Prime
NYUMA YA PAZIA: Rashford, Man United wanavyoachana katika msitu wa Amazon
Muktasari:
- Nilikuwa namsikiliza Marcus Rashord wiki iliyopita. Mambo yamefika mwisho. Akiongea na wanafunzi katika shule aliyosoma alidai kwamba umefika wakati akapate changamoto mpya nje ya Manchester United. Yeye ndiye ameamua kufungua boksi la Pandora.
NI kama simulizi ya watu wawili waliojaribu kupambana katikati ya misitu ya Amazon kule Amerika Kusini. Walikuwa pamoja kwa muda mrefu wakijaribu kujiokoa. Imefika mwisho. Kila mmoja ameamua kujiokoa kivyake.
Nilikuwa namsikiliza Marcus Rashord wiki iliyopita. Mambo yamefika mwisho. Akiongea na wanafunzi katika shule aliyosoma alidai kwamba umefika wakati akapate changamoto mpya nje ya Manchester United. Yeye ndiye ameamua kufungua boksi la Pandora.
Amefanya kitu sahihi. Hata kama Manchester United wangeamua kusema wao kwanza nadhani wangekuwa wamefanya uamuzi sahihi. Umefika wakati kwa Rashford na United kuachana. Ilikuwa ni kama simulizi nzuri ya mapenzi ambayo mwandishi ameshindwa kutengeneza ndoa iliyo sahihi kwa wapenzi wawili waliopendana vema.
Rashford na United walijaribu kuokoka pamoja lakini imeshindikana. Rashford alicheza mechi yake ya kwanza United mwaka 2016. Ilikuwa ni msimu wa tatu mfululizo United haijatwaa Ligi Kuu ya England. Wakati huo ndio ilikuwa imeanza kwenda chini.
Mambo mawili yalitakiwa. United imfanye Rashford kuwa staa mkubwa na pia Rashford airudishe United katika ufalme wake. Wote wawili walijikuta katika misitu ya Amazon wakijaribu kuokoana na kufika katika nchi ya ahadi.
Nadhani yote mawili yalishindikana. Kuanzia wakati huo mpaka sasa United haijatwaa Ligi Kuu ya England au taji kubwa la kuheshimika zaidi Ulaya na England. Wanaweza kusema wametwaa FA lakini sio kiu kubwa kwa mashabiki wa United.
United inaweza kumtazama Rashford na kuamini ni mmoja kati ya wachezaji ambao wameiangusha kufikia nchi ya ahadi. Rashford amekuwa hana mwendelezo wa ubora kuanzia mechi hadi mechi, au msimu hadi msimu.
Msimu huu anaweza kuwa moto lakini msimu ujao unashindwa kuamini kama unamtazama Rashford yule yule ambaye ulikuwa unamtazama msimu uliopita. Mfano ni fomu yake yake ya msimu wa 2022/23. Alifunga mabao 30. Msimu uliofuata hakufikisha mabao 15.
Huyu ndiye Rashford ambaye leo anataka kuachana na Manchester United na hata mashabiki wa timu hiyo hawajui kama walie au wacheke. Kwa mfano, Rashford waliyemuona katika msimu miwili iliyopita wanatamani auzwe aondoke zake. Hata hivyo, wakimkumbuka yule Rashford aliyefunga mabao 30 wanatamani labda aendelee arudishe kiwango chake.
Wakati Rashford akiwa hana mwendelezo wa ubora, kuna wachezaji ambao msimu baada ya msimu wamekuwa na mwendelezo wa ubora katika klabu zao na hivyo kuendelea kuziweka katika nafasi za juu. Mfano ni Mo Salah wa Liverpool na Bukayo Saka wa Arsenal. Unaposema kwamba wao ni mihimili ya mashambulizi katika timu zao unakuwa una uhakika na viwango vyao msimu baada ya msimu.
