NIPE, NIKUPE: Dili za kibabe za kubadilishana wachezaji kwenye soka

Muktasari:
- Chelsea inahitaji mchezaji kutoka Man United, lakini haina pesa ya kutosha, wakati Mashetani Wekundu nao kuna staa wanamtaka kutoka The Blues na haitaki kutumia pesa, hivyo dili la kubadilishana wachezaji linaweza kufanyika ili kufanikisha jambo hilo.
LONDON, ENGLAND: LISEMWALO kwa sasa kwenye dirisha hili la uhamisho wa wanasoka huko Ulaya, kuna uwezekano wa kutokea kwa dili tamu kabisa kwa klabu za Chelsea na Manchester United kubadilishana wachezaji.
Chelsea inahitaji mchezaji kutoka Man United, lakini haina pesa ya kutosha, wakati Mashetani Wekundu nao kuna staa wanamtaka kutoka The Blues na haitaki kutumia pesa, hivyo dili la kubadilishana wachezaji linaweza kufanyika ili kufanikisha jambo hilo.
Kinachoelezwa ni kwamba dili hilo linawahusu Alejandro Garnacho na Christopher Nkunku. Garnacho atakwenda Stamford Bridge, wakati Nkunku atapishana naye mlangoni akielekea Old Trafford. Je, dili hilo litatokea kwenye dirisha hili kabla halijafungwa? Usisema haiwezekani.
Hiyo kwa sababu ni mara ya kwanza kwenye soka kutokea dili za kubadilishana wachezaji baada ya hizi 11 zilizotokea miaka ya karibuni.
11. Francesco Coco & Clarence Seedorf
Ukitaja jina la Seedorf, basi kinachokumbukwa na makali yake kwenye soka la Ulaya, ambapo alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne akiwa na timu tofauti. Kiungo huyo wa Kidachi wakati Inter Milan alihusika katika dili la kubadilishana wachezaji na wing-back wa kushoto, Francesco Coco. Seedorf alitua AC Milan, Coco alitua Inter.

10. Diego Simeone & Christian Vieri
Serie A imeonekana kuwa ni kitu cha kawaida kwa wachezaji kuhusika kwenye dili za usajili wa kubadilishana. Diego Simeone na Christian Vieri – walihusika kwenye dili la kubadilishana kwenye timu za Lazio na Inter katika dirisha la majira ya kiangazi 1999. Kwenye dili hilo, Inter iliongeza Pauni 28 milioni ili kunasa dili hilo la Vieri.
9. Diego Milito & Thiago Motta & Leonardo Bonucci na wengineo
Wengi wanakumbuka jinsi Samuel Eto’o alivyohama kutoka Barcelona kwenda Inter Milan iliyokuwa chini ya kocha Jose Mourinho na kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji matatu 2010. Wachezaji wanakumbuka jinsi Inter ilivyowachukua Milito na Motta kutoka Genoa huku ikiwapeleka upande mwingine Bonucci, Robert Acquafresca, Francesco Bolzoni na Riccardo Meggiorini.

8. Julio Baptista & Jose Antonio Reyes
Marehamu Reyes kwenye kiwango chake bora alikuwa matata sana uwanjani, lakini wakati anatoka Arsenal kurudi Hispania mwaka 2006, dili lake lilihusisha kubadilishana na Julio Baptista. Reyes alijiunga na Real Madrid kwa msimu mmja, akifunga mabao saba na asisti nne kwenye La Liga akibeba taji, wakati Baptista alifunga mabao 10, manne alifunga kwenye mechi dhidi ya Liverpool na aliasisti mara nne pia akiwa na kkosi cha Arsenal, lakini hakubeba taji lolote.
7. Ashley Cole & William Gallas
Ni kitu kinachoweza kukushangaza kwamba Cole ameshinda mataji mengi ya Ligi Kuu England akiwa Arsenal kuliko alipokuwa Chelsea. Beki huyo wa kushoto kwa miaka minane Stamford Bridge, alishinda taji la ligi mara moja tu, huku dili lake lilihusu la kubadiliana na Gallas, ambaye alitimkia zake Emirates. Lakini, Arsenal ilipata na ziada ya pesa pia, Pauni 5 milioni.

6. Ricardo Quaresma & Deco
Dili safi kabisa la kubalishana wachezaji liliwahi kutokea. Baada ya kutamba kwenye kikosi cha Barcelona, Quaresma alirudi kwao Ureno kujiunga na mabingwa FC Porto, kwenye dili ambalo lilimshudia kiungo mbunifu, Deco akiondoka kwenye timu hiyo na kwenda kujiunga Nou Camp na kwenda kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2006. Porto ililipwa pia Pauni 13 milioni pamoja na mchezaji Quaresma.
5. Alexis Sanchez & Henrikh Mkhitaryan
Unakumbuka jinsi Manchester United ilivyomtambulisha Alexis Sanchez kwa staili ya kupiga kinanda iliponasa huduma yake kutoka Arsenal kwenye dili lililomshuhudia mchezaji Henrikh Mkhitaryan akitimkia upande mwingine. Kila timu ilimthaminisha mchezaji wake kuwa na thamani ya Pauni 35 milioni, hivyo dili hilo la kubadilishana wachezaji lilikuwa na maana ya thamani hiyo ya pesa.

4. Luis Garcia & Fernando Torres
Staa matata kabisa Luis Garcia aliondoka Liverpool kwenda Atletico Madrid katika dili lililomhusisha straika Fernando Torres akitua zake Anfield. Kwenye dili hilo, ukiweka kando ishu ya kubadilishana wachezaji, Liverpool iliilipa pia Atletico, Pauni 21.5 milioni ili kunasa saini ya straika wa mabao Mhispaniola, Torres, ambaye alikwenda kuifanya Liverpool kuwa timu balaa sana uwanjani chini ya kocha Rafael Benitez.
3. David Luiz & Nemanja Matic
Ni kitu kinachokushangaza kwamba kuna nyakati mastaa hao wawili walicheza pamoja huko Chelsea, lakini kabla ya hapo, waliwahi kutumika kwenye dili la kubadilishana. Mwanzoni wakati Chelsea inamsajili Luiz kutoka Benfica ilimjumuisha Matic kwenye dili hilo ikimpeleka Ureno. Lakini, Matic alipojipata huko Benfica, Chelsea ilienda kumsajili tena na kumpa nafasi ya kucheza na Luiz.

2. Miralem Pjanic & Arthur
Fundi wa Kibrazili, Arthur alikuwa moto Barcelona, lakini aliondoka kwenye timu hiyo kutimkia Juventus katika dili lililomhusisha Pjanic. Lakini, dili hilo lilifurahisha kwa sababu Juventus ilimchukua Arthur kwa Euro 80 milioni, lakini Barca ilimchukua Pjanic kwa Euro 60 milioni na hilo limefanyika kwa makubaliano ya pande mbili na ndiyo dili hilo linaonekana kama la kubadilishana wachezaji.
1. Zlatan Ibrahimovic & Samuel Eto’o
Hii ni kiboko zaidi. Wachezaji wawili waliokuwa kwenye viwango bora kabisa vya soka, kuhusishwa kwenye dili la kubadilishana. Eto’o alitoka Barcelona kwenda Inter Milan, alikokwenda kubeba taji la pili mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Ibrahimovic alienda upande mwingine, kujiunga na Barcelona na kushinda La Liga, huku akifunga mabao 22 katika mechi 46 alizocheza ndani yam waka mmoja kwenye kikosi hicho cha Camp Nou.