Prime
Mzizima Derby… Mtajua hamjui!
Muktasari:
- Rekodi zinaonyesha pia, Mkenya Mike Barasa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika pambano moja baina ya timu hizo akifanya hivyo katika mechi ya Machi 14, 2010 wakati Simba ikishinda ugenini mabao 2-0.
BAADA ya awali kuikosa burudani ya mchezo wa kwanza kati ya Azam FC na Simba uliopelekwa visiwani Zanzibar, safari hii mashabiki wa soka wamesogezewa uhondo wakati timu hizo zitakaporudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kutoka KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo la kukata na shoka linachezwa leo ikiwa ni Dabi ya Mzizima nyingine ambayo inashikilia hesabu za mbio za ubingwa kwa msimu huu.
Asikuambie mtu, pambano baina ya Azam na Simba lina mvuto na msisimko wake na huziweka juu juu roho za mashabiki kutokana na ushindani uliopo baina ya timu hizo tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008.
Ingawa timu hizi zimekuwa zikikutana na kuonyeshana kazi katika michuano mbalimbali ikiwamo ile ya Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA), Mapinduzi, Kombe la Muungano na Kombe la Kagame, hapa chini Mwanaspoti inakuletea rekodi kadhaa za michezo 33 ya ligi baina ya timu hizo tangu msimu wa 2008-2009, pale Azam ilipopanda daraja.
Utamu ni timu hizo zinakutana huku vikosi vyote viwili vikiwa chini ya makocha wa kigeni, Azam ikiwa na Mmorocco Rachid Taoussi na Simba ina Msauzi, Fadlu Davids wanaokutana kwa mara ya pili katika Ligi Kuu Bara, zote zikiwa na wachezaji mahiri waliobeba hatma ya matokeo.
UBABE UBABE
Katika michezo 33 baina ya timu hizo, Simba ndio wanaoonekana kuwa wababe zaidi mbele ya Azam kwa takwimu mbalimbali.
Simba imeshinda michezo mingi zaidi mbele ya Azam, ikifanya hivyo mara 15 dhidi ya sita tu ya Wanalambalamba, huku ikiongoza pia kwa idadi ya mabao ya kufunga ikiwa na 46 dhidi ya 29 ya wageni wa mchezo, yaani Azam.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zimeshindwa kutambiana katika mechi 12 iliyoisha kwa sare tofauti, huku Simba ikivuna jumla ya pointi 57 katika michezo yote 33 dhidi ya 30 za wapinzani wao ambao msimu huu walichezea kichapo cha mabao 2-0 zilipokutana katika mchezo wa kwanza pale New Amaan.
Simba imepoteza mechi nne ikiwa nyumbani, huku ikitoka sare tano ikiwa wenyeji, wakati ni mechi mbili tu ndizo ilizopoteza ikiwa ugenini na kutoka sare saba ikicheza huko.
Hali ni tofauti kwa Azam kwani imepoteza michezo nane nyumbani sawa na imepoteza saba ugenini na pia kupata sare saba wakiwa wenyeji, ilihali imeambulia sare tano ugenini mbele ya Simba.
Ni mara tatu timu hizo katika Ligi Kuu zimekutana nje ya Dar es Salaam baada ya lile la Sept 11, 2010 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, uliotumiwa kama uwanja wa nyumbani wa Azam na timu hiyo kulala 2-1 mbele ya Mnyama.
Mechi nyingine iliyopigwa nje ya Dar ni ile ya msimu uliopita lililochezwa Februari 9 mwaka huu na Simba ikiwa wenyeji waliupeleka CCM Kirumba, jijini Mwanza na kumalizika kwa sare ya 1-1, Mnyama ikichomoa dakika za lala salama bao la Prince Dube kupitia Clatous Chama na msimu huu zilienda kuvaana visiwani Zanzibar, Azam ikiwa wenyeji walilala 2-0. Mabao ya mchezo huo yaliwekwa kimiani na Leonel Ateba na Fabrice Ngoma.
Na kama hujui, pambano moja tu baina ya timu hizo katika Ligi Kuu liliwahi kulazwa kiporo na kulazimika kuchezwa siku mbili, likiwa ni lile ulilopigwa Machi 30, 2009 na la kwanza lilipigwa siku moja na kushindwa kumalizika kutokana na mvua kubwa na kurudiwa kesho yake na Azam iliyokuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano kwa msimu wa 2008-2009 ikalala mabao 3-0.
MABAO 75
Katika mechi hizo 33 zilizopigwa hadi sasa wanaume hao wamezalisha jumla ya mabao 75, ikiwa ni wastani wa kila mechi moja kuzalisha mabao 2.27, huku Simba ikiongoza kwa kufunga mabao 46 ikiwa ni wastani wa kufunga mabao 1.39 kwa kila mchezo, huku Azam yenye mabao 29 ikiwa na wastani wa 0.87 ya bao kwa kila mechi hizo 33 ilizocheza hadi sasa.
