Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanakwanguana! Hakuna kulala Ligi Kuu England

EPL Pict

Muktasari:

  • Katika raundi ya 10, kila timu itakuwa na sababu ya kupambana kupata matokeo mazuri. Twende pamoja!

LONDON, ENGLAND: ACHANA na matokeo ya mechi ya jana usiku kati ya Everton na Coventry City katika Ligi Kuu England (EPL). Mechi za leo Jumamosi, kesho Jumapili na keshokutwa Jumatatu zinatarajiwa kuleta vicheko na vilio kwa timu mbalimbali kabla ya mapumziko ya kalenda ya Fifa ya mechi za kimataifa inayoanza wiki ijayo.

Katika raundi ya 10, kila timu itakuwa na sababu ya kupambana kupata matokeo mazuri. Twende pamoja!


EP 02

LEO, JUMAMOSI

LEEDS UNITED VS SPURS

Tottenham Hotspur itakuwa ugenini dhidi ya Leeds United ikitafuta ushindi wa nne mfululizo wa ligi, jambo ambalo haijafanya tangu Septemba na Oktoba 2023. Hata hivyo, Spurs inapewa uwezekano wa asilimia 31.6 wa kushinda, ikilinganishwa na asilimia 41.7 za Leeds.

Leeds imekusanya pointi tano pekee katika mechi 13 zilizopita za ligi dhidi ya Spurs, ikiwa na ushindi mmoja, sare mbili na vipigo 10. Pia haijamaliza mchezo bila kuruhusu bao katika mechi 16 zilizopita dhidi ya Tottenham.

Licha ya rekodi hiyo, Leeds haijapoteza mechi nane za mwisho za nyumbani kwenye Uwanja wa Elland Road, ikishinda nne na kutoka sare nne. Hata hivyo, haijashinda mechi tano za mwisho za ligi, ikiwa na sare tatu na vipigo viwili, ikiwemo kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Bournemouth katika mchezo uliopita.

Mchezo huo unapewa uwezekano wa asilimia 26.7 wa kutoka sare, ukiwa miongoni mwa mechi mbili zenye nafasi kubwa zaidi ya matokeo hayo wikiendi hii.


EP 03

ARSENAL VS HULL CITY

Arsenal imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuifunga Liverpool wiki iliyopita. Kwa uwezekano wa asilimia 76.9, ndiyo timu inayotabiriwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda mwishoni mwa wiki hii.

Mpinzani wake, Hull City, hajashinda katika mechi saba zilizopita za ligi, ikiwa na sare tano na vipigo viwili. Hakuna timu iliyopata sare nyingi zaidi ya Hull msimu huu. Mchezo huo una uwezekano wa asilimia 13.8 kumalizika kwa sare, jambo ambalo linaweza kuifanya Arsenal kupata sare yake ya kwanza msimu huu.

Arsenal imeshinda mechi saba za mwisho za ligi ilizocheza nyumbani. Katika mechi 13 dhidi ya Hull kwenye mashindano yote, imepoteza moja pekee, ikishinda nane na kutoka sare nne. Hull inapewa uwezekano wa asilimia 9.3 tu wa kushinda.

Gunners hawajapoteza katika mechi 46 zilizopita za ligi dhidi ya timu zilizopanda daraja, wakishinda 41 na kutoka sare tano. Pia wameshinda mechi zote 17 za mwisho dhidi ya timu za aina hiyo.


EP 04

FULHAM VS NEWCASTLE UNITED

Newcastle United, inayopangiwa uwezekano wa asilimia 30.3 wa kushinda, imepoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Everton. Kocha Matthias Jaissle atakuwa na dhamira ya kubadili mwenendo huo itakapokuwa ugenini dhidi ya Fulham, inayopewa asilimia 43 za ushindi.

Fulham imeshinda mechi tatu kati ya nne za mwisho za ligi dhidi ya Newcastle na kupoteza moja. Kabla ya hapo, ilikuwa imecheza mechi nane bila ushindi dhidi ya wapinzani hao, ikitoka sare mbili na kupoteza sita.

Fulham haijapoteza mechi tatu zilizopita za ligi, ikishinda mbili na kutoka sare moja. Katika mechi sita za mwisho za mashindano hayo, imepoteza moja, ikishinda miwili na kutoka sare tatu.

Hakuna kati ya mechi 18 za ligi ambazo timu hizo zimecheza jijini London iliyomalizika kwa sare. Fulham imeshinda mara 11 na Newcastle mara saba. Hata hivyo, mchezo huu una uwezekano wa asilimia 26.7 wa kutoka sare.


