Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pale juu... Kwanini Arsenal wanaotea sana?

ARSENAL Pict

Muktasari:

  • Kocha Mikel Arteta amefanya kazi kubwa ya kuboresha taratibu, kwa umakini na ustadi mkubwa, karibu kila eneo la mchezo wa Arsenal.

LONDON, ENGLAND: ARSENAL wamekuwa wakiotea kwa wastani mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine yoyote katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England tangu mwaka 2009. Kwa nini wachezaji wao wanashindwa kubaki kwenye mstari wa kuotea?

Kocha Mikel Arteta amefanya kazi kubwa ya kuboresha taratibu, kwa umakini na ustadi mkubwa, karibu kila eneo la mchezo wa Arsenal. Matokeo ya kazi hiyo ya miaka kadhaa ni timu yenye ufanisi mkubwa katika ushindi, inayoruhusu nafasi chache sana kwa wapinzani, inayofanya makosa machache, iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita na ambayo ina nafasi kubwa ya kutwaa tena msimu huu.

Hata hivyo, Arteta ndiye wa kwanza kukiri kwamba timu yake haijakamilika kila kitu. Pia amekubali kuwa kuotea mara nyingi kupita kiasi ni miongoni mwa upungufu ambao si mdogo sana ndani ya kikosi chake. Wachezaji wa Arsenal wameotea mara 35 msimu huu, ikiwa ni angalau mara 11 zaidi ya timu nyingine yoyote (Spurs 24), na zaidi ya mara mbili ya idadi ya kuotea kwa karibu nusu ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Hata hivyo, idadi hiyo siyo kubwa tu ikilinganishwa na timu nyingine msimu huu. Wastani wa sasa wa Arsenal wa kuotea mara 3.5 kwa kila mchezo ndio mkubwa zaidi kwa timu yoyote katika msimu mmoja tangu Hull City ilipofanya hivyo kwa wastani wa mara 3.7 msimu wa 2008/09.

ARSN 01

Wastani mkubwa zaidi katika misimu 10 iliyopita, ambayo inafanana zaidi kutokana na uwezekano wa VAR kuwa na athari, haukaribii hata kidogo kiwango cha Arsenal msimu huu. Chelsea ndiyo iliyokuwa na wastani mkubwa zaidi wa mara 2.8 msimu wa 2017/18.

Arteta aliulizwa kuhusu suala hilo baada ya ushindi wa Arsenal wa bao 1-0 dhidi ya Hull City kabla ya kalenda ya Fifa kuanza, ambapo katika mchezo huo timu yake ilinyimwa penalti baada ya Kai Havertz kuamuliwa kuwa alikuwa ameotea alipofanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na Nobel Mendy.

Kwa haki ya Arsenal na Havertz, kama sheria zingetumika kwa usahihi, Havertz angehesabiwa amehusika katika mchezo pale tu alipofanya jitihada za kuucheza mpira. Hivyo, madhambi aliyofanyiwa yangetangulia kabla ya suala la kuotea kuzingatiwa. Kwa hiyo, katika tukio hilo, Arsenal waliadhibiwa kimakosa kwa kuotea.

Hata hivyo, idadi kubwa ya kuotea kwao haiwezi kuelezwa kwa makosa ya waamuzi. Hata ukiondoa kosa hilo dhidi ya Hull, Havertz bado anaongoza kwa tofauti kubwa katika ligi hiyo baada ya kuotea mara 15 peke yake. Hakuna mchezaji mwingine aliyeotea zaidi ya mara nane, huku timu sita zikiwa na idadi ya kuotea isiyozidi mara 15.

“Kwa hakika, ni nyingi kupita kiasi. Kuna maeneo mengi tunayohitaji kuboresha, hili ni mojawapo. Wakati mwingine linahusiana na muda wa kuanza kukimbia, mazingira ya tukio au nafasi ya mpinzani, mahali aliposimama na nafasi aliyokuachia,” anasema Arteta juu ya kuotea.


