Ibenge anavyotengeneza rekodi baada ya rekodi Azam FC
Muktasari:
- Azam FC iliandika historia mpya katika Michuano ya CAF, baada ya timu hiyo kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC.
HUENDA ukawa hukifuatilii zaidi kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC chini ya Kocha Mkongomani Florent Ibenge, ila unapaswa kutambua kuna vitu vingi unavikosa, kutokana na rekodi mbalimbali inazoziweka Ligi Kuu Bara.
Azam FC iliandika historia mpya katika Michuano ya CAF, baada ya timu hiyo kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC.
Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, waliopanda rasmi Ligi Kuu Julai 27, 2008, wameweka historia mpya chini ya Kocha Mkuu, Ibenge aliyejiunga nao Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Azam iliishia hatua ya makundi, baada ya kumaliza nafasi ya tatu ikiwa kundi B na pointi tisa nyuma ya AS Maniema Union ya DR Congo iliyokuwa ya pili na pointi zake 12.
Katika kundi hilo lililokuwa na ushindani mkubwa, lilishuhudia Wydad Casablanca kutoka Morocco ikiongoza na pointi 15, huku Nairobi United ya Kenya iliyoshiriki kwa mara ya kwanza kama Azam FC, ikiwa mkiani bila kuvuna pointi zozote zile.
Licha ya kutolewa, Azam imeandika rekodi hiyo, huku ikipata pointi nyingi ambazo haijatokea kwa klabu ya Tanzania katika ushiriki wake wa kwanza.
Azam imemaliza nafasi ya tatu na pointi tisa, ikiwa ni pointi nyingi zaidi kwa timu ya Tanzania katika ushiriki wake wa kwanza, kwani hata vigogo wa soka nchini Yanga, Simba na Namungo ziliposhiriki kwa mara ya kwanza hazijawahi kuzifikia.
Ukiachana na hilo, kwa sasa Ibenge anatengeneza rekodi nyingine ya kuvutia kwa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara na mbali na wadau kutozungumzia sana kama ilivyo kwa Yanga na Simba, ila nitakupitishia mambo kadhaa unayopaswa kuyafahamu.
MECHI 23 BILA KUPOTEZA
Tangu mara ya mwisho Azam FC ilipofungwa kwa mabao 2-1, dhidi ya Yanga, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini, Dar es Salaam, Aprili 10, 2025, kikosi hicho hakijakumbana na kichapo hadi leo.
Mechi hiyo ya 'Dar es Salaam Derby' iliyopigwa Aprili 10, 2025, mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua, dakika ya 11 na Prince Dube, dakika ya 34, huku lile la kufutia machozi kwa Azam FC, likifungwa na Lusajo Mwaikenda, dakika ya 81.
Tangu Aprili 10, 2025, ambao ni msimu wa 2024-2025, hadi sasa 2025-2026, Azam imecheza jumla ya mechi 23, za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, ikishinda 13 na sare 10, huku ikifunga mabao 43 na kuruhusu tisa.
Rekodi hiyo nzuri kwa Azam, inaifanya kushika nafasi ya pili kwa timu zilizocheza mechi nyingi za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza nyuma ya Yanga, ambayo hadi sasa haijapoteza tangu mara ya mwisho, Novemba 7, 2024, ilipochapwa mabao 3-1 na Tabora United sasa TRA United.
Mabao ya TRA United, yalifungwa na Offen Chikola, anayeichezea Singida Black Stars kwa mkopo akitokea Yanga, aliyefunga mawili dakika ya 19 na 45+4 na Nelson Munganga dakika ya 77, huku pia Clement Mzize akiifungia Yanga dakika ya 90+5.
Yanga imecheza jumla ya mechi 39, za Ligi Kuu bila ya kupoteza na imeshinda 33 na kutoka sare sita tu.
YAZIPIGA BAO YANGA, SIMBA
Moja ya kitu unachopaswa kutambua, Azam FC ndio timu pekee katika Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026, ambayo haijawahi kuruhusu bao katika uwanja wake wa nyumbani, ikizipiga bao Simba na Yanga ambazo tayari zimeruhusu.
Azam FC imecheza mechi tisa nyumbani, ikishinda tano na kutoka sare nne, huku ikifunga mabao 13, bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Kwa upande wa Yanga katika mechi zake 10 za nyumbani, imeshinda tisa na kutoka sare moja, ikifunga mabao 34 na kuruhusu mawili tu, huku Simba iliyocheza nane, imeshinda sita, sare moja na kupoteza moja, ikifunga mabao 17 na kuruhusu matatu.
Kwa maana hiyo, Azam inashikilia rekodi bora ya kucheza mechi za nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, bila ya kupoteza kama ilivyo pia kwa Yanga, ingawa, kutoruhusu bao ndio jambo la kuvutia kwa kikosi hicho cha Florent Ibenge.
Hata hivyo, Yanga ndio timu iliyokusanya pointi nyingi ikicheza nyumbani ikiwa nazo 28, katika mechi 10, ikifuatiwa na Azam iliyocheza tisa na Simba iliyoshuka uwanjani mara nane na timu hizo zote zimevuna pointi 19, kila mmoja wao.
