Pogba anakula bata, lakini ana siri nzito
Muktasari:
- Pogba anatembea kando ya eneo la ukuta wa gereji za timu katika mzunguko wa Marina Bay Street Circuit, nchini Singapore.
PARIS, UFARANSA: PAUL Pogba yupo katika hali ya sintofahamu. Bado anatafakari hatua inayofuata baada ya kuondoka Monaco kwa kushtukiza, huku nyota huyo wa zamani wa Man United akiitaka Man City irudishe mataji mawili ya Ligi Kuu England anayoamini chama lake lilibeba wakati akilichezea.
Inaanzaje? Sikia! Pogba anatembea kando ya eneo la ukuta wa gereji za timu katika mzunguko wa Marina Bay Street Circuit, nchini Singapore. Waandishi wa habari wanaanza kumzunguka, na muda mfupi baadaye, suala la Man City kupatikana na hatia linaibuka, Mfaransa huyo anatabasamu kwa kejeli, anainua mkono wake na kujibu, “Kwa hakika sina la kusema.”
MAN UNITED MOYONI?
Hata hivyo, Pogba ana jambo la kusema. Miaka minne inaweza kuwa imepita tangu kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 alipokuwa mara ya mwisho akichuana na Manchester City akiwa na wapinzani wao wakubwa, Manchester United, lakini bado ana maslahi katika matokeo ya rufaa ya klabu hiyo dhidi ya hukumu iliyotolewa kuhusiana na mashtaka 114 ya Ligi Kuu England.
“Natumaini tu kwamba hali hii haitaathiri Ligi Kuu England. Natumaini tunaweza kurejeshewa mataji mawili.” Pogba aliwahi kuwa mtu muhimu zaidi ndani ya United, akiwa mhimili mkuu katika timu mbili zilizokabiliana vikali na City wakati wapinzani hao walipokuwa katika ubora wao wa hali ya juu. Hata hivyo, katika matukio yote mawili, alijikuta upande ulioshindwa dhidi ya timu hiyo iliyokuwa ikitawala, huku Mashetani Wekundu wakimaliza nafasi ya pili nyuma ya wapinzani wao katika misimu ya 2017/18 na 2020/21.
Ni msimu mmoja tu kati ya hiyo miwili ambayo United ilikaribia kutwaa ubingwa, yaani 2017/18, ulioangukia katika kipindi ambacho City ilibainika kutumia mikataba na makubaliano ya udanganyifu ili kupotosha hesabu zake za kifedha kwa takribani Pauni 900 milioni.
Kwa hiyo, adhabu yoyote ambayo City inaweza kupewa, ikiwa itakuwepo, ina maana kwamba Pogba huenda akaishia kuota tu ndoto ya kurejeshewa taji moja la Ligi Kuu England.
BATA TU
Badala ya kuonyesha ufundi wake uwanjani, sasa anaishi maisha ya kifahari kwa kuhudhuria mashindano ya magari ya Formula One (F1), kama alivyofanya nchini Singapore alikoulizwa kuhusu City, pamoja na maonyesho ya mitindo katika baadhi ya majiji makubwa duniani. Pogba alihudhuria tukio kama hilo katika taifa hilo la kisiwa barani Asia kwa mwaliko wa mdhamini wake wa muda mrefu, Adidas, ambaye amekuwa akishirikiana naye kwa zaidi ya muongo mmoja. Tukio hilo lilifuatia kuhudhuria kwake pamoja na mkewe, Zulay, kwenye hafla ya The Business of Fashion 500 Gala iliyofanyika Paris.
Mara kwa mara Pogba amekuwa akionyesha chaguo lake la mavazi yenye mvuto wa kipekee nje ya shughuli zake za soka, baadhi yakiwa ya kuvutia na mengine yakizua maswali. Pia ana chapa yake mwenyewe ya mavazi. Chapa hiyo, inayoitwa POGBA MDXCIII” MDXCIII ikiwa ni namba 1593 kwa tarakimu za Kirumi, ambayo huenda ikarejerea tarehe yake ya kuzaliwa, Machi 15, 1993, ilizinduliwa Oktoba, mwaka jana.
Nyota huyo anaishi maisha ya kifahari na yenye matumizi makubwa ya fedha. Ikiwa akiamua kuachana kabisa na soka atakosa fursa nyingine za kujishughulisha nazo. Hata hivyo, hajatoa ishara yoyote kwamba anapanga kutundika daruga.
