Dabi kuahirishwa ni aibu, ila la Kocha Ahmad ni aibu zaidi
Muktasari:
- Kusimama kwa shughuli nyingi kulisababisha ratiba za mambo mbalimbali pia kuharibika ikiwamo ya Ligi Kuu Bara na mechi kadhaa zilizopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huo na mwanzoni mwa Novemba, kuahirishwa.
VUURUGU za siku kadhaa kuanzia Oktoba 29, ulipofanyika Uchaguzi Mkuu nchini, zilisababisha mambo mengi kusimama ikiwamo michezo.
Kusimama kwa shughuli nyingi kulisababisha ratiba za mambo mbalimbali pia kuharibika ikiwamo ya Ligi Kuu Bara na mechi kadhaa zilizopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huo na mwanzoni mwa Novemba, kuahirishwa.
Athari hizo za ratiba ziliigusa hadi ya mechi ya dabi ya watani wa jadi, Yanga na Simba na Bodi ya Ligi Kuu Bara imezipangia kukutana Machi Mosi mwakani, badala ya Desemba 13 mwaka huu.
Taarifa hizo zinasema mamlaka zinapanga mechi zilizoahirishwa zifanyike Desemba ingawa mwezi huo pia kutakuwa na ratiba ya mechi za Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 64 Bora na hiyo ya watani. Kwa kifupi, Desemba itakuwa na mechi nyingi zilizobanana.
Inaelezwa kusogezwa mbele kwa mechi hiyo inatokana na ishu ya maandalizi na wakubwa watakosa muda wa kujiandaa nayo.
Ni wazi mamlaka zinaona kuweka mechi ya watani katika mwezi wenye mechi nyingi halitokuwa jambo la busara na zile za FA zinazozihusu timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa huenda zikaondolewa.
Kamati ya Mashindano ya TFF iliwahi kupendekeza timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zisianzie hatua hii ya 64 Bora, lakini wakuu wa mpira wakakataa.
Lakini kwa namna ratiba ilivyobana sasa, wakuu hao wanajuta kwa kukataa pendekezo lile na kwa hali ilivyo, huenda msimu ujao likakubaliwa na likawa na maana kuliko kuhamisha mechi ya watani.
Ilitakiwa kama ratiba imebana, basi mechi hiyo itafutiwe muda mwingine kama mechi ya kiporo na siyo ile iliyopo katika ratiba, kwani tabia ya kuzidekeza Yanga na Simba ndizo baadaye huwatokea puani.
Mechi zinapaswa kuchezwa kulingana na ratiba hata kama ni ngumu, haitakiwi kuwapa upendeleo kwa baadhi ya timu.
Mamlaka za mpira ni kama hazijajifunza kwa kilichotokea msimu uliopita, wanataka kuleta tena malumbano yasiyo na maana.
Kupangua ratiba siyo kitu kigeni katika soka, hata Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lililazimika kufanya hivyo hivi karibuni baada ya droo ya hatua ya makundi kufanyika na wakatoa ratiba mpya na kuzijulisha klabu na wadau wa soka.
Ikumbukwe CAF ilitoa fomu kwa timu shiriki kuchagua siku na muda wa mechi zao za nyumbani na zikachagua tofauti na ule ambao CAF ilipanga awali...hivyo, ratiba ikavurugika.
Kisha siku chache baadaye CAF wakatoa tena ratiba nyingine kuibadili ile iliyopangwa na klabu kupitia fomu zilizotolewa na shirikisho hilo.
Haya yote yametokea ndani ya wiki moja tu...kwa hiyo Bodi ya Ligi kurekebisha ratiba haliwezi kuwa jambo kubwa.
Ila kuihamisha mechi ya Yanga na Simba kwa sababu ya kuwapa muda wa kujiandaa siyo sawa.
AIBU YA AHMAD ALLY
Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Ahmad Ally ameshindwa kusafiri na timu hiyo kwenda Misri kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Kuwait. Mechi hiyo ilipigwa Jumamosi na Stars kulala kwa mabao 4-3.
Sababu ya kocha huyo kushindwa kusafiri ni kukosa hati ya kusafiria, yaani pasipoti.
Hii ni aibu kubwa sana kwa kijana kama yeye. Siku zote yupo nchini na anajua anafanya kazi za mpira ambazo wakati wowote anaweza kusafiri nje, lakini alikaa tu.
Januari mwaka huu alipewa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars iliyoshiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024.
Hii ilikuwa ishara wakati wowote chochote kinaweza kutokea...lakini hakujipanga.
Umefika wakati anatakiwa kusafiri...hana pasipoti, aibu sana!
Hili ni fundisho kwa wadau wengine katika nyanja mbalimbali za mpira.
Wachezaji, waandishi, makocha, madaktari na kadhalika ni muhimu kuwa na pasipoti kwa sababu wakati wowote chochote kinaweza kutokea.