Mushi, Chuma wasikate tamaa Taifa Stars
Muktasari:
- Anaitendea haki sana nafasi yake japo sio mzoefu wa ligi na ndani ya muda mfupi amegeuka kivutio kwa tulioangalia mechi za Polisi Tanzania.
YULE beki na kapteni wa Polisi Tanzania, Denis Mushi ameonyesha kuanza vizuri msimu huu katika nafasi anayocheza ya beki wa kulia.
Anaitendea haki sana nafasi yake japo sio mzoefu wa ligi na ndani ya muda mfupi amegeuka kivutio kwa tulioangalia mechi za Polisi Tanzania.
Beki wa pembeni anatakiwa ajue kuzuia mawinga na pia apande mbele kusaidia kushambulia hasa kwa kupiga mitungi ndivyo anavyofanya Mushi.
Mwingine aliyetuvutia hapa kijiweni ni kipa wa Coastal Union, Chuma Ramadhan kutokana na uwezo wake wa kulinda goli la timu hiyo.
Timu yake imefungwa mabao nane kwenye ligi hadi sasa lakini ingefungwa mabao mengi zaidi ya hayo kama kipa huyo asingeonyesha kiwango bora cha kuokoa mashambulizi mengi ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake.
Basi tukajua kama hao madogo wawili wangeitwa katika kikosi cha Taifa Stars kutokana na kile ambacho wamekionyesha kwenye raundi tano za ligi ambazo zimechezwa.
Lakini kocha Gamondi hajawaita katika timu hiyo ambayo inakaribia kucheza mechi za kufuzu AFCON 2027 ambazo itacheza na Madagascar na Guinea Bissau.
Hata hivyo madogo wasikate tamaa bhana. Waendelee kuonyesha kiwango kizuri tu na ipo siku watapata fursa ya kuwemo katika timu ya taifa maana ina mechi nyingi mbele.
Bado ni vijana wadogo na umri unawaruhusu kuichezea Taifa Stars kwa muda mrefu zaidi kama watafanikiwa kuwa na muendelezo wa kiwango.