UGENINI KITENDAWILI
Licha ya rekodi bora ya Azam, ila mojawapo ya jambo kubwa linaloirudisha nyuma msimu huu ni kupata wakati mgumu ikicheza ugenini, kwani katika mechi 10, ilizocheza, imeshinda nne na kutoka sare sita, ikifunga mabao 13 na kuruhusu matano tu.
Kwa upande wa Yanga, imecheza mechi tisa ugenini msimu huu na imeshinda tano na kutoka sare nne, ikifunga mabao 10 na kuruhusu moja, huku Simba iliyocheza 11, imeshinda sita na sare tano tu, ikifumania nyavu mara 15 na kuruhusu manne.
Kwa maana hiyo, Simba ndio timu inayoongoza kwa kukusanya pointi nyingi ugenini msimu huu, ikiwa nazo 23 katika mechi 11 ilizocheza, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 19, baada ya kucheza tisa, huku Azam FC ikiwa imekusanya pointi zake 18.
Hadi sasa, Azam inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 37, baada ya kucheza mechi 19, ikishinda tisa na kutoa sare 10, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 26 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
Kwa upande wa Simba iliyocheza pia mechi 19, inashika nafasi ya pili na pointi 42, baada ya kushinda 12, sare sita na kupoteza moja, ikifunga mabao 32 na kuruhusu saba, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga inayoongoza pia ikiwa na pointi 47.
Yanga iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo, msimu huu imecheza mechi 19 na kati ya hizo imeshinda 14 na kutoka sare tano tu, huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao 44 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
(MECHI YA MWISHO AZAM FC KUPOTEZA LIGI KUU MSIMU WA 2024-2025)
Azam FC 1-2 Yanga (Aprili 10, 2025)
(Lusajo Mwaikenda '81') (Pacome Zouzoua '11, Prince Dube '34')
(1)-Kagera Sugar 2-4 Azam FC (Aprili 19, 2025)
(2)-Azam FC 5-0 Dodoma Jiji (Mei 13, 2025)
(3)-Azam FC 5-0 TRA United (Juni 18, 2025)
(4)-Fountain Gate 2-3 Azam FC (Juni 22, 2025)
(5)-Azam FC 2-0 Mbeya City (Septemba 24, 2025)
(6)-JKT TZ 1-1 Azam FC (Oktoba 1, 2025)
(7)-Namungo FC 1-1 Azam FC (Novemba 9, 2025)
(8)-Azam FC 0-0 Singida BS (Desemba 3, 2025)
(9)-Simba 0-2 Azam FC (Desemba 7, 2025)
(10)-Azam FC 3-0 Coastal Union (Januari 17, 2026)
(11)-Azam FC 0-0 Fountain Gate (Januari 20, 2026)
(12)-Azam FC 2-0 TRA United (Januari 29, 2026)
(13)-KMC FC 0-2 Azam FC (Februari 22, 2026)
(14)-Azam FC 3-0 Mtibwa Sugar (Februari 25, 2026)
(15)-Pamba Jiji 2-2 Azam FC (Machi 2, 2026)
(16)-TZ Prisons 0-0 Azam FC (Machi 5, 2026)
(17)-Dodoma Jiji 0-3 Azam FC (Machi 11, 2026)
(18)-Azam FC 0-0 Yanga (Machi 15, 2026)
(19)-Mashujaa FC 0-0 Azam FC (Machi 19, 2026)
(20)-Singida BS 1-2 Azam FC (Aprili 1, 2026)
(21)-Azam FC 0-0 Simba (Aprili 5, 2026)
(22)-Mbeya City 0-0 Azam FC (Aprili 9, 2026)
(23)-Azam FC 3-0 JKT TZ (Aprili 17, 2026)
MECHI-23
USHINDI-13
SARE-10
KUPOTEZA-0
MABAO YA KUFUNGA-43
MABAO YA KUFUNGWA-9
LIGI KUU MSIMU WA 2025-2026
MECHI ZA NYUMBANI
(1)-Azam FC 0-0 Yanga
(2)-Azam FC 3-0 Mtibwa Sugar
(3)-Azam FC 2-0 TRA United
(4)-Azam FC 0-0 Fountain Gate
(5)-Azam FC 3-0 Coastal Union
(6)-Azam FC 0-0 Singida BS
(7)-Azam FC 2-0 Mbeya City
(8)-Azam FC 0-0 Simba
(9)-Azam FC 3-0 JKT TZ
MECHI-9
USHINDI-5
SARE-4
MABAO YA KUFUNGA-13
MABAO YA KUFUNGWA-0
POINTI-19
MECHI ZA UGENINI
(1)-Mashujaa FC 0-0 Azam FC
(2)-Dodoma Jiji 0-3 Azam FC
(3)-TZ Prisons 0-0 Azam FC
(4)-Pamba Jiji 2-2 Azam FC
(5)-KMC FC 0-2 Azam FC
(6)-Simba 0-2 Azam FC
(7)-Namungo FC 1-1 Azam FC
(8)-JKT TZ 1-1 Azam FC
(9)-Singida BS 1-2 Azam FC
(10)-Mbeya City 0-0 Azam FC
MECHI-10
USHINDI-4
SARE-6
MABAO YA KUFUNGA-13
MABAO YA KUFUNGWA-5
POINTI-18