Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PUMZI YA MOTO: Kizungumkuti kitambaa cha unahodha Azam FC

Ijumaa ya Julai 14 mwaka huu Azam FC ilicheza mechi ya kirafiki na Al Hilal ya Sudan huko Tunisia. Katika mchezo huo, kitambaa cha unahodha kilivaliwa na Idris Mbombo ilhali Sospter Bajana akiwemo.
Nyota hao wawili walianza pamoja katika mchezo huo na walitolewa pamoja baada ya kipindi cha kwanza. Lakini Sospeter Bajana ambaye ndiyo alitarajiwa kuwa nahodha mkuu msimu huu, hakuvaa kitambaa.
Itakumbukwa kwamba msimu uliopita nahodha wa Azam FC alikuwa Agrey Moris ambaye alistaafu katikati ya msimu, na kumuachia Bruce Kangwa akisaidiwa na Bajana. Kuondoka kwa Kangwa kukaashiria kwamba Bajana anaenda kuwa nahodha mkuu moja kwa moja msimu mpya wa 2023/24. Lakini kilichotokea kwenye mchezo huo ndicho kinacholeta mjadala huu.
Kwanini Mbombo avae kitambaa katika mchezo ambao Bajana yumo? Au kocha Yousouph Dabo hajapata mtu sahihi anayedhani anafaa kubeba majukumu ya kuwaongoza wenzake? Bajana aliteuliwa kwa mara ya kwanza na kocha George Lwandamina kuwa nahodha  baada ya kusimamishwa kwa manahodha wa wakati huo; Agrey Moris, Mudathir Yahya na Salum Abubakary 'Sure Boy'.

Hii ilikuwa mwanzoni mwa msimu wa 2021/22 wakati Azam FC ikishiriki Kombe la Shirikisho la CAF. Manahodha hao waliingia mgogoro baada ya michezo miwili dhidi ya Horseed FC ya Somalia. Baada ya hapo Azam FC ikakutana na Pyramids ya Misri na Bajana akavaa kitambaa. Aliendelea kuvaa kitambaa hicho hadi Agrey Moris alipomaliza matatizo yake na klabu na kurudi rasmi.

Bajana akageuka na kuwa nahodha msaidizi nyuma ya Agrey na Mudathir, akichukua nafasi ya Salum Abubakary ambaye alikataa kurudi. Lakini baada ya msimu kumalizika, Mudathir naye akaondoka na nafasi yake ya usaidizi kuchukuliwa na Bruce Kangwa. Kwa hiyo msimu wa 2022/23 ulianza na Agrey Moris kama nahodha mkuu, Bruce Kangwa msaidizi namba moja na Sospeter Bajana msaidizi namba tatu.

Kuondoka kwa Agrey Moris na Bruce Kangwa kukatoa dalili kwamba Bajana atakuwa nahodha mkuu kwa msimu mpya wa 2023/24. Lakini hadi sasa kocha mkuu Yousouph Dabo hajatangaza nani atakuwa nahodha wake na kwa kile kinachoendelea kunatia picha tofauti. Haitashangaza kama kocha Dabo atamchagua Idris Mbombo kuwa nahodha mkuu ukizingatia uzoefu na mawasiliano.

Mbombo alikuwa nahodha wa Nkana FC ya Zambia, timu kubwa sana kuliko Azam FC. Kwa hiyo anato historia ya kuvaa kitambaa hicho. Ameshacheza soka sehemu mbalimbali ikiwemo kwao DRC, Zambia, Sudan, Saudi Arabia na Misri. Lakini pia anaongea lugha nyingi; Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa.
Na hizi ndizo lugha ambazo zinatumika ndani ya chumba cha kubadilishia cha Azam FC. Kwa hiyo kuwa na kiongozi ambaye ataweza kuwasiliana na wenzake wote Kwa kauli yake ni jambo jema. Na hii ndiyo kanuni aliyoitumia kocha wa Newcastle United, Sam Allardyce 'Big Sam' mwaka 2007.

Kocha huyo alimteua nyota wa Cameroon, Geremi Njitap, aliyejiunga na timu hiyo akitokea Chelsea. Chumba cha kubadilishia nguo cha Newcastle United wakati huo kilijaa wachezaji wanaozungumza kiingereza, Kifaransa na Kihispaniola, lugha ambazo Njitap alikuwa akizimudu barabara.
Kwa hiyo siyo ajabu ikitokea Dabo akampa jumla kitambaa Mbombo. Lakini ukiacha Bajana na Mbombo, nyota wengine wanaoweza kuwa manahodha wa Azam FC ni kama ifiatavyo.


1. Malickou Ndoye
Alikuwa nahodha msaidizi wa Tengueth FC chini ya kocha huyu huyu Yousouph Dabo. Maana yake anaweza kuwa nahodha ukizingatia atakuwa anafanya kazi chini ya kocha ambaye anamfahamu na anaweza kurahisisha mawasiliano kwa sababu anajua Kifaransa na Kiingereza.


2. Daniel Amoah
Amekuwa akivaa kitambaa cha unahodha mara kadhaa kutoka na ukongwe wake ndani ya timu. Alijiunga na Azam FC mwaka 2017, miaka SITA iliyopita, ikimaanisha anajua vizuri klabu na anaweza kuongoza njia. Tatizo lake pekee ni mawasiliano. Hajui vizuri kiingereza na hajui kabisa Kifaransa huku Kiswahili akiongea maneno machache sana.


3. Abdallah Kheri Sebo
Baada ya Bajana, huyu ndiyo mchezaji anayefuata kwa ukongwe ndani ya Azam FC. Alijiunga na timu hiyo mwaka 2015 akitokea Zimamoto ya Zanzibar akiwa na miaka chini ya 17. Kukaa kwake kwa muda mrefu klabuni kunaweza kuwa msaada kuwaongoza wengine lakini tatizo lake ni mawasiliano... kiingereza kinamopiga chenga.


4. James Akaminko
Anazo sifa nyingi za kuwa kiongozi wa wenzake uwanjani, lakini Hana sifa hizo nje ya uwanja. Uwanjani Akaminko huwa hataki utani, anaweza kumfokea yeyote wakati wowote kama hatekelezi majukumu yake ya msingi. Lakini nje ya uwanja Akaminko siyo mchezaji wa kitimu. Anapenda kujitenga tenga jambo ambalo hapaswi kuwa nalo kiongozi.


5. Ali Ahamada
Mzoefu wa soka la daraja la juu na mchezaji anayejitambua sana. Alichojifunza katika daraja la juu kama logo ya Ufaransa hata timu ya taifa ya vijana ya Ufaransa kinaweza kuwa msaada mkubwa. Anajua Kiingereza na Kifaransa kama silaha kwa mawasiliano. Tatizo lake ni kwamba hana uhakika  wa namba kikosini. Lakini hata hivyo, kuwa nahodha siyo jambo la dakika 90 bali maisha yote ya klabuni.
Kocha Dabo anawajua zaidi wachezaji wake na anaweza kuteua mmoja. Lakini hadi sasa hali bado kizungumkuti.