Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamba Ronaldo anaondokaje Ureno?

RONALDO Pict

Muktasari:

  • Wiki moja baadaye, Ureno imejikuta katika mzozo unaomhusu Ronaldo, huku nyota huyo mwenye rekodi bora ya dunia ya mechi nyingi zaidi za kimataifa kwa wanaume kwa nchi yake akionekana kutokuwa na uwezekano wa kuichezea tena nchi yake.

LISBON, URENO: BAADA ya kuondoka kwenye kambi ya mazoezi ya Ureno, inaonekana kazi ya Cristiano Ronaldo katika timu ya taifa imefikia mwisho wenye mvutano. Haikupaswa kuwa hivi. Miaka kadhaa ya mjadala kuhusu iwapo Ureno ilikuwa bora ikiwa Ronaldo yupo au hayupo katika kikosi cha kwanza, nyota huyo aliyepewa jukumu la kuibeba timu hiyo anaonekana kukubali kwamba nafasi yake chini ya kocha mpya mwenye msimamo mkali, Jorge Jesus, ambaye aliwahi kufanya naye kazi Al Nassr, huenda ikapungua kwa kiasi fulani, angalau uwanjani.

“Kocha akiamua kwamba jambo bora kwa timu ni mimi kuanza benchi, nitakubali hilo kikamilifu,” Ronaldo aliiambia RTP baada ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza katika ushindi wa bao 1-0 wa UEFA Nations League dhidi ya Wales wiki iliyopita.

“Nipo hapa kusaidia timu ya taifa kwa namna yoyote itakayohitajika. Kama sitapata nafasi ya kucheza, hilo pia siyo tatizo; jambo muhimu zaidi ni timu kushinda na kundi kuwa na umoja. Daima nimekuwa nikisema kwamba kundi ni kubwa kuliko mchezaji yeyote mmoja na niko tayari kikamilifu kutekeleza jukumu lolote nitakalopewa.”

Wiki moja baadaye, Ureno imejikuta katika mzozo unaomhusu Ronaldo, huku nyota huyo mwenye rekodi bora ya dunia ya mechi nyingi zaidi za kimataifa kwa wanaume kwa nchi yake akionekana kutokuwa na uwezekano wa kuichezea tena nchi yake.

Licha ya kusema yuko “tayari kikamilifu kutekeleza jukumu lolote nitakalopewa”, Ronaldo hakuonekana kufurahishwa na kuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumiwa katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway na baada ya filimbi ya mwisho alikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo badala ya kuungana na wenzake kuwashukuru mashabiki wa Ureno waliosafiri kwenda kushuhudia mchezo huo.

Kisha, kila kitu kilifikia kilele Jumatano, wiki hii. Ronaldo alithibitisha kwamba alikuwa ameondoka kwenye kambi ya mazoezi ya Ureno kufuatia “mazungumzo na rais wa Shirikisho la Soka la Ureno” kuhusu mkutano wa waandishi wa habari wa Jorge Jesus kabla ya mchezo wa Alhamisi dhidi ya Denmark.

RONAL 01

Kwa kutarajiwa, Ronaldo alikuwa miongoni mwa mada kuu katika mkutano huo na waandishi wa habari. Ingawa Jesus alikiri kwamba “alifanya kosa” la kumtaka Ronaldo afanye mazoezi ya kupasha mwili moto kwa dakika 30, huku pia akisisitiza kuwa taarifa za nahodha huyo kukataa kufanya mazoezi hazikuwa za kweli, aliweka wazi kwamba yeye ndiye mwenye uamuzi.

“Naweza kumwambia mchezaji yeyote kwamba unaanzia benchi. Kama nitakuhitaji kwa dakika 30 utaingia kucheza; kama sikuhitaji hutacheza.