Ni mapambano mawili tu yaliyowahi kuzalisha mabao mengi kwa kila dakika 90, likiwamo lile la Januari 23, 2011 na Simba iliifunga Azam kwa mabao 3-2, kisha Azam nayo ikaja kufanya kama hivyo Machi 4, 2020 ilipoichapa Simba pia kwa mabao 3-2.
Huku ni msimu mmoja tu wa 2017-2018 uliozalisha idadi ndogo ya mabao kwa kufungwa bao moja wakati Simba iliposhinda bao 1-0 katika mechi ya marudiano huku ile ya kwanza ikiisha kwa suluhu, ilihali msimu wa 2010-2011 na ule wa 2012-2013 ndiyo pekee iliyozalisha mabao mengi kwani kila moja ulishuhudiwa yakifungwa mabao manane kupitia mechi mbili za kila msimu.
Na wachezaji wawili pekee waliowahi kujifunga katika michezo hiyo 33 iliyopita kwa timu hizo katika ligi, wote wakiwa ni mabeki wa kati wa Azam, akianza Agrey Morris Machi 14, 2010 wkati Azam ikilala kwa mabao 2-0, kisha akafuata Abdallah Kheri 'Sebo' Februari 21, mwaka jana wakati akiisawazishia Simba bao dakika ya 90 katika harakati za kuokoa shuti la Kibu Denis.
WAKALI WA REKODI
Rekodi zinaonyesha Winga wa zamani wa kimataifa aliyewahi kukipiga katika hizo mbili, Jamal Mnyate ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika Dabi ya Mzizima.
Mnyate alifunga bao katika pambano la kwanza kwa timu hizo msimu wa 2008-2009 mchezo uliochezwa Oktoba 4, 2008 ambapo Simba ilicharazwa nyumbani 2-0. Mnyate enzi hizo akiwa Azam alifunga katika dakika ya 42 kabla ya Shekhan Rashid aliyewahi pia kuichezea Simba, kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 90+5 na kuwapa Wanalambalamba ushindi huo mtamu.
Rekodi zinaonyesha pia, Mkenya Mike Barasa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika pambano moja baina ya timu hizo akifanya hivyo katika mechi ya Machi 14, 2010 wakati Simba ikishinda ugenini mabao 2-0.
Ukiachana na rekodi hizo, nahodha aliwahi kuziongoza timu hizo kwa vipindi tofauti, John Bocco 'Adebayor' ndiye anayeongoza orodha ya kufunga mabao mengi zaidi, akitupia mabao manane, akifunga sita kipindi akiwa Azam na kuongeza mawili alipokuwa Simba iliyomtema msimu huu.
MK 14, Meddie Kagere aliyekuwa Simba anafuata kwa kufunga jumla ya mabao matano, akiwa ndiye mchezaji aliyeitesa Azam kwa miaka ya karibuni kwa kufunga mfululizo, akifuatiwa na Kipre Tchetche aliyefunga mabao manne enzi akiichezea Azam hadi anaondoka.
Prince Dube aliyepo Yanga kwa sasa ndiye anayefuata akiwa na mabao matatu akifuata nyayo za Kagere za kufunga mfululizo timu pinzani.
ITAKUWAJE?
Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili msimu huu, huku kila moja ikiwa chini ya kocha mpya na sura za wachezaji tofauti ambao wamepewa nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya mchezo huo baada ya awali Simba kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.
Kocha Fadlu Davids wa Simba aliyeibadilisha kabisa timu hiyo msimu huu ikiwa katika kinyang'anyiro cha ubingwa dhidi ya watetezi Yanga ataendelea kuwategemea kipa Moussa Camara, Leonel Ateba, Ellie Mpanzu, Charles Ahoua, Fabrice Ngoma, Ladack Chaambi na wengine walio na viwango bora kwa sasa.
Ahoua anayetokea Ivory Coast ana mabao 10 na asisti tano akiwa ndiye kinara aliyehusika na mabao mengi hadi sasa wa timu hiyo, akifuatiwa na Ateba mwenye mabao manane na asisti tatu watakuwa na kazi ya kuisumbua ngome ya Azam chini ya Yeison Fuentes, Yoro Diaby na viungo wanaojua soka, James Akaminko, Adolf Mtasingwa na Feisal Salum 'Fei Toto'.
Hata hivyo, Azam sio timu ya kubezwa, kwani ipo katika mbio za ubingwa na ikiwa imebadilika chini ya kocha Rachid Taoussi, licha ya siku chache zilizopita ilitulizwa na Pamba Jiji kwa kuchapwa bao 1-0 ugenini, hata kama imekuwa walaini kila inapokutana na Wekundu wa Msimbazi.
Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu iliyopita mbele ya Simba iliyokamata nafasi ya tatu, kwa sasa ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, saba pungufu na ilizonazo Simba yenye 50 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga na itaendelea kumtegemea kiungo mshambuliaji, Feisal Salum 'Fei Toto'.
