RAMAJAA: Majaji wanatuuza kwa pesa kidogo
Muktasari:
- Na ndani ya gym hiyo kuna mtu aliyebeba maono makubwa ambaye ni Ramadhani Amani maarufu Ramajaa ni kocha aliyepita kwenye ulingo kama bondia, akafundishwa na mkongwe Mzee Habibu ‘Master’ Kinyogoli na baadaye kurithi mikoba yake ya ukocha.
UKITAKA kujua maana halisi ya chuo cha ngumi za kulipwa nchini Tanzania, huna haja ya kutafuta tiketi ya kwenda nchini Mexico au Las Vegas, Marekani we katiza tu hadi mitaa ya Mabibo, jijini Dar es Salaam, mahali ambapo klabu maarufu ya Naccoz Gym imeweka makazi yake.
Na ndani ya gym hiyo kuna mtu aliyebeba maono makubwa ambaye ni Ramadhani Amani maarufu Ramajaa ni kocha aliyepita kwenye ulingo kama bondia, akafundishwa na mkongwe Mzee Habibu ‘Master’ Kinyogoli na baadaye kurithi mikoba yake ya ukocha.
Safari yake ilianza mwaka 1986 akiwa mtoto, kabla ya kucheza katika timu mbalimbali zikiwemo Simba, Redline, Urafiki, Kanuni na Yanga Boxing. Leo anajivunia kuwa amefundisha mabondia wengi na kuzalisha pia makocha wanaoendelea na kazi hiyo.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo, Mwanaspoti limezungumza na kocha huyo ambaye anafunguka mengi kuhusu hali ya ngumi Tanzania, kuanzia nidhamu ya mabondia, maandalizi ya kiafya, uhaba wa mapromota na wadhamini hadi kile anachodai kuwa ni baadhi ya majaji kuathiri matokeo ya mapambano.
MAJAJI CHANGAMOTO
Lakini linapokuja suala la maendeleo ya ngumi Tanzania, Ramajaa anadai baadhi ya majaji na viongozi wamekuwa wakifanya mambo yanayoweza kuathiri haki ya mabondia.
“Haki haitendeki kwenye ngumi zetu. Bondia anafanya mazoezi makali, anashinda pambano lakini ushindi anapewa mwingine,” anasema.
Ramajaa anasema hali hiyo inaweza kuwa na madhara kwa mabondia wanapokwenda kupambana nje ya nchi kwa sababu wanakuwa wamezoea kupata ushindi wa nyumbani ambao hauendani na uwezo wao halisi na wakikutana kimataifa ndio wanashindwa kufurukuta na kutoa sababu nyingi.
“Hiyo mbeleko ndiyo inayotuponza tukieda kwenye mechi za kimataifa, maana mabondia wanapigwa vibaya sana kwa sababu wamezoea kubebwa nyumbani.”
CHANZO VIFO VYA MABONDIA
Ramajaa pia ametaja ugonjwa wa malaria kama adui mkuu wa mabondia nchini, akitolea mfano wa kifo cha aliyekuwa Bingwa wa Afrika, Fadhili Awadhi Chui, aliyefariki dunia miaka sita iliyopita baada ya malaria iliyojificha kumshambulia akiwa mazoezini.
Anasisitiza pia umuhimu wa mabondia kufanya vipimo vya afya (checkup) mara kwa mara na baada ya mapambano badala ya kusubiri siku ya pambano pekee
“Wenzetu nje wanafanya sana labda kwa sababu ya pesa wanazopata lakini hapa nyumbani mtu akimaliza pambano akishakula hela yake ndio basi tena anakwenda nyumbani kulala bila kucheki kichwa kama kimeharibika sehemu,”anasema Ramajaa na kuongeza
“Ukipima inakuwa rahisi kujua kuna shida sehemu fulani sio kusubiri pambano lingine ndio uanze kupimwa sio kweli.”
KINYOGOLI ALIMPA MIKOBA
Ramajaa anamtaja Master Kinyogoli kama mtu aliyekuwa na nafasi kubwa katika maisha yake ya ngumi.
Anasema alikutana naye akiwa kwenye hatua za mwanzo za mchezo huo na kufundishwa wakati akiwa sehemu ya Simba Boxing Team, kabla ya safari yao kuendelea Redline Railway.
“Mwalimu wangu ni Master Kinyogoli. Alitulea tukiwa Simba Boxing Team kabla hatujahamia Redline Railway.”
Anasema enzi hizo alikuwa akishirikiana na mabondia wakubwa waliokuwa wakitamba miongoni mwao ni Stan Mabes, Ninja, Beca Mariego, Ernest Bujiku na Rashid Matumla.
Baada ya kucheza katika timu kadhaa, Ramajaa aligeukia ukocha na kuanza kujenga kizazi chake cha mabondia.
Kwa sasa anasema amefundisha zaidi ya wanafunzi 1,000 na kwamba Naccoz ina vituo katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Mbeya, Morogoro na Mbezi, Dar es Salaam.
IBADA KWANZAA
Ramajaa anasema nidhamu na imani ni sehemu ya msingi wa malezi anayowapa mabondia wake.
