NGOMA NGUMU: Kanuni kali migusano pigo la kona ilivyobadili mambo Ligi Kuu England
Muktasari:
- Katika miaka michache iliyopita, matukio ndani ya eneo la penalti wakati wa mipira ya kona, ambayo ndiyo aina inayotumika zaidi ya mipira iliyokufa katika mashambulizi ya soka yalikuwa yamegeuka kuwa kama mipambano ambayo ungeweza kutarajia kuiona jukwaani kuliko uwanjani.
LONDON, ENGLAND: WAAMUZI katika Ligi Kuu England (EPL), wameagizwa kuchukua hatua kali dhidi ya wachezaji wanaoshikana wakati wa mipira ya kona, na takwimu zinaonekana kuonyesha kwamba hatua hiyo imeanza kuwa na athari mara moja. Mipira ya kona ilikuwa imekuwa tatizo.
Katika miaka michache iliyopita, matukio ndani ya eneo la penalti wakati wa mipira ya kona, ambayo ndiyo aina inayotumika zaidi ya mipira iliyokufa katika mashambulizi ya soka yalikuwa yamegeuka kuwa kama mipambano ambayo ungeweza kutarajia kuiona jukwaani kuliko uwanjani.
Hali hiyo ilifikia kiwango kibaya zaidi msimu uliopita wa 2025/26, ambapo karibu kila kona ilionekana kila mchezaji akiwa amemshika mpinzani wake. Wengi hawakuwa na nia hata ya kuangalia au kufikiria mpira ulikuwa wapi. Hali ilikuwa mbaya sana huku mipira iliyokufa ikizidi kuwa sehemu kubwa ya soka la EPL kuliko ilivyowahi kuwa awali, licha ya uwezo wa kiufundi wa wachezaji kufikia kiwango kipya cha juu.
Mabao yalifungwa kwa wingi, huku 188 yakitokana na mipira ya kona, idadi kubwa zaidi katika msimu wowote tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo. Kwa ujumla, ni jambo zuri mabao yanapofungwa kwa wingi kwa sababu mara nyingi humaanisha mashabiki huburudika zaidi.
Lakini, kushikana kulikuwa kumezidi kiasi kwamba mipira ya kona ilikuwa imekuwa migumu kuilinda. Kuzuiana na kushikana kulikuwa kumeenea kukawa sehemu ya mbinu za kujaribu kufunga kupitia kona na kuwa jambo la kawaida kwa timu zinazoshambulia.
Kulikuwa na timu zilizokuwa zikichagua wachezaji kutokana na uwezo wao ndani ya eneo la penalti. Ongezeko la mabao lilikuwa limeanza kuwa tatizo badala ya faida. Jambo muhimu zaidi kwa wasimamizi wa mchezo huo, msongamano wa wachezaji ndani ya eneo la mita sita na ukweli kwamba karibu kila mtu alikuwa akimshika mwingine ulifanya iwe vigumu sana kwa waamuzi kusimamia ipasavyo. Mengi ya matukio hayo ya kushikana ambayo hayakuonekana na waamuzi yalichangia moja kwa moja baadhi ya mabao hayo kufungwa.
MSIMU HUU SASA
Msimu huu, Pro Ref, jina jipya la PGMOL, chombo kinachosimamia uamuzi wa mechi katika soka la England kilifanya tathmini upya. Uamuzi ukafikiwa kwamba kulikuwa na haja ya kuweka mkazo zaidi katika kutoa adhabu katika vitendo vya kushikana ambavyo vina athari ya wazi na ya moja kwa moja. Yaani, wachezaji kuzuiwa kufikia mpira kutokana na kushikwa na mpinzani.
Msisitizo uliwekwa kwenye kushikana kusikohusiana na kucheza mpira ambako hakuna nafasi kwenye uwanja wa soka. Pro Ref ilijaribu kubainisha kwa usahihi kile ambacho kingehesabiwa kuwa faulo, lakini kama ilivyo kwa karibu sheria zote za soka, mabadiliko hayo yalitegemea kwa kiwango fulani tafsiri ya mwamuzi, ikimaanisha hakukuwa na uwezekano wa kuzuia mijadala isiyoisha na uchambuzi wa kila uamuzi.
Hata hivyo, viongozi walitoa tahadhari; “tunajaribu kuwafanya waamuzi wawe na ujasiri kadiri wanavyoweza katika kutoa adhabu kwa kile wanachokiona,” alisema Howard Webb, mkuu wa waamuzi wa EPL.