Fei Toto anayeongoza kwa mabao wa timu hiyo akifunga mabao manne na kuasisti 10 akiwa ndiye kinara wa kuasisti katika Ligi Kuu, lakini akiwa na rekodi na bahati ya kuitungua Simba tangu alipokuwa Yanga, lakini kuna Paschal Msindo, Idd Selemen 'Nado', Nassoro Saadun, Abdul Suleiman 'Sopu' aliyerejea kutoka majeruhi na Allasane Diao kuisumbua ngome ya Simba chini ya Che Fondoh Malone na Abdulrazak Hamza na viungo Debora Mavambo na Fabrice Ngoma.
Kocha wa Taoussi ametamba kwamba hataki kirudie kilichotokea Zanzibar, kwa maana anataka kushinda ili kukusanya pointi za kutosha, wakati Faldu alisema mechi ya leo ni ngumu, lakini kiu yao ni kuendeleza wimbi la ushindi kwa nia ya kutimiza malengo ya kubeba ubingwa.
Vikosi vinavyoweza kuanza leo:
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Hamza, Che Malone, Kagoma, Chasambi, Ngoma, Ateba, Ahoua na Mpanzu
AZAM: Mustafa, Chilambo, Msindo, Diaby, Zouzou, Akaminko, Sillah, Zayd, Saadun, Fei Toto na Idd Nado
MATOKEO KWA MSIMU
2008-2009
Okt 4, 2008
Simba 0-2 Azam
Mar 30, 2009
Azam 0-3 Simba
2009-2010
Okt 24, 2009
Simba 1-0 Azam
Mar 14, 2010
Azam 0-2 Simba
2010-2011
Sept 11, 2010
Azam 1-2 Simba (Tanga)
Jan 23, 2011
Simba 2-3 Azam
2011-2012
Sept 11, 2011
Azam 0-0 Simba
Feb 11, 2012
Simba 2-0 Azam
2012-2013
Okt 27, 2012
Simba 3-1 Azam
Apr 14, 2013
Azam 2-2 Simba
2013-2014
Okt 28, 2013
Simba 1-2 Azam
Mar 30, 2014
Azam 2-1 Simba
2014-2015
Jan 25, 2015
Azam 1-1 Simba
Mei 21, 2015
Simba 2-1 Azam
2015-2016
Dec 25, 2015
Azam 2-2 Simba
Mei 11, 2016
Simba 0-0 Azam
2016-2017
Sept 17, 2016
Azam 0-1 Simba
Jan 28, 2017
Simba 0-1 Azam
2017-2018
Sept 09, 2017
Azam 0-0 Simba
Feb 02, 2018
Simba 1-0 Azam
2018-2019
Feb 22, 2019
Azam 1-3 Simba
Mei 13, 2019
Simba 0-0 Azam
2019-2020
Okt 23, 2019
Simba 1-0 Azam
Mar 04, 2020
Azam 2-3 Simba
2020-2021
Feb 07, 2021
Simba 2-2 Azam
Jul 15, 2021
Azam 1-1 Simba
2021-2022
Jan 01, 2022
Simba 2-1 Azam
Mei 18, 2022
Azam 1-1 Simba
2022-2023
Okt 27, 2022
Azam 1-0 Simba
Feb 21, 2023
Simba 1-1 Azam
2023-2024
Feb 09, 2024
Simba 1-1 Azam (Mwanza)
Mei 09, 2024
Azam 0-3 Simba
2024-2025
Sept 26, 2024
Azam 0-2 Simba (Zanzibar)
Feb 24, 2025
Simba ?? Azam
MSIMAMO ULIVYO 2008-2025
P W D L F A PTS
SIMBA 33 15 12 6 46 29 57
AZAM FC 33 6 12 15 29 46 30
SIMBA 5 ZILIZOPITA
Singida BS 0-1 Simba
Tabora Utd 0-3 Simba
Fountain Gate 1-1 Simba
Simba 3-0 TZ Prisons
Namungo 0-3 Simba
SIMBA 5 ZIJAZO
Mar 01, 2025
v Coastal Union (ugenini)
Mar 08, 2025
v Yanga (ugenini)
Mei 02, 2025
v Mashujaa (nyumbani)
Mei 05, 2025
v JKT Tanzania (ugenini)
Mei 08, 2025
v Pamba Jiji (nyumbani)
AZAM 5 ZILIZOPITA
Azam 3-1 JKT TZ
Azam 2-0 KMC
Pamba 1-0 Azam
Azam 2-0 Mashujaa
Coastal 0-0 Azam
AZAM 5 ZIJAZO
Feb 27, 2025
v Namung0 (nyumbani)
Mar 06, 2025
v TZ Prisons (nyumbani)
Apr 03, 2025
v KenGold (ugenini)
Apr 10, 2025
v Yanga (nyumbani)
Apr 19, 2025
v Kagera Sugar (ugenini)