ARSN 02

HAPA PIA

Kuotea mara nane kwa Arsenal dhidi ya Villa ndiko kulikokuwa kukubwa zaidi kwa timu yoyote katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu England kwa kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita, tangu Everton ilipootea mara 10 dhidi ya Burnley Aprili 2024.

Mchezo huo unapaswa kuwa wa kipekee kwa kiasi fulani, na kwa kuwa ni michezo 10 pekee iliyochezwa msimu huu, huenda umeathiri wastani wao. Wastani huo unaweza kushuka, na pengine utashuka, katika michezo 28 iliyobaki.

Hata hivyo, siyo kwamba tukio hilo lilikuwa la mara moja tu. Arsenal pia waliotea mara saba dhidi ya Leeds, mara tano dhidi ya Coventry, nne dhidi ya Hull na tatu dhidi ya Chelsea na Liverpool.

Kila mmoja wa wapinzani hao amechangia kuongeza wastani wao kufikia mara tatu au zaidi kwa mchezo. Hata kuotea mara mbili dhidi ya Sunderland ni muhimu, kwa sababu kunachangia asilimia 28.6 ya jumla ya mara saba ambazo Sunderland imewafanya wapinzani wake kuotea msimu mzima. Ni Everton pekee (mara tano) iliyowafanya wapinzani kuotea mara chache zaidi.

Sehemu ya sababu hizo inatokana na mazingira ya michezo waliyocheza. Arsenal wamekutana na timu sita zilizowafanya wapinzani wao kuotea mara nyingi zaidi katika Ligi Kuu England msimu huu, ambazo ni Villa, Coventry, Hull, Leeds, Liverpool na Brighton.

Pia, kwa kuwa ni timu inayotawala umiliki wa mpira na eneo la mchezo, Arsenal wana uwezekano wa kutengeneza mazingira mengi zaidi kuliko timu nyingi yanayoweza kuwafanya wachezaji wake waotee. Kwa mfano, Arsenal wanashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu England kwa takwimu za kutawala eneo la mpinzani (asilimia 64.1).

Pia wanashika nafasi ya pili kwa idadi ya pasi za kupenya safu ya ulinzi (through balls) walizojaribu (31), nafasi ya pili kwa pasi zilizomalizia katika theluthi ya mwisho ya uwanja wa wapinzani (1,662) na nafasi ya pili kwa pasi zinazopenya safu ya ulinzi wa wapinzani na kuelekezwa nyuma ya mabeki (207). Ni wazi kuwa mazingira ya kuotea mara nyingi yapo ndani ya namna wanavyocheza.


ARSN 03

HUKU JE?

Lakini, Arsenal siyo timu ya kwanza kutawala umiliki wa mpira kwa namna hiyo, wala siyo timu pekee inayofanya hivyo msimu huu. Kwa mfano, Manchester City na Tottenham wana wastani mkubwa zaidi wa umiliki wa mpira na takwimu za field tilt (utawala wa eneo la mpinzani au kiwango cha kutawala eneo la ushambuliaji) kuliko Arsenal, huku Brighton wakiwa karibu nao katika vipengele vyote viwili. Brighton pia wanapiga pasi nyingi zaidi zinazopenya safu ya ulinzi ya wapinzani.

Aidha, Arsenal wanashika nafasi ya sita kwa idadi ya mbio za kasi kubwa zinazofanywa bila mpira kuelekea nyuma ya safu ya ulinzi ya wapinzani wakati timu yao ikiwa na umiliki wa mpira (408). Hizi ndizo aina ya mbio zinazoweza kuongeza uwezekano wa mchezaji kuotea. Arsenal, na hasa Havertz, wameonyesha kutokuwa na ufanisi katika kupanga vizuri muda wa kufanya mbio hizo.

