Ramadhani Brothers watingisha Australia
Muktasari:
- Ndugu hao, Fadhili Rashidi na Ibrahim Mwaimise, wameingia kwenye orodha ya wasanii wa kimataifa wanaotoa burudani katika tamasha hilo linalofanyika Sydney Lyric Theatre, moja ya kumbi kubwa za maonyesho nchini Australia.
KAMA kuna kitu ambacho Ramadhani Brothers wamekifanya kwa miaka ya hivi karibuni ni kugeuza sarakasi kutoka kuwa kipaji cha Tanzania na kuwa bidhaa inayotazamwa kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa, safari yao ikiwa imefika tena Australia ambako sasa wanatikisa jukwaa la Sydney kupitia tamasha kubwa la Cirque Alice.
Ndugu hao, Fadhili Rashidi na Ibrahim Mwaimise, wameingia kwenye orodha ya wasanii wa kimataifa wanaotoa burudani katika tamasha hilo linalofanyika Sydney Lyric Theatre, moja ya kumbi kubwa za maonyesho nchini Australia.
Na safari hii hawapo tu kama wageni wa kawaida. Wamepewa nafasi ya kuwa The Knights, wakitumia silaha yao kubwa ambayo imewafanya watambulike duniani uwezo wa kunganisha miili yao kwa kutumia vichwa, nguvu na usahihi ambao umekuwa alama yao kwenye majukwaa mbalimbali.
Cirque Alice ni tamasha linalochukua msukumo kutoka simulizi maarufu ya Alice’s Adventures in Wonderland la Lewis Carroll, likichanganya sarakasi, dansi, muziki na komedi.
Kwa upande wa Sydney, tamasha hilo lilianza Septemba 25 na limepangwa kuendelea hadi Oktoba 11, 2026 siku moja baada ya kupigwa kwa dabi ya Kariakoo, likiwa na maonyesho ya mchana na usiku katika siku kadhaa za wiki.
WATANZANIA WAWILI WABEBE SHOW
Kinachowafanya Ramadhani Brothers kuwa habari kubwa ndani ya tamasha hilo ni aina ya sarakasi wanayoifanya.
Katika sehemu yao, Fadhili na Ibrahim wanatumia nguvu, balansi na kuaminiana kwa kiwango cha juu, huku wakifanya matukio ambayo kwa mtazamaji wa kawaida yanaonekana kama yanaenda kinyume na uwezo wa mwili wa binadamu.
Mapitio ya Musical Theatre Australia yamewataja Ramadhani Brothers kama “absolute highlight†ya tamasha hilo, likieleza kuwa walitoa burudani iliyokuwa miongoni mwa nyakati zilizokumbukwa zaidi na watazamaji.
Mapitio mengine ya State of the Art Media nayo yamewatenga wawili hao kama moja ya sehemu zilizovutia zaidi, yakisisitiza namna walivyoonyesha nguvu na balansi katika sehemu ya mwisho ya show.
Hiyo inaonyesha kwamba Tanzania haipo tu kwenye bango la wasanii wa Cirque Alice, bali ina wawakilishi wawili ambao wamekuwa sehemu ya kile wachambuzi wa sanaa nchini Australia wanachokiona kama kivutio cha tamasha hilo.
HEAD-TO-HEAD YAWASHTUA WATAZAMAJI
Katika moja ya sehemu zao maarufu, Ramadhani Brothers wanafanya kile ambacho ni ngumu kuamini kupitia vichwa vyao mmoja anasimama na mwingine anakaa juu ya kichwa cha mwingine bila kushika sehemu yoyote huku miili yao ikitegemeana katika mikao inayohitaji nguvu na umakini mkubwa.
The Plus Ones imeeleza kitendo chao kama moja ya nyakati zilizowafanya watazamaji kupigwa na butwaa, huku ikiangazia namna wawili hao wanavyoweza kuwa na balansi ya miili yao.
Mapitio ya Australian Stage nayo yanaeleza namna onyesho lao linavyowafanya watazamaji kushikilia pumzi, likisema walifanya kile kilichoonekana kama ‘headstand duel’ huku nguvu, ushindani na kuaminiana vikionekana kupitia kitendo hicho.
Hapa ndipo ukubwa wa kazi yao unapojitokeza. Kwa mtazamaji, sekunde chache za kusimama kupitia vichwa vyao mmoja juu ya mwingine ilionekana kuwa rahisi lakini kwa wasanii hao ni matokeo ya mazoezi ya muda mrefu, nidhamu ya mwili na uwezo wa kuaminiana wakati kila kosa linaweza kuharibu mpangilio mzima wa kitendo.
HATA MAKOSA YAMEKUWA SEHEMU YA SHOW
Katika moja ya maonyesho hayo, Ibrahim alikosea hatua moja, tukio ambalo liliwakumbusha watazamaji kuwa licha ya kuonekana kama wanafanya jambo lisilowezekana, bado ni binadamu wanaofanya vitendo vinavyohitaji umakini mkubwa.
Jambo hilo limeongeza pia uhalisia wa maonyesho yao kwa sababu hakuna kinachoweza kuondoa kabisa hatari iliyopo kwenye sarakasi za aina hiyo.
