Prime
MZIKI MNENE: Wamechemsha Ligi Kuu England, wakawa watamu La Liga
Muktasari:
- Kwa miaka kibao, kuna mastaa wengi wenye majina makubwa kwenye mchezo wa soka, ambao walikuwa moto huko watokako, lakini walipotua kwenye Ligi Kuu England, mambo yalikwenda tofauti kabisa na kuchemsha.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England ndiyo inayotazamwa sana na yenye upinzani zaidi ya ligi nyingi duniani, hivyo hata uwe mchezaji uliyejipambanua huko kwingine, mambo yanaweza kuwa magumu unapotua kweye ligi hiyo hata kama una jina kubwa.
Kwa miaka kibao, kuna mastaa wengi wenye majina makubwa kwenye mchezo wa soka, ambao walikuwa moto huko watokako, lakini walipotua kwenye Ligi Kuu England, mambo yalikwenda tofauti kabisa na kuchemsha.
Winga wa Manchester United, Antony alikuwa moto mkali Ajax kabla ya kunaswa na miamba hiyo ya Old Trafford.
Maisha ya Mbrazili huyo hayakuwa mazuri Man United na kuonekana kuwa ni mzigo tu, lakini baada ya kutolewa kwa mkopo kwenye dirisha la Januari kwenda Real Betis, staa huyo amekuwa moto wa kuotea mbali, akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi tatu mfululizo, huku akifunga mabao matatu na kuasisti mara moja katika mechi nne alizochezea timu mpya.
Hata hivyo, Antony si mchezaji wa kwanza kuchemsha kwenye Ligi Kuu England na kisha kwenda kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kwenda kukipiga kwenye La Liga.
Diego Forlan
Straika wa Uruguay alikuwa na hadhi kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini miaka yake miwili aliyokuwa kwenye kikosi cha Man United kuanzia 2002 hadi 2004 mambo hayakuwa matamu sana.
Staa huyo alifunga mabao 17 katika mechi 98, mchango ambao ulionekana kuwa mdogo kwa mchezaji wa kiwango chake na kuonekana kuwa wa kawaida. Lakini, mambo yalikuwa tofauti kabisa baada ya kuondoka Old Trafford kwenda kukipiga huko Hispania kwenye vikosi vya Villarreal na Atletico Madrid, ambako alichangia kwenye mabao 190 katika mechi 325, huku kwenye timu zote mbili alihesabika kama mmoja wa mastaa matata kabisa waliowahi kukipiga kwenye LaLiga.
Ubora wake ulihusisha pia kwenye timu ya taifa, ambapo alifunga mabao 36 huku kumbukumbu tamu kuhusu yeye inahusu Kombe la Dunia 2010, alipowatesa makipa na mpira wa Jubalani, uliomfanya awe kinara wa mabao wa fainali hizo na kushinda tuzo ya Golden Ball.
Iago Aspas
Aspas ni mfano halisi wa wachezaji waliofanya hovyo kwenye Ligi Kuu England na kwenda kuwa shujaa mkubwa huko Hispania. Akifahamika kama mchezaji aliyepiga kona ya hovyo zaidi katika mechi ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Chelsea uwanjani Anfield mwaka 2014, straika huyo alifunga bao moja tu katika mechi 15 alizochezea Liverpool kabla ya kuhama kwenda Celta Vigo.
Tangu wakati huo, uhamisho huo ulikuwa na faida kubwa kwake na kumfanya awe mmoja wa wachezaji tishio kabisa duniani. Amekuwa shujaa wa Celta Vigo akifunga mabao 210 katika mechi 510 na amekuwa akifunga mabao karibu kila wiki kuipa ushindi timu yake. Ameendelea kuwa tishio licha ya kuwa na umri wa miaka 37.
Alexander Sortloth
Ni mshabiki wa Crystal Palace pekee ndiyo watakaokumbuka kwamba Sorloth alicheza kwenye Ligi Kuu England huku ikifahamika wazi kundi kubwa la mashabiki watakuwa hawakumbuki kama mkali huyo alishawahi kukipiga England. Alifunga bao moja tu katika mechi 20 alizocheza na sehemu kubwa ya maisha yake alitolewa kwa mkopo Uturuki kabla ya kuondoka jumla 2020.
Baadaye alikwenda kupata mafanikio makubwa huko La Liga alipojiunga na Real Sociedad kwa mkopo akitokea RB Leipzig kabla ya kujiunga na Villarreal, alikofunga mabao 26 katika mechi 41.
