Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama Fatma Karume amelala na kadi namba moja ya Yanga

Muktasari:

  • Mama Karume amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 97 na alizikwa jana Jumanne, saa 10 jioni katika makaburi ya familia Mbweni.

MWAMBA wa michezo Zanzibar umeanguka! Ndivyo unavyoweza kuelezea pigo ambalo tasnia ya michezo Zanzibar na Tanzania kiujumla imepata baada ya kifo cha Mama Fatma Karume, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume kilichotokea juzi usiku, Unguja.

Mama Karume amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 97 na alizikwa jana Jumanne, saa 10 jioni katika makaburi ya familia Mbweni.

Historia ya ushiriki wake na mumewe Hayati Abeid Karume katika kuanzishwa Klabu ya Yanga na ununuzi wa eneo ambalo kumejengwa jengo la klabu hiyo, pia ujenzi wa jengo la Simba ni miongoni mwa alama za utambulisho wa namna Mama Fatma Karume alivyokuwa mdau wa soka na michezo kijumla na aliwahi kutangazwa na Yanga ndiye mwenye kadi namba moja ya uanachama ya timu hiyo.

“Yapo mambo mengi ya Karume (Abeid)  niliyokuwa nayafahamu kwa kushirikishwa. Mambo hayo ni kama vile ujenzi wa majengo ya klabu za Yanga na  Simba.

“Kwa Yanga, hayati Karume ndiye alitoa kiasi kikubwa kama sio chote kwa ajili ya ujenzi wa jengo la makao makuu ya Yanga. Alifanya hivyo kwa Yanga baada ya kushirikiana na Wanasimba kupata jengo lao kwenye Mtaa wa Msimbazi pia Kariakoo Dar es Salaam kwa kuchangia kiasi cha fedha. Kimsingi Karume alishiriki kujenga majengo yote mawili ya klabu za Simba na Yanga.

“Ukitaka kuamini jinsi jengo la Yanga lilivyo na uhusiano na Wazanzibari, tangaza sasa kulipiga mnada uone jinsi utakavyoshukiwa kwa hasira na Wazanzibari,” alinukuliwa Bi Fatma Karume katika mahojiano aliyowahi kuyafanya na gazeti la Mwanaspoti miaka ya nyuma.


MJUMBE BARAZA LA WADHAMINI YANGA

Mapenzi yake ya soka na hasa klabu ya Yanga, yalimfanya kuwa mwanamke aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika uongozi wa klabu na kwa zaidi ya miaka 20 alikuwa Mjumbe wa Barza la Wadhamini la Klabu ya Yanga.

Marehemu Fatma Karume aliwahi kufichua namna alivyoingia katika Baraza hilo la Wadhamini la Yanga na anasema klabu ilimpelekea maombi ambayo aliyakubali.

“Walinifuata wenyewe kuniomba niwe mdhamini wa klabu hiyo kwa vile marehemu mume wangu ndiye alikuwa muasisi wao.

“Nami sikuwa na hiyana nikawakubalia. Siku nikiona nimechoka, nitawaambia mimi udhamini tena basi,” alinukuliwa marehemu Fatma Karume.

Kabla hajaaga dunia, Fatma Karume aliwahi kufichua siri ya kilichochangia adumu muda mrefu katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wadhamini ni uwezo wa kutunza siri na kulinda mali za klabu.

“Siwezi kutangaza mali za Yanga ni zipi na zipi ila mali zote za Yanga nazifahamu vizuri sana. Kazi yangu ni kuzilinda. Siri ya ndani siwezi kuitoa nje,” alinukuliwa Bi Fatma Karume.


UFUKUZAJI MAKOCHA

Bi Fatma Karume aliwahi kukiri hadharani anaunga mkono ufukuzaji wa makocha ingawa alisistiza ni lazima uwe na sababu maalum.

“Kufungwa kunauma asikuambie mtu. Kama hawafanyi vizuri kwa nini wasifukuzwe? Kuna mgawanyo wa madaraka. Mimi siwezi kuwakataza wasifukuze makocha kwa kuwa wao ndio wapo karibu na timu,” alisema Bi Fatma Karume wakati wa uhai wake.


