Nguo tano mwanamke hutakiwi kuzikosa
Muktasari:
- Siri ya kuvaa vizuri si kuwa na nguo nyingi wala kutumia fedha nyingi kununua mavazi ya gharama, bali kuwa na nguo chache zinazoweza kuvaliwa katika mazingira tofauti na kuendana na mavazi mengine.
Kuna wanawake wana kabati lililojaa nguo lakini kila wanapofungua wanajikuta wakisema, “Leo nivae nini?” Nguo zimejaa, viatu vimejaa, lakini bado wanapata wakati mgumu kuchagua vazi linalowafanya waonekane nadhifu, wa kisasa na wenye kujiamini.
Siri ya kuvaa vizuri si kuwa na nguo nyingi wala kutumia fedha nyingi kununua mavazi ya gharama, bali kuwa na nguo chache zinazoweza kuvaliwa katika mazingira tofauti na kuendana na mavazi mengine.
Mwanamke mwenye kabati lililopangiliwa vizuri anaweza kubadilisha muonekano wake kwa urahisi bila kulazimika kununua vazi jipya kila anapokuwa na shughuli. Zipo nguo tano ambazo kila mwanamke anapaswa kuzitazama kama msingi wa kabati lake.
1. SHATI LA RANGI NYEUPE
Shati jeupe ni moja ya mavazi muhimu ambayo mwanamke hapaswi kuyakosa. Linaweza kuvaliwa kazini na suruali ya kitambaa, sketi ndefu au koti rasmi, lakini pia linaweza kuvaliwa kwenye matembezi kwa kulichanganya na jinzi na viatu vya kawaida.
Uzuri wake ni kwamba halifungi mtu kwenye mtindo mmoja na linaendana na rangi nyingi. Ni muhimu kuchagua shati linalokutosha vizuri, lisiloonyesha mwili kupita kiasi na lenye kitambaa kisichoonekana chepesi kupita kiasi. Mwanamke anaweza kuwa na shati moja zuri na kulitumia katika mitindo tofauti bila kuonekana kama amevaa kitu kilekile kila siku.
2. JEANS INAYOKUTOSHA VIZURI
Jinzi ni vazi linaloweza kuokoa siku nyingi ambazo mwanamke hana muda wa kufikiria mavazi ya kuvaa. Jinzi ya bluu iliyokolea au nyeusi inaweza kuvaliwa na shati jeupe, blauzi, fulana au sweta kulingana na shughuli za siku hiyo. Muhimu ni kuchagua inayokutosha vizuri kiunoni na miguuni bila kubana kiasi cha kukukosesha uhuru wa kutembea.
Kwa mazingira ya kawaida, unaweza kuivaa na raba, huku viatu vya kisigino kifupi vikikupa muonekano rasmi zaidi. Jinzi nzuri si lazima iwe ya chapa maarufu cha msingi ni ubora wa kitambaa, mshono na namna inavyokaa mwilini.
3. GAUNI LA RANGI ISIYOPIGA KELELE
Gauni la rangi nyeusi, bluu iliyokolea, kahawia au kijani cha wastani ni muhimu kwa mwanamke anayependa kuwa tayari kwa shughuli tofauti. Gauni lenye muundo rahisi linaweza kuvaliwa kazini, kwenye chakula cha jioni au kwenye hafla inayohitaji muonekano nadhifu kwa kubadilisha viatu, mkoba na mapambo.
Kwa mfano, gauni jeusi likivaliwa na viatu vya kawaida linaweza kufaa katika shughuli za mchana, lakini likiambatana na viatu vya kisigino na mkoba mdogo linaweza kufaa zaidi jioni. Ni vizuri kuchagua muundo unaokufaa na unaokupa nafasi ya kutembea na kukaa kwa uhuru.
4. BLAUZI AU SWETA
Blauzi zuri au sweta jepesi ni muhimu kwa sababu linaweza kuvaliwa peke yake au ndani ya koti, kutegemea hali ya hewa na mazingira. Mwanamke anaweza kulichanganya na jinzi kwa matembezi, au suruali ya kitambaa kwa shughuli za kikazi.
Rangi kama krimu, kijivu, kahawia na nyeusi ni rahisi kuendana na nguo nyingine. Ni vyema kuchagua kitambaa kinachopendeza kwenye ngozi na kisichopoteza umbo haraka baada ya kufuliwa. Vazi hili linafaa hasa kwa mwanamke anayehitaji kubadilisha mtindo bila kununua mavazi mengi.
5. SULUARI YA KITAMBAA
Suruali ya kitambaa ni vazi muhimu kwa mwanamke anayehitaji kuonekana nadhifu kazini, kwenye mikutano au katika shughuli rasmi. Suruali nyeusi, kijivu au ya kahawia inaweza kuvaliwa na shati jeupe, blauzi ya rangi au koti rasmi. Ukichagua suruali yenye mshono mzuri na urefu unaokufaa, unaweza kuitumia kwa muda mrefu bila kuchoshwa nayo. Ni muhimu kuzingatia ubora wa kitambaa na namna inavyokaa mwilini badala ya kununua kwa sababu tu mtindo huo umeonekana kwa watu wengine.
USHAURI
Mwanamke hakikisha unanunua nguo zinazolingana na maisha yake, kazi yake, mazingira anayoishi na uwezo wake wa kifedha badala ya kufuata kila mtindo unaoibuka. Kabla ya kununua vazi jipya, jiulize kama linaweza kuvaliwa na angalau nguo tatu ulizonazo tayari, kama linakutosha vizuri na kama kitambaa chake kina ubora unaostahili fedha unayotumia.