Rekodi nzuri, lakini je ni bondia bora?
Muktasari:
- Hapo ndipo tofauti kati ya kuwa na rekodi nzuri na kuwa bondia bora inapokuwa.Si kwamba rekodi haina maana. Ushindi ndio msingi wa taaluma ya bondia, lakini katika kutafuta ubora idadi ya ushindi hautoshi.
KWENYE ngumi za kulipwa kuna kitu ambacho wakati mwingine kinaweza kumchanganya shabiki. Bondia anaweza kuwa na rekodi nzuri, ushindi wa kutosha na hata idadi kubwa ya KO, lakini ukianza kuichambua safari yake kwa undani, unakutana na maswali amekuwa akiwapiga akina nani?
Hapo ndipo tofauti kati ya kuwa na rekodi nzuri na kuwa bondia bora inapokuwa.Si kwamba rekodi haina maana. Ushindi ndio msingi wa taaluma ya bondia, lakini katika kutafuta ubora idadi ya ushindi hautoshi. Ubora wa wapinzani, mapambano ya mataji, uzoefu wa kimataifa na namna bondia anavyofanya dhidi ya wapinzani wa viwango tofauti, navyo vina nafasi kubwa. Tanzania ina mifano ya kutosha ya kutufanya tujiulize swali hili.
MWAKINYO NA EGGINGTON
Mfano mzuri ni bondia Hassan Mwakinyo. Kwa rekodi yake, ni mmoja wa mabondia bora nchini Tanzania katika kizazi cha sasa, akiwa ameshinda mapambano 25 kati ya 28, huku 18 akishinda kwa knockout (KO) au Technical Knockout (TKO).
Lakini, kinachofanya jina lake likumbukwe zaidi si namba hizo pekee. Ni kile alichokifanya dhidi ya Sam Eggington nchini England mwaka 2018. Mwakinyo alimtwanga Eggington kwa TKO ya raundi ya pili, ushindi ambao ulimpa umaarufu mkubwa kimataifa.
Hapo ndipo kwenye somo lenyewe.Ushindi wa Mwakinyo haukuwa na thamani kwa sababu tu uliingia kwenye rekodi yake. Ulikuwa na uzito kwa sababu ulikuja dhidi ya mpinzani mwenye jina na kwenye uwanja wa mpinzani. Lakini pia historia yake inaonyesha upande mwingine wa kipimo hiki. Baadaye alipanda ulingoni dhidi ya Liam Smith nchini England na kupoteza kwa TKO mwaka 2022. Hilo halifuti ushindi wake dhidi ya Eggington; badala yake linatupa picha pana zaidi ya kiwango chake alipokutana na wapinzani wa madaraja tofauti.
MAJIHA NAYE
Mfano mwingine ni Fadhili Majiha bondia huyo alishinda dhidi ya Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini mwaka 2023 na kutwaa taji la WBC Africa katika uzani wa super bantamweight.
WBC yenyewe ilithibitisha ushindi huo na kueleza kuwa Majiha alidhibiti pambano hilo hadi majaji wote watatu na wote wakampa ushindi.
Hapo tena tunaona tofauti kati ya ushindi wa kawaida na ushindi wenye uzito.Majiha hakuwa anatafuta tu kuongeza pambano moja kwenye rekodi yake; alikuwa akipigania mkanda wa kikanda dhidi ya bondia kutoka nje ya Tanzania.
Zaidi ya hapo, Majiha aliwahi pia kutetea taji hilo dhidi ya Sabelo Ngebiyana wa Afrika Kusini mwaka 2024, akishinda kwa pointi. Hiyo ni aina ya rekodi ambayo inahitaji kutazamwa zaidi ya namba.
Kwa sasa, hata viwango vya WBC vinaonyesha athari ya uzoefu huo. Katika viwango vya Februari 2026, Majiha aliorodheshwa namba 27 duniani katika uzani wa super bantamweight, huku akitajwa kama bingwa wa WBC Africa.
HOJA IPO
Kama rekodi ndiyo kipimo pekee, basi bondia mwenye ushindi mwingi zaidi angekuwa bora moja kwa moja.
Lakini si hivyo.Tuchukulie mabondia wawili; mmoja ana mapambano 20, ameshinda 19, lakini wapinzani wake hawajawahi kufika kwenye mapambano ya ubingwa.
Mwingine ana mapambano 15, ameshinda 11, lakini amekutana mara kadhaa na mabondia wenye viwango vya juu na amewahi kupigania mikanda ya kimataifa. Ni nani bora? Hapo ndipo mjadala unakuwa mgumu.