IMANI UJENZI WA UWANJA YANGA

Mara zote Bi Fatma Karume alikuwa akionyesha imani chanya siku moja klabu hiyo itamiliki uwanja wa kisasa katika Makao Makuu yake mitaa ya Twiga na Jangwani.

“Kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Kaunda, naomba jambo hilo tuliache kama lilivyo. Ikifika wakati wa kujengwa, litajengwa,” alinukuliwa Fatma Karume.

KUKEMEA UHASAMA YANGA, SIMBA

Miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakimkera Fatma Karume ni tabia za uhasama baina ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga.

Mama Fatma Karume alilithibitisha hilo mwaka 2019 katika mkutano wa kuichangia klabu ya Yanga uliojulikana kama hafla ya Kubwa Kuliko na alikemea mbele ya hadhara, uhasama wa timu hizo mbili na kuhamasisha umoja baina yao.

“Marehemu Mzee Karume alikuwa yeye ni mwanachama wa Yanga. Lakini alipokuja Dar es Salaam mwaka 1964, akaangalia wakati akishakuwa yeye Rais wa Zanzibar, akaangalia namna ya Yanga na Simba na vilivyokuwa vyama viwili tu vya mpira hapa, alisaidia kuwajengea nyumba Yanga na hadi leo ipo na aliwapa fedha taslimu Simba wanunue nyumba na nadhani hadi leo wanayo.

Kwa kusema kweli, hatuwezi kuvaa uhasama wa upumbavu na wa ujinga katika nchi yetu. Tunatakiwa tuvae heri, salama na kujenga nchi yetu kwa imani, kitu kimoja kama hivi tulivyo. Vyama (timu) sio vya kugombana kwa sababu kama vinaleta hasama, basi siasa isingekuwepo nchi hii,” alinukuliwa Mama Karume.


MPENZI WA MUZIKI PIA

Bi Fatma Karume aliwahi kufichua mbali na soka, amekuwa akipendelea pia muziki na ndiyo ulimkutanisha na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume hadi wakafunga ndoa.

“Wakati ule mimi nilikuwa binti kigori. Nakumbuka siku hiyo aliyoniona, ilikuwa sikukuu ya Idd. Siku iliyofuata ilikuwa Idd pili, baba mkubwa akanichukua mimi na binamu yangu akatuambia twende dansini. Mimi nilikuwa napenda sana muziki. Basi tulipofika ndipo nilipojua kumbe Karume ni mwanamuziki.

“Nilikuta anaongoza wanamuziki wenzake basi wakaimba pale, marehemu (Karume) aliponiona akiwa jukwaani alishuka. Akaja moja kwa moja kwangu akaniambia ‘Waooh! umependeza, leo umekuja kutuangalia’, basi palepale ndipo alipoanza kuniambia ananipenda. Vijana wa siku hizi mnasema kusomesha.

“Mimi nilipenda kuwa huru. Nilipenda muziki, nikamkubali, tukafungua ukurasa wa mapenzi,” alifichua Bi Fatma Karume.

WADAU WA SOKA WAMLILIA

Klabu ya Yanga imeeleza kusikitishwa na kushtushwa na kifo cha Mama Karume kikimtaja kama mwanachama wao aliyetukuka.

“Huu ni msiba mkubwa kwetu. Tumepoteza kiongozi mkubwa mwenye busara, hekima na mapenzi makubwa na klabu yetu. Tutamkumbuka Mama yetu Fatma Karume kwa mengi mazuri aliyofanya ndani ya klabu yetu, ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya jengo letu la Makao Makuu, Jangwani jijini Dar es Salaam.

“Hakika, tumempoteza mwanachama na moja ya nembo ya klabu hii,” alisema Rais wa Yanga, Hersi Said.

Klabu ya Simba nayo imeonyesha kusikitishwa na msiba huo.

“Simba inaungana na Watanzania wote kuomboleza msiba huu na tunamuomba Mwenyezi Mungu aipe subira familia, ndugu jamaa wa marehemu katika kipindi hiki kigumu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema,” ilisema taarifa ya Simba.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema, “Kurasa nyingine ya thamani kwenye kitabu cha historia ya Klabu yetu ya Yanga imefunikwa milele. Pumzika kwa amani bibi yetu Fatma Karume,” alisema Kamwe.