“Kwa namna nilivyokuwa nikisoma mchezo (dhidi ya Norway), (Ronaldo) hakuingia. Kwa sababu siyo Cristiano, kama ambavyo haitawahi kuwa mchezaji yeyote atakayebadilisha mawazo yangu kama kocha. Kamwe. Siyo yeye, wala mtu yeyote katika soka. Si yeye, wala mtu yeyote, wala rais yeyote. Kamwe. Sifuri,” alisema kocha huyo.


NGOMA INGEENDA ASTEASTE?

Je, Jesus angeweza kuchukua mtazamo wa upole zaidi? Labda, lakini pia kuna hoja yenye nguvu kwamba Ureno imekuwa ikihitaji kocha mwenye aina hiyo ya haiba kwa muda mrefu; mtu mwenye msimamo na ujasiri wa kufanya uamuzi mgumu ambayo huenda hata ukawa wa kutatanisha.

Kocha wa zamani wa timu hiyo, Fernando Santos alionekana kuanza kumuweka Ronaldo pembeni taratibu alipomtoa mshambuliaji huyo katika mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Uswisi kwenye Kombe la Dunia 2022 lililopigwa nchini Qatar. Kisha, mbadala wake, Goncalo Ramos alifunga mabao matatu katika ushindi wa 6-1.

RONAL 02

Lakini, baada ya kufungwa na Morocco katika robo fainali, Santos alijiuzulu na hatimaye nafasi yake ikachukuliwa na Roberto Martinez, ambaye chini yake Ronaldo aliendelea kuwa miongoni mwa majina ya kwanza kwenye kikosi. Alianza katika mechi tisa kati ya 10 za Ureno za kufuzu Euro 2024 na michezo yote mitano ya fainali.

Ronaldo pia alikuwa kwenye kikosi cha kwanza katika mechi tano kati ya sita za kufuzu Kombe la Dunia 2026, pamoja na michezo yote mitano ya Ureno katika mashindano hayo yaliyofanyika Marekani, Canada na Mexico, ambapo Ureno ilimaliza nafasi ya pili kwenye kundi na kuishia  hatua ya 16 bora.


KUNA DARASA HAPA

Kimsingi Ronaldo alikuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao chini ya Martinez, lakini muda mrefu kabla ya kocha huyo hajaajiriwa kulikuwa na mijadala kuhusu iwapo mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid, Juventus na Manchester United alikuwa akiisaidia timu kwa kiwango cha kutosha katika maeneo mengine ili kuhalalisha kuanza mara kwa mara.

Katika zama hizi za soka ambapo nguvu ya kucheza bila mpira na presha kwa wapinzani vinapewa umuhimu mkubwa, kumtumia mchezaji ambaye anachangia kidogo katika maeneo hayo ni anasa ambayo timu chache zinaweza kumudu zinapokabiliana na wapinzani bora. Na zile zinazoweza kufanya hivyo zinapaswa kujenga timu zenye uwezo wa kubeba mzigo huo wa ziada, kama Argentina ilivyofanya kwa mafanikio ya miaka mingi ikiwa na Lionel Messi.

RONAL 03

Katika mchezo dhidi ya Hispania kwenye Kombe la Dunia 2026, Ronaldo aligusa mpira mara 19 katika dakika 90, na hakuna hata moja kati ya hizo iliyotokea baada ya dakika ya 80, licha ya mchezo kuwa suluhu hadi muda wa nyongeza.

Hata hivyo, siku chache kabla ya hapo, kocha Martínez alimpumzisha Ronaldo, jambo ambalo kwa kuonekana hakulifurahia; katika dakika ya 81 dhidi ya Croatia wakati matokeo yakiwa 1-1. Ramos alikuwa tayari ameingizwa mapema kidogo, lakini baada ya Ronaldo kupumzishwa Ramos akawa kiini cha mashambulizi na akafunga bao la ushindi la kusisimua mwishoni mwa mchezo lililoipeleka Ureno hatua iliyofuata.

