Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jabaar: “Ile kadi nyekundu ilinivuruga, Simba nimekuja kutwaa ubingwa”

Muktasari:

  • Jabaar, raia wa Nigeria aliyesajiliwa na Simba akitokea Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, amekuwa miongoni mwa wachezaji wapya waliopewa nafasi na kuonyesha kuwa na kitu mapema na kocha Steve Barker katika kikosi hicho kinacholenga kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara Msimbazi.

KIUNGO mpya wa Simba, Ibraheem Jabaar, amefunguka kuhusu changamoto kubwa aliyokutana nayo katika mwanzo wake wa maisha ya soka Tanzania, akitaja kadi nyekundu aliyopata dhidi ya Pamba Jiji kuwa funzo ambalo hataki kulirudia.

Jabaar, raia wa Nigeria aliyesajiliwa na Simba akitokea Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, amekuwa miongoni mwa wachezaji wapya waliopewa nafasi na kuonyesha kuwa na kitu mapema na kocha Steve Barker katika kikosi hicho kinacholenga kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara Msimbazi.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Simba Julai, mwaka huu baada ya kuachana na Stellenbosch, klabu ambayo aliitumikia kwa miaka miwili akiendelezwa na kujijengea uzoefu wa soka la Afrika Kusini.

Barker pia anamfahamu vizuri kutokana na kufanya kazi naye huko nyuma.

Lakini wakati mwanzo wake ukiwa umejaa ishara nzuri, Jabaar alijikuta akiingia kwenye vichwa vya habari baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika mchezo huo wa Agosti 19, Simba ilikuwa imeanza vizuri na kujenga uongozi wa mabao 2-0 kupitia Clatous Chama na Anicet Oura. Hata hivyo, kabla ya mapumziko, mchezo ukabadilika kwa upande wa Simba baada ya Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia tukio la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji.

Tukio hilo lilikuja baada ya mwamuzi kupitia mfumo wa Video Support System, hatua iliyomfanya Jabaar kuondolewa uwanjani huku Simba ikibaki na wachezaji 10. Pamba Jiji ilipata bao la kufutia machozi kupitia mkwaju wa penalti, lakini Simba ilifanikiwa kulinda ushindi wa mabao 2-1.

Ikiwa zimepita wiki chache baada ya tukio hilo, Jabaar amelizungumzia katika mahojiano na Mwanaspoti, akikiri kwamba ni sehemu ya changamoto ambazo mchezaji anaweza kukutana nazo, lakini akisisitiza kwamba amejifunza kutokana na kosa hilo.

“Nilijiambia ‘come on, Ibraheem unawezaje kufanya hivi.’ Unajua wakati mwingine kama mchezaji unashindwa kujizuia unajikuta unafanya kitu cha ajabu kwa sababu damu inakuwa imechemka, lakini unajifunza kutokana na makosa yako. Kwa hiyo nina uhakika haitatokea tena,’  anasema Jabaar.

Ndani ya raundi mbili za kwanza, Simba ilikuwa tayari imepoteza wachezaji wawili kwa kadi nyekundu akiwemo David Kameta ‘Duchu’, jambo lililomfanya Barker kuitisha kikao na wachezaji wake na kusisitiza umuhimu wa nidhamu.

Kwa Jabaar, hata hivyo, tukio hilo halijaondoa imani yake kwamba anaweza kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Simba msimu huu.

Akiwa katika msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Tanzania, anasema mazingira ya soka anayokutana nayo hapa yamekuwa ya kuvutia na tayari ameanza kuyaelewa.

“Ni jambo la kuvutia sana. Kawaida tunapopata pointi tatu, tunataka kuendelea kufanya vizuri katika ligi na kushinda ubingwa. Hilo ndilo lengo kuu,” anasema.

Jabaar anajua kwamba kuvaa jezi ya Simba si suala la kucheza mechi tu za ushindani kwa sababu ni timu yenye matarajio makubwa ndani na nje ya Tanzania, huku msimu huu ikiwa na kazi ya kupigania ubingwa wa ligi na wakati huohuo kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Hilo ndilo linalomfanya asiangalie maisha yake Simba kwa upande wa Ligi Kuu pekee.

“Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Kama unataka kufanya vizuri katika michuano hiyo, lazima uwe tayari kwa aina hii ya michezo. Utakutana na timu nyingi zenye presha, lakini sisi tuko vizuri kucheza dhidi ya aina yoyote ya timu,”  anasema.

Jabaar tayari amepata nafasi ya kuonja ushi ndani wa kimataifa akiwa na Simba, na hilo limempa picha ya ukubwa wa jukumu alilonalo katika kikosi hicho.

Kwa mtazamo wake, Simba ina ubora wa kutosha ndani ya kikosi chake kuweza kushindana katika mazingira hayo huku akiwataja baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakimvutia tangu alipowasili.

“Unaweza kuona tuna wachezaji wengi wenye ubora. Tuna wachezaji kama Chama, Libase, Maema na wengine, hao wote ni wachezaji wa kiwango cha juu, ambao wanaweza hata kusaidia timu katika mazingira magumu dhidi ya mpinzani yeyote,” anasema.

Lakini kabla ya kufika kwenye vita vya Afrika, Jabaar pia ameshaonja presha ya mechi kubwa za ndani, ikiwamo dabi dhidi ya Yanga.

Kwa mchezaji ambaye ametoka nje ya Tanzania, mchezo huo ulikuwa pia nafasi ya kuona kwa macho ukubwa wa ushindani uliopo kati ya timu hizo mbili na namna mashabiki wanavyoupa uzito mchezo huo.

“Ni mchezo mzuri, kusema kweli. Ni kwamba hatukupata pointi tatu tulizotaka katika Ngao ya Jamii, lakini ulikuwa mchezo wa kuvutia sana. Ninauangalia kwa hamu na ninatarajia michezo kama hiyo na imani yangu ni kwamba safari hii kwenye ligi tutafanya vizuri na kuendeleza mwanzo mzuri wa msimu ambao tumekuwa nao,” anasema.

Jabaar hakuficha kwamba kucheza Tanzania kuna tofauti na mazingira aliyoyazoea Afrika Kusini, lakini upande wa hali ya hewa haujawa tatizo kubwa kwake.

Anasema hali ya hewa ya Tanzania imemsaidia kuzoea kwa haraka kwa sababu inafanana kwa kiasi fulani na alikotoka Nigeria.

“Hali ya hewa ni kama Nigeria. Kwa hiyo inanifaa na inanifanya nijisikie kama niko kwenye mazingira ninayoyafahamu,” anasema.

Hata hivyo, anapoulizwa changamoto kubwa zaidi aliyoiona tangu afike Tanzania, Jabaar anasema: “Kusema kweli, changamoto pekee niliyopitia ni ile kadi nyekundu. Sikupanga hilo litokee.”

Lakini baada ya tukio hilo, anasema kinachobaki kwake ni kujifunza, kurekebisha makosa na kuendelea mbele. Kwa Jabaar, safari yake Simba bado iko mwanzoni. Anaamini tukio la kadi nyekundu halipaswi kuwa alama kubwa kuliko uwezo wake wa kucheza, hasa baada ya kufika Msimbazi akiwa na uzoefu wa kucheza soka la ushindani Afrika Kusini.

Alisajiliwa Simba kama sehemu ya mipango ya Barker ya kujenga kikosi chenye uwezo wa kushindania mafanikio ya ndani na kimataifa na tayari amepata nafasi ya kuanza baadhi ya michezo ya mwanzo ya msimu. “Tumekuwa muda mrefu bila kushinda ligi. Kwa hiyo lengo sasa ni kushinda ligi. Hilo ndilo jambo la kwanza na pia tunataka kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa,” anasema.

Huo ndio ujumbe ambao Jabaar anataka ubaki baada ya mwanzo wake wenye mchanganyiko wa furaha na changamoto Simba.

Amefika akiwa na matumaini makubwa, ameanza kupewa nafasi na Barker, ameonja ushindani wa Ligi Kuu, amepitia presha ya dabi na pia amekumbana na upande mgumu wa soka baada ya kadi nyekundu lakini yote hayo ni sehemu ya safari.