Kutoka ‘Gate Crasher’ hadi MC Gara B, safari ya yiaka 14 ya UMC
Muktasari:
- Alifika kwenye harusi kama mwanafunzi anayekwenda darasani, akakaa, akatazama, akasikiliza na kujifunza kila kilichokuwa kikiendelea jukwaani. Wakati mwingine alijikuta akiingia kama msaidizi wa DJ, huku nyakati nyingine akifanya kazi ya uhudumu wa vinywaji ili awe karibu na ma-MC na kuona wanavyofanya kazi zao kuanzia mwanzo hadi mwisho.
KUNA watu wanaingia kwenye kazi kwa mlango mkubwa, wengine wanabisha hodi, lakini Godfrey Deogratius Rugarabamu, maarufu MC Gara B, yeye alianza kwa kutafuta mwanya wa kuingia ndani ya sherehe hata kama jina lake halikuwepo kwenye orodha ya wageni.
Alifika kwenye harusi kama mwanafunzi anayekwenda darasani, akakaa, akatazama, akasikiliza na kujifunza kila kilichokuwa kikiendelea jukwaani. Wakati mwingine alijikuta akiingia kama msaidizi wa DJ, huku nyakati nyingine akifanya kazi ya uhudumu wa vinywaji ili awe karibu na ma-MC na kuona wanavyofanya kazi zao kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Leo, MC Gara B ni miongoni mwa majina yanayojulikana katika ulimwengu wa UMC, lakini safari yake haikuanza kwa kamera, umaarufu wala mialiko mikubwa. Ilianza na ndoto, kukosa nafasi kwenye vyombo vya habari na uamuzi wa kugeuza jukwaa la harusi kuwa fursa yake.
ELIMU UALIMU, MOYO KWENYE UTANGAZAJI
MC Gara B anasema licha ya kusomea taaluma ya ualimu, moyo wake ulikuwa kwenye utangazaji, jambo lililomfanya aanze kutafuta njia nyingine ya kufikia ndoto hiyo baada ya kukosa nafasi ya kuajiriwa kwenye vyombo vya habari.
“Nilisomea ualimu lakini nilikuwa na mapenzi makubwa ya utangazaji. Nilipokosa nafasi ya kuajiriwa kwenye vyombo vya habari, nikaona kwenye shughuli za kijamii na harusi kuna ma-MC wanafanya vizuri. Nikaanza kuliona jukwaa lile kama TV show yangu mwenyewe.”
Badala ya kusubiri nafasi ije kwake, MC Gara B alianza kufanya utafiti wake mwenyewe kwa kuzunguka kwenye shughuli mbalimbali na wakati mwingine kuingia bila kuwa mwalikwa rasmi.
“Nilikuwa naenda kwenye shughuli kama mwanafunzi aliye darasani. Wakati mwingine nilikuwa naingia kama gate crasher, wakati mwingine nilifanya kazi ya umasherie ili nipate nafasi ya kuwaona na kuwasikiliza ma-MC kuanzia mwanzo mpaka mwisho.”
MWONEKANO NDIO KILA KITU
MC Gara B anasema alipogundua ushindani uliokuwa kwenye soko, alitambua kuwa kipaji pekee hakikutosha, hivyo akaamua kuwekeza kwenye mwonekano wake. Akiwa na kipato kidogo, alianza kwenda soko la Karume kutafuta suti na makoti mazuri ambayo yangeweza kumtofautisha na ma-MC wengine.
“Nilisoma soko nikagundua mwonekano ni muhimu. Hata wakati ninaanza na kipato kidogo, nilikuwa naenda Karume kununua suti na makoti mazuri. Nilijua lazima nionekane tofauti,” anasema.
“Niliona hatuwezi kuendelea kuomba vigelegele na makofi tu. Nikaanza ku-hype nyimbo za wasanii wa ndani na nje wakati maharusi wanaingia. Hapo ndipo watu wakaanza kuona kuna kitu tofauti.”
