Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pochettino apewa vichwa sita Man United

SITA Pict

Muktasari:

  • Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 anatarajiwa kuanza kazi katika mazingira magumu, huku Man United ikiwa katika eneo la hatari ya kushuka daraja baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield.

MANCHESTER, ENGLAND: KUWASILI kwa kocha Mauricio Pochettino katika Klabu ya Manchester United kumeongeza mjadala kuhusu mipango ya usajili wa timu hiyo katika dirisha dogo la usajili la Januari 2027.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 anatarajiwa kuanza kazi katika mazingira magumu, huku Man United ikiwa katika eneo la hatari ya kushuka daraja baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield.

Manchester United ina matatizo mengi ambayo hayahusiani tu na benchi la ufundi, lakini upungufu katika maeneo mbalimbali ya kikosi umechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo. Nafasi ya beki wa kushoto imekuwa miongoni mwa maeneo yenye changamoto kubwa kutokana na kutopatikana kwa Luke Shaw.

Shaw mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika kipindi kikubwa cha maisha yake ya soka. Hata hivyo, Man United ilianza msimu huu ikiwa na beki huyo pekee mwenye uzoefu wa kutosha katika nafasi hiyo.

Msimu uliopita ulikuwa tofauti kwake, kwani alicheza michezo yote ya Ligi Kuu England, lakini kwa sasa amekosa mechi tisa zilizopita. Harry Amass haonekani kuwa na ubora unaohitajika katika kikosi cha kwanza, hali iliyolazimisha Diogo Dalot na Noussair Mazraoui kutumika katika nafasi ya beki wa kushoto, ingawa wote wamekuwa na wakati mgumu.

Mchezaji anayetamaniwa zaidi na Manchester United ni Lewis Hall wa Newcastle United, lakini uwezekano wa kumsajili Januari ni mdogo baada ya kuongeza mkataba wake na klabu hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Transfermarkt imechambua majina sita ya mabeki wa kushoto ambao Man United inaweza kuwasajili katika dirisha lijalo, wakiwa na thamani ya soko isiyozidi Euro 40 milioni.

Inaelezwa kuwa Pochettino anaweza kupewa beki wa kushoto wa kushindana na Luke Shaw kwa nafasi ya kucheza, huku klabu hiyo ikipanga kusajili mchezaji wa kiwango cha juu atakayekuwa chaguo la kwanza katika dirisha kubwa la majira ya kiangazi. Mabeki sita wanaotajwa kuwindwa na Man United Januari


SIT 06

ALEJANDRO BALDE (BARCELONA)

Man United iliulizia uwezekano wa kumsajili Alejandro Balde siku za mwisho za dirisha la usajili lililopita na inaelezwa kuwa huenda ikarejea tena kumfuatilia beki huyo wa Barcelona.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania amepoteza nafasi yake katika mipango ya kocha Hansi Flick na mpaka sasa amecheza mechi tano akitokea benchi, akitumia dakika 124.

Kuchomoza kwa Xavi Espart, ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kunaweza kuifanya Barcelona kufikiria kumuuza Balde katika dirisha la Januari. Kiuhalisia, Man United inaweza kujaribu kumsajili kwa mkopo ili kutathmini uwezo wake kabla ya kufanya uamuzi wa kudumu katika dirisha kubwa la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Balde anapaswa kuwa miongoni mwa majina ya juu katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa na klabu hiyo.


SIT 05

JOAQUIN SEYS (CLUB BRUGGE)

Kwa mujibu wa taarifa za Transfermarkt, Man United imekuwa ikimfuatilia kwa karibu Joaquin Seys na inaonekana kuwa anaweza kuwa mrithi wa muda mrefu wa Luke Shaw.

Seys mwenye umri wa miaka 21 ni zao la mfumo maarufu wa kukuza vipaji wa Club Brugge, lakini itakuwa vigumu kuishawishi klabu hiyo ya Ubelgiji kumuuza katika dirisha la Januari.

