Prime
Nassor Idrissa, Father aliyepenya Bodi ya Ligi katika tundu la sindano
RAIS wa Azam FC, Nassor Idrissa 'Father' amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) baada ya kumshinda mpinzani wake Hosseah Lugano (mwenyekiti wa Namungo FC) kwa tofauti ya kura moja.
Father alipata kua saba dhidi ya sita za Hosseah na kumfanya kuwa mwenyekiti aliyepata ushindi mdogo zaidi katika historia ya uchaguzi wa chombo hicho cha kuendesha ligi za kulipwa hapa nchini kinachosimamia uendeshaji wa ligi kubwa tatu za kulipwa nchini; Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship na First League.
Chombo hiki kilianzishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa ridhaa ya mkutano mkuu wa sita uliofanyika Aprili 21 hadi 22, mwaka 2012.
Awali mkutano huo ulitakiwa kufanyika Machi 24 hadi 25 mwaka huo, lakini Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 10 mwaka huo chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodeger Tenga, ikausongeza mbele.
Chombo hicho kikaanza kazi yake rasmi Novemba 2013 baada ya kufanya uchaguzi wake wa Oktoba 25 na kupata viongozi na Hamad Yahaya Juma, Mwenyekiti wa Mtibwa Sugar akachaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kupata kura zote 10 za wajumbe waliokuwepo siku hiyo.
Wakati TPLB ilikuwa na dhamana ya Ligi Kuu pekee na kulikuwa na timu 14, lakini nne hazikuhudhuria mkutano huo wa uchaguzi ambazo ni JKT Ruvu Stars (sasa JKT Tanzania), Mgambo Shooting ya Kabuku Tanga, Coastal Union ya Tanga na Rhino Rangers ya Tabora. Hamad hakuwa na mpinzani hivyo alipita bila kupingwa.
Uchaguzi uliofuata ulifanyika Oktoba 15, 2017 na Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alimwangusha Hamad kwa kura 10 dhidi ya sita.
Hata hivyo, Sanga hakudumu sana kwenye nafasi hiyo, kwani Julai 12, 2018 Kamati ya Utendaji ya TFF ilimvua uenyekiti na kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, aliyetoa taarifa hiyo uamuzi huo ulifuatia mapendekezo ya Kamati ya Sheria na Katiba ya TFF kwamba alipoteza sifa.
Sanga aligombea nafasi hiyo na kushinda akiwa kama mwenyekiti wa Yanga baada ya kujiuzulu kwa Yusuf Manji.
Ikumbukwe alikuwa makamu mwenyekiti wa Yanga kuanzia Julai 2012 baada ya uchaguzi wa kuziba viraka kutokana na kujiuzulu kwa mwenyekiti Lloyd Nchunga na makamu wake, Davies Mosha na Manji akachaguliwa kuwa mwenyekiti na Sanga kuwa makamu wake.
Hata hivyo, mwaka 2016 Manji akajiuzulu uenyekiti wa Yanga na Sanga kukaimu nafasi hiyo na hapo ndipo alipopata sifa ya kugombea uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu kwa sababu nafasi hiyo ni maalumu kwa viongozi wakuu wa klabu, wenyekiti au marais.
Juni 10, 2018 wanachama wa Yanga katika mkutano wao mkuu, walitoa kauli ya pamoja wakisema wanamtambua Manji kuwa bado mwenyekiti wao, hii ikamaanisha Sanga anarudi kwenye nafasi yake ya makamu mwenyekiti, hivyo akapoteza sifa.
Hapo ndipo Kamati ya Sheria na Katiba ya TFF ikapendekeza kwa Kamati ya Utendaji ya TFF kumvua uenyekiti Sanga na ndipo Julai 12 akavuliwa.
Desemba Mosi, 2018 ukafanyika uchaguzi ili kuziba nafasi ya Sanga na mwenyekiti wa Coastal Union, Stephen Mnguto akashinda kwani hakuwa na mpinzani...na akapata kura 16 kati ya 18, huku mbili zilimkataa.
Uchaguzi uliofuata ukapangwa ufafanyike Mei 14, 2021 lakini ukasogezwa mbele hadi Novemba 27, 2021 kutokana na mwitikio hafifu wa wagombea kwenye nafasi mbalimbali.
Pia Mnguto alipita bila kupingwa baada ya watia nia wenzake, Murtaza Mangungu (Mwenyekiti wa Simba) na Dk Mshindo Msolla (Mwenyekiti wa Yanga) kuenguliwa na kamati ya uchaguzi na hivyo, alikaa madarakani hadi Juni mwaka huu alipojiuzulu nafasi yake na makamu wake Nassor Idrissa kukaimu hadi ulipofanyika uchaguzi wa sasa.
MAANA YA USHINDI MWEMBAMBA
Soka ni mchezo wa siasa kuliko siasa zenyewe. Kitendo cha Father kushinda kwa pengo dogo, maana yake mpinzani wake anakubalika sana.
Kukubalika huku kunaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa Father katika utendaji wake endapo waliomkataa watacheza mdundo tofauti na hapa ndipo panapohitaji busara ya kiwango cha lami kuvuka vikwazo hivyo.
Siasa cha mpira katika uchaguzi uliompa nafasi Father, inasemekana kuna pande mbili zilizowekeza ili kumpata mtu wao.
Upande mmoja ulimtaka Mzee Said Soud wa Coastal Union ya Tanga aliyehamia Mtibwa na kuwa mwenyekiti.
Huyu ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Hadhi za Wachezaji, wakati wa kesi ya Feisal Salum 'Fei Toto'.
Upande mwingine ukamtaka Hosseah wa Namungo na kila kitu kikaenda sawa.
Hata hivyo, Said Soud akakatwa na kamati ya uchaguzi kwa sababu za kiufundi na upande uliokuwa unamtaka ukajikuta ukihamishia karata yao kwa Nassor Idrisa, ili tu kushindana na upande mwingine.
Kwa hiyo upande huo ukawa kwa 'Father' na ule mwingine ukawa kwa Lugano.
Uchaguzi ukageuka mechi ya pande mbili...ikawa kama dabi!
Hivyo ushindi wa Father ni ushindi wa upande uliomsapoti...ingawa kwa picha pana unapaswa kuwa ushindi wa mpira kwa jumla na ili hilo liwezekane inabidi kambi za uchaguzi zikazika tofauti zao na kuwa kitu kimoja na maneno ya Father baada ya ushindi ni ishara ya umoja katika soka letu.
Bodi ya Ligi iliyo imara ndio ligi imara...na ligi imara ndio mpira imara.