Pacha za moto Ligi Kuu England
Muktasari:
- Kwa kuzingatia hilo, takwimu katika soka ya Opta imechunguza wachezaji wanaocheza pamoja na kushirikiana vizuri zaidi katika safu ya ushambuliaji kuliko wengine katika ligi hiyo msimu wa 2026/27, na katika hilo uapo baadhi ya majina yanayovutia ambayo yamejitokeza.
LIVERPOOL, ENGLAND: NI wachezaji gani wawili wamekuwa na ufanisi mkubwa zaidi katika Ligi Kuu England msimu huu linapokuja suala la kutengenezeana nafasi za kufunga mabao? Soka ni mchezo wa timu, lakini bado kuna burudani ya kipekee kuwaona wachezaji wawili wakijenga ushirikiano maalumu ndani ya uwanja.
Kwa kuzingatia hilo, takwimu katika soka ya Opta imechunguza wachezaji wanaocheza pamoja na kushirikiana vizuri zaidi katika safu ya ushambuliaji kuliko wengine katika ligi hiyo msimu wa 2026/27, na katika hilo uapo baadhi ya majina yanayovutia ambayo yamejitokeza.
Sasa, ni jozi zipi zinazotengenezeana nafasi nyingi zaidi za mabao, na ni wachezaji gani wanaoshirikiana kufunga mabao kupitia pasi za mwisho kuliko wengine? Soma hapa!
UTENGENEZAJI NAFASI
Chelsea haijaanza msimu kikamilifu chini ya zama mpya za Xabi Alonso, lakini safu yake ya ushambuliaji imekuwa na mafanikio makubwa kwa kiasi kikubwa. Jambo muhimu katika mafanikio hayo ni jinsi Morgan Rogers alivyozoea haraka maisha yake katika Uwanja wa Stamford Bridge.
Sababu mojawapo ni uhusiano mzuri aliojenga na Cole Palmer, rafiki yake wa tangu utotoni na mchezaji mwenzake ambaye anafahamu namna ya kucheza naye kutokana na siku walizokuwa pamoja katika akademi ya Manchester City.
Rogers amemtengenezea Palmer nafasi 10 za kufunga mabao, idadi kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote aliyomtengezea nafasi mchezaji mwenzake mmoja katika ligi hiyo msimu huu.
Kwa upande mwingine, Palmer amemtengenezea Rogers nafasi nne. Hiyo inawafanya kuwa jozi yenye ufanisi mkubwa zaidi msimu wa 2026/27 linapokuja suala la kutengenezeana nafasi za mabao, wakiwa na jumla ya nafasi 14. Hata hivyo, kuna jozi nyingine ya Chelsea yenye ufanisi mkubwa zaidi katika kipengele kingine.
Nazo jozi ya Liverpool inayoundwa na Alexander Isak na Cody Gakpo, pamoja na Emersonn na Julio Enciso wa Ipswich Town, zinashika nafasi ya pili kwa pamoja zikiwa zimetengenezeana nafasi tisa kila moja.
Gakpo ndiye mtengeneza nafasi mkuu katika ushirikiano wake na Isak, akiwa amemtengenezea Mswideni huyo nafasi sita, ambapo tatu kati yake zimezaa mabao.
Hakuna mchezaji aliyempa mwenzake mmoja pasi nyingi zaidi za mabao katika Ligi Kuu England msimu huu kuliko Gakpo, aliyetoa tatu kwa Isak. Pia ndiye aliyezalisha idadi kubwa zaidi ya mabao yaliyotarajiwa kwa mchezaji mmoja, akiwa na wastani wa 1.29.
Francisco Evanilson wa Bournemouth naye ana idadi asisti kwa mchezaji mwenzake akiwa nazo tatu zilizotumika kufunga mabao ya Marcus Tavernier. Wawili hao wametengenezeana nafasi nane za mabao wakionyesha mchango mkubwa katika kufufua kiwango cha Bournemouth kipindi cha karibuni.
Emersonn na Enciso wamekuwa wakitengenezeana nafasi nyingi za mabao, tisa kwa jumla, lakini wamefanikiwa kupata pasi moja tu ya bao.
Kuna jozi nyingine tatu zilizotengenezeana nafasi nane za mabao kila moja. Ni Johan Manzambi na Nicolas Jackson wa Aston Villa, Alex Iwobi na Gonzalo García wa Fulham, pamoja na Palmer na Pedro Neto wa Chelsea. Manzambi na Jackson wanaongoza Ligi Kuu England kwa wastani wa nafasi wanazotengenezeana kwa kila dakika 90 wakiwa nazo 1.99 kwa kila dakika 90 wanazocheza pamoja.
PASI ZA MABAO
Gakpo kwa Isak na Evanilson kwa Tavernier ndizo jozi ambazo zimezalisha mabao mengi zaidi msimu huu kupitia ushirikiano wa upande mmoja. Hata hivyo, Isak na Tavernier hawajawalipa wenzao kwa kutoa pasi za mabao kwa upande mwingine na matokeo yake wawili hao wana jumla ya pasi tatu za mabao walizotoa kwa wenzao.
Jozi nyingine ya Chelsea ambayo bado hajaitajwa inaongoza katika orodha ya wachezaji waliotengenezeana mabao mengi zaidi ni ile ya Palmer na Joao Pedro ambao wametoa pasi mbili za mabao kila mmoja kwa mwenzake msimu huu. Hiyo inawafanya kuongoza Ligi Kuu England kama jozi yenye ufanisi mkubwa zaidi, wakiwa wametengenezeana mabao manne. Kinachofanya mafanikio hayo yawe ya kuvutia zaidi ni kwamba Pedro amekosa mechi mbili za Chelsea za ligi kutokana na jeraha.
Kuna jozi nyingine moja ya kuvutia, ambayo huenda ikashangaza wengi, iliyozalisha mabao matatu msimu huu. Inaundwa na mtengeneza nafasi mkuu wa Manchester City, Rayan Cherki, na beki Josko Gvardiol.
Cherki ametoa pasi mbili za mabao na Gvardiol moja. Wamefanikiwa kufanya hivyo katika dakika 391 pekee walizocheza pamoja uwanjani, idadi ambayo ni ndogo zaidi kwa mbali ikilinganishwa na jozi nyingine yoyote iliyozalisha mabao matatu au zaidi.
13 - Liverpool imekusanya pointi nyingi zaidi ugenini katika EPL msimu huu kuliko timu nyingine yoyote (13). Hiyo ni rekodi yake ya pointi nyingi zaidi kuwahi kukusanya katika mechi tano za kwanza za ugenini mwanzoni mwa msimu wa ligi.
700 - DHIDI ya Sunderland akiwa na Chelsea, Jordan Henderson kafikisha mechi 700 katika maisha yake ya soka la kulipwa ngazi ya klabu. Hatua hiyo ameifikia miaka 18 na siku saba tangu alipocheza mechi yake ya kwanza, ambayo pia ilikuwa dhidi ya Chelsea wakati akiitumikia Sunderland.