EP 05

NOTTINGHAM VS MAN CITY

Vipigo viwili mfululizo vimeifanya Manchester City kushuka hadi nafasi ya pili. Kikosi hicho kitakuwa na matumaini ya kurejea kwenye ushindi dhidi ya Nottingham Forest, ambayo haijawa na kiwango kizuri.

Vipigo hivyo viwili ni sawa na idadi ya vilivyopata katika mechi 33 zilizotangulia za ligi, ambazo City ilishinda 23 na kutoka sare nane. Hata hivyo, inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na morali baada ya kuifunga RB Leipzig mabao 3-2 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

City inapewa uwezekano wa asilimia 50.9 wa kushinda. Katika mechi tisa zilizopita za ligi dhidi ya Forest, imepoteza moja pekee, ikishinda tano na kutoka sare tatu. Hata hivyo, haijashinda mechi mbili mfululizo ikiwa ugenini dhidi ya Forest katika ligi hiyo tangu Januari 1925.

Forest, inayopangiwa asilimia 25.8 ya ushindi, haijashinda mechi sita za mwisho za ligi ilizocheza nyumbani, ikiwa na sare tatu na vipigo vitatu. Pia imeshindwa kufunga katika mechi nne zilizopita.

Licha ya kuwa na mashuti 152, idadi ya pili kwa wingi katika ligi msimu huu, Forest ndiyo timu iliyofunga mabao machache zaidi ikiwa na sita. Ina kiwango cha chini zaidi cha kubadilisha mashuti kuwa mabao, asilimia nne, na tofauti kubwa zaidi hasi kati ya mabao iliyofunga na matarajio ya mabao (xG), ikiwa ni -8.3.


EP 06

KESHO, JUMAPILI

BRIGHTON VS BRENTFORD

Brighton itakuwa ikitafuta kuendeleza presha kwa timu mbili za juu itakapokutana na Brentford, ambayo ilirejea kwenye ushindi dhidi ya Forest katika mchezo uliopita.

Brighton haijapoteza mechi za ligi ilizocheza dhidi ya Brentford kwenye Uwanja wa Amex, ikishinda tatu na kutoka sare mbili. Inapewa uwezekano wa asilimia 54.8 wa kushinda, huku Brentford ikiwa na asilimia 21.9.

Brighton imeweka rekodi ya kutoruhusu bao katika kila moja ya ushindi wake tisa wa mwisho wa ligi, ikiwemo mechi zote sita ilizoshinda msimu huu. Kwa upande mwingine, Brentford ndiyo timu pekee iliyofunga katika kila mchezo wa ligi msimu wa 2026/27. Pia imekuwa ya kwanza kufunga katika mechi nane, idadi kubwa zaidi kwenye ligi.

Brentford imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya 11 iliyopita ya ligi, ikishinda mitatu na kutoka sare saba. Inataka ushindi wa pili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Februari, lakini itakutana na timu inayoongoza kwa mabao mengi zaidi msimu huu ikiwa na 24.


EP 07

CRYSTAL PALACE VS LIVERPOOL

Shinikizo kwa kocha Pierre Sage linaongezeka katika Crystal Palace, ambayo inalenga kutoka kwenye eneo la kushuka daraja kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Liverpool ilipoteza mabao 3-2 dhidi ya Fenerbahce katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano. Hata hivyo, imekuwa na kiwango kizuri katika mechi za ugenini za ligi msimu huu, ikishinda tatu kati ya nne na kutoka sare moja.

Palace inapewa uwezekano wa asilimia 27.1 wa kushinda. Msimu uliopita, ilivunja mfululizo wa mechi 10 bila ushindi wa nyumbani dhidi ya Liverpool katika ligi kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 chini ya kocha Oliver Glasner. Hata hivyo, Palace haijashinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Liverpool tangu misimu ya 1990/91 na 1991/92. Liverpool inapewa asilimia 49 za ushindi.

Palace imepoteza mechi tatu za mwisho za ligi bila kufunga bao, huku ikiruhusu mabao tisa katika michezo hiyo.


EP 08

BOURNEMOUTH VS IPSWICH

Bournemouth, inayopangiwa uwezekano wa asilimia 42.6 wa kushinda, inataka kuendeleza matokeo mazuri itakapokutana na Ipswich Town, ambayo inapewa asilimia 32.1 za ushindi.

