Orodha ya wachezaji ghali Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Yamal amekuwa mfano wa kizazi kipya cha vipaji vya Barcelona baada ya kupanda kama mmoja wa wachezaji bora duniani kwenye nafasi ya winga wa kulia. Kwa upande wake, Haaland anaendelea kutambulika kuwa mmoja wa wafungaji hatari zaidi duniani kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu katika Ligi Kuu England na michuano ya Ulaya.
MANCHESTER, ENGLAND: KADRI Kombe la Dunia 2026 linavyokaribia, thamani za soko za baadhi ya nyota wa soka duniani zinaendelea kupaa na kuonyesha ukubwa wa vipaji vinavyotarajiwa kung'ara katika mashindano hayo.
Orodha ya hivi karibuni ya Transfmarkt ya wachezaji wenye thamani kubwa zaidi duniani inaongozwa na kizazi kipya cha nyota wanaotikisa soka la Ulaya na kileleni mwa yupo nyota wa Hispania na Barcelona, Lamine Yamal, ambaye akiwa na umri wa miaka 18 amefikia thamani ya Euro 200 milioni.
Katika nafasi hiyo Yamal yupo sambamba na mshambuliaji wa kimataifa wa Norway na Manchester City, Erling Haaland pamoja na nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe wa Real Madrid. Wachezaji hao watatu ndio pekee duniani waliofikia kiwango hicho cha soko, jambo linaloonyesha ushawishi wao mkubwa ndani na nje ya uwanja.
Yamal amekuwa mfano wa kizazi kipya cha vipaji vya Barcelona baada ya kupanda kama mmoja wa wachezaji bora duniani kwenye nafasi ya winga wa kulia. Kwa upande wake, Haaland anaendelea kutambulika kuwa mmoja wa wafungaji hatari zaidi duniani kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu katika Ligi Kuu England na michuano ya Ulaya.
Kwa upande wake Mbappe naye ameendelea kuthibitisha hadhi yake tangu ahamie Real Madrid, akiwa mmoja wa nyota wanaovutia zaidi katika soka la kisasa. Nyuma yao yupo kiungo mahiri wa Barcelona, Pedri, mwenye thamani ya Euro 150 milioni.
Akiwa na umri wa miaka 23, Pedri anaendelea kuwa mhimili wa timu ya taifa ya Hispania na Barcelona kutokana na uwezo wake wa kutawala kiungo na kusambaza mpira. Nyota huyo analingana thamani na Vinicius Junior wa Real Madrid na Michael Olise wa Bayern Munich, ambao wote wanakadiriwa kuwa na thamani ya Euro 150 milioni.
Naye Michael Olise amepanda kwa kasi baada ya msimu mzuri akiwa Bayern Munich, huku Vinicius Jr akiendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Real Madrid. Uwezo wao wa kuamua matokeo ya mechi kwa mabao, asisti na ubunifu umewafanya kuwa miongoni mwa nyota wenye thamani kubwa zaidi duniani.
PSG ina wawakilishi wengi katika orodha hiyo. Joao Neves, Vitinha, Khvicha Kvaratskhelia na Desire Doue ni miongoni mwa nyota wanaothibitisha nguvu ya mabingwa hao wa Ufaransa.
Neves, kiungo wa kati wa Ureno mwenye miaka 21 ana thamani ya Euro 140 milioni sawa na Vitinha na Kvaratskhelia. Doue mwenye miaka 21 ana thamani ya Euro 120 milioni na anatajwa kuwa mmoja wa vipaji vinavyokua kwa kasi zaidi Ulaya.
Real Madrid pia inaendelea kutawala katika suala la thamani za wachezaji. Mbali na Mbappe na Vinicius, klabu hiyo inajivunia Jude Bellingham mwenye thamani ya Euro 140 milioni, Federico Valverde Euro 120 milioni na Arda Guler Euro 90 milioni.
Bellingham amekuwa mmoja wa viungo bora duniani, huku Valverde akijulikana kwa uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi na kufanya kazi kubwa uwanjani.
Katika Ligi Kuu England, Arsenal ina wawakilishi watatu. Declan Rice na William Saliba wana thamani ya Euro 120 milioni na 100 mtawalia, huku Bukayo Saka akiwa thamani yake ni Euro 110 milioni. Rice ameendelea kuwa mmoja wa viungo bora wa ulinzi duniani, Saliba ni nguzo ya safu ya ulinzi wakati Saka ameendelea kuwa tishio katika mashambulizi.
Kwa upande wa Chelsea inawakilishwa na Moises Caicedo na Cole Palmer ambao kila mmoja ana thamani ya Euro 100 milioni. Caicedo ni mmoja wa viungo bora wakabaji na waporaji mipira, huku Palmer akiendelea kuvutia kutokana na mchango wake mkubwa wa mabao na asisti.
Liverpool imepata uwakilishi kupitia Florian Wirtz na Dominik Szoboszlai, ambapo Wirtz, ambaye alihamia Anfield akiwa mmoja wa viungo washambuliaji bora wa kizazi chake ana thamani ya Euro 100 milioni sawa na Szoboszlai ambaye ameendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi.
Bayern Munich inaendelea kuzalisha na kuvutia vipaji vikubwa. Mbali na Olise, klabu hiyo ina Jamal Musiala na Aleksandar Pavlovic wenye thamani ya Euro 100 milioni na 90 milioni mtawalia. Musiala ameendelea kuwa mmoja wa viungo washambuliaji wenye ubunifu mkubwa zaidi Ulaya.
Katika safu ya wachezaji vijana wanaopanda kwa kasi, Yan Diomande wa Ivory Coast na RB Leipzig amefikia thamani ya Euro 90 milioni akiwa na miaka 19. Nyota huyo anatajwa kuwa mmoja wa mawinga hatari zaidi wa kizazi kipya kutokana na kasi, chenga na uwezo wa kufunga mabao.
Kwa ujumla, orodha hiyo inaonyesha jinsi soka la kisasa linavyoendelea kutawaliwa na vijana wenye vipaji vikubwa. Wachezaji 25 waliopo katika kundi hilo wana thamani ya zaidi ya Euro 3.2 bilioni kwa pamoja, jambo linalodhihirisha ukubwa wa uwekezaji unaofanywa na klabu kubwa za Ulaya.
Pia inaonyesha kuwa Kombe la Dunia 2026 litakuwa jukwaa la baadhi ya wachezaji wenye thamani kubwa zaidi kuwahi kuonekana katika historia ya mashindano hayo.