Hata hivyo, wakati mwingine unaweza kusimama upande wa Rashford na kuichambua Manchester United. Je ni klabu ambayo ilimfanya awe bora? Hapo unatilia shaka. Labda mastaa wenzake wa timu nyingine wamekuwa wakicheza katika timu ambazo ni bora na hivyo kufanya maisha kuwa rahisi.
Kuanzia mwaka 2013 wakati Sir Alex Ferguson alipochukua ubingwa wa England kwa mara ya mwisho, mpaka leo, United imekuwa ikiungaunga. Kuanzia katika utawala, makocha wanaopita na wachezaji wanaosajiliwa. Hapo ndipo unapoweza kusimama upande wa Rashford. Je, timu ilimsaidia awe staa zaidi ya alivyo?
Kucheza sambamba na kina Harry Maguire, Aaron van Bissaka, John Evans, Scott MacTominay na wachezaji wa namna hii, kungeweza kumsaidia kuwa staa mkubwa? Je angecheza United ya kipindi kile cha kina Wayne Rooney, Paul Scholes, Roy Keane, David Beckham, Ryan Giggs na wachezaji wa aina ile angeweza kuwa kama hivi au angekuwa staa mkubwa zaidi?
Mwisho wa yote uamuzi ambao Rashford amefikia nadhani ni sahihi na una maslahi kwa pande zote mbili. Pande zote hazikusaidiana kufikia malengo. Uamuzi sahihi zaidi nadhani ni kuachana ili kila mtu atimize malengo yake.
Inaweza pia ukawa mwanzo wa kocha Ruben Amorim kutengeneza kikosi chake kipya. Siku chache kabla ya kauli ya Rashford tulisikia uvumi kwamba United walikuwa tayari kusikiliza ofa za Rashford katika dirisha la Januari. Labda United ilishafanya uamuzi mapema na ikamuachia mchezaji heshima ya kuanza kutangaza jambo hili.
Makocha wanaopewa miradi ya kusuka kikosi upya, hasa kilichodorora kama United, wanahitaji uamuzi mgumu wa muda mrefu. Inawezekana Amorim alitoka zake Lisbon akijua wazi kwamba mchezaji kama Rashford sio aina ya mchezaji ambaye atamuhitaji kikosini.
Lakini pia inawezekana ndani ya siku chache alizokaa naye Carrington amegundua kwamba hawezi kwenda na mchezaji mwenye tabia kama zake. Hapa ndipo inapowezekana kabisa kuwa Rashford amepewa heshima tu ya kutangaza uamuzi ambao si ajabu ulishafikiwa mapema na pande zote mbili.
Mikel Arteta aliwasafisha wachezaji kama Mesut Ozil na Pierre Emerick Aubameyang ndani ya miezi michache tu baada ya kuwasili klabuni hapo alipogundua mienendo yao isingeendana na namna alivyotaka kukisuka upya kikosi cha Arsenal ambacho alikikuta kikiwa taabani.
Mtihani ambao utakuwepo kwa sasa ni kuona namna gani United inaweza kusonga mbele bila ya mazoea ya kuwa na mchezaji kama Rashford. Hakuna shaka pengo lake linazibika. Ni suala la kocha tu kuamua kuchukua mchezaji sahihi na kutengeneza mfumo sahihi.
Lakini mtihani mwingine pia unabakia kwa Rashford. Sasa anataka kuondoka katika eneo ambalo alikuwa anaishi kwa mazoea. Ni wakati wake wa kuthibitisha uwezo wake wa kwenda katika klabu ambayo ina mastaa wazuri kuliko kina Maguire na kuifanya kazi yake kwa usahihi.
Ana miaka 27 tu na kama anaona alikuwa katika timu ambayo haikuwa sahihi kumfanya staa mkubwa duniani basi ana nafasi ya kwenda katika klabu kama hiyo na kugeuka kuwa staa mkubwa ulimwenguni. Ni wakati wake sasa kuthibitisha kwamba United ilikuwa inamkwamisha kama ambavyo ni wakati wa United kuthibitisha kwamba wachezaji kama Rashford walikuwa wanawakwamisha kupambana na kina Manchester City, Liverpool na Arsenal.