Bournemouth haijapoteza katika mechi nne za ligi ilizocheza ugenini dhidi ya Ipswich kwenye Uwanja wa Portman Road, ikishinda moja na kutoka sare tatu. Hata hivyo, haijashinda mechi sita zilizopita za ligi dhidi ya timu zilizopanda daraja. Katika mechi hizo, imetoka sare tano na kupoteza moja. Mchezo huu una uwezekano wa asilimia 25.3 wa kumalizika kwa sare. Ipswich imekusanya pointi saba katika mechi nne za nyumbani msimu huu, ikishinda mbili, kutoka sare moja na kupoteza moja.

Pointi hizo saba ni sawa na ilizokusanya katika michezo yote ya nyumbani kwenye Uwanja wa Portman Road msimu mzima wa 2024/25, iliposhinda moja, kutoka sare nne na kupoteza 14. Bournemouth italazimika kumwangalia Evanilson, ambaye amehusika katika mabao manane katika mechi tisa za ligi msimu huu, akifunga manne na kutoa asisti nne. Amefunga katika kila moja ya mechi nne zilizopita, huku hakuna mchezaji wa Bournemouth aliyewahi kufunga katika mechi tano mfululizo.


EP 09

SUNDERLAND VS CHELSEA

Sunderland imekuwa na wakati mgumu kurejea katika kiwango cha msimu uliopita, ilipoifunga Chelsea katika siku ya mwisho ya ligi na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Europa. Sasa inashika mkia wa msimamo baada ya kucheza mechi tisa. Chelsea inapewa asilimia 43.7 za ushindi, huku Sunderland ikiwa na asilimia 31.2. Hata hivyo, Chelsea imepoteza mechi mbili zilizopita za ligi dhidi ya Sunderland.

The Blues imeshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita za ligi na kupoteza moja. Idadi hiyo ya ushindi ni sawa na ile iliyopata katika mechi 14 zilizotangulia, ambazo ilishinda tatu, kutoka sare mbili na kupoteza tisa. Sunderland imepoteza mechi tano kati ya sita zilizopita za ligi na kutoka sare moja. Vipigo hivyo ni vingi kuliko ilivyopata katika mechi 14 zilizotangulia.

Chini ya kocha Regis Le Bris, Sunderland imeshindwa kufunga katika mechi tatu za mwisho za ligi kwenye Uwanja wa Stadium of Light. Pia imeruhusu mabao 17 katika mechi tisa za msimu huu. Sasa inakutana na Chelsea iliyofunga mabao 19 msimu huu na inayoongoza ligi kwa mashuti yaliyolenga lango ikiwa na 53.


EP 10

JUMATATU

MAN UNITED VS ASTON VILLA

Wikiendi itafikia tamati katika Uwanja wa Old Trafford, ambako Manchester United itakuwa ikitafuta kuendeleza matokeo mazuri baada ya kuifunga Roma katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.

Kocha Michael Carrick bado anakabiliwa na shinikizo kubwa, lakini ushindi walioupata Jumanne unaweza kumpa muda zaidi wa kuendelea kukinoa kikosi hicho. Hata hivyo, ushindi pekee wa Man United msimu huu ulikuwa dhidi ya Ipswich Town mwezi Agosti, timu iliyopanda daraja. Katika mechi nyingine, imepata sare nne na vipigo vinne. Matokeo hayo yanaifanya United kushika nafasi ya 17, ikiwa juu kidogo ya eneo la kushuka daraja kutokana na tofauti ya mabao. Mara ya mwisho kuanza msimu ikiwa na ushindi mmoja pekee katika mechi 10 za mwanzo ilikuwa 1972/73, iliposhinda moja, kutoka sare nne na kupoteza tano.

Aston Villa imekuwa na matokeo mazuri zaidi licha ya kufungwa mabao 3-0 na Barcelona katikati ya wiki. Haijapoteza katika mechi tano za mwisho za ligi. Novemba 2022, Villa iliifunga Man United katika mchezo wa kwanza chini ya kocha Unai Emery, ambaye katika mchezo huu atakuwa akiongoza timu yake kwa mara ya 200 katika mashindano hayo. Hata hivyo, tangu wakati huo, Villa imeshinda mchezo mmoja pekee kati ya saba dhidi ya United, ikitoka sare moja na kupoteza mitano.

Man United inapewa asilimia 39 za ushindi, ikilinganishwa na asilimia 34.4 za Aston Villa. United inataka kusitisha mfululizo wa mechi saba bila ushindi katika ligi, ikiwa na sare nne na vipigo vitatu. Mchezo huo pia una uwezekano wa asilimia 26.5 wa kumalizika kwa sare.