“Yote yanahusu muda sahihi,” anasema Arteta na kuongeza: “Kuna ishara inayotolewa na mchezaji mwenye mpira, na unatakiwa kupanga muda wa kuanza kukimbia kulingana na ishara hiyo. Ukichelewa kwa sekunde moja au hata nusu sekunde, tayari unakuwa umechelewa.”

Licha ya mtazamo kwamba Havertz ni kiungo wa zamani anayecheza mbele na anayependa kushuka chini kutafuta mpira, ukweli ni kwamba anajaribu sana kukimbilia nyuma ya safu ya ulinzi ya wapinzani.

ARSN 05
ARSN 05

Ni Gonzalo Garcia wa Fulham (145) na Bryan Mbeumo wa Manchester United (141) pekee waliofanya mbio nyingi zaidi za kasi kubwa kuelekea nyuma ya safu ya ulinzi katika Ligi Kuu England msimu huu kuliko Havertz (125).

Hata hivyo, wachezaji hao wawili wameotea mara mbili na nne mtawalia, ikilinganishwa na mara 15 za Havertz. Wote wawili pia wamecheza angalau dakika 90 zaidi ya mshambuliaji huyo wa Arsenal.

Havertz ameotea katika mazingira ya aina mbalimbali. Katika baadhi ya matukio, amekuwa na bahati mbaya kidogo, lakini mengi sana yangeweza kuepukika na yamekuwa yakikeresha. Mfano ni tukio dhidi ya Villa, ambapo alishindwa kujirudisha kwenye nafasi sahihi licha ya kuwa na muda na nafasi ya kutosha kufanya hivyo……na pia katika pigo  la adhabu lililofanywa haraka, wakati alipokuwa na nafasi ya kuangalia safu nzima ya ulinzi ya Liverpool katika Uwanja wa Anfield.

Pia ameotea mara mbili katika mipira ya adhabu iliyopigwa mbali sana na kipa David Raya kuelekea upande wa pili wa uwanja. Matukio hayo ya mwisho ni matatu kati ya mara 11 ambazo wachezaji wa Arsenal wameotea ndani ya sekunde 15 baada ya mchezo kusimama kutokana na mpira kufa msimu huu.

Baadhi ya matukio mengine yalikuwa ya karibu sana ndani ya eneo lenye wachezaji wengi, kama pale Ezri Konsa alipoamuliwa kuwa ameotea wakati VAR ilipokuwa ikikagua bao la kusawazisha la Riccardo Calafiori lililokataliwa dhidi ya Chelsea. Hata hivyo, siyo sahihi kwa Arsenal kusema kuwa maamuzi ya karibu katika mipira ya adhabu ndiyo yanayoeleza idadi kubwa ya kuotea kwao kwa ujumla.


ARSN 04

SA' INAKUWAJE?

Ukweli ni kwamba hali hiyo haijamuumiza Arteta na wachezaji wake. Wanaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano na, kwa kuwa hakuna mpinzani anayeonekana kuwa tishio kubwa, wana nafasi kubwa ya kuendelea na kutwaa ubingwa.

Safu yao ya ulinzi ni imara kiasi kwamba wamekuwa wakihitaji bao moja pekee kushinda michezo yao msimu huu. Hata hivyo, kuna uwezekano kwamba upotevu wa umiliki wa mpira mara 35 uliotokana na kuotea kwao umeathiri uwezo wao wa kufunga mabao.

Wamefunga mabao 15 pekee katika michezo 10. Kwa mwenendo huo, wanaweza kumaliza msimu wakiwa na mabao 57, jambo ambalo litavunja rekodi ya timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa na mabao machache zaidi, ambayo ni 67 yaliyofungwa na Manchester United 1992/93.

Kwa sasa, wanaweza kutegemea uimara wa safu ya ulinzi, lakini huenda ukafika wakati watakapohitaji kufunga mabao mengi zaidi. Kujitahidi kubaki kwenye nafasi sahihi na kuepuka kuotea mara kwa mara kunaweza kuwa mwanzo mzuri.