ENZI ZAKE
Kiungo huyo, ambaye wakati mmoja alihesabiwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi duniani, alikuwa akijaribu kufufua upya taaluma yake aliposaini mkataba wa awali wa miaka miwili na Monaco. Alishindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya kuthibitishwa kwa uhamisho huo, ambao ulikuwa hatua yake ya kwanza kuelekea kujijenga upya baada ya kutumikia adhabu ya miezi 18 ya kujihusisha na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.
Mchezo wake wa kwanza kwa klabu hiyo ulikuja baada ya siku 808 tangu alipovaa viatu vya kuchezea kwa mara ya mwisho akiwa na klabu yake ya awali, Juventus. Kipindi hicho kirefu kilitokana na adhabu ya kusimamishwa kwa miaka minne aliyokuwa amepatiwa awali alipokuwa katika klabu hiyo ya Italia baada ya vipimo kubaini uwepo wa dawa iliyopigwa marufuku iitwayo DHEA. Adhabu hiyo ilimfanya moja ya majina makubwa katika soka duniani kutoweka kwa muda mrefu kwenye ramani ya mchezo huo.
Pogba alikuwa amekiri Juventus kwamba alitumia virutubisho vya lishe alivyopewa na daktari mmoja anayeishi Miami. Hata hivyo, alidai hakujua kama vilikuwa na testosterone, hali iliyosababisha adhabu yake.
Katika mwaka uliofuata, nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Juventus aliishi maisha yasiyo na kelele nyingi, akijiepusha kuonekana sana hadharani. Hali hiyo iliendelea hadi Oktoba 2024, wakati adhabu yake ilipopunguzwa na kuwa miezi 18. Kutoka katika kipindi hicho cha giza, Pogba alianza kuona mwanga wa matumaini.
Kupunguzwa kwa adhabu hiyo kulimruhusu Pogba kurejea katika soka la kulipwa, jambo alilolifanya kwa kujiunga na Monaco. Hata hivyo, baada ya kucheza mechi sita pekee katika msimu mmoja akiwa na klabu hiyo, huku akilipwa Pauni 44,000 kwa wiki, mkataba wake ulisitishwa kabla ya muda wake. Baada ya yote aliyopitia, sasa amejikuta akianza upya, na inaonekana huenda asiendelee na maisha yake ya soka Ulaya, wala kuhamia Saudi Arabia. Hata hivyo, Ligi Kuu Marekani (MLS) inaonekana kuwa ndilo chaguo lenye uwezekano mkubwa kwa sasa.
Daily Mail Sport inaelewa kuwa Pogba alipelekwa katika timu mbalimbali zinazoshiriki ligi hiyo mwezi Agosti, mwaka huu ili kuangalia uwezekano wa kujiunga nazo. Maslahi ilikuwa ishu kubwa kwake. Inaelezwa kwamba awali alifanya mazungumzo na DC United, huku Inter Miami ya David Beckham ambako Lionel Messi anacheza nayo ikiwahi kuhusishwa na kiungo huyo.
Pia kumekuwapo na uvumi kuhusu uwezekano wa kuanza maisha mapya katika jiji la New York, huku Pogba akihusishwa na New York City. Hiyo ndiyo klabu ambayo Frank Lampard alijiunga nayo kumalizia maisha yake ya soka baada ya kipindi cha miaka 13 kilichojaa mataji akiwa Chelsea.
Hata hivyo, hadi sasa Pogba hajafanya mazungumzo yoyote ya kina na klabu inayotaka kumsajili.
MSAADA KWA WENGINE
Wakati uvumi kuhusu mustakabali wake ukiendelea kusambaa, Pogba, ambaye alicheza vipindi viwili tofauti akiwa Manchester United akiichezea zaidi ya mechi 230, akifunga mabao 39 na asisti 51, anawasaidia wachezaji wanaopitia njia aliyowahi kupitia akiwa Manchester.
Carlos Baleba, aliyesajiliwa katika dirisha lililopita, hivi karibuni alifichua kwamba Pogba alikuwa mtu wa kwanza kumpongeza baada ya kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 70 milioni kutoka Brighton.
“Alikuwa Paul Pogba. Alisema Manchester ni klabu kubwa, ni jiji zuri na kwamba alifurahia sana kuwa hapa,” Baleba alisema alipoulizwa ni nani aliyemtumia ujumbe wa kwanza baada ya uhamisho huo.