Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Hivi ni nani kawaroga Manchester City?

Muktasari:

  • Mara nyingi katika safu hii tumeandika kuhusu hadithi nzuri ya uwekezaji mkubwa na mafanikio ya klabu ya Manchester City iliyopo Ligi Kuu ya England.

MPIRA una maajabu yake! Ni maneno tuliyoyazoea kuyasikia lakini sidhani kama ni maneno ambayo ni rahisi kuyaishi, hasa maajabu yanapokuwa ya matokeo hasi. Ni maneno ambayo mara nyingi tunayasikia lakini hatuoni maajabu kwa maana ya ajabu.

Mara nyingi katika safu hii tumeandika kuhusu hadithi nzuri ya uwekezaji mkubwa na mafanikio ya klabu ya Manchester City iliyopo Ligi Kuu ya England. Tumekuwa tukiandika kuhusu mafanikio yao ndani na nje ya uwanja. Tumeandika kuhusu utitiri wa pesa walizonazo na mataji waliyoyapata katika kipindi cha miaka 20 ya hivi karibuni. Wachezaji wazuri na viwango vya juu wamekuwa ni mali ya Manchester City na pia kocha wa viwango vya juu kabisa duniani na mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa katika Ulaya, Joseph 'Pep' Guardiola.

Hakuna mafanikio ambayo Man City hawakuweza kuyapata, kuanzia ubingwa wa England na vikombe mbalimbali vya ndani hadi ubingwa wa Ulaya na wa Dunia.

Mara ghafla, maajabu ya soka yameikumba klabu hiyo ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa kinara wa jiji la Manchester. Wanasema unapokwea hadi kileleni, anguko lako linakuwa na mshindo mkuu. Anguko la Man City limeishangaza dunia, kiasi kwamba hakuna anayejua kwa yakini chanzo na mwisho wa madhira wanayopitia.

Man City imekuwa na matokeo mabaya katika mashindano yote kiasi hata kocha Pep Guardiola anakiri kutojua chanzo cha ‘kipindi hiki kigumu’, kama ambavyo hajui mwisho wake.

Kinachoongeza mshangao ni ukweli kwamba Man City imechukua ubingwa wake wa nne wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita. Pia Man City iliuanza msimu huu vizuri na hadi sasa mshambuliaji wake kinara, ambaye sasa amekaukiwa, Erling Haaland tayari alikuwa amevuna mabao 13.

Pep na baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba majeraha kwa wachezaji wake muhimu yanaweza kuwa chanzo cha hali wanayopitia City. Hili linaweza kuwa na ukweli fulani, kwani wachezaji muhimu, hasa kiungo wao Rodri, kuwa nje ya uwanja kunaweza kuwa kumeiathiri timu kwa kiasi kikubwa.

Kiufundi timu inayofanya vizuri huzoea na uendelea kufanya vizuri ikiwa na kikosi ambacho hakibadilishwi sana. Inapotokea mchezaji au wachezaji muhimu wakakosekana basi timu hiyo inaweza kuwa na wakati mgumu kujitafuta kwa sababu itabidi kubadilisha aina ya uchezaji na wakati mwingine kunakuwa hakuna utayari kutoka kwa wachezaji ambao kwa muda mwingi wamekuwa hawatumiki sana.

Hakuna mwenye wasiwasi kuhusu uwezo wa Pep Guardiola kufundisha timu ikacheza mpira mzuri na kushinda. Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Barcelona ana tatizo la kuwa mchaguzi kupindukia. Pep siku zote atataka wachezaji wanaoingia moja kwa moja kwenye mfumo wake na kamwe hawezi kuingia katika mfumo wa wachezaji alionao. Tunakumbuka ndani ya Barcelona alivyomfukuza Samuel Eto’o na hata kumchezesha kwa muda, Thierry Henry ambao wote walikuwa wachezaji wa viwango vya juu isipokuwa kwa Pep. Hata alipohamia City akitokea Bayern Munich ya Ujerumani, Pep alimweka benchi Yaya Toure ambaye alikuwa na kiwango chake kizuri lakini si machoni mwa kocha huyo. Kuna msemo kwamba ombaomba hatakiwi kuwa mchaguzi. Inawezekana tabia hii ya kuwa mchaguzi inachangia kwa kiasi kikubwa kwa matokeo mabaya ya Pep. Hajajiandaa kucheza aina ya mpira inayoendana na wachezaji alionao. Yawezekana ameshalemazwa na mpira wake wa kishikwambi kiasi kwamba hawezi kufundisha mpira wa muhimu ushindi kama walivyokuwa wakifanya akina Mourinho na Mzee Alex Ferguson.

Kupoteza michezo 9 katika michezo 12 si jambo ambalo Pep amewahi kukumbana nalo. Kabla ya hapo Man City walipoteza michezo tisa katika michezo 106. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani hili anguko ni la mshindo mkuu.

Unajiuliza ni kwa muda gani uongozi wa Man City utamvumilia Guardiola? Ni kweli ameshinda karibu kila kitu na klabu hiyo na hata wakimtimua hawajajiandaa na kocha mbadala. Yeye mwenyewe haonyeshi dalili ya kujiuzulu kabla ya kumaliza mkataba alooongezewa kwa miaka miwili.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, Pep anaweza kujenga hoja kwamba kikosi kimechakaa hivyo kuomba kuimarisha kikosi ili kiwe imara wakati atakapokabidhi kwa kocha atakayemrithi. Kuchakaa kwa kikosi ni kitu kinachowezekana hasa kama ujenzi na usajili haukutilia maanani sana swala la uendelevu (sustainability) wa timu.

Inasemekana wakati mambo hayaendi vizuri pale Barcelona, Pep aliwahi kuwauliza marafiki wawili Babu Alex Ferguson na Raphael Benitez kuhusu nini cha kufanya wachezaji wanapokuwa hawakuelewi kama kocha. Marafiki zake walimwambia hali ya kutokueleweka ikijitokeza haondoki kocha bali wachezaji. Hivyo ndivyo inavyoelekea atafanya Pep; ataanza kupunguza wachezaji na kuajiri wachezaji wapya watakaomuelewa. Ataajiri wachezaji wenye njaa ya mafanikio.

Suala la ubingwa wa England na Ulaya itabidi kwa sasa ajitahidi kulisahau na kujaribu kumaliza vizuri inavyowezekana. Japo mpira ni mchezo wa maajabu, bado maajabu yako mbali kuweza kupambana sio na Liverpool pekee, lakini kuna Chelsea na Arsenal.

Si pesa za tajiri wa Ghuba, Sheikh Mansour na mbinu za Pep Guardiola zilizoitisha Ulaya ambazo zimefaa kutibu ugonjwa ulioikumba Etihad. Hadi hapa haijulikani kama Sheikh Mansour ataendelea kumwaga maburungutu ya fedha kadri atakavyozihitaji kocha huyo kutoka Catalunia au ataamua kuvunjilia mbali kandarasi ya kocha huyo na kuleta kocha mpya. Bila kuujua ugonjwa kuna hatari ya kupoteza fedha katika kujaribu kuutibu. Ni maajabu ya mpira yatakayoirudisha City relini katika mbio za ubingwa wa EPL 2024/25.


Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.