Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTU WA MPIRA: Tweet za Mo Dewji na mabadiliko ya Simba

NI miaka sita sasa na mchakato wa mabadiliko pale Simba haujakamilika. Hii si kauli yangu. Ni ya mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji.

Wiki iliyomalizika Dewji aliibua mjadala mkubwa kwenye mtandao wa Twitter baada ya kuandika kuwa anakaribia kukata tamaa kutokana na mchakato huo kushindwa kukamilika.

Ikumbukwe kuwa awali Dewji aliwahi kusema kuna watu ndani ya Simba wanakwamisha mchakato huo. Hatufahamu haya yana ukweli gani ila uhalisia ni kwamba mchakato huo bado haujakamilika. Inashangaza sana.

Simba ilifanya mchakato huu kwa kasi ya Kimbunga. Ikabadili Katiba kwa haraka. Hata hivyo Serikali ikawapa maelekezo mengine ikiwemo kufanya mgawanyo wa hisa kuwa asilimia 51 kwa Wanachama na 49 kwa mwekezaji. Awali mwekezaji alikuwa amepewa asilimia nyingi zaidi.

Pamoja na hivyo bado Dewji alikubali kununua asilimia hizo 49 kwa Shilingi 20 Bilioni. Hakukuwa na tatizo katika hilo. Kwanini mpaka Leo mchakato haujakamilika? Nitakueleza.

Japokuwa maswali mengi ni kuwa kama mchakato haujakamilika, ilikuwaje mwaka jana Dewji akaitisha mkutano na Wanahabari kutangaza kuwa ametoa fedha za uwekezaji wake? Ni kweli aliweka fedha hizo? Na kama aliweka ni kwa maelekezo gani? Ni maswali magumu yanayohitaji majibu.

Pengine Dewji aliambiwa aweke fedha hizo ili mchakato ukamilike lakini mambo bado hayajakwenda katika njia inayopaswa.

Soka kwa sasa ni Biashara. Dewji anaweka fedha nyingi pale Simba kila msimu. Uimara wa Simba katika miaka hii sita imewezekana kwa fedha za Mo Dewji. Chapa ya Simba imekuwa kwa kasi sana.

Leo hii wadhamini ambao tunaona wanamiminika pale Simba ni kutokana na nguvu ya fedha za Mo Dewji katika miaka hii sita kuifanya Simba kuwa imara.

Hivyo Mo Dewji ana haki ya kulalamika kama mchakato huo haujakamilika. Japokuwa mara nyingi anatumia njia isiyo sahihi kuwasilisha malalamiko yake.
Tulitarajia malalamiko haya yangewasilishwa katika Mkutano

Mkuu wa Klabu ili Wanasimba wajadili Pamoja. Huku kungekuwa na suluhisho la pamoja.
Ila kwa upande mwingine pamoja na mchakato kutokukamilika, lakini tayari unafanya kazi kwa upande wa Mo Dewji. Kwa sasa upande wake ndio una nguvu kwenye Bodi ya Wakurugenzi.
Upande wa mwekezaji ndio unaendesha Klabu kwa sasa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Tryagain’ ndiye mwenye sauti kubwa na siyo Rais wa Klabu, Mangungu.
Kwa kifupi Mo Dewji ndio anaendesha Simba. Ndio ana sauti kubwa. Kwanini akate tamaa wakati mpaka sasa ndiye mwenye nguvu kubwa ndani ya Klabu?

Ni kweli kwamba hanufaiki na timu? Hapana. Kwa miaka hii sita amekuwa pia akinufaika na timu ya Simba pia. Kuna matangazo mangapi ya kampuni zake kwenye jezi ya Simba? Ni mengi.
Jina na chapa ya bidhaa zake zimekua sana sokoni kwa miaka hii sita. Nadhani hata yeye moyoni anakiri kuwa biashara zake zimeimarika kwa nguvu ya Simba.

Pia, mwanzoni ni kweli alikuwa akitoa fedha nyingi sana pale Simba miaka ya mwanzo Ila kwa sasa vitu vingi vimebadilika.
Simba ilikuwa ikijiendesha kwa hasara lakini kwa mara ya kwanza msimu uliopita walipata faida. Ni ishara kuwa Simba sasa imeanza kukaa kwenye njia sahihi.

Kwanini tajiri akate tamaa wakati ambao timu inakaribia kuanza kujiendesha kwa faida? Inafikirisha sana.
Simba wakati Mo Dewji anaingia haikuwa na fedha za kueleweka. Mapato ya klabu hayakuwa yakifika hata Shilingi 3 bilioni. MO Dewji alilazimika kutoa fedha nyingi sana kuendesha klabu.
Kwa sasa Simba ina mapato yanayozidi Shilingi 11 bilioni kwa mwaka. Ni fedha nyingi. Ila haya yamewezekana kwa nguvu ya Dewji. Kwanini akate tamaa wakati mambo yameanza kuwa mazuri?

Upande mwingine Wanasimba wanapaswa kusimama pamoja kuhakikisha huu mchakato wa mabadiliko unakamilika. Sitamani kuona Simba ikirejea katika nyakati zile za ukata.
Mpira wa kisasa unahitaji wawekezaji Kama MO Dewji. Sote tunafahamu hilo. Kama ataondoka sasa itakuwa ni pigo pia kwa Simba.

Tazama namna ambavyo pia Yanga imeimarika chini ya GSM. Ila haiwezi kuwa hivyo kwa miaka yote kama mchakato wa mabadiliko hautakamilika. Kazi kwao.