Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamba Kevin Keegan amelala

KEEGAN Pict

Muktasari:

  • Keegan anakumbukwa kama mmoja wa wachezaji bora na maarufu zaidi wa kizazi chake, akiwa mchezaji pekee wa Uingereza kuwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d'Or mara mbili mfululizo.

LONDON, ENGLAND: DUNIA ya soka inaomboleza kufuatia kifo cha nahodha, mchezaji, na kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya England na klabu ya Liverpool, Kevin Keegan, aliyefariki dunia juzi akiwa na familia yake.

Keegan mwenye umri  wa miaka 75 amefariki dunia  baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya hatua ya nne kwa muda mrefu.

Taarifa iliyotolewa na familia yake kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa nguli huyo amefariki dunia akiwa amezungukwa na mkewe, Jean, pamoja na binti zake katika nyakati zake za mwisho.

Keegan anakumbukwa kama mmoja wa wachezaji bora na maarufu zaidi wa kizazi chake, akiwa mchezaji pekee wa Uingereza kuwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d'Or mara mbili mfululizo.

Alitoka katika familia ya wachimbaji madini wa South Yorkshire akiwa mtoto wa kawaida, akaanzia safari yake ya soka katika Scunthorpe United, lakini baadaye akawa mmoja wa mastaa wakubwa kuwahi kutokea England na Ulaya. Huyo ndiye Kevin Keegan mwanamume ambaye hakupendwa kwa kipaji chake pekee, bali kwa moyo wake mkubwa, mapenzi yake kwa mchezo na roho ya kutokata tamaa.

Keegan alipewa jina la utani "Mighty Mouse", jina lililoendana kabisa na maisha yake uwanjani. Hakuwa mrefu wala mwenye mwili mkubwa, lakini alikuwa mpiganaji asiyejua kukubali kushindwa. Alikuwa mchezaji aliyepambana dhidi ya kila changamoto na mara zote alionyesha kuwa ukubwa wa moyo ni muhimu kuliko ukubwa wa mwili.

Katika historia ya soka la England, Keegan anabaki kuwa mmoja wa wachezaji wa kipekee zaidi. Wakati mwingine mafanikio yake kama kocha, hasa akiwa Newcastle United, pamoja na kipindi ambacho timu ya taifa ya England haikufanya vizuri, yamefanya wengi kusahau kiwango cha juu alichokifikia akiwa mchezaji.

KEEG 04

Lakini rekodi hazidanganyi.

Keegan ndiye Muingereza pekee aliyewahi kushinda tuzo ya Ballon d'Or mara mbili mfululizo, mwaka 1978 na 1979 akiwa na Hamburger SV nchini Ujerumani. Mafanikio hayo yanamweka katika kundi moja na mastaa wakubwa kama Franz Beckenbauer, Alfredo Di Stefano, Karl-Heinz Rummenigge na Ronaldo wa Brazil.

Kwa unyenyekevu wake aliwahi kusema: "Huenda mimi ndiye mchezaji wa kawaida zaidi kuwahi kushinda Ballon d'Or mara mbili."

Lakini ukweli ni kwamba, hakuna kilichokuwa cha kawaida kuhusu Kevin Keegan.

Mbali na kipaji chake, Keegan alikuwa mtu aliyewavutia mashabiki kila alipokuwa. Aliweza kuwafanya watu wabakie wakimsikiliza kwa saa nyingi, na baada ya hafla yoyote hakuwahi kuondoka kabla ya kusaini kila ombi la autograph au kuzungumza na mashabiki wote waliomsubiri.

Katika enzi ambazo wachezaji walihimizwa kuficha hisia zao, Keegan alikuwa tofauti. Alionesha furaha, hasira, maumivu na mapenzi yake kwa soka hadharani. Mashabiki walimpenda kwa sababu alikuwa halisi.

Umaarufu wake uliongezeka zaidi kupitia kipindi maarufu cha televisheni cha Superstars, ambapo wanamichezo walishindana katika michezo mbalimbali. Hata baada ya kupata ajali mbaya ya baiskeli wakati wa mashindano hayo, Keegan alikataa kukata tamaa. Mbio zilipoanzishwa upya, aliibuka mshindi na kuandika moja ya simulizi zinazokumbukwa zaidi katika historia ya kipindi hicho.

KEEG 03

Kutawala Liverpool na Ulaya

Baada ya kuanza maisha ya soka Scunthorpe United, Keegan alivutiwa na kocha mashuhuri Bill Shankly na kujiunga na Liverpool.

Akiwa Anfield, alikua nyota wa kikosi kilichokuja kutwaa Kombe la Ulaya mwaka 1977 chini ya Bob Paisley. Katika fainali dhidi ya Borussia Monchengladbach mjini Rome, Keegan aliisumbua ngome ya wapinzani na kushinda penalti iliyohitimisha ushindi wa mabao 3-1, ushindi ulioweka msingi wa Liverpool kuwa moja ya klabu kubwa zaidi Ulaya.

Alipoondoka kwenda Hamburger SV, wengi walihofia enzi ya Liverpool ingeisha. Badala yake, klabu hiyo ilimsajili Kenny Dalglish ambaye aliendeleza mafanikio hayo.

KEEG 01

Kocha aliyeipa Newcastle ndoto

Baada ya kutundika daruga, Keegan aligeuka kuwa kocha aliyebadilisha sura ya Newcastle United.

Aliijenga timu iliyocheza soka la kuvutia, la kushambulia na lililowafanya mashabiki wengi wasiokuwa wa Newcastle kuitamani timu hiyo itwae ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 1995/96.

Ingawa walipoteza mbio hizo dhidi ya Manchester United ya Sir Alex Ferguson, Newcastle ya Keegan ilibaki mioyoni mwa wengi kwa kandanda safi na ya kushambulia.

Katika msimu huo ndipo Keegan alipotoa kauli maarufu zaidi katika historia ya soka la England aliposema kwa hasira mbele ya kamera:

"Tutapigania ubingwa huu... na nitafurahi sana tukiwafunga. Nitafurahi sana!"

Kauli hiyo iligeuka sehemu ya historia ya Premier League.


Mwisho wa Safari England

Mwaka 1999 alikabidhiwa timu ya taifa ya England, lakini safari yake haikudumu.

Baada ya England kufungwa bao 1-0 na Ujerumani katika mchezo wa mwisho uliochezwa kwenye Wembley ya zamani mwaka 2000, Keegan alijiuzulu mara moja ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, akiamini ulikuwa wakati wa kuondoka.

KEEG 02

Urithi usiofutika

Keegan hakuwahi kuwa mtu wa kuficha hisia zake. Alikuwa mkweli, mwenye shauku isiyoisha na aliyeishi maisha yake kwa nguvu zote.

Mashabiki wa Newcastle bado wanamwabudu kwa heshima aliyoirudisha klabuni na kwa kandanda la burudani alilowapa. Mashabiki wa Liverpool wanamkumbuka kama mmoja wa nyota walioweka msingi wa mafanikio yao barani Ulaya. Na England inamkumbuka kama mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kuvaa jezi ya taifa.

 Keegan hakuwa tu nyota wa soka. Alikuwa alama ya ujasiri, mapenzi ya mchezo na moyo usiokubali kushindwa.