Prime
Njia ya Ibenge anavyoweza kuifikisha mbali Azam CAF
MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC tayari wameandika rekodi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF msimu huu wa 2025-2026, ikiwa ni mara ya kwanza katika miaka 21 ya historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima.
Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, waliopanda Ligi Kuu Julai 27, 2008, wameweka historia hiyo mpya wakiwa chini ya kocha Mkongomani Florent Ibenge aliyejiunga nao Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Azam ilianza kampeni za kufika nchi ya ahadi katika hatua ya kwanza kwa kuitoa El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, kisha raundi ya pili ikakutana na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) na kukitoa kwa jumla ya mabao 9-0.
Baada ya historia hiyo mpya, Azam huenda ikaandika rekodi nyingine ya kutinga robo fainali ikiwa itachanga karata zake vizuri, kufuatia kupangwa kundi B pamoja na Wydad Casablanca (Morocco), AS Maniema Union (DR Congo) na Nairobi United ya Kenya.
Kutokana na kundi hilo ambalo kiuhalisia ni gumu kwa sababu ya wapinzani waliopo, Mwanaspoti linakuletea wasifu kwa timu zote tatu ambazo zitapambana na matajiri hao wa Azam kusaka tiketi ya kwenda robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
WYDAD AC (MOROCCO)
Timu hii iliyoanzishwa rasmi Mei 8, 1937, imetimiza miaka 88, ikijulikana kwa jina la utani la Wydad Al Oumma au Wydad of the Nation, ambapo kikosi hicho kimesheheni mastaa wakubwa akiwamo, Hakim Ziyech aliyetamba na Chelsea katika Ligi Kuu ya England.
Ziyech aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuondoka Al-Duhail SC ya Qatar, ni nyota anayetazamwa zaidi kutokana na uzoefu wake mkubwa alionao, huku akiwahi kuzichezea pia, Ajax, Twente na Heerenveen zote za Uholanzi na Galatasaray ya Uturuki.
Wydad imechukua mataji 22 ya Ligi Kuu ya Morocco ‘Botola Pro’, Moroccan Throne Cup mara tisa, Independence Cup (1), Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu kuanzia 1992, 2017 na 2021-2022, CAF Super Cup mara moja mwaka 2018 na African Cup Winners’ Cup 2002.
Mataji mengine ni Afro-Asian Club Championship 1993, Mohammed V Cup mara moja pia 1979, Arab Club Champions Cup 1989, Arab Super Cup 1992, North African Cup 1949 na North African Championship ililochukua kwa mara tatu 1948, 1949 na 1950.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika imeshiriki mara 16, huku mafanikio makubwa ni kuchukua ubingwa mwaka 1992, 2017 na 2021-22, ikifika pia nusu fainali mwaka 2016, kisha msimu wa 2019-20 na 2020-21 na robo fainali mwaka 1991 na 2018.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika, inashiriki mara ya tano, huku ikiwa haina pia rekodi nzuri, kuanzia mwaka 2004, 2007 na 2012 ilipotinga makundi, kisha 2013 ikatolewa raundi ya pili na sasa imefika hatua ya makundi msimu huu wa 2025-2026.
CAF Super Cup imeshiriki mara nne huku mafanikio makubwa ni kuchukua ubingwa mwaka 2018, ikishiriki African Cup Winners’ Cup mara tatu na kutwaa taji hilo mwaka 2002 na kufika pia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo mara mbili, 1998 na 2003.
Katika CAF Cup, Wydad imeshiriki mara tatu na mafanikio makubwa ni kufika robo fainali mwaka 2001, ikishiriki pia 1999 na 2000, ambapo wapinzani wakubwa ni Raja Casablanca waliotengeneza dabi inayojulikana kwa jina la ‘Casablanca Derby’.
Wydad na Azam, ni mechi inayosubiriwa kwa hamu msimu huu kwani licha ya Ziyech kuwepo kikosini humo, nyota mwingine ni Stephane Aziz KI aliyewahi kucheza Yanga anayesubiriwa kukutana na aliyekuwa mpinzani wake, ‘Feisal Salum ‘Fei Toto’.
AS MANIEMA UNION (DR CONGO)
Association Sportive Maniema Union ambayo kwa jina la utani inajulikana Greens and Blacks, imepishana mwaka mmoja tu na Azam, ambapo kikosi hiki kimeanzishwa rasmi 2005, katika mji wa Kindu, ikiwa haina rekodi nzuri kwenye michuano ya CAF.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, AS Maniema imeshiriki mara moja tu msimu wa 2024-2025 na kuishia hatua ya makundi, huku Kombe la Shirikisho Afrika inayoshiriki pia msimu huu ikiwa ni mara ya nne baada ya 2008, 2018, 2019-2020 na 2025-2026.
Misimu yote iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, huu ndio msimu pekee imefika hatua ya makundi, kwani mara tatu zote iliishia raundi ya awali na ya kwanza ikifanya hivyo mwaka 2008, 2018 na msimu wa 2019-2020 ilipoaga mashindano mapema.
Timu hiyo imetwaa mataji matatu ya Coupe du Congo mwaka 2007, 2017, 2019, huku ikitwaa taji la Maniema Provincial League mwaka 2006, ambapo ilianza kampeni za kusaka makundi msimu huu kwa kuitoa Pamplemousses ya Mauritania kwa jumla ya mabao 4-3.
Baada ya hapo ikatinga raundi ya pili na kuitoa Royal Leopards ya Eswatini kwa penalti 4-3, baada ya timu hizo kufungana kwa jumla ya mabao 2-2, ambapo pambano la kwanza zilitoka sare ya bao 1-1, huku lile la marudiano zikafungana tena 1-1.
NAIROBI UNITED (KENYA)
Timu hii ni changa ila tayari imeanza kupata mafanikio makubwa katika soka la Kenya, ambapo kikosi hicho kilichoanzishwa rasmi mwaka 2015, kikifahamika kwa jina la Balaji EPZ huko Nairobi Kenya, kilianza kucheza kuanzia Ligi ngazi ya chini.
Mwaka 2022, jina lake lilibadilishwa rasmi na kuitwa Nairobi United FC, ambapo miaka michache ilipanda hadi FKF Division One League, kisha National Super League (NSL) na kuongoza msimu wa 2024-2025 na kupanda Ligi Kuu ya Kenya yaani FKF Premier League.
Msimu wa 2024-2025, ilimaliza ikiwa mabingwa wa NSL, kisha kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, huku ikishangaza pia wengi baada ya kutwaa ubingwa wa FKF Cup mwaka 2025 kwa kuifunga Gor Mahia.
Ubingwa huo ndio ulioipa nafasi ya kuiwakilisha Kenya katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kwenye historia, ambapo iliitoa NEC FC ya Uganda kwa faida ya bao la ugenini, baada ya sare ya kufungana jumla ya mabao 3-3.
Baada ya hapo, ikaendelea kushangaza wengi kwa kuitoa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa penalti 7-6, ikishinda Kenya mabao 2-0, kisha kwenda ugenini kuchapwa pia 2-0, hivyo, pambano hilo kuisha kwa timu hizo kufungana kwa jumla ya mabao 2-2 kabla ya kuamuliwa kwa ‘matuta’.
Ikishiriki kwa mara ya kwanza kimataifa, timu hiyo imefika hadi hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, jambo linaloonyesha sio ya kubezwa na Wydad Casablanca, Azam na AS Maniema zinapaswa kujipanga na kutoichukulia poa.