“(Hii inamaanisha) kutoa maonyo machache, adhabu kwa matukio mengi zaidi, na ikiwa kutakuwa na kupungua kwa makosa yanayotolewa adhabu, hilo linapaswa kuwa matokeo ya mabadiliko ya tabia za wachezaji badala ya sisi kuacha tena kutumia sheria hiyo.”
TANO ZA KWANZA
Mechi tano za kwanza za ligi hiyo msimu wa 2026/27 zimetoa nini kuhusu mipira ya kona? Je, tabia zimebadilika kama Webb alivyotarajia, na je, kumekuwa na mabadiliko yoyote katika matokeo ya mipira ya kona? Jambo la kwanza la kuzingatia ni kwamba inaonekana kama kuna kushikana kidogo. Mipira ya kona inaonekana kuwa na vurugu kidogo msimu huu, na ingawa bado zimecheza mechi tano pekee, ni muhimu kwamba hakujawa na matukio mengi makubwa ya kutatanisha.
Kwa mfano, hakuna penalti hata moja iliyotolewa ndani ya sekunde 25 baada ya mpira wa kona kupigwa msimu huu kwa kosa la aina yoyote wakati msimu uliopita kulikuwa na penalti 21. Hii inamaanisha wametoka kwenye penalti moja kutolewa kwenye kona kila baada ya mechi 18 msimu uliopita hadi kutokuwepo kwa penalti hata moja katika mechi 50 zilizochezwa hadi sasa msimu wa 2026/27.
Hata hivyo, mipira mingi zaidi ya kona imesababisha faulo kutolewa kwa timu inayolinda. Asilimia 3.8 ya mipira ya kona ambayo ilisababisha faulo kutolewa ndani ya sekunde tano baada ya kona kupigwa msimu huu ndiyo kubwa zaidi katika misimu saba ambayo takwimu hizi zinapatikana kuanzia 2020/21.
Hilo linaashiria kwamba tabia za mabeki zimebadilika kwa kuhofia kutoa penalti, wakati washambuliaji wanajaribu kufanya vitendo hivyo bila kuadhibiwa (ingawa haijulikani kwa kiwango gani hasa), lakini wanaadhibiwa zaidi wanapofanya hivyo. Hatari ni kubwa mno kwa mabeki, lakini kwa washambuliaji, uwezekano wa kupewa faulo wakati kuna nafasi ya kufunga ni hatari ambayo wanaweza kuwa tayari kuibeba. Pia huenda mabeki wanatumia vizuri mawasiliano yoyote ya mwili, wakijua kwamba waamuzi wanatazama kwa makini zaidi faulo za aina hiyo.
Kuna penalti iliyotolewa kutokana na kushikana katika aina nyingine ya mpira uliokufa msimu huu, Sunderland wakipewa dhidi ya Arsenal baada ya mpira wa kurusha, ambapo Ezri Konsa aliamuliwa kuwa amemfanyia faulo Dan Ballard, lakini jopo la EPL la matukio muhimu ya mechi baadaye liliamua kwamba ilitolewa kimakosa.
Hivyo, hata penalti hiyo moja iliyotolewa kutokana na kushikana ndani ya eneo la penalti baadaye iliamuliwa kuwa tukio hilo halikuwa baya kama lilivyoonekana mwanzoni, jambo linaloendelea kuashiria kwamba mabeki wanakuwa waangalifu zaidi ndani ya maeneo ya penalti.
Kutokana na mwanzo wa msimu huu, inaonekana kwamba tishio la usimamizi mkali zaidi wa sheria limefanya matumaini ya Webb yaanze kutimia, huku wachezaji wakibadilisha tabia zao.
HAKUNA NAMNA, JE NAMBA VIPI?
Hata kama tabia za washambuliaji hazijabadilika vya kutosha, ongezeko la faulo zinazotolewa kwa timu inayolinda huenda hatimaye likasaidia kutatua suala hilo. Pia kumekuwapo na upungufu mkubwa wa idadi ya mabao yanayofungwa kutokana na mipira ya kona, jambo ambalo linaweza kuwa matokeo ya ongezeko la faulo zinazotolewa, lakini pia linaweza kuonyesha kwamba washambuliaji wanapata ugumu zaidi kuliko awali kuwazuia au kuwashika wapinzani wao kwa “vitendo visivyohusiana na kucheza mpira.”