Kwa sasa staa huyo wa kimataifa wa Norway amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Atletico Madrid chini ya kocha Diego Simeone na kiwango chake cha soka si mchezo kwenye LaLiga.
Alberto Moreno
Wakati nyakati za Moreno kwenye kikosi cha Liverpool zikiwa kwenye mapito mengi, mashabiki walikuwa hawamwelewi kabisa beki huyo katika kipindi chake alipokuwa na kikosi cha miamba hiyo ya Anfield.
Kitu cha zaidi kuhusu beki huyo wa pembeni anayeshambulia, hakuwa na wakati mzuri kwenye kujilinda tofauti na ilivyokuwa kwa mchezaji Andy Robertson, aliyeibukia Liverpool mwaka 2017 na kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi. Moreno aliondoka Liverpool kwenda Villarreal mwaka 2019, mahali ambako alikwenda kucheza soka la mafanikio kwa miaka mitano, akitamba na kushinda ubingwa wa Europa League kwa kuichapa Manchester United kwenye fainali.
Katika kipindi chake huko Villarreal, alicheza mechi 124 na zingekuwa mechi nyingi zaidi kama asingekumbana na majeruhi yaliyomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Como ya Italia chini ya kocha Cesc Fabregas.
Suso
Staa mwingine wa Liverpool kwenye orodha hii ya wachezaji waliochemsha kwenye Ligi Kuu England, lakini walienda kuwa watamu baada ya kutua kukipiga huko Hispania. Suso alikuwa mchezaji wa Kihispaniola aliyekuwa na kipaji kikubwa, ambapo aliibukia kutokea kwenye akademia ya Liverpool.
Hata hivyo, alkifunga bao moja tu katika mechi 21 alizocheza timu hiyo ya Anfield kabla ya kuondoka. Uhamisho wake wa kwanza alikwenda AC Milan, lakini alikwenda kuwa bora zaidi baada ya kutua Sevilla, ambako alituliza daruga zake tangu mwaka 2020, akishinda Europa League mara mbili na kucheza mechi 164 katika timu hiyo.
Licha ya kwamba majeraha yamekuwa yakimsumbua tangu aliporudi Hispania, lakini kiwango cha soka lake kimekuwa bora zaidi Hispania tofauti na alivyokuwa England.
Gerard Pique
Kabla ya kuwa beki wa mpira na kutamba sana katika kikosi cha Barcelona, ambacho alibeba mataji kibao, Pique alikuwapo kwenye kikosi cha Man United iliyokuwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Hata hivyo, kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, Pique alishindwa kuwa na maajabu makubwa ya kupata namba mbele ya mabeki wa kati wawili, Rio Ferdinand na Nemanja Vidic.
Pique alionekana wa kawaida hata mbele ya mabeki wengine akiwamo Jonny Evans na Wes Brown, hivyo aliondoka kwenda kukipiga huko Barcelona. Kwenye kikosi cha Man United, Pique alicheza mechi 23 tu kabla ya kuondoka kwenda Barca alikocheza mechi 616 na kufanikiwa kuitumikia Hispania pia kwenye mechi 102 na kushinda mataji makubwa, Kombe la Dunia, Euro mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne.
Fabio Silva
Alisajiliwa kama straika kinda mwenye kipaji kikubwa na matarajio makubwa, Silva alijikuta akionekana kuwa mchezaji wa kawaida kwenye Ligi Kuu England alipokuwa akikipiga katika kikosi cha Wolves, ambako alikuwa akitumika zaidi kama mchezaji wa kiungo ya ulinzi na kiwango chake kilikuwa cha kupanda na kushuka kama homa za vipindi.
Akitokea kwenye akademia za Porto na Benfica, alisaini mkataba wa kujiunga na Porto alipokuwa na umri wa miaka 18, kipindi cha janga la maambukizi ya uviko 19. Alifunga mabao matano katika mechi 72 na kuonekana kama vile mambo yake hayakuwa sawasawa kwenye Ligi Kuu England kabla ya kwenda kwa mkopo Las Palmas.
Baada ya kutua kwenye La Liga, mkali huyo amefunga mabao saba katika mechi 17, alitikisa nyavu pia kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya Barcelona na kwenye kichapo kutoka kwa Real Madrid huku matumaini makubwa yakiibuka kwa mchezaji huyo wa miaka 22 kwamba atafanya jambo bora uwanjani baada ya kutua kwenye La Liga.