Nani anaweza kusema kwamba matokeo ya Ureno dhidi ya Hispania katika fainali za Kombe la Dunia 2026 yangekuwa tofauti iwapo Ramos au mchezaji mwingine yeyote angeanza badala ya Ronaldo? Ingawa ilikuwa jambo la kushangaza kwamba Ramos hakupata nafasi kabisa ya kuingia, hata kama Martínez alikuwa akimuandaa kwa dakika 30 za muda wa ziada ambazo hazikutokea kwa sababu Hispania ilifunga bao la ushindi mwishoni. Ilionekana kama kocha wa Ureno alishindwa kuzingatia somo muhimu kutoka kwenye mchezo dhidi ya Croatia.

RONALDO Pict

MTU BORA KABISA

Ingawa ubora wa Ronaldo kwa miaka mingi ni mkubwa kuliko mashindano mengi aliyoshiriki, pia inafaa kuzingatia kwamba rekodi yake ya kufunga mabao kwenye Kombe la Dunia haikuwa ya kipekee sana. Ni kweli, ni wachezaji wanane pekee waliowahi kufunga mabao mengi zaidi, lakini Ronaldo alifunga mabao yake katika mechi 27; wachezaji saba kati ya hao wanane waliomtangulia wamecheza mechi chache zaidi.

Hata hivyo, haikuwa jambo la kushangaza sana kwamba Ronaldo hakustaafu soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia 2026, wala haukuwa mshangao mkubwa wakati kocha Jesus aliposema alikuwa tayari kuendelea kumtegemea Ronaldo kwa kuwa tayari walikuwa wamewahi kufanya kazi pamoja Al Nassr.

Baada ya yote, Ronaldo ana uzoefu mkubwa na haiba kiasi kwamba, iwapo angekubali jukumu lililopunguzwa la kucheza, bado angeweza kutoa mchango mkubwa kwa kikosi kupitia ushawishi na hadhi yake katika mchezo. Ilikuwa inaeleweka kabisa kwamba Jesus angependa kumuweka kwenye kikosi kwa mtazamo huo, na kwa kuwa Ronaldo ana miaka 41 ungeweza kufikiri kwamba angezingatia hali yake na ukomavu wa kutambua kwamba huenda asiwe tena chaguo bora la kuiongoza safu ya ushambuliaji mara kwa mara.

Hata hivyo, pengine ni kutia chumvi kidogo kusema kwamba tukio la majuzi litachafua urithi wa Ronaldo katika timu ya taifa. Watu watakapoangalia nyuma kazi yake katika timu ya taifa ya Ureno baada ya miaka mitano, 10, 15 au 20, wataangazia idadi yake ya kushangaza ya mechi 234 na mabao 146, ambayo yote ni rekodi katika soka la kimataifa pamoja na ukweli kwamba aliiongoza Ureno kutwaa taji la kwanza kubwa la mashindano ya kimataifa katika Euro 2016.

Baadhi ya watu huenda hata wakataja mataji mawili ya Uefa Nations League ikiwa umuhimu wa mashindano hayo utaongezeka.

Kwa mtazamo mpana, siku zake za mwisho katika timu ya taifa za Ronaldo ambazo inaonekana huenda zikawa za mwisho kabisa huenda zikabaki tu kama maelezo machache katika historia yake, yatakayotajwa zaidi katika uchambuzi wa kina na makala zitakazomzungumzia kwa undani zaidi maisha yake ya soka.

Kwa wakati huu, inaonekana ni jambo la kusikitisha kwa moja ya mashine za ajabu zaidi kuwahi kutokea katika soka la kimataifa kuonekana kumalizika kwa namna yenye mzozo na isiyokuwa ya lazima. Lakini, bila vurugu na mijadala isiyokoma kuhusu uwepo wake, Ureno ya mwaka 2026 na miaka inayofuata huenda hatimaye ikawa bora zaidi bila Ronaldo huyu.