2012 ALIANZA KULIPWA
Baada ya miaka ya kujifunza na kutafuta nafasi, MC Gara B anasema mwaka 2012 ndio aliouanza kuuchukulia UMC kama ajira rasmi baada ya kuanza kulipwa kwa kazi hizo.
“Nilipoingia nilikuta ma-MC kama Dr. Chen, Anthony Luvanda, Dr. Ndimbo, MC A, Uncle na Kwayu. Kwa Anthony nilijifunza mengi na Dr. Ndimbo pia alikuwa mtu muhimu kwangu,” anasema Gara B.
Kabla ya kujikita kikamilifu kwenye UMC, MC Gara B alikuwa akifanya kazi zaidi ya moja. Asubuhi alikuwa mwalimu, kuanzia saa 1:00 hadi saa 8:00 mchana, kisha akaendelea na kazi ya huduma kwa wateja kwenye kampuni ya simu na usiku akifanya kazi kwenye kiwanda cha mabati.
“Nilikuwa nimepata kazi ya kuendesha harusi ya mfanyakazi mwenzangu. Kwa kuwa nilitakiwa kuwepo kazini, nikachukua sick sheet. Lakini bosi wangu naye akawa amehudhuria ile harusi na akanikuta niko jukwaani naendesha shughuli,” anasema.
Kabla ya kufikia hatua ya kupata malipo makubwa, anasema baadhi ya kazi zake za kwanza alizifanya bure kwa lengo la kujenga jina na kupata jukwaa la kuonyesha uwezo wake.
Anasema kuwa, “nilianza kwa kufanya kazi bure ili nipate platform ya kuonyesha uwezo wangu. Kuna wakati nilikuwa nalipwa Sh10,000 au Sh20,000, lakini hiyo ilikuwa zaidi kwa ajili ya nauli.”
SIMU ZILIMJENGEA JINA, MITANDAO NI OFISI
Baada ya kuanza kujulikana, MC Gara B alianza kupata simu za dharura kutoka kwa ma-MC wakubwa waliokuwa wakishindwa kufika kwenye shughuli walizokuwa wamebookiwa.
“Nilianza kupata simu za dharura kutoka kwa ma-MC wakubwa waliokuwa wameshindwa kwenda kwenye shughuli. Nikienda naendesha shughuli yote kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Hapo wateja wakaanza kunitafuta mimi moja kwa moja.”
MC Gara B hakutaka kazi zake ziishie ukumbini. Akaanza kuwekeza kwenye picha na video ili kila shughuli aliyofanya ibaki kama kumbukumbu na wakati huohuo iwe matangazo ya kazi yake.
“Nilitaka picha na video zipatikane kwa wakati. Sikutaka kusubiri timu ya harusi mpaka wiki au mwezi mmoja baadaye. Nilihakikisha nina mtu wangu anayepiga picha na video na kisha kazi hizo nikaziweka Facebook, Instagram na YouTube.”
BOOKING ZAIDI YA 60 TAREHE MOJA
Kadiri jina lake lilivyozidi kukua, changamoto nyingine nayo ikaibuka. MC Gara B anasema wakati mwingine maombi ya booking yanaweza kufika zaidi ya 60 kwa tarehe moja.
“Changamoto kubwa ya UMC ni kwamba MC hawezi kugawanyika. Kuna siku unaweza kupata booking zaidi ya 60 kwenye tarehe moja, lakini huwezi kwenda zote.”
MTOKO MMOJA MILIONI MOJA
MC Gara B anasema vazi moja analovaa kwenye shughuli kuanzia juu hadi chini haliwezi kugharimu chini ya Sh1 milioni, huku kila kitu kikichaguliwa kwa umakini, kuanzia koti, viatu, saa hadi skafu.
“Vazi langu moja kuanzia juu mpaka chini halipungui milioni moja. Kila detail naiangalia kwa sababu nikifika kwenye shughuli namwakilisha mteja.”
MC Gara B anasema mteja halipii mtu anayeshika kipaza sauti pekee, bali analipia mfumo mzima wa taasisi yake unaohusisha ofisi, wafanyakazi zaidi ya 20, ushauri pamoja na huduma za picha na video.
