikiwa kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Cody Gakpo. Shida kubwa kwenye fowadi ya Liverpool ya sasa kuna ubinafsi mwingi, tofauti na fowazi zilizopita.