Hadi sasa msimu huu, mabao 14 yamefungwa kutokana na mipira ya kona yakichangia asilimia 9.9 ya mabao yote. Hiyo ni asilimia ya pili kwa uchache katika msimu wowote wa Ligi Kuu England, jambo ambalo linavutia zaidi kwa sababu linakuja baada ya msimu wa 2025/26 ambao ulizalisha kwa mbali asilimia kubwa zaidi ya mabao yaliyofungwa kutokana na mipira ya kona (18.0%).
Arsenal ambao waliweka rekodi mpya ya kufunga mabao mengi zaidi kutokana na mipira ya kona katika msimu mmoja walipokuwa wakielekea kutwaa taji la ligi hiyo msimu uliopita wakifunga mara 19, wanaweza kusema kwamba mipira ya kona ni njia halali ya kushambulia. Tottenham Hotspur pia ambao walinusurika kushuka daraja kutokana na mabao 18 ya mipira ya kona (idadi ya pili kwa wingi katika msimu mmoja wa ligi hiyo baada ya Arsenal), wanaweza kukubaliana na wapinzani wao. Hakuna hata mmoja kati yao aliyefunga bao la kona msimu huu, na Spurs wanapata wakati mgumu.
Lakini, inakubalika kwa kiasi kikubwa kwamba mkazo uliowekwa kwenye mipira ya kona ulikuwa mkubwa kupita kiasi msimu uliopita; kwamba mipira iliyokufa ilichukua nafasi kubwa. Kuna fedha nyingi na vipaji vingi katika soka la ligi hiyo siku hizi kiasi kwamba ilionekana kama ni jambo la kusikitisha kuwaona mastaa wakibadilishwa kuwa wanaopambana kwa nguvu ndani ya eneo la penalti.
Kwa wale wanaoona hivyo, huenda kukawa na matumaini sasa kwa kuwa karibu idadi ya chini kabisa kuwahi kutokea ya mabao inafungwa kutokana na mipira ya kona. Hilo linaweza kusababisha kupungua kwa muda, umakini na nguvu ambazo timu zinaweka katika kupanga mipira iliyokufa. Ikiwa mipira ya kona haitakuwa tena njia yenye tija kubwa ya kufunga mabao timu chache zitasumbuka kupanga mbinu tata na zisizopendeza za kuzuiana zinapopata nafasi ya kupiga kona.
Lakini, je mbele ya safari utaonekana ufanisi wa mipira ya kona ukipungua? Huenda isiwe hivyo, kwa sababu nafasi zinaendelea kutengenezwa kwa kiwango cha kawaida. Wastani wa mabao yanayotarajiwa (XG) kwa kila mchezo kutokana na mipira ya kona umepungua kidogo kutoka msimu uliopita 0.46 kwa kila mchezo hadi 0.38.
Sababu ya kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mabao huenda ikawa katika kiwango cha chini cha ufungaji ukilinganisha na mabao yanayotarajiwa kwenye mipira ya kona. Mabao 14 ya kona yaliyofungwa msimu huu yametokana na yanayotarajiwa (xG) 19.2.
Iwapo mashuti yangekuwa yamefunga kwa kiwango kinacholingana na mabao tarajiwa kwenye mipira ya kona msimu huu, yangekuwa yamezaa mabao 19. Hilo lingemaanisha mabao ya kona yangechangia asilimia 13.0 ya mabao yote ambayo yangekuwa asilimia ya 12 kwa wingi katika historia ya Ligi Kuu England kwa kiwango cha bao 0.38 kwa kila mchezo, ambacho kingekuwa cha tano kwa ukubwa kuwahi kutokea.
Kwa maneno mengine, iwapo umaliziaji kwenye mipira ya kona ungekuwa na ufanisi unaotarajiwa kulingana na mabao tarajiwa mashabiki wangeshuhudia idadi kubwa kiasi ya mabao ikifungwa badala ya karibu kuwa kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea.
Mipira ya kona bado ni njia yenye ufanisi mkubwa ya kufunga mabao, na timu zitaendelea kuitumia kadiri zinavyoweza ili kuongeza nafasi ya kupata mafanikio. Huenda mashabiki wakashuhudia tabia bora zaidi kwa ujumla mwanzoni mwa msimu huu, lakini hilo halitazizuia timu kuendelea kusukuma kile wanachoweza kufanya bila kuadhibiwa wakati wa mipira ya kona.