Kila hatua, mkao na mabadiliko ya mwili yanahitaji muda sahihi. Ndiyo maana Ramadhani Brothers wanapokuwa jukwaani, sehemu kubwa ya mvuto si tu kile wanachokifanya, bali pia swali la watazamaji: Watawezaje kufanya hivi bila kuanguka?
Hata hivyo hakuna madhara ambayo yalitokea na badala yake waliendelea kutoa burudani.
SHOW YA MAMILIONI
Lakini nyuma ya burudani hiyo kuna biashara kubwa. Cirque Alice inafanyika katika Sydney Lyric Theatre, ukumbi ambao unaweza kubadilishwa kuwa na uwezo wa kuchukua kati ya viti 1,350 hadi 2,000, kulingana na mpangilio wa show.
Kwa upande wa tiketi, bei rasmi za Cirque Alice Sydney zimetajwa kuwa kati ya Dola za Australia 69 na 149, sawa na takribani Sh126,000 hadi Sh272,000 kwa kutumia kiwango cha karibu Sh1,822 kwa Dola moja ya Australia cha Oktoba 4, 2026.
Hivyo, ukubwa wa biashara hiyo sio mchezo mabilioni ya fedha yametengenezwa. Kwa mfano, kama ukumbi ungejaa kwa wastani wa watu 1,500 kwa kila moja ya maonyesho 21 yaliyopangwa Sydney na wastani wa tiketi ukawa Dola 100 za Australia, mapato ya tiketi pekee yangekuwa karibu Dola 3.15 milioni za Australia kwa fedha za Tanzania, hiyo ni zaidi ya Sh5.7 bilioni.
Lakini hiyo ni hesabu ya mfano wa mapato ya tiketi ya show, si fedha ambazo Ramadhani Brothers wamepewa.
Kwa sababu gharama za uzalishaji, ukumbi, wafanyakazi, usafiri, matangazo, kodi, tiketi na malipo ya wasanii hukatwa kabla ya kubaki faida ya waandaaji.
RAMADHANI BROTHERS WANAWEZA KUVUNA KIASI GANI?
Kwa sasa, hakuna takwimu rasmi ya mkataba wa Fadhili na Ibrahim kwa Cirque Alice iliyowekwa wazi hadharani. Hivyo, haiwezekani kusema kwa uhakika kwamba wamepewa Dola fulani kwa shoo, kwa wiki au kwa ziara nzima.
Katika uzalishaji wa kimataifa wa aina hii, wasanii wanaweza kulipwa kwa mfumo tofauti mshahara wa kipindi fulani, malipo kwa kila onyesho, mkataba wa ziara au makubaliano mengine ya uzalishaji.
Kwa hiyo, kiasi wanachoweza kuweka mfukoni kinaweza kuwa tofauti kabisa na mapato ya tiketi ya show lakini kitu kimoja kiko wazi thamani yao ya kibiashara imeongezeka.
Kushiriki katika uzalishaji unaouzwa katika ukumbi wenye uwezo wa karibu watu 2,000, pamoja na kupewa nafasi ya kutajwa na wachambuzin kama moja ya sehemu bora za show, kunaongeza thamani ya jina la Ramadhani Brothers kwenye soko la kimataifa la sarakasi.
SI SYDNEY PEKEE
Safari ya Cirque Alice haishii Australia.
Taarifa za uzalishaji huo zinaonyesha kuwa baada ya vituo vya Australia, show imepangwa kuendelea na safari yake ya kimataifa, ikiwemo Manila na London.
Hii inaweza kuwa habari kubwa zaidi kwa Ramadhani Brothers kwa sababu kila mji mpya una maana ya soko jipya, watazamaji wapya na uwezekano wa kuendelea kuonekana kwenye uzalishaji mwingine wa kimataifa.
Kwa wasanii wa aina yao, thamani kubwa wakati mwingine haipo kwenye malipo ya show moja pekee, bali kwenye kile kinachokuja baada ya watu wenye ushawishi ndani ya tasnia kuwaona wakifanya kazi.
TANZANIA YABAKI KWENYE RAMANI
Jina la Ramadhani Brothers sasa limekuwa zaidi ya jina la ndugu wawili wanaofanya sarakasi. Ni moja ya mifano ya Watanzania ambao wameweza kutumia kipaji cha ndani na kukifikisha kwenye soko la kimataifa.
Katika Cirque Alice, wanakutana na wasanii kutoka sehemu mbalimbali duniani, lakini mapitio ya Australia yameendelea kuwatenga kama miongoni mwa vivutio vinavyobeba shoo hiyo.
Na hapo ndipo mafanikio yao yanapokuwa na maana nyingine kwa Tanzania.
Wakati nchi nyingi zikitafuta njia za kuuza vipaji vyao nje kupitia muziki, filamu na michezo, Ramadhani Brothers wanaonyesha kwamba hata sarakasi inaweza kuwa bidhaa ya kimataifa ikiwa kipaji kitaandaliwa, kikiendelezwa na kupewa nafasi.
Kwa sasa, macho yao yako Sydney hadi Oktoba 11, lakini kwa kuangalia ratiba ya Cirque Alice, safari hiyo inaonekana kuwa sehemu tu ya ukurasa mwingine katika maisha yao ya kimataifa.