IBRAHIM CLASS
Mfano mwingine ni Ibrahim Class, ambaye ni mmoja wa mabondia wanaoongoza kimataifa katika kizazi cha sasa. Hapa pia hatuangalii tu nafasi yake kwenye viwango, bali kuangalia safari iliyomfikisha hapo na ubora wa wapinzani aliokutana nao.
Hii ndiyo sababu viwango vya BoxRec, WBC au mashirika mengine vinaweza kuwa sehemu ya uchambuzi, lakini si lazima viwe jibu lote.
Kiwango kinakupa picha ya mahali bondia alipo.
MAPAMBANO MAKUBWA
Kuna bondia anaweza kuwa maarufu Tanzania kwa sababu ameshinda mapambano mengi hapa nyumbani.
Lakini akipewa pambano la kimataifa, dhidi ya mpinzani mwenye uzoefu mkubwa, ndipo tunapata majibu mengine. Je, anaweza kucheza nje ya Tanzania? anaweza kupambana kwenye mazingira ambayo mashabiki wengi wako upande wa mpinzani? Je, anaweza kudhibiti pambano linapokuwa gumu? na anaweza kurudi baada ya kupigwa na kubadilisha mbinu? Haya ndiyo maswali yanayoweza kutenganisha bondia mwenye rekodi nzuri na bondia mwenye kiwango cha juu. Na hapa ndipo mfano wa Mwakinyo dhidi ya Eggington unakuwa muhimu. Ushindi ule uliongeza thamani kwenye jina lake kwa sababu ulifanyika katika mazingira ambayo yalihitaji zaidi ya kushinda pambano la kawaida.
KO SIYO KILA KITU
Pia tusifanye kosa la kuamini kwamba bondia mwenye KO nyingi ndiye bora zaidi. KO ni silaha, lakini ngumi ina mambo mengine. Kuna bondia anayejua kutumia miguu, kudhibiti umbali, kubadilisha kasi na kusoma mpinzani. Anaweza kushinda kwa pointi lakini akawa bondia mwenye uwezo mkubwa wa kiufundi. Ndiyo maana wakati wa kumlinganisha bondia mmoja na mwingine, ni muhimu kuangalia picha nzima.
MIKANDA INABADILI HADHI
Halafu kuna mikanda.Kushinda mkanda wa ndani ni jambo moja. Kushinda ubingwa wa kikanda ni hatua nyingine. Kuufanya mkanda huo uwe sehemu ya safari kuelekea kiwango cha dunia ni jambo kubwa zaidi.
Majiha anatoa mfano mzuri. Alishinda WBC Africa mwaka 2023, akautetea mwaka uliofuata, na akafika kwenye viwango vya juu vya WBC. Hata hivyo, hadithi yake pia inaonyesha kwamba kuufikia mkanda na kuudumisha ni vitu viwili tofauti.
Mwaka 2026, WBC ilimvua Majiha taji lake baada ya kutolitetea kwa muda uliotakiwa. Hilo nalo ni somo kubwa kwa mabondia wa Tanzania.Bondia anaweza kuwa na uwezo wa kushinda mikanda, lakini usimamizi wa taaluma, ratiba ya mapambano na maandalizi ya kutetea taji vinaweza kuamua kama atadumu kileleni.
TUNAWAPIMAJE?
Kocha kutoka Zugo Gym, Selemani Zugo anasema bondia bora kwanza kwa ubora wake lakini pia ubora wa wapinzani anaokutana nao. “Unakuta bondia anapigana chaka tu chaka lakini rekodi zake zipo ameshinda sasa unajiuliza huyo ni bora, bondia mzuri ni yule anayekutana na wapinzani mgumu,” amesema Zugo.
Kwa upande wa Kocha Ramadhan Chorilla anasema bondia anapimwa kwenye mikanda aliyoshinda na kuitetea mwenyewe. “Ndio maana kuna zile rekodi huwa zinabadilika mfano labda Mwakinyo mwaka fulani alikuwa nafasi ya 10 duniani lakini mwaka uliofuata akashuka hiyo inatokana na mwaka huo alifanya nini na aliweza kutetea,” anasema kocha huyo.
Bondia Hussein Azenga anasema kwake bondia mzuri ni yule anayeonyesha kiwango bora katika mapambano ya kimataifa. “Huwezi kuitwa bondia mzuri kama hujapigana nje tena na wapinzani wenye uwezo na viwango tofauti ili wakujue lazima uwe hivyo.”