Anasema kila Jumatatu huwa anawakumbusha wanafunzi wake kuhusu wajibu wao wa kidini na kuwaondoa kwenye tabia anazoziona zinaweza kuwaharibia maisha.
“Jumatatu ikifika tunaulizana, jana Jumapili mlifanya ibada nyinyi Wakristo? Waislamu je, mnasimamisha swala tano? Mabondia wangu wote wanatakiwa waache mambo ya kihuni kwa sababu mchezo huu ukitumbukiza na mambo ya ajabu huwezi kutoboa,” anasema.
Ramajaa pia anasema katika kambi yao iliyopo Mbezi wanaendelea na ujenzi wa msikiti, akisisitiza kuwa kwake ibada ni muhimu zaidi kuliko mafanikio ya ulingoni.
AMEZALISHA WABABE, MAKOCHA
Miongoni mwa mabondia waliopita mikononi mwake anawataja Omar Ramadhani, Raja Bungemba, marehemu Liston na Doto Kipenga.
Omar Ramadhani, kwa mujibu wa Ramajaa, aliwahi kupigania mataji ya IBF na WBC nchini Ujerumani.
Hata hivyo, kazi yake haijaishia kwa mabondia pekee. Anaongeza pia amewahi kumfundisha Batman, kocha wa Timu ya Taifa ya Ngumi, pamoja na Kocha Ramadhan Cholila wa Cholila Boxing.
“Ni faraja kuona nimezalisha mabondia wengi na makocha kiufupi ngumi inatawala, mabindia kama Mfaume Mfaume, Oscar Richard, Fabian Limo ‘Lampard’, ambaye kwa sasa anaishi Marekani hayo ni baadhi ya matunda yaliyotoka mikononi mwangu lakini wako wengi.”
SIRI YAKE
Ramajaa anasema siri mojawapo ya kazi yake ni kutowafundisha mabondia wote kwa mfumo mmoja.
Anaamini kila bondia ana uwezo wake na udhaifu wake, hivyo kocha anatakiwa kuangalia sifa za bondia kabla ya kumpa mbinu za kutumia ulingoni.
Anataja mbinu kama kupiga body punch, ducking, boping pamoja na kutumia mkono wa kushoto au kulia kulingana na uwezo wa bondia.
Pia anasema kabla ya pambano huwapa mabondia wake maelekezo ya kufuata raundi kwa raundi na kuwaweka tayari kisaikolojia.
“Siri mojawapo ya kazi yangu ni kutowafundisha mabondia wote kwa mfumo mmoja. Kuna anayefaa kutumia body punch, mwingine ducking au bobbing, na wengine kutumia zaidi mkono wa kushoto au kulia.”
LISHE YA MABONDIA
Eneo lingine ambalo Ramajaa analipa uzito ni lishe ya mabondia.
Anasema mabondia wanahitaji protini, mboga za majani na matunda, huku akitaja bamia, nyanya chungu, mchicha na kabichi miongoni mwa vyakula anavyovipa uzito.
Pia anawashauri kutumia nyama nyeupe kama kuku na samaki, huku akipunguza ulaji wa nyama nyekundu na wanga kwa wingi.
Ramajaa anasema kwa uzoefu wake, bondia anatakiwa pia kunywa maji salama na kuzingatia afya yake hata akiwa hana pambano.
MAPROMOTA WACHACHE
Ramajaa pia anagusa suala la mapambano machache kwa mabondia na kusema Tanzania bado inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye mchezo huo.
Kocha huyo anasema bondia anahitaji kupata mapambano ya kutosha ili kuendelea kukua, akitoa mfano wa mabondia waliokuwa wakipigana mara nyingi katika vipindi vyao vya mafanikio.
“Ndio maana tunaulizana kwanini bondia fulani kashuka kiwango kimataifa sababu ya kucheza mapambano machache, ili uweze kuwa top lazima upigane angalau mapambano 10 hadi 15 kwa mwaka.”
NGUMI ZIMEMPA MAGARI, NYUMBA
Kwa wale wanaoona ukocha wa ngumi kama kazi isiyokuwa na faida, Ramajaa ana mtazamo tofauti.
Anasema mafanikio yake ya maisha yametokana kwa kiasi kikubwa na kazi hiyo, hasa kutokana na kuwa na mabondia wengi wanaopigana ndani na nje ya nchi.
“Ukocha unalipa ukiwa na mabondia wengi wanaokwenda Ulaya na kurudi na fedha za kigeni lazima na kocha utapata sasa wewe una mabondia wawili au watatu utategemea kupata pesa,” anasema.
Anawataja baadhi ya mabondia aliowahi kufanya nao kazi akiwemo Halima Vunja Bei, Pius Mpenda, Oscar Richard na Mfaume Mfaume.
Ramajaa anasema mafanikio hayo yamemwezesha kujenga nyumba jijini Dar es Salaam na kumiliki magari karibu sita ikiwemo daladala, akisisitiza kuwa ngumi kwake si mchezo tu bali ni sehemu ya maisha yake.