Club Brugge haina presha ya kifedha inayoweza kuilazimisha kuuza wachezaji wake. Hata hivyo, uhamisho wa Christos Tzolis kwenda Arsenal kwa Euro 40 milioni katika majira ya kiangazi ndiyo uliokuwa mauzo makubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Kutokana na hilo, huenda Seys asiwe mchezaji atakayehitaji ada kubwa kupindukia ili kuondoka, ingawa bado haitakuwa rahisi kwa United kufanikisha dili hilo.


SIT 04

TYRICK MITCHELL (CRYSTAL PALACE)

Katika madirisha kadhaa ya usajili yaliyopita, Man United imeonyesha kulenga kusajili wachezaji ambao tayari wana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu England, na Tyrick Mitchell anaingia katika kundi hilo. Zaidi ya hapo, Mitchell anaweza kupatikana kwa ada ndogo kutokana na mkataba wake na Crystal Palace kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Crystal Palace inaweza kushawishika kumuuza dirisha la Januari ili kupata fedha badala ya kumpoteza bure mwishoni mwa msimu, jambo linaloweza kuipa Man United nafasi ya kumsajili.

Mitchell ni mchezaji mwenye uwezo mzuri katika ligi hiyo na anaweza kusaidia kwa muda mfupi, huku pia akiipa United chaguo lenye uzoefu kama mchezaji wa akiba endapo itasajili beki mwingine wa kiwango cha juu katika majira ya kiangazi.


SIT 03

DAVID RAUM (RB LEIPZIG)

David Raum yupo katika mazingira yanayofanana na Tyrick Mitchell, kwani mkataba wake na RB Leipzig unamalizika mwishoni mwa msimu ujao. Hata hivyo, mazungumzo na RB Leipzig yanaweza kuwa magumu kwa sababu haina ulazima wa kumuuza, hasa baada ya kufanya mauzo makubwa ya Yan Diomande dirisha kubwa lililopita.

Pia, Leipzig itakuwa na nia ya kuhakikisha inafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo haitakuwa rahisi kuachana na wachezaji wake muhimu. Raum alihusishwa na uwezekano wa kujiunga na Man United katika dirisha la kiangazi lililopita. Ni mchezaji mwenye ubora na uzoefu mkubwa, akiwa ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi 40.


SIT 02

ARSENE KOUASSI (LORIENT)

Arsène Kouassi siyo mchezaji anayefahamika sana nje ya Ufaransa, lakini alikuwa chipukizi bora wa mwaka katika Ligue 1 msimu uliopita, na kwa mujibu wa Transfermarkt ana thamani ya Euro 15 milioni na anaweza kuwa chaguo nafuu kwa Man United kutoka Lorient.

Hata hivyo, hatua ya kutoka Ligue 1 kwenda Ligi Kuu England ni kubwa na inahitaji mchezaji kuwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani wa kiwango cha juu. Inaelezwa kuwa Kouassi anaweza kupatikana kwa kiasi ambacho kinaweza kuivutia Manchester United.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ana kasi, bidii na uwezo mzuri wa kushinda mipambano ya kuwania mpira. Alihusishwa na Manchester United wakati wa utawala wa Ruben Amorim kutokana na uwezo wake wa kucheza kama beki wa pembeni anayepanda na kushuka (wing-back), lakini pia anaweza kucheza kama beki wa kushoto wa kawaida.


SIT 01

JORGE SALINAS (SANTANDER)

Man United ilifikiria kumsajili Jorge Salinas katika dirisha la majira ya kiangazi baada ya kufanya vizuri katika msimu ambao Racing Santander ilipanda tena kucheza Ligi Kuu Hispania (LaLiga).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ameanza karibu michezo yote ya Santander katika LiLiga msimu huu, isipokuwa mchezo mmoja, jambo lililompa nafasi ya kuonyesha uwezo wake. Kwa sasa Salinas bado hajafikia kiwango kinachohitajika ili kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza cha Man United.

Hata hivyo, ana kipaji na uwezo mkubwa wa kukua, huku kipengele cha kuvunja mkataba wake cha Euro 16 milioni kikimfanya kuwa chaguo ambalo halina hatari kubwa ya kifedha kwa United.