Mtihani mgumu Arsenal kutetea ubingwa 2026/27
Muktasari:
- Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, moja ya mitihani mikubwa iliyonayo msimu ujao ni kutetea taji hilo.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kuifunga MK Dons mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki wiki mbili zilizopita, Arsenal ilitarajiwa kuanza rasmi maandalizi ya msimu mpya kwa mechi dhidi ya Girona juzi, Jumamosi jioni kabla ya kuahirishwa. Hata hivyo, kesho inacheza na Real Betis.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, moja ya mitihani mikubwa iliyonayo msimu ujao ni kutetea taji hilo.
Ni Manchester City pekee iliyofanya hivyo mara tatu tangu Manchester United ilipotwaa kwa mfululizo huo kati ya 2007 na 2009.
Chelsea FC imefanya hivyo mara moja, huku Liverpool yenyewe ikisubiri kwa takriban miaka 40 kubeba taji hilo na ilishindwa kulitetea.
Ni wazi Mikel Arteta na chama lake ana changamoto ya kuyafikia mafanikio ya msimu uliopita ikiwamo kufika fainali ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu wa 2021/22, Man City ndiyo pekee kati ya timu tano za England zilizowahi kufika fainali katika miaka ya karibuni na kufika nusu fainali msimu uliofuata.
Kwa sasa ushindani Ligi Kuu England ni mkubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote, huku ugumu mwingine ukiwa ni kushindana katika mashindano mawili kwa wakati mmoja.
Kinachoweza kuibeba timu ni usajili na Arsenal imeongeza baadhi ya nyota na matumizi ya fedha hadi sasa yamekuwa ya wastani.
Imetumia nusu ya Pauni 79 milioni kukamilisha usajili wa Piero Hincapie aliyekuwa akicheza kwa mkopo kalbuni hapo msimu uliopita 2025/26.
SUALA LA VINI JR
Arsenal kwa sasa inahusishwa na nyota wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Junior anayekipiga Real Madrid ya Hispania.
Ingawa kunaonekana kuna ugumu wa kunasa saini yake, ni wazi akitua ataufanya upande wa kushoto wa kikosi hicho kuwa hatari.
Msimu uliopita Vini alitembea na mpira mara 92 kwa wastani wa mita tano ambazo ziliishia ama kupiga mashuti (49) au kutengeneza nafasi ya bao (43). Hiyo ikiwa ni idadi kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote katika ligi tano bora za Ulaya.
Kwa Arsenal ambayo mara nyingi imekuwa ikitegemea mipira iliyokufa (set pieces) kupata mabao, uwepo wa Vini utaongeza kwa kiasi kikubwa tishio kwa wapinzani.
Hata hivyo, viongozi wa idara ya fedha Arsenal wanaweza kusita. Takwimu za mishahara kutoka Capology zinaonyesha Vini ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi katika ligi tano kubwa za Ulaya, akiwa anapata Pauni 100,000 zaidi kwa wiki zaidi ya mshahara wa mchezaji anayelipwa zaidi Arsenal.
Hata hivyo, swali linabaki, je Arsenal itavunja utaratimu wake wa mishahara? Hii pia inaweza kusababisha mawakala wa nyota wengine kudai ongezeko la mishahara kwa wachezaji wanaowasimamia.
KAZI IPO KWA BERTA
Arsenal tayari imemsajili winga wa Ugiriki kutoka Club Brugge, Christos Tzolis, kama mbadala wa Leandro Trossard ambaye wanapishana miaka saba na anatajwa kama mmoja wa nyota watakaotisha msimu ujao.
Pia inawafukuzia nyota wengine akiwamo Bradley Barcola ambaye pia anawaniwa na Liverpool ambao wana uhitaji mkubwa zaidi wa mawinga.
Huu ndiyo mtihani unaomkabili Andrea Berta, mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, kuboresha kikosi na tangu atue mwaka uliopita na moja ya malengo ilikuwa kuwanasa Alexander Isak kutoka Newcastle United na Benjamin Sesko aliyekuwa RB Leipzig.
MAJERUHI TATIZO
Msimu uliopita licha ya kubeba ubingwa na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsenal ilisuasua kutokana na kuwa na majeruhi wengi.
Mmoja wa nyota waliokosa mechi nyingi ni Kai Havertz na aliyekuwa analipwa zaidi kabla ya Bukayo Saka kuongeza mkataa.
Kai alianza mechi saba tu za ligi, huku nahodha Martin Odegaard pia alikosa baadhi ya mechi kutokana na majeraha, hivyo yeye na Saka walianza pamoja mechi 10 tu za Ligi Kuu msimu wa 2025-26.
Hata hivyo, licha ya majeruhi Arsenal ilikuwa na wachezaji watano kati ya 20 bora wa Ligi Kuu England waliocheza dakika nyingi katika mashindano yote wakiwamo kipa David Raya.
Waliocheza zaidi ya dakika 4,200 ni na Declan Rice (dk 4,456) akishika nafasi ya 11 kwa klabu za Ligi Kuu England, huku Martin Zubimendi (4,298) akiwa wa 15, William Saliba (4,254) akishika namba 17 na Gabriel Magalhaes dakika 4,210 akishika namba 19 na wote hao ni nguzo muhimu ya timu.
Saliba pia alicheza dakika 795 akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa katika Fainali za Kombe la Dunia na kuvuka dakika 5,000, hata hivyo, safari yake iliisha mapema baada ya kupata jeraha la mgongo litakalomweka nje kwa muda mrefu.
Rice pia aliichezea England dakika 1,026 katika fainali hizo baada ya kumaliza msimu na Arsenal licha ya kuwa na maumivu ya misuli ya paja na kwa kiasi fulani kuliathiri kiwango chake ambacho kimezua hofu kwa Arteta.
Viktor Gyokeres pia alicheza dakika nyingi akiwa na Sweden na kufanya Arsenal kuwa na wachezaji sita waliocheza angalau dakika 4,400 kwa klabu na timu za taifa tangu mwanzo wa Agosti, mwaka jana.
MAANDALIZI MEPESI YA MSIMU MPYA
Huenda hilo ndilo lililosababisha Arsenal kuchagua maandalizi yasiyo na safari nyingi kwa ajili ya msimu ujao, kwani msimu uliopita walitembelea Asia, lakini mwaka huu safari kubwa ni kwenda Catalonia, Hispania ambako watacheza dhidi ya Girona.
Pia watacheza Dublin, Ireland dhidi ya Real Betis na Cardiff dhidi ya Manchester City katika Ngao ya Jamii, huku wakiwa na mechi za nyumbani dhidi ya Borussia Dortmund na Como.
Kwa kuwa wachezaji bado wanapona uchovu wa Kombe la Dunia, huenda ikachukua muda kabla hatujaiona Arsenal halisi.
Mchanganyiko wa uchovu, majeraha na uwezekano wa kuongeza wachezaji wapya unaweza kufanya mchakato wa kufikia kiwango bora uchukue muda mrefu kuliko ambavyo kocha Arteta angependa.