“Mteja halipii MC mmoja tu. Analipia taasisi, kuna kodi ya ofisi, wafanyakazi zaidi ya 20, consultation, picha na video na huduma nyingine. Ndiyo maana ukiangalia bei lazima uangalie thamani anayopata mteja.”
HARMONIZE MTU POA
MC Gara B amepata pia nafasi ya kufanya kazi na mastaa mbalimbali, akiwemo Harmonize na Kajala, ambao aliwafanyia shughuli mbili za uchumba.
“Harmonize ananiheshimu sana kama kaka. Anaweza kuja ofisini kwangu kushona suti na tunasaidiana au kushauriana kwenye mambo ya maisha na mahusiano kwa simu moja.”
Kwa MC Gara B, umaarufu wa wasanii hauondoi ukweli kwamba nao ni binadamu wenye changamoto zao.
“Wasanii ni binadamu wa kawaida. Wamebeba gunia la misumari kwa sababu wanatakiwa kulinda taswira yao mbele ya jamii. Kuna mambo mengi wanapitia ambayo watu hawaoni,” anasema.
MAFANIKIO YAKE, MC WA GHARAMA
MC Gara B anasema moja ya mafanikio makubwa anayojivunia si fedha pekee, bali ni mtandao wa watu alioujenga kutokana na kazi yake. Anataja viongozi wa serikali, mawaziri na maaskofu kuwa sehemu ya mtandao huo, huku taasisi yake ikiwa imekuwa chanzo cha ajira kwa vijana zaidi ya 20.
“Moja ya mafanikio makubwa ninayojivunia si fedha pekee. Nimeweza kujenga mtandao mkubwa wa watu kutokana na kazi yangu. Nimekutana na viongozi wa serikali, mawaziri, maaskofu na watu wengi mbalimbali. Pia taasisi yangu imekuwa chanzo cha ajira kwa vijana zaidi ya 20, jambo ambalo kwangu ni mafanikio makubwa,” anasema MC Gara B.
MC Gara B pia amegeuka kuwa mwalimu wa kizazi kipya cha ma-MC kupitia programu yake ya ‘UpSkill Class’, ambayo amekuwa akiendesha kwa takribani miaka saba akishirikiana na MC Mchoma.
“Nilitaka kile nilichojifunza kwa miaka mingi kisiishie kwangu. Ndiyo maana nikaanza UpSkill Class. Tunawafundisha ma-MC wapya ili waweze kuelewa soko na kujua namna ya kujiendesha.”
SIMBA DAMU, STARS IPEWE KIPAUMBELE
MC Gara B ni shabiki wa Simba, ushabiki ambao anasema ulianza nyumbani kupitia kaka yake aliyekuwa golikipa na aliyetamani kuwa kama Mohamed Mameja. Mchezaji anayemtaja kama mmoja wa bora zaidi aliowahi kumuona Simba ni Juma Kaseja, huku Clatous Chama akiwa miongoni mwa wachezaji anaowakubali.
“Mimi ni Simba damu. Ushabiki wangu ulianzia nyumbani kupitia kaka yangu ambaye alikuwa golikipa na alikuwa anatamani kuwa kama Mohamed Mameja. Kwa hiyo tangu hapo nikawa nimeingia kwenye Simba. Kwenye wachezaji, Juma Kaseja ni mmoja wa makipa bora ambao nimewahi kuwaona Simba, na Clatous Chama pia ni mchezaji ninayemkubali,” anasema.
Akizungumzia Taifa Stars, MC Gara B anasema TFF, Wizara na wadau wa soka wanapaswa kuelekeza nguvu kwenye maandalizi ya timu ya taifa kuelekea AFCON.
“Tunapoelekea AFCON, TFF, Wizara na wadau wote wanapaswa kuweka nguvu kwenye maandalizi ya Taifa Stars. Tusipoteze muda kwenye siasa au migogoro ya midahalo ya jezi. Timu yetu inahitaji maandalizi mazuri,” anasema.